Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akiwa
amenyanyua mkoba wa Bajeti Kuu ya Serikali, ya mwaka 2020/2021 Bungeni jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akiwasilisha bungeni jijini Dodoma Mapendekezo
ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2020/2021
ambapo Serikali imepanga kukusanya na kutumia takribani shilingi trilioni 34.9 kwa matumizi ya maendeleo na matumizi mengine.
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu
lipokee, lijadili na kukubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya
Serikali kwa mwaka 2020/21. Bajeti hii ni ya tano ya Serikali inayoongozwa na
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Bajeti hii inawasilishwa kwa mujibu wa matakwa ya Ibara ya 137 ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ikisomwa pamoja na
Kifungu cha 26 cha Sheria ya Bajeti, Sura 439.
2.
Mheshimiwa Spika, hotuba hii inaambatana na vitabu vinne vya bajeti.
Kitabu cha Kwanza ni Makadirio ya Mapato; Kitabu cha Pili ni Makadirio ya
Matumizi ya Kawaida kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, na Wakala wa Serikali;
Kitabu cha Tatu ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Sekretarieti za Mikoa
na Mamlaka za Serikali za Mitaa; na Kitabu cha Nne ni Makadirio ya Matumizi ya
Maendeleo kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Sekretarieti
za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha
wa mwaka 2020 pamoja na Muswada wa Sheria ya Matumizi ya Serikali wa mwaka 2020
ambavyo ni sehemu ya bajeti hii.
I.
TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2019/20
Mwenendo wa Mapato
3.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya
mwaka 2019/20, Serikali ilitarajia kukusanya jumla ya shilingi trilioni 33.11
kutoka katika vyanzo vyote vya ndani na nje ambapo hadi Aprili 2020 kiasi cha
shilingi trilioni 26.13 kimekusanywa sawa na asilimia 93.2 ya lengo la mwaka.
Mchanganuo wa mapato yaliyopatikana hadi Aprili 2020 ikilinganishwa na lengo la
kipindi hicho ni kama ifuatavyo:
(i)
Mapato yaliyokusanywa kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA), yalikuwa ni shilingi trilioni 14.64, sawa na asilimia 93.5 ya lengo;
(ii)
Mapato yasiyo ya kodi yalifikia shilingi trilioni 2.25,
sawa na asilimia 87.2 ya lengo;
(iii)
Mapato ya Halmashauri yalifikia shilingi bilioni 561.49,
sawa na asilimia 88.1 ya lengo;
(iv)
Misaada na mikopo iliyopokelewa ilikuwa shilingi trilioni
2.41 sawa na asilimia 94.5 ya lengo;
(v)
Mikopo ya ndani ikijumuisha mikopo ya kulipia dhamana za
Serikali zilizoiva ilifikia shilingi trilioni 4.45, sawa na asilimia 103.8 ya
lengo; na
(vi)
Mikopo ya masharti ya kibiashara ya nje ilifikia shilingi
trilioni 1.82 sawa na asilimia 78.7 ya lengo.
4.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai
2019 hadi Aprili 2020, mapato yaliyokusanywa na TRA yamekua kwa asilimia 13.6
ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2018/19. Ukuaji huo umetokana na: kuimarisha
usimamizi wa sheria za kodi na matumizi sahihi ya mashine za kutolea risiti za
kielektroniki ili kudhibiti upotevu wa mapato; utoaji wa elimu na maboresho ya
huduma kwa mlipa kodi; na kuimarika kwa udhibiti wa madini. Aidha, wananchi wamehamasika
kulipa kodi kutokana na kuimarika kwa utoaji wa huduma za kiuchumi na kijamii
ikijumuisha maji, elimu, afya, miundombinu wezeshi ya barabara na umeme; na
kufutwa kwa ada na tozo za kero ili kuboresha mazingira ya kufanya biashara na
kuwekeza hapa nchini.
5.
Mheshimiwa Spika, mwenendo wa upatikanaji wa
fedha kutoka soko la ndani umeimarika kutokana na: Kuongezeka kwa ukwasi kwenye
benki za kibiashara; Serikali kuendelea kuorodhesha Hatifungani za Serikali
katika Soko la Hisa la Dar es Salaam; na kutoa elimu kwa umma ili kuhamasisha
ushiriki wao katika kuwekeza kwenye Hatifungani na Dhamana za Serikali.
6.
Mheshimiwa Spika, mwenendo mzuri wa
misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo umetokana na juhudi
za Serikali katika kutekeleza misingi ya ushirikiano kama ilivyoainishwa katika
Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo (Development Cooperation
Framework – DCF). Mwongozo huo unatoa fursa mbalimbali za majadiliano
yanayowezesha kufikia makubaliano ya utoaji fedha za maendeleo kwa wakati ili
kutekeleza miradi ya maendeleo.
Mwenendo wa Matumizi
7.
Mheshimiwa Spika, makadirio ya
matumizi kwa mwaka wa fedha 2019/20 yalikuwa shilingi trilioni 33.11 ambapo
shilingi trilioni 20.86 ni matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 12.25 ni
matumizi ya maendeleo. Katika kipindi cha Julai, 2019 hadi Aprili 2020, jumla
ya shilingi trilioni 24.85 zimetolewa sawa na asilimia 88.6 ya lengo. Kati ya
kiasi hicho, shilingi trilioni 17.22 zilikuwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida
ambazo zinajumuisha shilingi trilioni 5.83 kwa ajili ya mishahara ya watumishi
wa umma, shilingi trilioni 2.91 kwa ajili ya matumizi mengineyo na shilingi
trilioni 8.48 kwa ajili ya kugharamia deni la Serikali na mahitaji mengine ya
Mfuko Mkuu.
8.
Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 2020,
jumla ya shilingi trilioni 7.63 sawa na asilimia 65.9 ya lengo zimetolewa kwa
ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo shilingi trilioni 6.65 ni
fedha za ndani sawa na asilimia 87.2 na shilingi bilioni 976.9 ni fedha za nje
sawa na asilimia 12.8. Aidha, kiasi cha shilingi trilioni 1.28 zilielekezwa
moja kwa moja na Washirika wa Maendeleo kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali
bila kupitia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.
9.
Mheshimiwa Spika, naomba nieleze
baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa bajeti kwa kipindi cha
Julai 2019 hadi Aprili 2020 kama ifuatavyo:
(i)
Jumla ya shilingi trilioni 2.44 zimetolewa kwa ajili ya
utekelezaji wa miradi ya barabara, reli na viwanja vya ndege;
(ii)
Serikali ilifanikiwa kugharamia mikopo ya wanafunzi wa
elimu ya juu, uimarishaji wa vyuo vya VETA na kukuza ujuzi kwa vijana ambapo
shilingi bilioni 467.89 zimetolewa;
(iii)
Serikali imegharamia utekelezaji wa miradi ya maji mijini na
vijijini ambapo jumla ya shilingi bilioni 346.01 zimetolewa;
(iv)
Serikali imelipa jumla ya shilingi bilioni 315.20 kwa ajili
ya kukamilisha malipo ya awali ya ununuzi wa ndege mpya 3 (shilingi bilioni
85.6), uimarishaji wa Shirika la Ndege la Tanzania (shilingi bilioni 14.67) na
malipo ya mwisho ya ndege mbili aina ya Boeing 787-8 Dreamliner na Havilland
Dash 8-400 (shilingi bilioni 214.93);
(v)
Serikali imeendelea kutekeleza mradi wa kufua umeme unaotokana
na nguvu za maji katika Mto Rufiji ambapo shilingi bilioni 356.72 zimetolewa;
(vi)
Serikali imeendelea kutekeleza Awamu ya Tatu ya Mradi wa
Kupeleka Umeme Vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambapo jumla
ya shilingi bilioni 280.95 zimetolewa;
(vii)
Serikali imeendelea kugharamia elimumsingi bila ada ambapo
zimetolewa shilingi bilioni 211.28;
(viii)
Serikali imeendeleza ujenzi na ukarabati wa meli katika
maziwa makuu ambapo zimetolewa shilingi bilioni 53.49;
(ix)
Serikali imegharamia ujenzi na ukarabati wa hospitali za
mikoa, vituo vya kutolea huduma za afya katika ngazi ya Halmashauri ambapo
jumla ya shilingi bilioni 35.73 zimetolewa. Aidha, Serikali imetoa shilingi
bilioni 9.10 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maboma ya nyumba 364 za walimu
wa shule za msingi hasa kwenye maeneo yenye mazingira magumu; na
(x)
Serikali imegharamia shughuli za Mfuko wa Kuchochea
Maendeleo ya Jimbo (Constituency Development Catalyst Fund - CDCF)
ambapo shilingi bilioni 11.0 zimetolewa.
