HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 11, 2020

SAFISHA VITASA KATIKA MAENEO YA BIASHARA NA MAKAZI YETU

Mfanyabiashara wa duka la dawa baridi, eneo la Tabata Jijini Dar es Salaam akisafisha kitasa na kioo cha duka lake ikiwa ni sehemu ya maeneo hatarishi kupata virusi vya Corona kutoka na kushikwa mara kwa mara na wateja.

Na WAMJW- PWANI

Mkuu wa Kitengo cha maji na usafi wa mazingira, Wizara ya Afya, Ndg. Anyitike Mwakitalima ametoa wito kwa Watanzania wote kujenga tabia ya kusafisha vitasa na maeneo yote yanayoshikwa mara kwa mara katika maeneo ya shughuli za kila siku na makazi yetu.

Ndg. Anyitike ameyasema hayo wakati akitoa elimu kwa wakazi wa Kisarawe na Bagamoyo Mkoa wa Pwani, kuhusu kuchukua tahadhari za kujikinga dhidi ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona katika maeneo ya biashara na makazi.

"Tuhakikishe tunasafisha maeneo yote tunayoyashika mara kwa mara kwa maji yenye sabuni, sanitizer au spirit, futa maeneo yote yanayoshikwa mara kwa mara, lakini kumbuka kufuta sehemu za vitasa vya mlango na meza " alisema

Pia, alisisitiza kuwa, ni muhimu kujenga tabia ya kufuta katika maeneo yote ambayo watu wanapendelea kukaa kama vile maeneo ya viti, meza na vioo katika maeneo ya biashara bila kusahau milango.

Aidha, Ndg. Anyitike Mwakitalima ametoa rai kwa wananchi hususan vinyozi katika maeneo ya saluni kuhakikisha wanavaa Barakoa (mask) pindi wanapokuwa katika maeneo yao ya kazi, ili kuvunja mnyororo wa maambukizi Corona kutoka mtu mmoja kwenda kwa mwingine endapo utakuwepo.

"Unapoenda saluni usikubali kinyozi yoyote akunyoe nywele kama hajavaa Barakoa hali itayosaidia kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Corona katika maeneo ya kazi na kuvunja mnyororo wa maambukizi ya virusi hivyo" alisema.

Nae, Sfaff sergeant (S/Sgt ) Valentine Ngowi, ameendelea kuwakumbusha wazazi na walezi, kuhakikisha wanawalinda Watoto dhidi ya ugonjwa wa Corona, kwa kuwapa elimu, na kuhakikisha hawazululi hovyo mtaani, hasa katika kipindi hiki ambacho shule zimefungwa ili kuepusha misongamano inayoweza sababisha kusambaa kwa ugonjwa wa Corona.

"Tuhakikishe Watoto wanakaa nyumbani, Watoto wasiende kuzulula hovyo, ni rahisi Watoto kupata maambukizi ya Corona kwasababu ya ufahamu na uelewa wao juu ya madhara ya ugonjwa huu wa Corona " alisema.

Kwa upande wake, Balozi wa kampeni ya Mikoni safi, Tanzania salama, Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) amewaasa wafanyabiashara wa Barakoa kutoruhusu wateja kujaribu barakoa na kuzirudisha, hali inaweka wanunuzi wengine katika hatari yakupata maambukizi ya virusi vya Corona.

" kwa wauzaji wa Barakoa, chonde chonde usiruhusu mtu ajaribu Barakoa alafu akaiacha, hii itasaidia kuvunja mnyororo wa maambukizi ya virusi vya Corona kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine endapo atatokea mtu mwenye maambukizi" alisema.

Timu ya Wizara ya Afya na Wadau kutoka Shirika lisilo Lakiserikali la Project CLEAR kupitia kampeni ya Mikono Safi, Tanzania Salama imeendelea kutoa elimu ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona katika, Wilaya ya Bagamoyo, Wilaya ya Kisarawe na Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani.

No comments:

Post a Comment

Pages