Mdau wa
maendeleo Mkoa wa Iringa, Fadhili Ngajilo (wa pili kulia) akiwa katika
picha ya pamoja na watu wasioona baada ya kuwakabidhi msaada wa Barakao
200 na Sanitezer 40 kwa ajili ya Chama cha Wasioona Manispaa ya Iringa kwa
lengo la kupambana na virusi vya corona. (Picha na Denis
Mlowe).
Na Denis Mlowe, Iringa
JAMII imeshauriwa kuwashika mkono watu wenye ulemavu
wa macho hasa katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya kuenea kwa virusi vya
Corona COVID 19 kwani wamekuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali kutokana
na hali zao.
Hayo yamezungumzwa na mganga mkuu wa Manispaa ya
Iringa, Dk. Jesca Leba wakati wa mafunzo na kupokea msaada wa Barakao 200 na
Sanitezer 40 kwa ajili ya walemavu wa macho uliotolewa na mdau wa maendeleo
mkoa wa Iringa, Fadhili Ngajilo kuweza kuwasaidia kwa ajili ya mapambano dhidi
ya Corona.
Dk. Leba alisema kwamba kutokana na hali walizonazo
walemavu wa macho kuna umuhimu mkubwa wa jamii kuwa nao sambamba kwani wako
katika hali ya hatari zaidi kutokana na hali zao za kutokuona hivyo elimu na
kuwaongoza namna ya kunawa mikono itasaidia katika mapambano hayo.
Alisema kuwa kama manispaa wametoa mafunzo kwa
walemavu na wataendelea kutoa mafunzo kwa makundi mbalimbali ya walemavu kwa
ajili ya kushikwa mkono kwani changamoto kubwa kwenye vyombo vya kunawia mikono
wanashindwa kuelewa mahali ilipo.
“Kwa kweli kuna changamoto kubwa kwa walemavu na ndio
maana tumeamua kufanya mafunzo kwao tena maalum kwa kundi la walemavu wa macho
na tutafanya mafunzo haya kwa makundi yote kwa sababu watu wanaohitaji kushikwa
mikono katika kuwaongoza” alisema
Aidha katika mafunzo hayo, Dk Leba aliwataka walemavu
wa macho kuepuka kushika macho, pua na mdomo kwa mikono isiyo safi kwa sababu
mikono ni rahisi kubeba vimelea vya maradhi na kuzingatia ustaarabu wa kuzuia
pua na mdomo wakati wa kukohoa au kupiga chafya.
Alisema kuwa endapo binaamu atahisi kuwa na mafua
makali, homa, kikohozi na kushindwa kuhema nenda hospitali kupata msaada wa
kitaalamu na kuepuka kuwa sehemu yenye msongamano kama vyombo vya usafiri,
maduka na maeneo yenye mgandamizo wa hewa.
Kwa upande wake , Mdau wa maendeleo ambaye aliwahi
kuwa mwenyekiti wa UVccm mkoa wa Iringa, Fadhili Ngajilo alisema kuwa msaada una
lengo la kuwasaidia walemavu wa macho kwani wamesaulika sana katika mapambano
dhidi ya kuenea kwa virusi vya Corona.
Alisema kuwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu
jamii inatakiwa kuungana kwani hali ya kuleta au kutaka sifa kisiasa sio wakati
wake na kumpongeza Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuri kwa kuwa mstari wa
mbele katika kupambana dhidi ya kuenea kwa virusi vya corona.
Aliwataka wakosoaji dhidi ya mapambano haya watumie
lugha za staha na kuacha tabia ya kushutumiana ila ni wakati wa kuungana kuweza
kumtokomeza adui aliyeko mbele ya jamii kwa sasa ambaye ni virusi vya corona.
Naye mwenyekiti wa chama wa Wasioona manispaa ya
Iringa, Huruma Maketa alisema kuwa wamejifunza vizuri zaidi tofauti na mwanzo kuhusu gonjwa la Corona na kumshukuru mdau wa maendeleo Fadhili Ngajilo kwa kutoa
msaada barakao na sanitizer kwa walemavu wa macho.
Aidha alishukuru
mafunzo waliyopatiwa ya kujikinga na kuwakinga wengine dhidi ya Corona
kwani mafunzo hayo yalikuwa muhimu kwa jamii ya wasioona hivyo elimu hiyo
watatumia vyema kuepukana na kuambukizwa na virusi vya corona.
No comments:
Post a Comment