Ulipaji wa
Malimbikizo ya Madai
10.
Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 2020,
Serikali imehakiki na kulipa madai ya wazabuni, wakandarasi na watumishi yenye
jumla ya shilingi bilioni 734.99, sawa na asilimia 122.5 ya bajeti iliyotengwa.
Kati ya kiasi hicho, wakandarasi wamelipwa shilingi bilioni 327.62, wazabuni
shilingi bilioni 148.95, watumishi shilingi bilioni 103.69 na shilingi bilioni
154.73 kwa ajili ya watoa huduma na madeni mengineyo. Ulipaji huu wa madai
umesaidia kuongeza ukwasi na hivyo kuongeza mzunguko wa fedha kwenye uchumi.
Tathmini ya Uhimilivu wa Deni la Taifa
11.
Mheshimiwa Spika, Serikali
imeendelea kusimamia deni la Taifa kwa mujibu wa Sheria ya Mikopo, Dhamana na
Misaada Sura ya 134 kwa lengo la kuhakikisha linakuwa himilivu muda wote. Tathmini ya uhimilivu wa
deni la Taifa iliyofanyika Desemba, 2019 ilibainisha kuwa deni ni himilivu kwa
muda mfupi, wa kati na mrefu. Katika tathmini hiyo, viashiria vinavyopima uwezo
wa nchi kukopa vinaonesha kuwa: Katika mwaka 2019/20, uwiano wa thamani ya sasa
ya deni lote kwa Pato la Taifa ni asilimia 27.1 ikilinganishwa na ukomo wa
asilimia 70; uwiano wa thamani ya sasa ya deni la nje kwa Pato la Taifa ni
asilimia 16.3 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 55; na uwiano wa thamani ya
sasa ya deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 103.9 ikilinganishwa na ukomo
wa asilimia 240.
12.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa viashiria
vinavyopima uwezo wa nchi kulipa deni, matokeo yalibainisha kuwa, uwiano wa
ulipaji wa deni la nje kwa mapato ya ndani ni asilimia 11.9 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 23 na uwiano wa ulipaji wa deni la nje kwa mapato yatokanayo
na mauzo ya nje ni asilimia 11.9 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 21.
Mwenendo wa Sekta ya Fedha
13.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka unaoishia Aprili
2020, viwango vya riba za mikopo ya benki kwa ujumla vilipungua hadi asilimia
16.91 kutoka wastani wa asilimia 17.25 katika kipindi kama hicho mwaka 2019.
Aidha, riba za mikopo za kipindi cha mwaka mmoja zimepungua na kufikia wastani
wa asilimia 16.37 kutoka asilimia 16.94.
Pamoja na mafanikio hayo, bado viwango vya riba za mikopo vimeendelea
kuwa juu kinyume na matarajio ya Serikali. Hivyo, Serikali imedhamiria kuweka
msukumo zaidi katika usimamizi ili kuongeza kasi ya kushuka kwa viwango vya
riba.
14.
Mheshimiwa Spika, ukwasi
umeendelea kuwa juu ya kiwango cha kisheria cha asilimia 20 ya amana zinazoweza
kubadilishwa kwa muda mfupi kuwa fedha taslimu (Demand liabilities) na
kufikia asilimia 32.7 mwezi Aprili 2020. Aidha, ubora wa
rasilimali za sekta ya benki umebaki kama ulivyokuwa mwaka 2019. Uwiano wa
mikopo chechefu na mikopo yote umepungua kwa kiasi kidogo kutoka asilimia 11.10
ya mikopo yote mwezi Aprili 2019 hadi asilimia 11.04 Aprili 2020. Vile
vile, mikopo kwa sekta binafsi imekua kwa asilimia 5.8 Aprili 2020 na kufikia
shilingi trilioni 19.7 kutoka shilingi trilioni 18.6 Aprili 2019. Ukuaji huo
unaenda sambamba na utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kuongeza ukwasi
kwenye uchumi, na utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kuboresha mazingira ya
biashara nchini.
II. MAFANIKIO
YA SERIKALI YA AWAMU YA TANO
15.
Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha miaka minne na miezi saba ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano,
yapo mafanikio mengi yaliyopatikana kupitia utekelezaji wa Ilani ya CCM Kwa
Ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 pamoja na ahadi alizotoa Mheshimiwa Dkt.
John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mafanikio
makubwa ya kujivunia yamepatikana katika nyanja mbalimbali hususan uchumi,
miundombinu, huduma za kijamii, madini na udhibiti wa rasilimali za Taifa,
ardhi na mazingira na utawala bora.
Uchumi
16.
Mheshimiwa Spika, kama
nilivyoeleza katika hotuba yangu kuhusu hali ya uchumi leo asubuhi, Serikali ya
Awamu ya Tano ilipoingia madarakani mwaka 2015, ukuaji wa Pato la Taifa ulikuwa
asilimia 6.2. Katika kipindi cha utawala wa Rais Magufuli, ukuaji wa Pato la
Taifa uliongezeka na kufikia wastani wa asilimia 6.9. Ukuaji huu umetokana na utekelezaji
wa miradi mikubwa ya miundombinu ya kiuchumi (ujenzi, uchukuzi na nishati) na ugharamiaji
wa huduma za jamii (afya, elimu na maji). Mwenendo mzuri wa ukuaji wa Pato la
Taifa umeiwezesha nchi yetu kuwa miongoni mwa nchi kumi (10) za bara la Afrika
zenye uchumi mkubwa zaidi (10 largest economies in Africa) na hii ni kwa
mujibu wa taarifa ya IMF (2019). Aidha, ukuaji wa uchumi wa Taifa umewezesha
kuongezeka kwa mapato ya Serikali na uwezo wa Serikali kugharamia miradi ya
maendeleo, kuboresha huduma za kijamii na kuongeza fursa za kiuchumi kwa
wananchi.
17.
Mheshimiwa Spika, mfumuko wa
bei uliendelea kuwa tulivu na kubakia katika wigo wa tarakimu moja ya wastani
wa asilimia 4.4 kwa kipindi chote cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano
ambapo mwaka 2019, mfumuko wa bei ulifikia asilimia 3.4. Kiwango hiki ni cha
chini kabisa kuwahi kutokea kwa kipindi cha nusu karne tangu mwaka 1970
tulipokuwa na mfumuko wa bei wa asilimia 2.4. Kudhibitiwa kwa mfumuko wa bei
kumetokana na usimamizi madhubuti wa sera za fedha na bajeti, kuimarika kwa bei
za mafuta pamoja na upatikanaji wa chakula katika masoko ya ndani na nchi
jirani. Aidha, mwenendo huu mzuri wa mfumuko wa bei umesaidia kupunguza kasi ya
kupanda kwa gharama za maisha kwa wananchi na ni kiashiria kizuri cha kuvutia
uwekezaji nchini.
18.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2019/20 akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kuridhisha na kukidhi
mahitaji ya kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi. Hadi Aprili 2020, akiba ya
fedha za kigeni ilifikia dola za Marekani bilioni 5.3. Kiasi hiki kinatosheleza
mahitaji ya fedha za kigeni za kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi kwa kipindi
cha miezi 6.1 ikilinganishwa na dola za Marekani bilioni 4.4 kilichotosheleza
mahitaji ya fedha za kigeni za kuagiza bidhaa na huduma kwa kipindi cha miezi
4.3 kwa kipindi kama hicho mwaka 2015. Ongezeko hili lilitokana na kuongezeka
kwa uwekezaji wa kigeni na mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi. Aidha,
kiwango cha akiba ya fedha za kigeni kilichofikiwa ni zaidi ya lengo la kuwa na
akiba ya kutosha kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi kwa muda wa miezi 4.0 na
pia ni juu ya lengo la miezi 4.5 lililowekwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki na lengo la miezi isiyopungua 6.0 kwa nchi za Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika - SADC.
Mapato
19.
Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, mapato ya ndani yameongezeka
kufikia shilingi trilioni 18.5 mwaka 2018/19 kutoka shilingi trilioni 11.0
mwaka 2014/15, sawa na ongezeko la asilimia 69.1. Wastani wa mapato ya kodi kwa
mwezi umeongezeka kutoka shilingi bilioni 825 mwaka 2014/15 hadi wastani wa shilingi
trilioni 1.3 mwaka 2018/19 na kuongezeka zaidi hadi wastani wa shilingi
trilioni 1.5 kwa mwezi katika kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020. Aidha, mapato
ya kodi yameongezeka kutoka shilingi trilioni 9.9 mwaka 2014/15 hadi shilingi trilioni
15.5 mwaka 2018/19, sawa na ongezeko la asilimia 56.5. Vile vile, mapato yasiyo
ya kodi yameongezeka kutoka shilingi bilioni 688.7 mwaka 2014/15 hadi shilingi trilioni
2.4 mwaka 2018/19 na shilingi trilioni 2.25 katika kipindi cha miezi kumi ya
kwanza ya mwaka 2019/20. Kama nilivyoeleza awali, ongezeko la mapato limetokana
na juhudi zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kudhibiti upotevu wa mapato
kwa kuimarisha usimamizi wa Sheria za kodi na matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika
ukusanyaji wa mapato.
