Mfanyabiashara Said Nasser Nassor 'Bopar' (kushoto),
akimkabidhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Mashine za
Kupimia Joto kukamilisha ahadi aliyotoa Wiki iliyopita ya mchango wake wa
kusaidia Vifaa kwenye mapambano dhidi ya Virusi vya Corona.
Balozi Seif akiangalia moja ya mashine hiyo ya kupimia joto la mwili inayosaidia kutoa viashiria vya kutambua matatizo ya maradhi
kwenye mwili wa mwanaadamu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,
Balozi Seif Ali Iddi, akitoa shukrani mara baada ya kupokea Mchango wa Mashine
na Mashuka kutoka kwa Mfanyabiashara Said Bopar Ofisini kwake Vuga Mjini
anzibar. (Picha na – OMPR – ZNZ).
VUGA, ZANZIBAR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
ametahadharisha kwamba wakati umefika sasa kwa kila Mwanajamii kujenga
Utamaduni wa kuvaa Kibarkoa katika harakati zake za Kimaisha ili kujiepusha maambukizi
ya Virusi vya Corona.
Alisema Taifa bado liko katika kipindi kigumu kutokana na
wimbi la Maambukizo ya Virusi hivyo ambavyo hivi sasa vinazunguuka ndani ya
Mitaa baada ya Serikali kufanikiwa kuzuia maambukizi kutoka Nje ya Nchi kwa
kufuta muingiliano wa safari za Kimataifa.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa tahadhari hiyo hapo Ofisini
kwake Vuga Mjini Zanzibar mara baada ya kupokea msaada wa Mashuka 20 na Mashine
30 za kupimia joto la mwili zilizotolewa na mfanyabiashara maarufu nchini Said Nasser Nassor 'Bopar' akikamilisha msaada aliyoahidi kutoa katika kuungana
na Serikali Kuu kwenye mapambano dhidi ya kuenea kwa Virusi vya Corona Nchini.
Balozi Seif alisema Ugonjwa wa Mafua na Homa kali ya mapafu inayosababishwa
kupumua kwa shida pamoja na kikohozi kutokana na Virusi hatari vya Corona umo
ndani ya jamii ukisambaa jambo ambalo linahitaji kuchukuliwa kwa tahadhari
kubwa.
Alisema katika vita hivyo vigumu Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar inahamasisha Viwanda Vidogo Vidogo nchini kutengeneza vibarkoa ili
kuwapunguzia gharama kubwa Wananchi hasa wale wa kipato cha chini wanaolazimika
kununua vifaa hivyo kutoka Nje ya Nchi kwa bei ya juu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza na kumshukuru mfanyabiashara Said Nasser Nassor 'Bopar' kwa Uzalendo wake anaojitolea wa
kusaidia Jamii pale inapopata changamoto na mitihani tofauti.
Balozi Seif
alibainisha wazi kwamba msaada huo wa mashuka na Mashine za kupimia joto
la Mwili zinazoashiria kuelewa kuutambua Ugonjwa mapema ni muhimu na kwa upande
mwengine zitasaidia nguvu ya Serikali katika jitihada zake za kupambana na
maradhi yanayowasumbua Wananchi.
Aliwakumbusha Wananchi kutoona shinda kuendelea kutumia Dawa
za asili kama vile nyungu na vyakula vyenye asili ya ukali {Vitamin C} ambavyo kwa
mujibu wa Wataalamu wa Afya ni rahisi kusaidia kupambana na Virusi Thakili vya
Corona.
Mapema akikabidhi mashuka na Mashine hizo za kupimia Joto la
Mwili kukamilisha ahadi yake Mfanyabiashara Said Nasser Nassor 'Bopar '
ameendelea kusisitiza kwamba yuko tayari Siku na muda wowote kusaidia Jamii na
Serikali pale linapotokea suala la dharura inayoikumba Jamii.
Said Bopar alisema yeye kama Mzalendo na Mwananchi wa Taifa
hili hana sababu ya kutoiunga mkono Serikali Kuu pale inapotokea dharura au
kuombwa kufanya hivyo kwa maslahi ya Taifa na Wananchi wake wote.
Wiki iliyopita Mfanyabiashara huyo tayari ameshakabidhi
msaada wa Vitanda, Sabuni, Vitakasa Mikono, Dawa ya Mbu, Magodoro, Mito, Tishu
na Mashuka kwa ajili ya kuhudumia Mapambano dhidi ya kuangamiza Virusi vya
Corona hapa Nchini.
No comments:
Post a Comment