Naibu Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, akiongea na wakimbizi walioko katika
Kambi ya Nduta mkoani Kigoma, ambapo amewahamiza kuendelea kujiandikisha katika
orodha ya wanaotaka kurejea nchini Burundi. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Na Mwandishi
Wetu, Kigoma
Serikali ya Tanzania na
Burundi zimewahakikishia kurejea kwa amani na utulivu katika nchi zao wakimbizi na waomba hifadhi walioko katika
makambi mbalimbali nchini huku serikali ya Tanzania ikiweka wazi haijalazimisha
zoezi la urejeaji makwao kwa wakimbizi hao.
Hayo yamesemwa na Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni wakati wa ziara yake
katika kambi ya Nduta iliyoko wilayani Kibondo mkoani Kigoma ikiwa na ukubwa wa
kilometa za mraba 36 na ikihifadhi wakimbizi 62,127,waomba hifadhi 11,841 huku
wenye hadhi nyingine wakifikia 1,168.
“Novemba 29, mwaka jana
pande tatu ikiwemo Serikali ya Tanzania,Serikali ya Burundi na Shirika la Umoja
wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) walishawekeana saini mkataba wa
urejeshwaji wa wakimbizi wanaotaka kurejea kwao kwa hiari yao wenyewe,pande
hizo zilikaa vikao kadhaa ikiwemo kutembelea nchi husika na walijiridhisha
kurejea kwa amani na utulivu kabla ya kusaini mkataba huo,nawasihi sasa
mjitahidi kujiandikisha ili muweze kwenda kuijenga nchi yenu,Burundi
inawahitaji zaidi” alisema Masauni
“Amani imerejea katika
maeneo yenu na sasa hivi ni kipindi cha uchaguzi jiandikisheni ili muweze
kurejea kwenye nchi yenu muende mkatumie haki yenu ya kidemokrasia ya kuchagua
viongozi.
Awali akisoma taarifa
ya urejeaji wa hiari wa wakimbizi na waomba hifadhi,Mratibu wa Wakimbizi Kanda
ya Kigoma,Athman Igwe alisema suluhisho la kudumu la wakimbizi ni kuwarejesha
katika nchi ya asili kwa hiari,kuwahamishia nchi ya tatu na kupewa uraia katika
nchi ya kimbilio huku akiweka wazi idadi ya waliorejea na walioomba kurejea.
“Mheshimiwa Naibu
Waziri idadi ya wakimbizi na waomba hifadhi waliorejea tangu kuanza kwa zoezi
hilo mwaka 2017 ni familia 27,459 zenye watu 80,072 huku kwa mwaka huu jumla ya
familia 715 zenye wakimbizi 1,247 wakirejea kwao na sasa tuna maombi ya familia
31,723 zenye jumla ya wakimbizi 93,503 walioomba kurejea lakini tuna familia
3,163 zenye wakimbizi 10,883 wamebadilisha nia ya kurejea nchini kwao” alisema
Mratibu Igwe
“Lakini katika mpango
wa kuwahamishia wakimbizi nchi ya tatu kupitia Shirika IOM,Mei 2007 hadi
kufikia Februari mwaka huu jumla ya wakimbizi 36,127 walihamishiwa nchi ya tatu
na hivi karibuni tayari wakimbizi 200 walienda nchi za Marekani na Australia.
Akizungumzia suala la
wahamiaji haramu katika kambi za wakimbizi Mratibu wa Kanda ya Kigoma,Athman Igwe,
alisema jumla ya wahamiaji haramu 1,094 walichukuliwa hatua huku hali ya ulinzi
na usalama ikiimarika na kuripotiwa kutokuwepo kwa tukio lolote ambalo
lingeashiria usalama wa makambi yote katika mkoa wa Kigoma ambao kwa ujumla
wake unahifadhi jumla ya wakimbizi 266,482.
Ni takribani miezi
kadhaa sasa imepita tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. John
Magufuli kwenye ziara yake katika mkoa wa Katavi kuagiza pande zote zinahusika
na wakimbizi wakutane ili kuweza kujadili suala la warundi wanaojiandikisha kwa
hiari kurudi nchini kwao,akiwaambia umefika wakati sasa wakurudi katika nchi
zao kwenda kuzijenga huku akiwaonya wakimbizi wanaoshiriki katika matukio ya
uhalifu hapa nchini.
No comments:
Post a Comment