*Sh. bilioni 334 zatumika kununua dawa, chanjo, vifaa tiba na vitendanishi
* Sh. bilioni 325.9
zatolewa miradi maji, uchimbaji
wa visima
Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson akiongozwa na wapambe kutoka
kwenye ukumbi wa Bunge jijini Dodoma baada ya Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa kusoma hotuba ya kuahirisha Bunge, Februari 7, 2020. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu).
Dodoma, Tanzania
WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amesema Serikali imeboresha utoaji wa huduma za afya kwa kugharamia
ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya vituo 487 vya kutolea huduma za afya.
“Maboresho hayo
yanajumuisha vituo vya afya 320, hospitali za halmashauri za wilaya 70,
hospitali za zamani tisa na zahanati 88,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa
kauli hiyo leo (Ijumaa,
Februari 7, 2020) wakati akitoa hotuba ya kuahirisha Mkutano wa 18
wa Bunge jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Machi
31, mwaka huu.
Mbali na hayo,
Waziri Mkuu amesema Serikali imejenga na kuboresha miundombinu ya hospitali za
rufaa za Njombe, Simiyu, Mara, Geita, Songwe, Katavi, Sekou Toure, Burigi -
Chato, Mwananyamala, na hospitali za rufaa za kanda ya Kusini Mtwara, kanda ya
Nyanda za Juu Kusini Mbeya, hospitali ya Kibong’oto na ujenzi wa Isolation centre katika hospitali ya
Taifa Muhimbili.
“Serikali
imekamilisha ujenzi wa nyumba 320 za watumishi wa sekta ya afya pamoja na
kugharamia ununuzi wa dawa, chanjo, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kwa
gharama ya sh. bilioni 334,” ameongeza.
Amesema katika
kipindi hicho, jumla ya madaktari bingwa 311 wameendelea kulipiwa gharama za masomo ya uzamili katika vyuo vikuu vya ndani na nje
ya nchi na kwamba, katika kipindi cha
nusu ya pili, Serikali inakusudia kuajiri zaidi ya watumishi 4,000 wa sekta ya
afya.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu ameelezea
mafanikio yaliyofikiwa kwenye sekta ya maji katika kipindi cha
Julai hadi Desemba 2019 ambapo sh. bilioni 325.9
zimetolewa kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maji ikiwemo uchimbaji wa visima vifupi,
vya kati na virefu.
Amesema fedha hizo zimetumika kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama vijijini na
mijini. Chini ya utekelezaji wa miradi
hiyo, miradi 631 inaendelea kujengwa ikiwemo 558 ya maji vijijini na 73 ya maji
mijini.
“Miongoni mwa
miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa ni pamoja na mradi wa maji Arusha,
mradi wa maji wa Same – Mwanga - Korogwe
na mradi wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda katika miji ya Isaka, Tinde,
Kagongwa, Tabora, Igunga, Uyui na Nzega.
Waziri Mkuu ameema
lengo la Serikali ya Awamu
ya Tano ni kuwahudumia wananchi sambamba na kuratibu vyema utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya kimkakati. Amesema miradi hiyo inayohusisha sekta ya miundombinu
wezeshi, nishati, maji, afya na elimu imekuwa chachu ya kuboresha maisha ya
Watanzania kupitia ukuaji wa sekta rasmi na isiyo rasmi.
No comments:
Post a Comment