Mifumo ya kielektroniki
20.
Mheshimiwa Spika, Sera za
Mapato na Matumizi za Serikali ya Awamu ya tano zinalenga kuimarisha ukusanyaji
wa mapato ya ndani na kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma. Katika
kutekeleza sera hizo, Serikali imejenga na kuimarisha mifumo mbalimbali ikiwemo
mfumo wa Serikali wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato (Government
e-Payment Gateway System-GePGs), Mfumo wa Usimamizi wa Utoaji wa Risiti za
Kielektroniki za Kodi (Electronic Fiscal Device Management System-EFDMS),
Mfumo Jumuishi wa Forodha (Tanzania Customs Intergrated System-TANCIS), Mfumo
wa Ulipaji Serikalini (MUSE), Mfumo wa Usimamizi wa Mali za Serikali (Government
Assets Management Information System-GAMIS), Mfumo wa Serikali wa Malipo ya
Mishahara (Government Salary Payment Platform-GSPP), Mfumo wa Ununuzi
Serikalini (Tanzanian National e-Procurement System-TANePS) na Mfumo wa
Akaunti Jumuifu ya Hazina (Treasury Single Account-TSA).
21.
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla
mifumo hii imeleta manufaa yafuatayo:
(i)
Kudhibiti upotevu wa mapato na
kurahisisha upatikanaji wa taarifa za makusanyo kwa wakati pamoja na
kuwarahisishia wananchi kulipia huduma mbalimbali za Serikali;
(ii)
Kurahisisha uandaaji wa Hesabu za
Serikali;
(iii)
Kuongeza ufanisi katika usimamizi
na udhibiti wa mali za Serikali;
(iv)
Kuimarisha usimamizi na ulipaji
wa mishahara kwa watumishi wanaostahili na kwa wakati;
(v)
Kuongeza uwazi katika taratibu za
ununuzi na kuiwezesha Serikali kupata thamani halisi ya fedha zinazotumika
katika ununuzi wa bidhaa, huduma na kazi za ujenzi; na
(vi)
Kuimarisha ukwasi kwenye Mfuko
Mkuu wa Serikali, hivyo kurahisisha utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya
Serikali.
22.
Mheshimiwa Spika, jambo la kujivunia ni kuwa, mifumo
yote hii imejengwa na inasimamiwa na wataalamu wa ndani wa Serikali na hivyo
kuokoa fedha zilizokuwa zinatumika awali kulipia gharama za ujenzi na
uendeshaji wa mifumo ya kielektroniki.
Ulipaji wa Madai
23.
Mheshimiwa Spika, Serikali
ya Awamu ya Tano imeendelea kulipa madai ya wakandarasi, wazabuni, watoa huduma
na watumishi. Tangu Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli
iingie madarakani hadi Aprili, 2020 Serikali imelipa madai mbalimbali yenye
jumla ya shilingi trilioni 3.2. Vile vile, Serikali imelipa madai ya kimshahara
ya watumishi wa Umma ya jumla ya shilingi bilioni 114.5. Azma ya Serikali ya
Awamu ya Tano ni kuendelea kuhakiki na kulipa madai yote ya watoa huduma,
wazabuni, wakandarasi na watumishi kwa lengo la kuchochea shughuli za kiuchumi
na kudhibiti madai hewa bila kuathiri mitaji na utendaji kazi katika sekta
binafsi.
Huduma za Jamii
24.
Mheshimiwa Spika, katika
kuendeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kufungamanisha ukuaji wa uchumi
na maendeleo ya watu, Serikali imechukua hatua madhubuti katika kuboresha
upatikanaji wa huduma za jamii kwa wananchi zikiwemo afya, elimu na maji katika
maeneo ya mijini na vijijini.
25.
Mheshimiwa Spika, kwa upande
wa uboreshaji wa huduma za afya mafanikio yaliyopatikana katika awamu hii ya
uongozi hadi Aprili 2020 ni pamoja na: kuboresha miundombinu ya afya kwa
kujenga zahanati 1,198, vituo vya afya 487, hospitali za Halmashauri za Wilaya 71,
hospitali za rufaa za Mikoa 10 na hospitali za rufaa za kanda tatu (3); kuongezeka
kwa bajeti ya dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kutoka shilingi bilioni
31 mwaka 2015 hadi bilioni 269 mwaka 2019; na kuimarika kwa upatikanaji wa dawa
muhimu katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini kufikia asilimia 94.4
mwaka 2019/20 kutoka asilimia 36 mwaka 2014/15. Aidha, kuimarika kwa huduma za
afya nchini kumesaidia kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopewa rufaa za matibabu
kwenda nje ya nchi kwa asilimia 95 na kuokoa takribani shilingi bilioni 20
ambazo zingetumika kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi.
26.
Mheshimiwa Spika, Serikali
imeendelea kuchukua hatua katika kuboresha upatikanaji wa huduma za maji safi
na salama mijini na vijijini ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Mfuko wa Maji
ambapo katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, kiwango cha
upatikanaji wa maji vijijini kimeongezeka kufikia asilimia 70.1 na mijini
asilimia 84. Aidha, Serikali imejenga na kukarabati miundombinu ya maji 1,423
ambapo miradi 1,268 ni ya vijijini na 155 ni ya mijini. Utekelezaji wa miradi
ya maji imegharimu jumla ya shilingi trilioni 1.55 kati ya mwaka 2015/16 hadi
Aprili 2020. Kuongozeka kwa kiwango cha upatikanaji maji nchini kumeokoa muda
ambao wananchi hususan wanawake walikuwa wakiutumia kutafuta maji na kwa sasa
wanautumia katika shughuli za uzalishaji mali ikijumuisha kilimo na biashara.
Vile vile, upatikanaji wa maji safi na salama mijini na vijjini umepunguza
kiwango cha maradhi kwa wananchi, hivyo kuokoa gharama za matibabu na
kuimarisha nguvu kazi kuwa yenye afya bora na tija.
27.
Mheshimiwa Spika, mafanikio
yaliyopatikana katika eneo la elimu ni pamoja na: Kugharamia elimumsingi bila
ada ambapo jumla ya shilingi trilioni 1.03 zilitumika kati ya mwaka 2015/16
hadi 2019/20; kugharamia ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kufundishia na
kujifunzia ikiwemo madarasa, maabara, maktaba na mabweni; kuongezeka kwa ufaulu
wa wanafunzi waliomaliza elimu ya msingi na wahitimu wa kidato cha nne kutoka
asilimia 67.8 na asilimia 67.9 mwaka 2015 hadi asilimia 81.5 na asilimia 80.6
mwaka 2019 mtawalia; uimarishaji wa vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi stadi;
na kuimarisha upatikanaji wa elimu ya juu kwa kutoa ruzuku kwa vyuo vya elimu
ya juu na mikopo kwa wanafunzi. Mikopo
kwa wanafunzi wa elimu ya juu iliongezeka kutoka shilingi bilioni 348.7 mwaka
2014/15 hadi shilingi bilioni 450 mwaka 2019/20. Jumla ya shilingi trilioni
2.20 zimetumika kugharamia mikopo katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2020,
hivyo kuwezesha wanafunzi wengi zaidi kutoka familia zenye kipato cha chini kupata
elimu ya juu. Jitihada hizi za Serikali zimesaidia kupunguza mzigo kwa wananchi
kugharamia huduma za elimu, kuongezeka kwa uandikishaji, udahili na ufaulu wa
wanafunzi katika ngazi zote za elimu. Aidha, napenda nichukue fursa hii
kuishukuru Benki ya Dunia kwa kutukopesha dola za kimarekani milioni 500 sawa
na shilingi Trilioni 1.25 kwa ajili kuboresha miundombinu ya Elimu nchi nzima
hasa kwa watoto wa kike. Nawapongeza Waziri wa Elimu, Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Wilson Masilingi na Timu ya
Wataalam wa Wizara ya Fedha na Mipango waliofanya kazi usiku na mchana
kuhakikisha mkopo huo unapatikana.
Miundombinu ya Ujenzi, Uchukuzi
na Nishati
Ujenzi
28.
