NAIBU WAZIRI, Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa amewataka Watanzania
waendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu (COVID-19) huku wakimtanguliza Mungu.
“Hakuna njia nyingine yoyote
isipokuwa kunyenyekea chini ya mkono wa Mungu. Tuendelee kuchukua tahadhari
wakati bado tunaendelea kumtumainia Mungu. Ni heri kumwishia Mungu, na Roho
Mtakatifu atatupa njia ya kutoka hapa tulipo,” alisema.
Ametoa kauli hiyo
jana jioni (Jumapili,
Aprili 26, 2020) wakati akizungumza na viongozi wa dini mbalimbali walioshiriki
Maombi
Maalum ya Kitaifa kwa mkoa wa Dodoma dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa
na virusi vya corona (COVID-19) yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha VETA,
Dodoma.
Amesema
Serikali ya awamu ya tano inaongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ambaye ana hofu
ya Mungu na ndiyo maana aliomba Watanzania kwa imani zao wafanye maombi kwa
siku tatu.
Alisema
Serikali inatambua mchango wa viongozi wa kiroho na akawataka waliombee Taifa
kwani mwaka huu linajiandaa kwa uchaguzi mkuu. “Mwaka huu tunatarajia kufanya
uchaguzi mkuu, kwa hiyo tunaomba tumtangulize Rais wetu, tumuombee sana kwa yale
anayoyafanya kwa nchi yetu.”
Akizungumza
wakati wa kufungua maombi hayo, Rais wa Chama cha Maaskofu na Wachungaji (Tanzania
Pastors’ Association – TPA), Askofu Samson Mlawi alitoa maombi akimuomba Mungu
aifute COVID-19 kwenye mipaka ya Tanzania.
Naye mwakilishi wa Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Sheikh Kisusu
Mvumbo alisema dunia huwa inaandika historia kila kunapotokea tukio kubwa akitolea
mfano wa vita kuu ya dunia. “Vita ya kwanza ya dunia iliandika historia, ikaja
vita ya pili ya dunia nayo ikapita.
“Sasa hivi, tishio
juu ya mdudu huyu corona pia inaendelea. Dunia haiendi imesimama, imekwama
kiuchumi sababu ya mdudu corona. Tumsihi Mwenyezi Mungu atuepushe na hili
janga,” alisema katika maombi yake.
Kwa upande wake, mwakilishi kutoka madhehebu ya Khoja
Shia mkoa wa Dodoma, Ustaadh Haidary Bakari alisema anamuomba Mungu aiponye
Tanzania na pia akaombea uchaguzi Mkuu ujao uwe wa heri na amani.
Akimalizia
maombi hayo, Mwenyekiti wa Mtandao wa Maombezi wa Wanawake Barani Afrika, Prof,
Margareth Kilimali alisema anamshukuru kwa kuwakutanisha viongozi hao wa dini
wa mkoa wa Dodoma bila kujali tofauti zao za dini.
“Tunamshukuru Mungu
kwa kuwa ana uwezo wa kutokomeza janga hili kwa nchi yetu ya Tanzania na bara zima
la Afrika. Asante ka fursa ya uchaguzi mkuu kwani umeshapanga ni jinsi gani utaendeshwa
kwa amani wakati ukifika,” alisema.
Alisema
Tanzania haitaabika na janga la corona kwa sababu imemtumaini Mungu. “Tanzania
haitaaibika kwa sababu tumekujua wewe ni Mungu na unaweza kutuponya, Afrika
haitaaibika kwa sababu nao wamekukimbilia wewe,” alisema.
Wakati huohuo, Mratibu wa TPA, Askofu Gerald Nzwalla alisema neno kuu
la maombi hayo ya kitaifa ni limetoka nyakati wa pili, sura ya saba mstari wa
14 na wa 15 (2Nya.7: 14-15) na waliona
ni muhimu maombi hayo yafanyike jijini Dodoma kwa sababu ni makao mkuu ya nchi
na ndipo mahali anaishi Rais wa nchi.
Maombi hayo
maalum yaliandaliwa na TPA kwa kushirikiana na BAKWATA, SHIA, HAMADIA, HINDU, AGA
KHAN, KKKT, EAGT, FPCT, MENONITE NA MOROVIAN.
No comments:
Post a Comment