HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 09, 2019

Wagonjwa wa malaria SADC waongezeka

Na Suleiman Msuya

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema idadi ya wagonjwa wa ugonjwa wa malaria katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), imeongezeka kwa asilimia 10.

Aidha Waziri Mwalimu amesema rasilimali mali za kudhibiti malaria zimepungua.

Waziri Mwalimu aliyasema hayo leo katika kilele cha siku ya malaria kwa nchi 16 za SADC kilichofanyika kwenye Kiwanda cha Kutengeneza Viwadudu Wadhurifu (TBPL) kilichopo wilayani Kibaha mkoani Pwani.

Mwalimu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mawziri wa Afya na Ukimwi SADC alisema kumekuwepo na jitihada nyingi za kukabiliana na ugonjwa huo lakini bado changamoto ni kubwa hivyo kusisitiza matumizi ya viuadudu kama njia muafaka.

"Kampeni ya " Ziro Malaria inaanza na mimi" ni endelevu kuelekea kutokomeza malaria nchi za SADC, "alisema.
 
Alisema takwimu kwa nchi za SADC zinaonesha idadi ya wagonjwa imeongezeka kwa takribani asilimia 10 huku kukiwa na changamoto ya rasilimali ya kudhibiti ikijitokeza.

"Jitihada za pamoja zinahitajika kuijengea uwezo jamii, ili iweze kushiriki katika utekelezaji wa afua mbalimbali katika mapambano dhidi ya malaria," alisema.

Waziri Mwalimu alitolea mfano nchi ya Tanzania ambayo maambukizi yamepungua kwa takribani asilimia 50 kutoka asilimia 14.8 mwaka 2015 hadi asilimia 7.3 mwaka 2017.

Mwenyekiti huyo alisema kupungua huko kunatokana na kuongezeka kwa matumizi ya vyandarua hadi kufikia asilimia 63 kutoka asilimia kutoka 52.

"Kuongezeka idadi ya watu wanaothibitishwa kwa vipimo hadi kufikia asilimia 99 mwaka 2018 kutoka asilimia 64 mwaka 2015, kupungua idadi ya vifo vitokanavyo na malaria kwa asilimia 63 kutoka vifo 6,737  mwaka 2015 hadi vifo 2,540 mwaka 2018," alisema.

Aidha Waziri Mwalimu alisema Tanzania imefanikiwa kupambana na malaria kwa kupitia Mpango Mkakati wa 2015 hadi 2020 ambapo nchi imegawa mikoa na halmashauri kulingana na ukubwa wa tatizo la malaria ili kuweza kupanga kitita cha afua kulingana maambukizi.

Alisema jitihada nyingine ni kujenga kiwanda cha kuzalisha viuadudu vya kibailojia kwa ajili ya kuua mbu hatua ya mazalia.

Mwalimu alitoa rai kwa nchi za SADC kununua viuadudu vya kibailojia vinavyotumika kuuwa mazalia ya mbu wa malaria na magonwa mengine kama dengue, zika na magonjwa mengine.

Akizungumza katika kilele hicho Katibu Mtendaji wa Chama cha Wabunge Wanaopambana na Malaria  (TAPAMA), Dk.Rafael Chegeni alizika nchi za SADC zinapaswa kutekeleza mambo yote wanayokubaliana na kuachana na maneno.

"Huu sio wakati maneno tunataka utekelezaji katika mapambano hata ya malaria. Ili zero malaria ianze na mimi tunapaswa kutekeleza na sio kupanga," alisema.

Mwenyekiti wa TAPAMA, Riziki Lulida aliiomba nchi za SADC kutekeleza kampeni hiyo kwa kushirikisha makundi yote katika jamii.

"Kundi la watu wenye ulemavu limekuwa likisahaulika mara kwa mara katika hizi kampeni naomba kampeni ya " Ziro malaria inaanza na mimi" isiwasahau,"alisema.

Kwa upande wa wadau wa Maendeleo na mashirika ya kimataifa walisema wataendelea kushirikiana na nchi za SADC kuhakikiasha kampeni ya "Ziro Malaria inaanza na mimi " inatimia.

No comments:

Post a Comment

Pages