Mheshimiwa Spika, mafanikio
yaliyopatikana katika eneo la ujenzi ni: Kuendelea na ujenzi wa barabara kwa
kiwango cha lami zikiwemo barabara kuu, barabara za mikoa na za wilaya ambapo
kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi Aprili 2020, ujenzi wa barabara kwa
kiwango cha lami zenye urefu wa km 2,624.27 umekamilika; ujenzi wa daraja la
juu la Mfugale (Dar es Salaam), daraja la Furahisha (Mwanza) na daraja la
Magufuli (mto Kilombero) umekamilika; ujenzi wa barabara kuu kwa kiwango cha
lami zenye urefu wa km 1,298.44 unaendelea; ujenzi wa barabara ya pete (Ubungo
interchange) umefikia asilimia 77; ujenzi wa barabara ya njia nane kutoka
Kimara hadi Kibaha (km 19.2) umefikia asilimia 80; Aidha, ujenzi unaendelea kwa daraja la New Selander
(Dar es Salaam) lenye urefu wa km 1.03 pamoja na barabara unganishi zenye urefu
wa km 5.2 na umefikia asilimia 38.2, daraja la Kigongo hadi Busisi (Mwanza)
lenye urefu wa km 3.2, daraja jipya mto Wami katika barabara ya Chalinze hadi
Segera litakalokuwa na urefu wa m 513.5 pamoja na barabara unganishi zenye
urefu wa km 4.3 umefikia asilimia 39 na daraja la Ruhuhu (Ruvuma) umefikia
asilimia 86. Miradi ya ujenzi wa barabara, madaraja na vivuko imegharimu jumla
ya shilingi trilioni 7.63 kati ya mwaka 2015/16 hadi Aprili 2020. Kati ya kiasi
hicho, ujenzi wa barabara umegharimu shilingi trilioni 6.4 fedha za ndani na
shilingi trilioni 1.02 fedha za nje, ujenzi wa madaraja shilingi bilioni 205.0
na ujenzi wa vivuko shilingi bilioni 20.1. Utekelezaji wa miradi hii umechochea
shughuli mbalimbali za kiuchumi na kuwawezesha wananchi kupata huduma za jamii
kama vile shule na zahanati na kutoa fursa mbalimbali za ajira. Aidha, miradi
iliyokamilika imepunguza muda uliokuwa unatumiwa na wananchi kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
29.
Mheshimiwa Spika, hatua
iliyofikiwa katika uboreshaji wa huduma za Bandari ni pamoja na: kukamilika kwa
uboreshaji wa gati namba moja hadi nne na gati la kupakia na kupakua magari (Ro-Ro)
na uwekaji wa Mfumo Jumuishi wa Ulinzi wa Bandari (Intergrated Port
Security) na ufungaji wa mashine za kukagua mizigo katika Bandari ya Dar es
Salaam ambao umegharimu jumla ya dola za Marekani milioni 113.9 sawa na
shilingi bilioni 284.75; ujenzi wa gati lenye urefu wa mita 300 katika bandari
ya Mtwara; ukarabati wa maghala na gati namba moja na mbili katika Bandari ya
Tanga; kukamilika kwa uongezaji wa kina cha bandari ya Tanga; na ujenzi na
ukarabati wa magati ya Lushamba, Ntama, Nyamirembe, Magarine na gati la majahazi
Mwigobero katika mwambao wa Ziwa Viktoria; magati ya Kagunga, Sibwesa, Kabwe,
Lagosa na Kibirizi katika mwambao wa Ziwa Tanganyika na gati la Ndumbi kule Ziwa
Nyasa. Ukarabati huu umewezesha meli kubwa kuingia na kutoka katika bandari
zetu kwa ajili ya kushusha na kupakia mizigo. Aidha, umeongeza ukusanyaji wa
mapato kwa kupunguza ukwepaji wa kodi.
30.
Mheshimiwa Spika, mafanikio
mengine yaliyopatikana ni: Kuendelea na ujenzi wa meli mpya yenye uwezo wa
kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo katika Ziwa Victoria na ujenzi wa
chelezo; ukarabati wa meli ya MV Victoria na MV Butiama ambapo katika kipindi
cha mwaka 2015/16 hadi Aprili, 2020 jumla ya shilingi bilioni 111.7 zimetumika.
Vile vile, Serikali imekamilisha ujenzi wa meli moja mpya yenye uwezo wa kubeba
abiria 200 na tani 200 za mizigo katika Ziwa Nyasa; ujenzi wa vivuko vya MV
Kigamboni, MV Utete, kivuko cha Kigongo – Busisi, kivuko cha MV Sengerema, kivuko
cha Nyamisati kwenda Mafia; na ukarabati wa meli ya mafuta ya MT Sangara katika
Ziwa Tanganyika.
Uchukuzi
31.
Mheshimiwa Spika, katika
kuimarisha miundombinu ya uchukuzi, mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na:
Kuanza ujenzi wa mradi wa kihistoria wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Kimataifa (Standard
Gauge Railway) kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro (km 300) na kipande
cha Morogoro hadi Makutupora (km 422) ambapo jumla ya shilingi bilioni 170 na
dola za Marekani bilioni 1.5 sawa na shilingi Trilioni 3.75 zimetumika hadi
sasa. Utekelezaji wa mradi huu umewezesha kupatikana kwa ajira 13,177 kwa
wananchi na ushiriki wa wakandarasi wa ndani 640. Mafanikio mengine
yaliyopatikana katika eneo la reli ni: kurejesha huduma ya kusafirisha shehena
za mizigo kwa njia ya reli kutoka bandari ya Dar es Salaam kwenda Uganda; Kukamilisha
ukarabati wa reli ya Dar es Salaam hadi Moshi (km 558.8) na kuanza kutumika;
kukamilisha ukarabati wa reli ya Tanga hadi Korogwe (km 84); ukarabati wa reli
ya Moshi hadi Arusha (Km 86) umekamilika na imeanza kufanya kazi; na ukarabati
wa reli ya Dar es Salaam hadi Kilosa (Km 283) na Kilosa hadi Isaka (Km 687)
unaendelea.
32.
Mheshimiwa Spika, kwa upande
wa usafiri wa anga, mafanikio yaliyopatikana ni: Kuimarisha Shirika la Ndege
Tanzania (ATCL) kwa kununua ndege mpya 11 ambapo hadi Aprili,
2020 ndege nane (8) mpya zenye thamani ya shilingi trilioni 1.27
zimepokelewa na kuanza kutoa huduma katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya
nchi; kukamilisha malipo ya awali ya shilingi
bilioni 85.7 kwa ajili ya ununuzi wa ndege nyingine mpya tatu (3); na kukamilika
na kuanza kutumika kwa Jengo la Tatu la Abiria katika Kiwanja cha Ndege cha
Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) ambalo liligharimu takribani shilingi
bilioni 722.1. Jengo hilo lina uwezo wa kuhudumia abiria milioni sita kwa mwaka.
Aidha, ufungaji wa rada tatu za kuongozea ndege za kiraia katika viwanja vya
ndege vya JNIA, KIA, na Mwanza umekamilika; ukarabati wa viwanja vya ndege vya
Kilimanjaro na Dodoma umekamilika na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege
vya baadhi ya mikoa upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji ambavyo vyote
kwa pamoja vimegharimu kiasi cha shilingi bilioni 445.9.
Nishati
33.
Mheshimiwa Spika, kwa upande
wa utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya nishati, baadhi ya mafanikio ni: Kuanza
ujenzi wa mradi wa kihistoria wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (MW
2,115) katika mto Rufiji ambao hadi sasa umegharimu kiasi cha shilingi trilioni
1.42; kuendelea na utekelezaji wa miradi ya kufua umeme ya Kinyerezi I - Extension
(MW 185) na Kinyerezi II (MW 240) ambayo kwa pamoja imegharimu shilingi
trilioni 1.22; kuendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa ya usafirishaji umeme
ya North - West Grid Extension kV 400 (Mbeya – Sumbawanga- Mpanda – Kigoma
– Nyakanazi), kV 220 (Makambako – Songea), kV 400 (Singida - Arusha – Namanga),
kV 400 (Rufiji – Chalinze – Kinyerezi na Chalinze – Dodoma), kV 220 (Rusumo –
Nyakanazi), kV 220 (Geita – Nyakanazi) na kV 220 (Bulyanhulu – Geita).
34.
Mheshimiwa Spika, katika
kuimarisha upatikanaji wa huduma ya umeme vijijini, Serikali imeendelea
kutekeleza miradi ya umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
ambapo hadi Aprili 2020 jumla ya vijiji
9,112 kati ya 12,268 vya Tanzania Bara vimeunganishwa na umeme kutoka vijiji
2,118 mwaka 2015. Gharama zilizotumika katika utekelezaji wa mradi huu
kuanzia mwaka 2015/16 hadi Aprili 2020
ni shilingi trilioni 2.27. Utekelezaji wa miradi hii umenufaisha wananchi
vijijini na pia taasisi 11,128 zikiwemo za elimu, afya, maji na dini, pamoja na
huduma za biashara.
