Meneja Mwandamizi wa Bima wa Benki ya NMB, Martine Massawe (kushoto),
akikabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya Sh. Milioni 35 kwa Mkurugenzi
Mtendaji wa African Digital Banking Summit Limited, Baraka Mtavangu,
kwa ajili ya udhamini wa NMB Bima Marathon, mbio zitazofanyika Machi 28
jijini Dar es Salaam. Katikati ni Meneja wa NMB Jogging Club,
Elifadhili Mramba. (Na Mpiga Picha Wetu).
Na Mwandishi Wetu
Na Mwandishi Wetu
BENKI ya NMB, imetangazwa kuwa Mdhamini
Mkuu wa Mbio za Bima Marathon 2020, zinazotarajiwa kufanyika Machi 28 jijini
Dar es Salaam, chini ya uratibu wa Kampuni ya African Digital Banking Summit.
Kwa udhamini huo, mbio hizo
zinazoenda kufanyika kwa mara ya pili mfululizo, zitatambulika kwa jina la NMB
Bima Marathon 2020, ambazo zitahusisha mbio za kilomita 21, kilomita 10 na kilomita
tano.
NMB imedhamini mbio hizo kwa
kitita cha Sh. Milioni 35, ambako hafla ya NMB kutangaza udhamini wake huo katika
mashindano hayo imefanyika jana jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa kukabidhi
mfano wa hundi ya udhamini, Meneja Mwandamizi wa Bima wa NMB, Martine Massawe,
alisema wamevutiwa kudhamini Bima Marathon kutokana na mlengo wake.
"Mashindano haya yanatumika kama
jukwaa la kutoa elimu ya Bima kwa Watanzania, lakini pia kuimarisha afya. Nasi tumeona
ni fursa tunayoweza kuitumia kutangaza huduma mpya ya Bancassuarance. Lakini hii sio mara ya kwanza
kwetu NMB kudhamini michezo, tumefanya hivyo katika soka ambako tumeidhamini
Taifa Stars na timu za Azam FC na Singida United. Tumefanya hivyo pia katika
mpira wa magongo, gofu na kriketi na kadhalika,” alisema Massawe.
Alitumia fursa hiyo kuwatakia Watanzania
kujenga utamaduni chanya wa kutumia bima kadri ya matahitaji yao, kwa
kutembelea matawi yote 224 kote nchini na kukata bima mbalimbali zikiwamo za maisha,
magari, afya, nyumba, kilimo na dhamana kutoka kwa wabia wake.
Huduma za bima zitakazopatikana
katika matawi ya NMB ni pamoja na zile za Kampuni za Sanlam Life, UAP, Shirika
la Bima la Taifa (NIC), Jubilee Insurance, Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC) na
Reliance Insurance.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
Mtendaji wa Kampuni ya African Digital Banking Summit inayoratibu mbio hizo,
Baraka Mtavangu, aliipongeza NMB kwa udhamini, anaoamini unaenda kubadili
taswira ya mashindano hayo.
Alibainisha kuwa, mbio hizo
zitanatarajia kushirikisha wakimbiaji watu wazima wapatao 3,500 na watoto 500,
na kwamba usajili unafanyika katika vituo mbalimbali, ikiwemo Mlimani city na
baadhi ya matawi ya NMB kwa Sh. 20,000 kwa watu wazima na Sh. 15,000 kwa
watoto.
“Kutakuwa na Washindi wa kwanza
hadi wa tano katika mbio za kilomita 21 na kilomita 10, ambako mshindi wa km 21
atatwaa Sh. Mil. 1, huku mshindi wa km 10 atajishindia Sh. 700,000. Zawadi
zingine zitatangazwa baadaye,” alisema Mtavangu.
Mratibu huyo alilishukuru
Shirikisho la Riadhaa Tanzania (RT) kwa sapoti, ushirikiano na kibali cha
uendeshaji wa mbio hizo, ambazo alisema zitashirikisha Watanzania na wageni
wanaoishi nchini, huku wakimbiaji wa nje wakitakiwa kujiandikisha kupitia chama
cha riadha nchini .
#Umebima?
No comments:
Post a Comment