HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 10, 2020

THBUB yashauriwa kuelimisha wananchi kuhusu haki ardhi, mirathi

 Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Rehema Madenge akizungumza wakati akiukaribisha ujumbe wa THBUB na Viongozi wa Haki Maendeleo walipotembelea ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Lindi. Kulia Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi.
 Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, akizungumza na ujumbe wa THBUB na Viongozi wa Haki Maendeleo (hawapo pichani) katika ofisi zake Mkoani Lindi. Kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Rehema Madenge.
 Kamishna wa THBUB, Amina Talib Ali (kushoto), akitoa mkono wa pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, walipomtembelea ofisi kwake kufuatia mafuriko ya mvua yaliyopelekea maafa makubwa mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi (Katikati) akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa THBUB na Viongozi wa Haki Maendeleo. Waliosimama mbele kutoka kulia ni Muwakilishi wa Asasi ya Haki Maendeleo, Dkt. Abdallah Mrindoko, wa pili kulia ni Kiongozi wa Haki Maendeleo, Wilfred Warioba na wa tatu kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Rehema Madenge. Kutoka kushoto ni Afisa Mfawidhi wa THBUB wa Mkoani Lindi, Noel Chiponde, wa pili kushoto ni Mkurugenzi wa Sheria wa THBUB, Nabor Assey na wa tatu kushoto ni Kamishna wa THBUB, Amina Talib Ali.



Na Mbaraka Kambona


Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imeshauriwa kujikita katika kutoa elimu ya haki ya ardhi na mirathi kwa kuwa maeneo hayo yameonekana kuwa na changamoto kubwa sana kwa jamii nchini.

Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi alipokutana na ujumbe wa THBUB na viongozi wa Asasi ya kiraia, Haki Maendeleo walipomtembelea ofisini kwake kumpa pole kufuatia maafa waliyoyapata yaliyosababishwa na  mafuriko ya mvua yaliyotokea mkoani humo hivi karibuni.

Akiongea katika kikao hicho kilichofanyika leo Februari 8, 2020 katika ofisi zake mkoani Lindi, RC Zambi  alisema kuwa tume iwaelimishe wananchi kuhusu haki zao ili wazijue na waeleweshwe taratibu za kufuata pindi wanapotaka kudai haki zao zitakapokuwa zimevunjwa.

Alisema kuwa shida  ipo kwa wananchi wa chini ambao kwa kiasi kikubwa hawajui haki zao na hata ikitokea kuwa wanazifahamu bado hawajui njia sahihi za kufuata pale haki yake inapokuwa imevunjwa ili kuidai.

Aliendelea kusema kuwa matatizo mengi yapo katika ardhi na mirathi hivyo aliishauri tume kutoa elimu zaidi katika maeneo hayo ili watu wajue haki zao na njia za kufuata pindi wanapotaka kudai haki zao.

“Kwenye mirathi huko kuna matatizo, watu hawajui haki zao, ardhi pia kuna shida sana lakini wananchi hawajui njia za kufuata kudai haki zao, tuwasaidie wananchi hawa ili wajue njia za kufuata kudai haki zao ”, alisema Zambi
“Mheshimiwa Rais Magufuli anatuambia kila siku kuwa ametutuma ili tukatatue kero za wananchi, tena wananchi wa chini”,aliongeza.

“Tunatambua kuwa tume hamuwezi kwenda kila mahali, sisi tupo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi kutatua kero zao, hivyo tushirikiane katika kutatua kero hizo”, alisisitiza
Kamishna wa THBUB, Amina Talib Ali, ambaye ndiye alikuwa mkuu wa msafara huo alimueleza mkuu wa mkoa kuwa tume imekuwa ikifanya kazi zake kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo za serikali, binafsi na taasisi za kimataifa katika kuhakikisha haki za binadamu na misingi ya utawala bora inalindwa na kukuzwa nchini.

Amina alimueleza mkuu wa mkoa kuwa itaendele kushirikiana na wadau wote katika kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa na kuzingatiwa. Hata hivyo, Katika kuimalisha ushirikiano huo Kamisha alimueleza mkuu wa Mkoa kuwa  wametoa mafunzo kwa Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya mkoa huo wa Lindi ili kuwajengea uwezo wa masuala ya haki za binadamu na utawala bora. Mafunzo hayo yalitolewa na THBUB kwa kushirikiana na Asasi ya Kiraia, Haki Maendeleo ambayo ndio iliwezesha mkutano huo kufanyika.

Kikao hicho cha Mkuu wa Mkoa  na THBUB pamoja na viongozi wa Haki Maendeleo pia kilihudhuriwa na Katibu Tawala wa Mkao wa Lindi, Rehema Madenge na Wakuu wa Wilaya tano za Mkoani humo.

No comments:

Post a Comment

Pages