35.
Mheshimiwa Spika, napenda
nisisitize kuwa miradi ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu wezeshi katika
sekta za ujenzi, uchukuzi na nishati niliyoeleza italiwezesha Taifa letu kuwa
na uchumi imara wenye kuhimili ushindani. Aidha, miradi hii imekuwa chanzo cha
ajira kwa Watanzania na kuwasaidia kujiongezea kipato. Vile vile, miradi hii
itaongeza ufanisi wa upatikanaji wa huduma na kuchochea ukuaji wa miji na sekta
nyingine kama vile kilimo, viwanda, utalii na biashara na kupanua wigo wa
mapato ya Serikali.
Madini
36.
Mheshimiwa Spika, mafanikio
yaliyopatikana katika sekta ya madini ni pamoja na: Kuongezeka kwa maduhuli
yatokanayo na madini kutoka shilingi bilioni 196.0 kwa mwaka 2015/16 hadi
shilingi bilioni 470.0 kwa kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili, 2020; marekebisho
ya sheria na mikataba ya uwekezaji na hivyo kuanzishwa kwa Kampuni mpya ya Twiga
Minerals Corporation Limited inayomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali (hisa
asilimia 16) na Kampuni ya Barrick (hisa asilimia 84); na kupelekea malipo ya
fidia ya dola za kimarekani milioni 100 sawa na shilingi bilioni 250 kutoka
Kampuni ya Barrick ikiwa ni sehemu ya kwanza
ya kiasi cha makubaliano ya awali ya kulipa fidia ya dola milioni 300
sawa na shilingi bilioni 750. Naomba nichukue fursa hii kuipongeza timu ya
Wataalam wa Serikali ikiongozwa Mhe. Prof. Paramagamba Kabudi (Mb.) Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Prof. Florens Luoga Gavana
wa Benki Kuu ya Tanzania kwa kazi nzuri sana ya Kizalendo waliyolifanyia Taifa
hili kufikia mafanikio niliyoyataja. Aidha, marekebisho ya sheria yamewezesha
kuanza majadiliano baina ya Serikali na makampuni yote makubwa ya madini kwa
lengo la kupata asilimia 16 ya hisa kwa Serikali. Vile vile, Serikali imefanikiwa
kuanzisha masoko 28 na vituo 25 vya ununuzi wa madini nchini; imekamilisha
ujenzi wa vituo vinne (4) vya umahiri kule Bukoba, Handeni, Bariadi, na Musoma;
kukamilika kwa ujenzi wa viwanda 2 vya mfano vya kuchenjua dhahabu vya Lwamgasa
na Katente; na kukamilika kwa ujenzi wa one stop center Mirerani,
kuimarika kwa udhibiti wa madini na kupungua kwa utoroshaji madini hasa
kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa ukuta wenye mzingo wa kilomita 24.5 kuzunguka
mgodi wa madini ya Tanzanite, Mirerani.
Mazingira
ya Biashara na Uwekezaji
37.
Mheshimiwa Spika, Serikali
imeendelea kutekeleza Mpango Kazi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji
nchini (The Government Roadmap for Improvement of Business and Investment
Climate) na Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara (Blue
Print for regulatory Reform to Improve Business Environment) kwa lengo la
kuhakikisha vikwazo na kero mbalimbali za biashara na uwekezaji zinaondolewa
ili kuvutia uwekezaji zaidi nchini. Utekelezaji wa programu hizo umewezesha: Kufutwa
kwa tozo 114 katika Sekta za Kilimo,
mifugo na uvuvi kwa mwaka 2017/2018, kufutwa kwa tozo tano (5) zilizokuwa
zinatozwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi, na tozo 54 katika sekta
mbalimbali mwaka 2018/19 ambazo kwa ujumla ni tozo 173; kuanzishwa kwa vituo
vya utoaji huduma kwa pamoja mpakani (One Stop Border Posts-OSBPs)
katika mipaka ya Tanzania na nchi jirani ambavyo vimeimarisha biashara baina ya
Tanzania na nchi hizo; kuanzishwa kwa One stop Service Centres ambazo
zimewezesha utoaji wa huduma kwa wateja kwa uharaka zaidi; na kuhuishwa kwa
majukumu ya Shirika la Viwango (TBS) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (zamani ikiitwa
Mamlaka ya Chakula na Dawa) ambazo zilikuwa na majukumu yanayoingiliana.
Utekelezaji wa hatua hizo umewezesha mazingira ya biashara nchini kuimarika. Na
hii imedhihirishwa na Taarifa ya Benki ya Dunia ya Wepesi wa Kufanya Biashara (Ease
of Doing Business Report) ya mwaka 2020 inayoonesha Tanzania imepanda kwa
nafasi 3 kufikia nafasi ya 141 kutoka nafasi ya 144 mwaka 2019.
Viwanda
38.
Mheshimiwa Spika, sekta ya
viwanda imeendelea kukua kwa kipindi chote cha awamu ya kwanza ya utawala wa Serikali
ya Awamu ya Tano ambapo hadi Aprili 2020 jumla ya viwanda vipya 8,477 vimeanzishwa
katika maeneo mbalimbali nchini na hivyo kuwezesha ongezeko la ajira 482,601
viwandani. Ongezeko hilo la viwanda ambalo pia lilienda sambamba na ongezeko la
uwezo wa uzalishaji, limeongeza utoshelevu wa bidhaa nchini. Mathalani, uwezo
wa uzalishaji wa saruji umeongezeka kutoka tani milioni 4.7 mwaka 2015 hadi
tani milioni 9.1 mwaka 2019. Aidha, uzalishaji halisi wa saruji umeongezeka
kufikia tani milioni 6.5 mwaka 2019 ikilinganishwa na tani milioni 3.3 mwaka
2015. Mahitaji halisi ya saruji nchini yalikuwa tani milioni 4.8 mwaka 2019 na
hivyo kuiwezesha nchi kukidhi mahitaji ya ndani na kuuza ziada nje ya nchi. Viwanda
16 vya nondo kati ya 25 vilivyoko nchini vina uwezo wa kuzalisha nondo tani
milioni 1.083 kwa mwaka ikilinganishwa na mahitaji ya tani 295,000 kwa mwaka.
Vile vile, ongezeko la viwanda limewezesha upatikanaji wa masoko ya mazao ya
kilimo, mifugo na uvuvi ambayo yanatumika kama malighafi viwandani na
upatikanaji wa bidhaa muhimu kwa mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.
Kilimo, Mifugo na Uvuvi
39.
Mheshimiwa Spika, mafanikio
yaliyopatikana katika Sekta ya Kilimo ni pamoja na: Kuongezeka kwa eneo la
umwagiliaji kutoka hekta 461,326 mwaka
2015 hadi hekta 694,715 mwaka 2020; kuongezeka kwa uwezo wa kuhifadhi mazao ya
chakula kwa Taasisi za Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA na Bodi ya Nafaka
na Mazao Mchanganyiko Tanzania (CPB) umeongezeka kutoka tani 371,000 mwaka 2015
hadi tani 621,000 mwaka 2020; kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao makuu ya biashara kutoka tani 796,502
mwaka 2015/2016 hadi tani
1,144,631 mwaka 2018/2019; kuongezeka kwa thamani ya mauzo ya mazao ya bustani
yakiwemo mbogamboga na maua nje ya nchi kutoka Dola za Marekani milioni 412 sawa na
shilingi Trilioni 1.03 mwaka 2015 hadi Dola za Marekani milioni 779 sawa na
shilingi Trilioni 1.9 mwaka 2018/2019; na
kuanzishwa kwa Bima ya Mazao yenye lengo la kumsadia mkulima kujikinga na
athari za majanga ya asili na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kupata dhamana
ya mikopo.
40.
Mheshimiwa Spika, mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya mifugo ni pamoja na: Kuongezeka kwa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho kufikia hekta
milioni 2.82 Aprili 2020 kutoka hekta milioni 1.4 mwaka 2015. Ongezeko hili
limewezesha kupungua kwa migogoro ya ardhi baina ya wafugaji na wakulima
nchini. Aidha, sekta ya mifugo ilifanikiwa kupata mikopo yenye thamani
ya shilingi bilioni 22 kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB)
ikilinganishwa na mwaka 2015 ambapo hakukuwa na mkopo kutoka TADB. Vile vile,
ujenzi wa viwanda vya nyama vya Tan Choice Limited, Elia Foods Overseas Ltd,
Binjiang Company Ltd na kiwanda cha kusindika maziwa cha Galaxy chenye
uwezo wa kusindika lita 75,000 kwa siku umekamilika.
