HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 11, 2020

WAHITIMU WA MUZIKI WA DINI YA KIKRISTO WAISHUKURU SERIKALI, TaSUBa

 Mgeni rasmi katika mahafali hayo ya nne Katibu Mkuu wa Jimbo Kuu la Kusini mwa Tanzania,  Mchungaji  Dk. Rabson Ntambala, akitoa hotuba yake katika mahafali hayo.
 Mgeni rasmi katika mahafali hayo ya nne Katibu Mkuu wa Jimbo Kuu la Kusini mwa Tanzania,  Mchungaji  Dk. Rabson Ntambala akikabidhi vyeti kwa baadhi ya wahitimu  katika mahafali hayo.
 Mgeni rasmi katika mahafali hayo ya nne Katibu Mkuu wa Jimbo Kuu la Kusini mwa Tanzania,  Mchungaji  Dk. Rabson Ntambala akikabidhi vyeti kwa baadhi ya wahitimu.

 
NA ANDREW CHALE, BAGAMOYO

WAHITIMU  wa kozi ya muziki kwa waumini wa dini ya Kikristo wameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa kufanikisha kutoa mafunzo ya muzki kupitia Taasisi yake ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa).

Mbali na kutoa shukrani hizo pia wametoa mapendekezo kwa kanisa na  Serikali kuwatangaza ndani na nje ya nchi baada ya kuhitimu mafunzo yao.

Akizungumza katika mahafali ya nne kwa kozi maalum ya muziki kwa madhehebu mbalimbali katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) yaliyofanyika hivi karibuni, mhitimu wa mwaka wa tatu wa kozi ya muziki, Frank Fuwe alisema sambamba na ombi hilo, chuo kinatakiwa kuwapokea wakati wowote hata kama wamemaliza mafunzo yao.

Fuwe alisema Kanisa linatakiwa kuongeza nguvu kwa kutangaza kazi zao katika vyombo mbalimbali vya habari ili kufikisha ujumbe kwa jamii.

Alisema pia Kanisa linatakiwa kuwa na mkakati wa kuwashawishi wakristo wengine kuimba nyimbo za Kristo kwa kufuata misingi ya  muziki kutoka chuo hicho cha Serikali TaSUBa.

Mhitimu huyo alitoa shukrani kwa uongozi wa TaSUBa kwa msaada mkubwa wa kuwapatia mafunzo sambamba na Kanisa kwa kufanikisha kupata elimu chuoni hapo tena bila upendeleo wa kuchagua madhehebu.

“Tunawashukuru kwa Kanisa kuandaa program maalum kwa ajili ya mafunzo ambayo yametubadilisha kwa kiasi kikubwa, tutautumia muziki tuliojifunza kwa ajili ya kumtukuza na kumuimbia Mungu ipasavyo,” alisema Fuwe.

Naye Katibu Mkuu wa Jimbo Kuu la Kusini mwa Tanzania,  Mchungaji Dk. Rabson Ntambala alisema wanajivunia hatua hiyo muhimu kwani wakati unavyozidi kwenda mbele ndivyo maendeleo yanaonekana.

Dk. Ntambala alisema watayafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na wahitimu  kupitia tathmini itakayowasaidia kutekeleza hatua hiyo muhimu.

Mwakilishi wa Mkuu wa TaSUBa, Dk Herbert Makoye katika mahafali hayo, Thomas Nyindo alisema amefurahishwa kwa hatua hiyo na kupendekeza kwamba umoja  uliopo uendelezwe kwa lengo la kufikisha ujumbe kwa waumini wa madhehebu mbalimbali.

Nyindo aliwapongeza wahitimu waliomaliza kwani ubora walionao kwenye muziki ni tofauti na walivyoanza na kuongeza kuwa elimu waliyoipata sio jambo dogo.

“Tunawaomba wahitimu wawe mabalozi wazuri wa TaSUBa huko waendako,” alisema Nyindo.

Mratibu wa kozi hiyo ambaye pia ni Mwalimu  wa Sanaa chuoni hapo, Heri Kaare alitoa wito kwa waumini wa madhehebu mbalimbali kujitokeza chuoni hapo ili kupata elimu ya muziki.

Wahitimu 39 walihitimu mafunzo hayo, mwaka wa kwanza walikuwa 20, mwaka wa pili 10 na mwaka wa tatu 9.

TaSUBa imekuwa ikitoa kozi mbalimbali za Sanaa ikiwemo muziki, ngoma, maigizo, ufundi wa Sanaa ikiwemo uandaaji wa filamu, muziki na maigizo pamoja na sarakasi na nyingine nyingi.

No comments:

Post a Comment

Pages