Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.
Philip Isdor Mpango (Mb), akipeana mkono na Katibu Mkuu wa Shirika la Forodha
Duniani (WCO), Dkt. Kunio Mikuriya, baada ya Mkutano kati yao uliofanyika
jijini Dodoma. (Picha na Veronika Kazimoto na
Peter Haule).
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.
Philip Isdor Mpango (Mb), akielezea umuhimu wa kuboreshwa kwa Idara ya Forodha
kwa lengo la kuongeza urahisi wa ufanyaji wa biashara, wakati wa Mkutano na
Katibu Mkuu wa Shirika la Forodha Duniani (WCO), Dkt. Kunio Mikuriya (hayupo
pichani), kulia ni Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt.
Edwin Mhede, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dodoma.
Mkutano kati ya Waziri wa Fedha na
Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa tatu kushoto) na Katibu Mkuu wa
Shirika la Forodha Duniani (WCO), Dkt. Kunio Mikuriya (wa kwanza kulia), katika
ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.
Na Peter Haule, WFM, Dodoma
Serikali imekubaliana na Shirika la
Forodha Duniani (WCO) kuisaidia nchi zana zenye teknolojia za kisasa zinazoweza
kung’amua watu wanaofanya biashara za magendo na kuifanya Forodha kuongeza
ufanisi wa ufanyaji biashara na ukusanyaji wa mapato.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha na
Mipango, Dkt. Philip Mpango, alipokutana nan a kufanya mazungumzo na Katibu
Mkuu wa Shirika la Forodha Duniani (WCO), Dkt. Kunio Mikuriya, jijini Dodoma.
Dkt. Mpango alisema kuwa Shirika la WCO
limekubali kutoa Boti, mashine za kupiga picha ndani ya Kontena na vifaa
vingine vyenye teknolojia za kisasa vinavyoweza kung’amua watu wanaofanya
biashara za magendo, hivyo kuifanya Serikali kuwa na uwezo zaidi wa kudhibiti
shughuli hizo haramu.
“Ujio wa Katibu Mkuu wa WCO,
katika nchi za Afrika hususani Tanzania na Kenya umelenga kuziwezesha nchi hizo
kuzitumia fursa zilizopo katika Shirika hilo na kushirikiana na Idara ya
Forodha hapa nchini kurahisisha biashara na ukusanyaji wa mapato jambo ambalo
pia ni agenda ya Serikali ya Tanzania”, alieleza Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango alisema kuwa, Forodha kwa
maana ya Bandari na Vituo vya Forodha vilivyopo katika mipaka ni eneo muhimu
katika kukuza biashara katika nchi na Ukanda wa Kusini mwa Afrika, ikizingatiwa
kuwa Tanzania ni mlango wa kupitisha mizigo kwenda nchi za Zambia, Zimbabwe,
Rwanda, Burundi, Malawi, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na nyingine,
hivyo kuwepo kwa Teknolojia hiyo kutakuwa nguzo muhimu ya kuifanya Forodha kuwa
ya Kisasa na inayorahisisha biashara.
Alisema kuwa wamekubaliana kutoa fursa
kwa vijana wa Forodha kupata uzoefu wa Forodha nyingine zinavyoendeshwa kwa
ufanisi na pia kutoa mafunzo kwa wakufunzi ambao si tu watatoa mafunzo nchini
lakini pia nje ya nchi.
Wakati huo huo, Dkt. Mpango amewaonya
wafanyabiashara za magendo nchini kuachana na biashara hiyo kwa kuwa watapoteza
mitaji baada ya Serikali kujipanga kwa teknolojia mpya ya kuwadhibiti kwa kuwa
biashara hizo ni hatari kwa uchumi wa Taifa na pia Afya za wananchi.
“Wito wangu ni kwamba watanzania
wote na wengine walio nje ya nchi wanaoshiriki katika biashara za magendo
waache vitendo hivyo na wafuate taratibu za Forodha kinyume na hapo watapoteza
mitaji yao kwa kuwa tutawakamata’’, alieleza Dkt. Mpango
Waziri Mpango amemuagiza Kamishna Mkuu
wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Edwin Mhede, kuhakikisha Ushirikiano
na WCO unaimarika kwa kuwa Shirika hilo lina manufaa kwa Maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Shirika
la Forodha Duniani (WCO), Dkt. Kunio Mikuriya, alisema kuwa katika kuifanya
Forodha iwe na ufanisi lazima kuwe na dhamira njema ya kisiasa, Ushirikiano na
wafanyabiashara,wakala na Forodha nyingine nje ya nchi na pia kuwekeza kwenye
rasilimali watu, jambo ambalo amehakikishiwa
na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mpango kwamba lipo.
Dkt. Mikuriya ameahidi kuwa Shirika lake
litafanya kazi kwa karibu na Tanzania katika mambo yote ambayo wamekubaliana
ili kuleta tija katika Sekta hiyo ya Forodha ndani na nje ya Tanzania.
Naye Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe.
Innocent Bashungwa, ameliomba Shirika la WCO kuondoa changamoto zinazoweza
kuwakwamisha wafanyabiashara wa Tanzania kuuza bidhaa katika masoko ya
Kimataifa na pia waweze kuzitumia fursa za kibiashara katika masoko hayo.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Edwin Mhede, alisema kuwa wamekubaliana
na Shirika la WCO, kujenga Maabara ambayo itasaidia kutambua na kupima bidhaa
zinazoingizwa kutoka nje ya nchi ili kujiridhisha kama zimezingatia utaratibu,
lengo likiwa ni kurahisisha uthaminishaji wa mizigo na uondoshaji wa mizigo
bandarini kwa wakati.
“Maabara hiyo itakayojengwa katika Ofisi
za Mamlaka ya Mapato Jijini Dar es Salaam, itakua miongoni mwa maabara chache
Afrika ambayo itakuwa ya mfano katika kusimamia eneo hilo la Forodha”, alieleza
Dkt. Mhede.
Alisema kuwa wamekubaliana pia kuweka
miundombinu itakayochunguza mizigo inayopita katika Ukanda wa Kusini (Mtwara
Corridor), ikizingatiwa kuwa barabara ya Ukanda huo imesajiliwa kwa lengo la
kuhakikisha Wajasiliamali na wenye viwanda wanaitumia kwa tija.
No comments:
Post a Comment