41.
Mheshimiwa Spika, mafanikio
yaliyopatikana katika sekta ya uvuvi ni pamoja na: Kuongezeka kwa mauzo ya
samaki nje ya nchi kufikia wastani wa shilingi bilioni 692 kwa mwaka kutoka
wastani wa shilingi bilioni 379; kuimarika kwa usimamizi na udhibiti wa
rasilimali za uvuvi nchini; kuongezeka kwa samaki waliovuliwa kutoka tani
387,543 na kufikia tani 448,467; kuongezeka kwa wingi wa samaki aina ya Sangara
kutoka tani 417,936 mwaka 2015 hadi
kufikia tani 816,964 mwaka 2020; kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO); na
kudhibiti uvuvi haramu kwa asilimia zaidi ya 80 katika maji baridi na asilimia
100 kwa uvuvi wa kutumia mabomu kwa ukanda wa pwani ya bahari. Aidha, Serikali
imeendelea kuhamasisha uwekezaji katika tasnia ya ufugaji samaki na kufanikiwa
kuongeza idadi ya wafugaji samaki kutoka 18,843 hadi 26,474 mwaka 2020.
Ardhi
42.
Mheshimiwa Spika, mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya
ardhi ni pamoja na: Kupungua kwa migogoro ya ardhi; kuongezeka kwa kasi ya
upimaji wa mashamba na viwanja; kujenga kituo cha Taifa cha Taarifa za Ardhi na
kusimika mfumo unganishi wa kielektroniki wa kuhifadhi kumbukumbu za ardhi
ambapo jumla ya kumbukumbu za majalada yenye taarifa 728,370 za usajili wa
hati, upimaji na umilikishaji wa ardhi yamebadilishwa kutoka mfumo wa analojia
na kuwa wa kidijitali zilizowezesha kuanza kutolewa kwa hati za kielektroniki;
na kuimarishwa kwa huduma za ardhi kwa wananchi kwa kuanzisha Ofisi za Ardhi za
Mikoa yote na kuimarisha ofisi za ardhi za halmashauri 185. Hatua hizi
zimeimarisha usalama wa milki na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya
Serikali ambapo mapato yanayotokana na ardhi yaliongezeka kutoka shilingi
bilioni 54.55 mwaka 2014/15 hadi kufikia wastani wa shilingi bilioni 100 mwaka
2019/20.
Utalii,
Maliasili na Mazingira
43.
Mheshimiwa
Spika,
baadhi ya mafanikio katika maeneo hayo ni pamoja na kuanzishwa na kupandishwa
hadhi maeneo ya hifadhi ya wanyamapori, misitu na nyuki ili kuimarisha uhifadhi
na kuendeleza utalii kutoka hifadhi 15 mwaka 2015 hadi 22 mwaka 2020. Aidha, Serikali
imeendelea kutoa elimu na miongozo mbalimbali kwa umma juu ya umuhimu wa
hifadhi ya mazingira nchini kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.
Utawala
bora, Ulinzi na Usalama
44.
Mheshimiwa Spika, juhudi zilizochukuliwa na Serikali katika
kukabiliana na vitendo vya rushwa na biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini
ikiwa ni pamoja na kuendelea kuimarisha TAKUKURU, kuanzishwa kwa mahakama ya makosa
ya rushwa na uhujumu uchumi katika Mahakama Kuu na kuanzisha Mamlaka ya
Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya, zimeleta mafanikio makubwa kwa kuokoa
fedha za umma, kuzuia uingizaji wa heroin
na kemikali bashirifu (zinazotumika kutengeneza dawa za kulevya), kuanzisha
vituo vya kuhudumia walioathirika na dawa za kulevya, kuongeza nidhamu,
uadilifu na uwajibikaji katika nyanja mbalimbali zikiwemo za utumishi wa umma,
biashara, na kuongeza tija katika ukusanyaji mapato na matumizi ya fedha za
umma. Taarifa ya utafiti wa taasisi ya kimataifa ya Transparency
International ya mwaka 2019 imeonesha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 96
kati ya nchi 180 duniani ikilinganishwa na nafasi ya 119 ya mwaka 2015. Aidha, chini
ya Serikali ya Awamu ya Tano, umoja, amani na usalama nchini vimeendelea
kutamalaki na hivyo kutoa fursa kwa wananchi kuendelea kufanya kazi zao kwa
utulivu. Aidha, Serikali imeendelea kuboresha makazi ya askari na maafisa wa
vyombo vya ulinzi na usalama. Vile vile, chini ya Serikali ya Awamu ya Tano, muungano
umeendelea kudumishwa na kuimarishwa na vyombo vya utoaji haki ikiwemo mahakama
vimeendelea kuboreshwa ikiwemo kuongezeka kwa idadi ya Waheshimiwa Majaji na watumishi
wa sekta ya mahakama pamoja miundombinu ya mahakama.
Kwa upande wa udhibiti wa uhalifu na utoaji wa haki, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa
kushirikiana na wadau, imeendesha kesi na kufanikiwa kupata amri ya Mahakama
kutaifisha jumla ya kilo 398.45 za dhahabu zenye thamani ya Sh. bilioni 32.3
zilizokuwa zinatoroshwa. Madini mengine
yaliyotaifishwa ni madini ya bati na madini ya vito yenye thamani ya shs.
Bilioni 42.27 ambazo zilijumuisha pia faini zilizolipwa na washtakiwa. Aidha, Sh. bilioni 17.22 zilitaifishwa kutoka
kwa wahalifu mbalimbali na kuwekwa kwenye akaunti ya Asset
Forfeiture Recovery iliyoko Benki Kuu ya Tanzania. Vile vile, jumla ya shilingi bilioni 13.52
zimelipwa kutoka kwa washitakiwa waliokiri makosa yao (plea bargain) ya
ukwepaji kodi. Hivyo, hadi mei, 2020
jumla ya shilingi bilioni 73.0 zililipwa kutokana na makosa mbalimbali. Pamoja na fedha hizo, Serikali imepata amri
ya kutaifisha nyumba 24, magari 65, viwanja 9, mashamba 2, mbao 6,894, Jahazi
1, XRF mashine mbili (2) za kupima ubora wa madini. Kadhalika, katika kusimamia utawala wa
sheria, washtakiwa (mahabusu) 2,812 wamefutiwa kesi na Mkurugenzi wa Mashtaka
(DPP) katika zoezi la ukaguzi wa magereza na kusikiliza changamoto za wafungwa
na mahabusu.
45.
Mheshimiwa Spika, Serikali
inatambua majukumu muhimu ya Bunge na hivyo ilihakikisha kwamba inaliwezesha ili
liweze kutekeleza majukumu yake. Serikali imekuwa ikitoa kwa Bunge lako Tukufu
taarifa zote muhimu zilizohitajika na kwa wakati na vile vile kuhakikisha kuwa
fedha kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya Bunge zinatolewa kwa wakati.
Hali
ya Umaskini
46.
Mheshimiwa Spika, hali ya
umaskini wa kipato na usio wa kipato iliendelea kupungua ambapo kiwango cha
umaskini wa mahitaji ya msingi (basic needs poverty) kimepungua kutoka
asilima 28.2 mwaka 2011/12 hadi asilimia 26.4 mwaka 2017/18. Kiwango cha umaskini
kimepungua katika maeneo yote ya mijini na vijijini ambapo katika maeneo ya mijini,
umaskini ulipungua kutoka asilimia 21.7 hadi asilimia 15.8 na maeneo ya
vijijini ulipungua kutoka asilimia 33.3 hadi asilimia 31.3. Aidha, kina cha
umaskini (poverty depth) kilipungua kutoka asilimia 6.7 mwaka 2011/12
hadi asilimia 6.2 mwaka 2017/18 na ukali wa umaskini (poverty severity)
ulipungua kutoka asilimia 2.3 hadi asilimia 2.1. Wastani wa matumizi ya kaya
kwa mwezi yameongezeka kutoka shilingi 258,751 hadi shilingi 416,927.
47.
