Na Peter Haule na Saidina Msangi, WFM, Dodoma
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.
Ashatu Kijaji, amesema hakuna ubadhirifu unaoendelea katika
Shirika la Bima la Taifa (NIC) baada ya Serikali kuchukua hatua kadhaa ikiwemo
kubadili uongozi wa Shirika hilo pamoja na kuimarisha mifumo yake ya ukusanyaji
mapato.
Hayo yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Dkt. Kijaji, wakati
akijibu swali la msingi la Mbunge wa Ubungo.
Mhe. Saed Kubenea, aliyetaka kujua ukweli kuhusu kuendelea kwa ubadhirifu
katika Shirika la NIC na mpango wa Serikali wa kulisaidia shirika hilo
kukabiliana na ushindani wa kibiashara.
Alisema kuwa hivi sasa Shirika hilo
linatumia Mfumo wa Ukusanyaji Mapato ya Serikali (GePG) hatua iliyoimarisha
mapato yake pamoja na kuanza kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA) kufanya malipo yake yote badala ya kutumia Hundi.
Dkt. Kijaji alisema kuwa Shirika la NIC lilianza kutumia Mfumo
wa Makusanyo ya Mapato ya Serikali kuanzia Novemba, 2019 na kuondoa ukusanyaji
wa mapato kwa fedha taslimu pamoja na kuongeza udhibiti katika ulipaji wa madai
ikiwemo kufanya ukaguzi maalum wa madai yote ya bima za maisha ili kujiridhisha
kuhusu uhalali wake.
Alisema
Matumizi ya Hundi (cheque) yamesitishwa kuanzia Desemba, 2019 katika malipo
yake yote na kuanza kutumia mfumo wa malipo wa kielektroniki, ili kuongeza
udhibiti wa uwezekano wa matumizi ya hundi za kughushi.
Dkt.
Kijaji alisema pamoja na kufanya mabadiliko ya Uongozi wa Shirika hilo,
pia imelipatia Shirika hilo wataalam katika nyanja za mifumo
ya TEHAMA na mifumo ya utunzaji wa kumbukumbu (e-Office) ili kuongeza
ufanisi
wa kiutendaji
Alisema kuwa Serikali imechukua hatua ya kuliimarisha Shirika la
NIC kitaalam kwa kuliondoa shirika hilo kutoka kwenye mashirika yaliyotakiwa
kubinafsishwa na kuliwezesha kushiriki katika biashara ya bima kwa ushindani.
Katika kuongeza udhibiti wa matumizi ya fedha za Shirika,
ufungaji wa Mfumo wa Usimamizi wa Shughuli za Kihasibu na Malipo katika Taasisi
za Umma (MUSE) uko katika hatua za mwisho na kwamba mfumo huo utakapokamilika
utaongeza udhibiti katika malipo yote yanayofanyika.
Alingeza kuwa Serikali inaendelea kupitia upya Mpango Mkakati wa
NIC ili uendane na mahitaji halisi ya biashara ya ushindani, kuongeza uwekezaji
katika mifumo ya TEHAMA ili kuwafikia wateja wengi zaidi, kuongeza ubora wa
huduma na kulipa madai, kutoa gawio kubwa kwa Serikali na kushiriki katika
shughuli za maendeleo ya Taifa.
No comments:
Post a Comment