HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 03, 2020

Rotary Klabu O'bay yapima afya watoto 1,500 Msasani

Mtoto akipimwa malaria wakati wa kambi hiyo.
Madaktari wakiwapima macho watoto waliofika kwenye kambi ya afya iliyoandaliwa na Klabu ya Rotary ya Oystebay jijini Dar es Salaam.

 
Na Irene Mark

KLABU ya Rotary Oysterbay jijini Dar es Salaam imefanikisha uchunguzi wa afya kwa watoto 1,500 wa Kata ya Msasani na kuwabaini wengi kuwa na maradhi ya masikio, ngozi na utapiamlo.

Klabu hiyo jana iliweka kambi ya siku moja kwenye Shule ya Msingi Msasani jijini Dar es Salaam ambapo madaktari waliwapima watoto macho, kinywa, masikio, maleria, ngozi, hedhi salama, kuwapa dawa za malaria, minyoo bure, chakula na vinywaji baridi.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa upimaji huo, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Abdallah Singano, alisema ni utaratibu wao kila mwaka kuisaidia jamii kwenye sekta za afya, elimu na maji.

"Tumepata ufadhili kutoka DTB, Whitedent, Knight Support na wengine wengi lengo ni kuisaidia jamii hasa watoto wawe na afya njema.

"Leo hapa tunahudumia watoto 1,500 hao watachunguzwa na madaktari wa kujitolea watakaobainika na maradhi tutawatibu na watakaokuwa salama tutawapa ushauri na dawa za minyoo," alisema Singano.

Daktari Helga Mutasingwa alisema wazazi hawana utaratibu wa kuchunguza afya za watoto wao hivyo Rotary Klabu ya Oysterbay inatumia kambi ya afya kuwakumbusha wazazi na walezi.

"Tunafanya hivi kila mwaka lengo letu ni kuonesha njia kwa wengine nao wasaidie jamii kwa nafasi ndogo waliyonayo... hii italeta ustawi bora kwa kizazi kijacho na taifa salama.

"Tunawafundisha pia kuhusu hedhi salama na kuwapa taulo za kike zile za kufua ambazo watazitumia mwaka mzima," alisema Dk. Mutasingwa.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Msasani A, Edward Mollel aliishukuru Klabu ya Rotary kwa huduma hiyo huku akibainisha kwamba watoto wa Kata ya Msasani wamenufaika.

Alitoa wito kwa wazazi na walezi kuwachunguza watoto wao na kuwapeleka hospitali kwa uchunguzi zaidi huku akikiri kwamba chakula bora ni changamoto kwa watoto wengi.

"Kuanzia wiki ijayo Kamati ya shule itahakikisha chakula kinapatikana hapa shule hasa kwa watoto kuanzia darasa la nne hadi la saba," alisema Mwalimu Mollel.

No comments:

Post a Comment

Pages