Mheshimiwa Spika, kupungua kwa umaskini kumetokana na juhudi
kubwa zilizofanywa na Wananchi na Serikali yao kupambana na umaskini wa kipato
na usio wa kipato. Juhudi za Serikali zinahusisha: uwekezaji katika miundombinu
wezeshi kwa shughuli za uzalishaji mali na
biashara ili kukuza uchumi na hatimaye kuongeza pato la wastani kwa kila
Mtanzania; kusimamia na kuboresha sekta ya fedha; kuongeza upatikanaji wa
huduma za msingi kama vile afya, elimu, maji na
umeme hususan maeneo ya vijijini; na kuendelea kutekeleza Mpango wa
Kunusuru Kaya Maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya jamii (TASAF) ili
kuongeza kipato chao na kuwawezesha kupata mahitaji ya msingi. Hatua iliyofikiwa
katika utekelezaji wa TASAF III ni pamoja na: kutambuliwa na kuandikishwa kwa
kaya takribani 1,084,018 zenye wanakaya 5,217,985 katika vijiji na mitaa 9,785
kwenye Halmashauri 159 Tanzania Bara na kaya 34,490 zenye wanakaya 196,301
katika shehia 204 za Zanzibar. Aidha, ruzuku ya fedha shilingi bilioni 968.73
imehawilishwa katika kaya hizo. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 935.94 ni
kwa Tanzania Bara na shilingi bilioni 32.79 ni kwa Zanzibar. Kazi nyingine
zilizofanyika ni pamoja na kutekeleza miradi 8,384 ambayo imezalisha ajira za
muda kwa kaya 230,738 Tanzania Bara na kaya 14,555 katika miradi 251 kwa
Zanzibar. Aidha, miradi 47 ya kuendeleza miundombinu katika sekta za elimu,
afya na maji Tanzania Bara na miradi 8 katika sekta za elimu na afya kwa
Zanzibar imekamilika.
48.
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Serikali, natoa pongezi kwa Watanzania
wote (wafanyabiashara, wenye viwanda, wafanyakazi na wakulima) waliotikia wito
wa Rais wetu wa kulipa kodi stahiki, jambo ambalo limepelekea kupatikana kwa
mafanikio haya ya kishindo.
49.
Mheshimiwa Spika, ugonjwa wa homa kali ya mapafu
inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) ulianzia nchini China
mwishoni mwa mwaka 2019 na kusambaa kwa kasi katika nchi mbalimbali duniani. COVID-19
sio janga la kiafya pekee kwa maana ya kusababisha vifo vya watu wengi na
kuongeza mara dufu mahitaji ya sekta ya afya, bali ni janga la kiuchumi pia
kwani limeambatana na kuvurugika kwa mfumo wa uzalishaji na uhitaji (disruption
in supply and demand chain) duniani. Mataifa mengi yalikumbana na
changamoto zifuatazo: kasi kubwa ya maambukizi kwa raia; vifo vya watu wengi;
sekta ya afya kukabiliwa na jukumu la ziada la kuhudumia waathirika; na
upungufu wa vifaa, dawa na watoa huduma za afya. Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF)
limetabiri kuwa ukuaji wa uchumi wa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara (SSA)
utaanguka kutoka makadirio ya awali ya asilimia 3.6 mwaka 2020 hadi asilimia hasi
1.6. Aidha, uchambuzi huo wa IMF unabashiri kuwa takribani asilimia 60 ya nchi
za SSA zitakuwa na ukuaji hasi katika mwaka 2020 kutokana na athari za
mlipuko wa COVID-19. Vile vile, nchi ambazo Uchumi wao unategemea zaidi
utalii na zile zinazozalisha mafuta ndizo zinatabiriwa kuwa zitaathirika zaidi.
50.
Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na janga hili, nchi mbalimbali duniani zimechukua
hatua kadhaa zikiwemo kulazimisha wananchi wao kubaki majumbani (lockdown);
kuzuia safari za ndege kuingia na kutoka; kuzuia mikusanyiko kama michezo na
hata ibada; kufunga mipaka ya nchi; na kuweka udhibiti katika usafiri wa ndani.
Hatua za kiuchumi zilizochukuliwa na Mataifa hayo ni pamoja na kupunguza kodi
na gharama za ukopaji ili kusaidia biashara; kuahirisha malipo ya kodi hususan
kodi ya mapato na kodi ya ongezeko la thamani; kutoa msaada wa kifedha kwa kaya
maskini; na kusaidia kampuni na mashirika yaliyoathirika zaidi kupata mikopo,
ruzuku na unafuu wa urejeshaji wa mikopo. Kwa upande wa sekta binafsi, baadhi
ya makampuni yalifunga shughuli za uzalishaji/biashara na kupunguza wafanyakazi
au mishahara.
51.
Mheshimiwa Spika, mataifa 20 tajiri duniani (G20) yalipendekeza kwa
wakopeshaji (bilateral official creditors) kutoa unafuu wa madeni kwa
mataifa maskini duniani ikiwemo Tanzania. Mpango huo unahusisha kuahirisha
malipo ya madeni yanayoiva kwa kipindi kinachoanzia Mei hadi Desemba 2020 ili
ahueni hiyo itumike kukabiliana na COVID-19 na kunusuru uchumi. Serikali
imeshaanza mazungumzo na wakopeshaji ili kunufaika na hatua hiyo. Aidha, Serikali iko katika mazungumzo na taasisi mbalimbali
za fedha za kimataifa ili kupata fedha za kukabiliana na COVID-19 na
kutegemeza uchumi. Katika mazungumzo hayo, IMF imeridhia kuifutia Tanzania
mikopo kupitia Mapango wa Wakfu wa Misaada na Uzuiaji wa Maafa (Catastrophe
Containment and Relief Trust - CCRT) kiasi cha dola za Marekani milioni
14.3 sawa na shilingi bilioni 32.6. Bodi ya IMF imefanya uamuzi huo jana tarehe
10 Juni, 2020. Kiasi hicho kinaweza kuongezeka hadi kufikia dola za Marekani
milioni 25.7 sawa na shilingi bilioni 58.6. Kwa niaba ya Serikali, napenda kutoa shukrani kwa IMF kwa
hatua hii muhimu kwetu katika kukabiliana na athari za COVID-19, mahitaji
mengine ya dharura na kuimarisha urari wa malipo (Balance of payments support).
Taasisi nyingine ambazo Serikali inaendelea na mazungumzo nazo ni pamoja
na: Benki ya Dunia kupitia Dirisha la Pandemic
Emergency Financing Facility (PEF) kiasi cha dola za kimarekani milioni
3.98 sawa na shilingi bilioni 9.2; Mfuko wa Ushirikiano na Maendeleo ya Uchumi (Economic
Development Cooperation Fund – ECDF) kupitia Exim Bank ya Korea dola za Marekani 501,169 sawa na shilingi
bilioni 1.2; BADEA
dola za Marekani milioni 1.7 sawa na shilingi
bilioni 3.91; msaada wa
kibajeti kutoka Umoja wa Nchi za Ulaya kupitia dirisha la EU COVID-19 Response
Package Euro milioni 27 sawa na
shilingi bilioni 70.2; na IMF ili
kupata mkopo chini ya mpango wa Rapid Credit Facility
(RCF) ambapo Serikali inaweza kukopa hadi Special Drawing
Rights (SDR) milioni 198.9 sawa na takribani dola za Marekani milioni 272
kwa ajili ya kuimarisha urari wa malipo. Vile vile, Benki ya Maendeleo ya
Afrika imeahidi kutoa mkopo wa kibajeti wenye masharti nafuu (concessional
loan) wa dola za Marekani milioni 50 sawa na
shilingi bilioni 125 ambapo Serikali
itapanga matumizi ya fedha hizo kwa mujibu wa vipaumbele vyake.
52.
Mheshimiwa Spika, tathmini ya kiuchumi iliyofanyika
kwa kipindi cha Januari hadi Aprili 2020 inaonesha kuwa tofauti na nchi nyingi
ambazo uchumi wao umeporomoka, kwa upande wa Tanzania athari za COVID-19
kwenye uchumi ni ndogo. Mwenendo huo umetokana kwa kiasi kikubwa na maono na
ujasiri wa Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ambaye alielekeza wananchi wake kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili
kujenga uchumi na kujipatia kipato lakini wakati huo huo wakiendelea kuzingatia
maelekezo ya wataalam wa afya kujikinga na COVID-19, kushinda hofu ya
ugonjwa huu na pia kumuomba mwenyezi Mungu. Kwa muhtasari, tathmini inaonesha
kuwa kuna maeneo ambayo athari za COVID-19 ni kidogo au hazijajitokeza waziwazi
katika kipindi cha marejeo. Maeneo ambayo hayakuathirika ni pamoja na:
(a)
Mapato ya ndani kwa
ujumla yaliongezeka kwa asilimia 8.2 kwa kipindi cha Januari hadi Aprili 2020
kufikia shilingi trilioni 6.8 ikilinganishwa na makusanyo ya shilingi trilioni 6.3
kwa kipindi kama hicho mwaka 2019;
(b)
Uzalishaji wa
mazao ya chakula umeendelea kuwa mzuri ambapo utoshelevu wa chakula nchini kwa
mwaka 2019/20 umefikia asilimia 118;
(c)
Thamani ya mauzo
ya dhahabu nje ya nchi iliongezeka mara mbili kufikia dola za Marekani milioni
631.0 sawa na
shilingi Trilioni 1.5 Aprili 2020 kutoka dola milioni 323.4 sawa na shilingi bilioni 743.8 Aprili
2019, kutokana na kuongezeka kwa mauzo na kupanda kwa bei kwenye soko la dunia;
(d)
Sekta ya benki
imeendelea kuwa imara kwa viashiria muhimu vya mtaji, ubora wa mali, ukwasi na
faida kwa kipindi kilichoishia Aprili, 2020. Kwa ujumla ukwasi wa benki
umeendelea kuwa juu ya kiwango cha kisheria cha asilimia 20 ya amana zinazoweza
kubadilishwa kwa muda mfupi kuwa fedha taslimu na kufikia asilimia 32.7 mwezi
Aprili 2020.
