Naibu Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kushoto), akikagua orodha ya mahabusu
wakati wa ziara ya kutembelea Vituo vya Polisi lengo ikiwa ni kukagua
utekelezaji wa maagizo ya serikali katika kupambana na ugonjwa wa Corona ambapo
ameagiza Makamanda wa Polisi nchini na Wakuu wa Magereza kuhakikisha watuhumiwa
wanaoruhusiwa kupata dhamana kisheria wapewe ili kuepusha misongamano katika
vituo mbalimbali vya polisi nchini. (Picha
na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi).
Naibu Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kushoto), akizungumza na wananchi
waliokusanyika nje ya Kituo cha Polisi Kati kilichopo wilaya ya Dodoma Mjini
ambapo ameagiza wananchi hao kuhudumiwa haraka ili kuepusha misongamano ikiwa
ni kutekeleza maagizo ya serikali ya kutokuwepo kwa mikusanyiko ili kupambana
na ugonjwa wa Corona.
Na
Mwandishi Wetu, Dodoma
Serikali imewaagiza
Makamanda wa Polisi na Wakuu wa Magereza mikoa yote nchini kuhakikisha inawapa
dhamana mahabusu wote wanaokidhi vigezo vya dhamana na kuharakisha upelekwaji
haraka wa kesi kwa watuhumiwa waliopo katika magereza mbalimbali nchini ili
kuweza kuepusha na kupambana na ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na
virusi vya corona(Covid 19) usiweze kuingia katika mahabusu za polisi na
magereza.
Hayo yamesemwa na Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni wakati alipofanya
ziara ya kushtukiza katika Vituo mbalimbali vya Polisi mkoani Dodoma ambapo
alibaini kuwepo msongamano wa mahabusu katika vituo vya polisi huku akifanikiwa
kuzungumza na baadhi ya mahabusu ambao ilionekana kesi zao zinadhaminika huku
wengine wakiruhusiwa katika ziara hiyo.
“Maagizo ya Serikali na
wataalamu wa afya ni kuepusha misongamano sasa nimetembelea kituo hiki cha kati
nimekuta mahabusu wengine wamekaa siku kumi na nne,na wengine wanaingia wakiwa
wametoka nje huko hali iliyopelekea msongamano mkubwa katika kituo hiki, na
kuna mahabusu mmoja nimekuta wamemuweka siku tatu hapa kosa lake wamemkamata tu
anapita nje ya bunge hii sio sawa huku hana kosa lolote.
“Sasa natoa maagizo kwa
Makamanda wa Polisi nchi nzima katika kukabiliana na ugonjwa wa corona
wahakikishe mahabusu wote ambao kesi zao zinadhaminika watolewe, agizo hili pia
liende kwa wakuu wa magereza yote nchini kuhakikisha watuhumiwa wote kesi zao
zinaharakishwa kupelekwa mahakamani hii yote ikiwa ni mkakati wa kupambana na
gonjwa la Corona sasa watu wamerundikwa tu hakuna kinachoendelea hii si sawa”
alisema Masauni
Pia alipata fursa ya
kuzungumza na wananchi waliokusanyika nje ya vituo vya polisi wakija kuwaona
ndugu zao huku akisisitiza washughulikiwe haraka kwani wamekusanyana wengi huku
serikali ikiwa imepiga marufuku mkusanyiko wa watu na wataalamu wakishauri
umbali kati ya mtu na mtu uwe mita moja.
“Wananchi wamekuja
kuona ndugu zao waliopo mahabusu tunajua ni haki yao pamoja na kuwaletea chakula
lakini muwahudumie haraka waondoke hii mikusanyiko ishakatazwa ni hatari sana”
alisema Masauni.
No comments:
Post a Comment