HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 20, 2020

KALIUA YAKISIA KUKUSANYA BILIONI 38.7 MWAKA UJAO WA FEDHA

Na Tiganya Vincent

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kaliua imeomba kuidhinishiwa shilingi bilioni 38.7 ikiwa ni  makisio ya mapato na matumizi ya mwaka ujao wa fedha wa 2020/21.
Fedha hizo zinatokana na makusanyo ya vyanzo mbalimbali ikiwemo ruzuku toka Serikali kuu na makusanyo ya mapato ya ndani ya Halmashauri.

Kauli hiyo imetolewa leo na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua Edwin Mashala wakati wa kikao na Sekretaieti ya Mkoa wa Tabora cha kuchambua na kujadili mapendekezo ya makisio ya mipango na bajeti za Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa mwaka ujao wa fedha.

Alisema kati ya fedha hizo bilioni 35 .4 ni ruzuku kutoka Serikali kuu  na bilioni 3.2  zitatokana na makusanyo yanayotokana na mapato ya ndani.

Mashala  alisema mapendekezo ya bejeti ijayo yamezingatia kuendeleza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya , Vituo vya Afya Usinge, Mwongozo na Uyowa na kuendeleza ukamilishaji wa miundombinu ya shule na huduma za elimu.

Alisema eneo jingine ni uimarishaji wa makusanyo ya ndani kwa kutumia mfumo wa kielektroniki na kuongeza vyanzo vya mapato vipya ili kuongeza mapato na uwezeshaji wananchi kiuchumi kupitia mikopo ya wanawake , vijana na walemavu.

Mashala aliongeza kuwa kipaumbele kingine ni uchongaji wa barabara katika maeneo yaliyopimwa na ulipaji wa fidia ya maeneo yalitwaliwa na Halmashauri kwa shughuli za umma.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Hamis Mkunga aliwataka viongozi wa Halmashauri hiyo kuongeza juhudi katika kuimarisha vyanzo vya makusanyo ili wawe na  uwezo wa kujitegemea ifikapo mwaka 2025 kama Serikali ilivyoagiza.

Kwa upande wa Katibu Tawala Msaidizi Rukia Manduta alitaka Halmashauri kujitahidi kutozalisha madeni kwani Serikali Kuu haitakuwa tayari kulipa madeni yao.

Alisema jambo la msingi ni kujitahidi kukusanya fedha kutokana na mapato ya ndani ili waweze kulipa madeni yao.

Aidha Katibu Tawala Msaidizi huyo aliwakumbushia kuhakikisha wanatenga  wa fedha katika bajeti ijayo kwa ajili ya ununuzi wa taulo za wanafunzi wa kike mashule, asilimia 10 kwa ajili ya mikopo ya wanawake , vijana na walemavu  na kutenga fedha kwa ajili ya uendeshaji wa shule mpya

No comments:

Post a Comment

Pages