Wachezaji
wa timu ya Taswa FC na Stanbic wakiwa katika picha ya pamoja baada ya
mchezo wa kirafiki uliochezwa kwenye Uwanja wa Gymkhana, jijini Dar es
Salaam juzi. Stanbic ilishinda 3-2. (Na Mpiga Picha Wetu).
NA MWANDISHI WETU
TIMU ya soka ya waandishi wa habari, Taswa FC, imefungwa mabao
3-2 na kikosi cha Benki ya Stanbic katika mchezo wa kirafiki uliochezwa juzi kwenye
Uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam.
Mchezo huo wa aina yake, uliandaliwa na Benki ya Stanbic kama
sehemu ya kudumisha uhusiano na ushirikiano baina ya pande hizo mbili.
Katika mchezo huo uliohudhuriwa na wafanyakazi wa Benki ya
Stanbic, wanahabari na wadau wengineo wa soka, Taswa FC ndiyo iliyokuwa ya
kwanza kupata bao lililofungwa na Mbozi Katala, huku Zico George
akifunga la pili.
Kwa upande wa Stanbic Bank, mabao yao yaliwekwa
kimiani na Ally Masoud na Amrany Mlawa aliyecheka na nyavu mara mbili.
Kwa ujumla, mchezo huo ulikuwa mkali na wenye msisimko
kwa dakika zote 90, ukitoa bonge la burudani kwa mashabiki wa soka
waliojitokeza uwanjani hapo.
Baada ya mchezo huo, wachezaji wa timu zote mbili, wanahabari,
wafanyakazi wa Stanbic Bank na wengineo, walijumuika kwa pamoja katika hafla ya
chakula cha mchana iliyoambatana na vinywaji vya kila aina.
Akizungumza baada ya tukio hilo, meneja wa Taswa FC, Hussein
Omari, aliipongeza Stanbic kwa tukio hilo, kuanzia mchezo huo uliokuwa wa aina
yake, lakini pia kwa hafla fupi ya chakula cha mchana.
“Pongezi ziwaendee Benki ya Stanbic kwa kutukutanisha na
kufurahi pamoja.
“Mchezo ulikuwa ni mzuri na wenye upinzani mkubwa, ila
Stanbic FC washukuru Mungu kuna baadhi ya wachezaji wetu tishio hawakuweza
kufika, akiwamo Mwenyekiti wetu, Majuto Omari ambaye yupo nje ya nchi kikazi.
Pia, tuwashukuru kwa chakula na vinywaji kwani tumekula na kunywa hadi
tumesaza,” alisema Hussein.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha
Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Stanbic, Desideria Mwegelo, aliwashukuru viongozi
wa Taswa FC kwa kukubali kushiriki tukio hilo, lakini pia wanahabari wengineo
waliojitokeza wka wingi.
“Wanahabari ni sehemu muhimu mno katika jamii hivyo sisi kama
Stanbic Bank tumefarijika na umoja baina yetu licha ya kwamba tumewafunga Taswa
FC," alisema.
Akizungumza kutoka nchini Morocco alikokwenda kikazi, Mwenyekiti
wa Taswa FC, Majuto, aliwapongeza Stanbic Bank kwa ushindi na kuwataka
kuendeleza ushirikiano huo baina yao kwa manufaa ya pande zote mbili.
No comments:
Post a Comment