Mkuu
wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo, alipokuwa akitoa maagizo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Kalambo na timu yake (hawapo pichani) ambayo imeshindwa kutekeleza
maagizo ya Waziri wa Uvuvi.
Na Mwandishi Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo, amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo
pamoja na kamati aliyoundwa kutathmini miundombinu ya soko la samaki Kasanga
kufika mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa kueleza sababu za kushindwa
kutekeleza maagizo saba yaliyoachwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi nchini Luhaga Mpina juu ya uboreshwaji wa Soko hilo.
Waziri Mpina ambaye aliacha
maagizo hayo alipofanya ziara yake ya kikazi mkoani Rukwa tarehe 30.10.2019 na
kujionea miundombinu chakavu iliyopo katika soko hilo pamoja na kusikiliza
kilio cha wavuvi na wananchi wanaoishi karibu na soko hilo ambalo tangu
kuzinduliwa kwake mwaka 2013 na aliyekuwa makamu wa Rais Dkt. Gharib Bilal
halijawahi kutumika hadi leo.
Katika kusisitiza hilo, Wangabo alisema kuwa miongoni mwa maagizo yaliyoachwa ni kuwa soko lianze
kutumika kuanzia tarehe 31.12.2019 lakini halmashauri haina mpango huo, na
kuongeza kuwa soko hilo ni chanzo cha mapato cha halmashauri kwani kukamilika
kwake halmashauri itapata ushuru na
kuongeza mapato katika halmashauri hiyo ambayo ipo hoi katika makusanyo na
hivyo kuwataka watumie pesa kupata pesa.
“Wala msitegemee wizara ndio
itafanya kila kitu hapa ili soko liweze kufanya kazi, lazima ninyi mtumie pesa
ili mpate pesa, sasa kama hamtumii pesa kuuvuta umeme kutoka pale, ilikuwa ni
changamoto kubwa mkasema hakuna transfoma tukamwambia meneja wa TANESCO leta
transfoma akaleta ile pale mwaka jana, kutoa pale ule umeme kuja hapa imekuwa
shughuli mnataka mwaka mwingine uishe, viongozi waendelee kutoka Dodoma, Dar es
Salaam wanakuja hapa kwaajili ya mambo madogo madogo, haiwezekani, amkeni,”
Alisisitiza.
Wakati akisoma taarifa ya
mkoa juu ya utekelezaji wa maagizo hayo ya waziri Kaimu Katibu Tawala msaidizi
seksheni ya Uchumi na Uzalishaji Respich Mayengo alisema kuwa Waziri mpina
aliagiza kufanyika kwa maandalizi ya kuhakikisha kwamba soko la samaki
linafanya kazi kuanzia tarehe 1.12020 na hivyo masuala yote yakamilike ndani ya
miezi miwili kutoka 30.10.2019.
“Soko halijaanza kufanya
kazi kwa kuwa mfumo wa umeme ndani ya soko haujakamilika licha ya kuwekewa
transfoma, elimu na hamasa kwa wavuvi wa kata ya Kasanga na samazi haijatolewa
na Katibu Tawala Mkoa alimwandikia DED Kalambo barua kuhusu kuanza kufanya kazi
kwa soko hili na kutekeleza maelekezo ya waziri na kumpa ‘deadline’ ya terehe
20.1.2020 lakini hadi sasa barua hiyo haijajibiwa,” alisema.
Kwa upande wake katibu wa
kamati hiyo Afisa Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Sadick Senge alisema
kuwa hivi karibuni wizara ilituma timu kufanya tathmini ya gharama (BOQ)
kwaajili ya miundombinu ambayo wizara inaweza kuichukua na kuweza kuikarabati.
“Baadhi ya miundombinu hiyo
ambayo wizara inaweza kuifanyia kazi ni Blast freezer, kuweka mashine na jengo
la Soko lakini pia ilikuwa imefanya BOQ kwaajili ya mradi wa barafu na vilevile
kuweka mtambo wa utakatishaji maji (water treatment plant) kwaajili ya
kuzalisha barafu,” Alisema
Wakati alipopewa nafasi ya
kuwasemea wavuvi wa Kata ya Kasanga Mwenyekiti wa Wavuvi hao Khalfan Saidi ameshauri
kuwa umeme uwashwe ili mashine ya barafu ifanye kazi na barafu zikiwepo samakai
watakuwepo, na kutahadharisha kuwa bila ya kuwepo kwa barafu hizo wavuvi
hawawezi kuuza samaki wao kwenye soko hilo.
“Cha ajabu tangu wameweka
transfoma pale kuunganisha tu umeme pale kwenye zile jenereta ili umeme uwake
mwezi umeisha, kuunganisha tu pale mwezi umeisha kwahiyo imekuwa ni kila siku
wakija tunazungumzia hili hili la kusema soko lifanye kazi, wavuvi wako tayari
kuleta samaki hapa, sasa unamuamrishaje mvuvi kuleta samaki hapa hata barafu
hakuna akileta samaki zake zisipouzikana hawezi kuhifadhi matokeo yake watu
hukimbia na samaki zao vijiji, kwasababu vijijini kuna watu wenye friza
wanatengeneza barafu,” Alisema.
No comments:
Post a Comment