HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 25, 2020

SHINYANGA YATAKIWA KUKAMILISHA MIRADI MIKUBWA KWA WAKATI

 Katibu Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Eng. Joseph Nyamhanga (kushoto), akimsikiliza Muhandisi wa Halmashauri ya Shinyanga Bw. William Lusiu kuhusu ujenzi wa Hospitali ya Wilaya hiyo jana   alipofanya ziara ya Siku moja Mkoani Shinyanga kujionea miradi ya maendeleo inayoendelea Mkoani Shinyanga, katikati ni Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Bw. Albert Msovera.
 Katibu Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Eng. Joseph Nyamhanga akifafanua jambo kwa waandishi wa habari kuhusu ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Shinyanga jana   alipofanya ziara ya Siku moja Mkoani Shinyanga kujionea miradi ya maendeleo inayoendelea Mkoani Shinyanga.
  Katibu Mkuu TAMISEMI Eng.Joseph Nyamuhanga pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Bi. Yasinta Mboneko alipotembelea mradi wa machinjio ya kisasa yaliyoko nje kidogo ya mji wa Shinyanga.
Katibu Mkuu TAMISEMI Eng. Joseph Nyamhanga akiwa na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Shinyanga alipotembelea mradi wa machinjio ya kisasa yaliyoko nje kidogo ya mji wa Shinyanga.




Na Mwandishi Wetu, Shinyanga
Miradi mikubwa inayoendelea katika Mkoa wa Shinyanga imetakiwa kwa kukamilishwa kwa wakati ndani ya muda uliopangwa ili Serikali ianze kutekeleza miradi ya mwaka mpya wa fedha kama iliyopangwa kufanyika katika bajeti mwaka wa fedha 2020/21.
Agizo hilo kwa Serikali ya Mkoa wa Shinyanga lilitolewa na Katibu Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Eng. Joseph Nyamhanga alipofanya ziara ya Siku moja Mkoani Shinyanga kujionea miradi ya maendeleo inayoendelea Mkoani Shinyanga.
Miradi iliyotembelewa na kiongozi huyo ni miradi mitatu iliyoko Manispaa ya Shinyanga inayojumuisha Km 13.1 za barabara za Manispaa bil.15, Mradi wa Machinjio ya Kisasa ya nyama wenye thamani ya sh. Bil.5 na ujenzi wa dampo la taka lenye thamani ya Sh. Mil.400 miradi ambayo inatakiwa kukamilika ifikapo Juni 30, 2020.
Akiongelea kuhusu ujenzi wa Machinjio ya Kisasa unaoendelea Mkoani Shinyanga Eng. Nyamhanga alishauri uongozi wa Mkoa kuhakikisha unamsimamia mkandarasi wa mradi huo ili aweze kukamilisha ujenzi wa mradi huo  kwa kipindi cha  mwezi mmoja na kuharakisha ufungaji wa majokofu ya kuifadhi nyama na miundombinu nyingine inayohusu machinjio hayo ya kisasa.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Bw.Geofrey Mwangulumbi aliyataja Machinjio hayo ya Kisasa kuwa yana uwezo wa kuhifadhi ngo’mbe 100 kwa siku pamoja na kutoa huduma ya nyama kwa wafanyabiashara mkoani Shinyanga na maeneo mengine nje ya mkoa huo.
Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Bw. Albert Msovera aliongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaongeza udhibiti wa ubora wa nyama itakayokuwa inauzwa Mkoani hapo ikiwemo kuongeza mapato ya Halmashauri pamoja na Serikali.    
Pamoja na kutembelea miradi hiyo ya Manispaa ya Shinyanga Eng. Nyamhanga pia alipata fursa ya kutembelea ujenzi wa Hospitali mpya ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini iliyoko Makao Makuu ya Wilaya hiyo yaliyoko Kata ya Iselamagazi Shinyanga vijijini ambayo ni sehemu ya hospitali nyingine 98 zinazojengwa hapa nchini ambayo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 80.
Katibu Mkuu Nyamhanga alionesha kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa hospitali hiyo yenye thamani ya sh. mil. 500 na kupongeza uongozi wa Mkoa kwa kuweza kutumia kiwango hicho cha fedha kuongeza jengo la kuifadhia maiti pamoja na jengo la mionzi kwani ujenzi wa majengo hayo awali haukuwa sehemu ya makadilio ya fedha za ujenzi wa hospitali hiyo.
Aidha Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Bw. Albert Msovela alimwambia kiongozi huyo kuwa Serikali Mkoani Shinyanga itaendelea na usimamizi wa ujenzi wa wa hospital hiyo na kutaja changamoto upungufu  wa watumishi wa Afya katika Wilaya hiyo na kuongeza kuwa mahitaji ya watumishi katika Wilaya hiyo ni takribani watumishi 500.
Pamoja na changamoto ya watumishi wa Afya Bw. Msovela aliongeza kuwa kukamilika kwa hospitali hiyo kutasaidia kupunguza hadha za wakazi wa Iselamagazi na maeneo jilani kwani awali walilazimika kutembea km 50 kufuata huduma za matibabu Shinyanga mjini.
Miradi hiyo mikubwa inayoendelea Mkoani Shinyanga iko katika hatua za mwisho za utekelezaji wake ikijumuisha miradi mingine iliyoko katika Wilaya nyingine Mkoani Shinyanga amabayo pia  inatarajia kukamilika kabla ya kuanza kwa mwaka mpya wa fedha 2020/21.

No comments:

Post a Comment

Pages