HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 10, 2020

TANZANIA YATAKA AMANI KUPUNGUZA MZIGO WA WAKIMBIZI AFRIKA

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiteta jambo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) katika ukumbi wa Mkutano wa Umoja wa Afrika Addis Ababa,Ethiopia. Anayeshuhudia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan


Na Mwandishi Wetu


 Tanzania imetaka Umoja wa Afrika na Jumuiya za Kimataifa kuongeza jitihada na nguvu katika kuleta amani katika maeneo yenye migogoro Barani afrika hususani katika Nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ili kuipunguzia Tanzania mzigo wa wakimbizi ulioubeba kwa muda mrefu hivi sasa.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassani ameyasema hayo katika siku ya kwanza ya Mkutano wa 33 wa kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika unaofanyika Addis Ababa Nchini Ethiopia ambapo ameongeza kuwa kauli mbiu ya mkutano wa mwaka huu ya kunyamazisha silaha (silencing the gun) umekuja wakati muafaka kwa kuwa mapigano na kutokuwepo utulivu katika baadhi ya nchi za Afrika zinachelewesha maendeleo katika Bara hilo.

Ameongeza kuwa endapo Umoja wa Afrika na Jumuiya za Kimataifa zitaongeza nguvu katika kunyamazisha silaha na kukawepo amani na utengamano,ni dhahiri viongozi wataelekeza nguvu kubwa  katika maendeleo endelevu ya wananchi na hivyo kupunguza umasikini katika Bara la Afrika ambalo linaonekana kama Bara lililoghubikwa na migogoro na mapigano.

Mhe. Samia Suluhu Hassani pia ameuahidi Umoja wa Afrika kuwa Tanzania itatekeleza kwa kasi mpango wa Umoja huo katika Mapambano dhidi ya Malaria na kwamba Tanzania imedhamiria kuutokomeza kabisa ugonjwa wa Malaria ifikapo mwaka 2030.

Katika Mkutano huo wa 33 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika wameshuhudia mabadilishano ya uenyekiti ambapo Mwenyekiti anayemaliza muda wake  Mhe.Abdel Fattah el-Sisiambae pia ni Rais wa Misri amekabidhi Uenyekiti kwa Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kusini Mhe. Cyrill Ramaphosa ambae anakuwa Mwenyekiti Mpya wa Umoja wa Afrika.

No comments:

Post a Comment

Pages