Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo.
Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda.
Na Mwandishi Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa
Mh. Joachim Wangabo ametoa wito kwa wananchi na wadau wote mkoani humo
kuhakikisha wananchukua hatua za tahadhari ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu
inayosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19) kwa kufuata maelekezo ya
wataalamu wa Afya pamoja na kushauri matumizi ya Nyungu kwaajili ya kujifukiza.
Amehamasisha hayo ikiwa
ni katika kuunga mkono kauli ya Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI) pamoja na viongozi wengine wa juu nchini katika
kupambana na Covid – 19 ambao huenezwa kwa kuingiwa na majimaji yatokayo kwa njia
ya hewa wakati mgonjwa anapokohoa au kupiga chafya au kugusa majimaji yanayotoka
puani mwa mtu aliyeathirika.
“Nitoe wito kwa wadau
wote ikiwa ni pamoja na nyini waheshimiwa madiwani kuchukua hatua za tahadhari
ya ugonjwa huu kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wetu wa afya. Tukumbuke kuwa
virusi vya Corona ni janga la kidunia na linaua, Aidha matumizi ya Nyungu
kwaajili ya kujifukizia yanashauriwa na Mh. Jafo waziri wa OR-TAMISEMI pamoja
na viongozi wengine wa juu tuyazingatie, watu wapige Nyungu,” Alisisitiza.
Kwa upande wake Mkuu
wa Wilaya ya Nkasi ambaye pia anakaimu Wilaya ya Sumbawanga Mh. Said Mtanda akifafanua
michanganyiko ya aina tatu inayoshauriwa na wataalamu wa tiba ya asili
yaliyofanyiwa majaribio na kituo cha Tiba asili kinachotambulika na serikali
amesema moja ya mchanganyiko ni kutumia mti wa mwarobaini, tangawizi
iliyopondwa, majani ya mpera, limao zilizokatwa unachemsha pamoja na kisha kujifunika na
kuvuta moshi kwa pua na mdomo ili moshi huo uingie mwilini na hatimae kwenda
kuua virusi vya Corona.
“Sisi kule Namanyere (Wilayani Nkasi) tumeweka utaratibu wa kuhamasishana kujifukiza, kwasababu ukiona aibu matatizo
kweli utayapata, kwahiyo kiongozi ukiwa unajifukiza unakapiga kapicha kidogo
unawatumia wengine ili waseme hee hata Diwani kajifukiza, kwahiyo wale
unaowaongoza watahamasiska kujifukiza kwasababu wataona kumbe sasa hili sio
suala la aibu,” Alisema.
Viongozi hao wamesema
hayo wakati wa vikao vya madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo na
Wilaya ya Sumbawanga katika vikao vya Mabaraza ya Madiwani ya Halmashauri hizo
kuhusu utekelezaji wa hoja za ukaguzi na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali nchini.
No comments:
Post a Comment