HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 18, 2020

Corona yakimbiza kongamano la Mabadiliko Tabianchi

Na Suleiman Msuya

KUPATIKANA kwa raia wenye virusi vya COVID-19 Corona kumesababisha kongamano  na maonesho ya sita ya Mabadiliko ya Tabianchi ambalo lilipangwa kufanyika Machi 25 hadi 26 mwaka huu katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), kuahirishwa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari leo na Mkurugenzi wa Program wa Shirika lisilo la Kiserikali la FORUMCC, Angela Damas (pichani), ilisema wamelazimika kuahirisha kongamano hilo kutokana na hali ya Corona ilivyo nchini.

Damas alisema kongamano hilo la sita la mwaka 2020 lilkitarajiwa kukutanisha zaidi ya wadau kutoka Serikali, taasisi za kiraia, watafiti na wananchi 200 kutoka kona mbalimbali za nchi litapangwa wakati mwingine.

“Tunapenda kuwatarifu wadau wetu kuwa kongamano ambalo tuliandaa kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU), limeahgirishwa kutokana na kubainika kwa wagonjwa wa virusi vya Corona nchini tutatoa taarifa mpya,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema FORUMCC, inawaomba Watanzania wote kuchukua hatua zote ambazo zinaelekezwa na Serikali ili kuweza kukabiliana na maambukizi ya Corona.

“Tunaahidi kushirikiana pamoja katika kukabiliana na janga hili na kuhamasisha uwepo wa mazingira endelevu,” alisema.

 

Alisema FORUMCC itaendelea kuhamasisha mapambano ya Mabadiliko ya Tabianchi kupia njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii.

 

Kongamano hilo lilitarajiwa kushirikisha wadau mbalimbali wa kudhibiti Mabadiliko ya Tabianchi ambao ni pamoja na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mussa Zungu, mabalozi, watafiti na wadau wengine.

No comments:

Post a Comment

Pages