(e)
Mikopo chechefu
imepungua japo kwa kasi ndogo kutoka asilimia 11.10 Aprili, 2019 hadi asilimia
11.04 Aprili, 2020.
(f)
Akiba ya fedha za
kigeni ilifikia dola za Marekani bilioni 5.3 Aprili 2020, ambayo ilikuwa
inatosha kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha miezi 6.1,
ikilinganishwa na kiasi cha dola za Marekani bilioni 4.4
kilichokuwa kinatosha kuagiza bidhaa na huduma kwa miezi 4.3 mwaka 2019;
(g)
Mauzo katika Soko
la Hisa la Dar es Salaam yameanza kuongezeka baada ya kuyumba katika kipindi
cha mwezi Machi 2020 kutokana na kupungua kwa ushiriki wa wawekezaji wa kigeni
kutokana na janga la COVID-19; na
(h)
Hali ya
upatikanaji wa mafuta nchini kwa sasa ni nzuri. Nchi ina kiasi cha mafuta cha
kutosha, yaani wastani wa siku 40 kwa aina zote za mafuta.
53.
Mheshimiwa Spika, mbali na athari za kiafya zinazojumuisha vifo, ugonjwa, ongezeko
la mahitaji ya madaktari na watumishi wa afya, vituo vya kuhudumia wagonjwa na
gharama za vifaa, vifaa tiba, dawa na vitendanishi, yapo maeneo
mengine ambayo yamebainika kuwa yameathirika japo siyo athari zote zimetokana
na COVID-19 pekee. Baadhi ya maeneo hayo ni yafuatayo:
(a)
Uchumi jumla: Tathmini
ya awali ya Serikali inaonesha kuwa ukuaji wa uchumi wa Taifa utapungua kutoka
makadirio ya awali ya asilimia 6.9 mwaka 2020 hadi asilimia 5.5 kutokana na
sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na athari za COVID-19 na mvua nyingi
zilizopelekea mafuriko na uharibifu wa miundombinu ya usafirishaji na kuchelewa
kwa utekelezaji wa baadhi ya miradi;
(b)
Usafiri wa
anga na utalii: Jumla ya mashirika ya Kimataifa 21 ya ndege yalifuta
safari 632 zilizopangwa kufanyika kuja hapa nchini kuanzia tarehe 20 Machi 2020.
Hatua hii imesababisha kudorora kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi hususan
biashara ya utalii na huduma husika kama usafirishaji wa watalii, malazi,
chakula, vinywaji na burudani. Aidha, baadhi ya hoteli zilifungwa au kupunguza
watumishi. Vile vile, nchi yetu ilifunga anga yake na kuzuia ndege
kutua/kuruka. Mathalani, taasisi za sekta ya utalii ambazo ni Shirika la
Hifadhi za Taifa Tanzania, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Mamlaka ya
Hifadhi ya Wanyamapori Tanzania zimeathiriwa sana na ukosefu wa mapato kufuatia
kuporomoka kwa utalii baada ya kusambaa kwa COVID-19 katika nchi zinazoleta
watalii wengi nchini;
(c)
Uchukuzi na
usafirishaji: Usafirishaji wa mizigo kwenda na kutoka nchi jirani (transit
goods) ulipungua kufuatia baadhi ya nchi hizo kufunga mipaka na kudhibiti
biashara mipakani;
(d)
Bei za
bidhaa za mazao (pamba, korosho, kahawa na chai) katika soko la dunia
imepungua kutokana na kupungua kwa mahitaji;
(e)
Michezo,
sanaa na burudani: Serikali ilisitisha shughuli za michezo, sanaa na burudani
kama sehemu ya hatua za kudhibiti misongamano ya watu kuepuka CORONA kusambaa
kwa kasi;
(f)
Biashara: Biashara
za jumla na rejareja zilipungua hususan zile zilizohusu bidhaa zinazoagizwa kutoka
nchi kama China, India na baadhi ya nchi za Ulaya;
(g)
Mapato ya
Serikali: Mapato ya kodi na maduhuli kutoka katika sekta zilizoathirika
zaidi na COVID-19 yalipungua hususan mapato ya sekta ya utalii, tozo/ada za
Visa, kodi zinazolipwa na hoteli, ada za viingilio kwenye viwanja vya michezo
na maeneo ya sanaa na burudani; na
(h)
Mikopo kwa
sekta binafsi: Kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi imepungua
kutoka asilimia 10.6 kwa mwaka ulioishia Aprili 2019 hadi asilimia 5.8 mwaka
ulioishia Aprili 2020.
54.
Mheshimiwa Spika, hatua zilizochukuliwa awali na
Serikali kukabiliana na COVID-19 ilikuwa ni pamoja na: kusitisha masomo
katika ngazi zote za elimu ili kudhibiti kasi ya maambukizi. Hata hivyo, walimu
katika shule za Serikali na vyuo waliendelea kulipwa mishahara kama kawaida;
kudhibiti safari zisizo za lazima; kusambaza vifaa na vifaa tiba katika maeneo
mbalimbali nchini vikiwemo vipima joto, magari ya kubeba wagonjwa na mavazi
maalum ya kujikinga yanayotumiwa na madaktari na wahudumu wa afya; Kutoa elimu kwa
jamii juu ya dalili na namna ya kujikinga na COVID-19; kujenga na
kuimarisha maeneo maalum ya kutenga na kutibu wagonjwa; na kuahirisha baadhi ya matumizi yaliyopangwa
katika bajeti ya 2019/20 hususan gharama za safari na mafunzo ya nje ya nchi na
maadhimisho ya sherehe za kitaifa na kuelekeza fedha hizo kwenye mapambano
dhidi ya COVID-19.
55.
Mheshimiwa Spika, Serikali
ilitoa jumla ya shilingi bilioni 19.5 hadi mwezi Mei 2020 kwa ajili ya
kukabiliana na COVID-19. Kati ya
hizo, shilingi milioni 500 zilizokuwa zitumike katika sherehe za Muungano
zilielekezwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na shilingi bilioni 14.3 ni fedha
zilizotokana na Global Fund ambazo awali zilikuwa zimetengwa kwa ajili
ya mradi wa Malaria, Kifua Kikuu na UKIMWI. Aidha, Wadau mbalimbali wameendelea
kushiriki mapambano dhidi ya COVID-19 kwa kutoa michango ya fedha na
vifaa. Hadi mwezi Mei 2020, wadau mbalimbali walichangia kupitia Mfuko wa Maafa
jumla ya shilingi bilioni 3.4 na pia Serikali ilipokea vifaa na vifaa tiba kwa
ajili ya kujilinda na kujikinga na maambukizi ya COVID-19 vyenye thamani
ya shilingi bilioni 3.3. Serikali inawashukuru kwa dhati wadau wote wa ndani na
nje waliochangia fedha na vifaa hivyo kusaidia katika mapambano dhidi ya COVID-19.
56.
Mheshimiwa Spika, katika mapambano hayo, kipaumbele cha kwanza cha
Serikali kilikuwa ni kukinga watoa huduma za afya pamoja na wananchi kwa ujumla
wasiathirike na janga la COVID-19. Hivyo, mikakati ya
Serikali ya kukabiliana na athari za ugonjwa huu kwa upande wa sekta ya afya ni
pamoja na: kugharamia upatikanaji wa mahitaji ya msingi kwa watoa huduma za
afya; kuongeza idadi ya madaktari na watoa huduma wa afya; kuhamasisha matumizi
ya tiba asili badala ya kutegemea tiba za kisasa pekee pamoja na kuimarisha
taasisi za uchunguzi na utafiti wa tiba/dawa asili. Aidha, Serikali imefungua
maabara mpya yenye mashine tano (5) zenye uwezo wa kupima sampuli 1,800 kwa
siku na kutoa ajira za watumishi wa sekta ya afya elfu moja (1,000).
Mikakati ya Kutegemeza Uchumi
57.
Mheshimiwa
Spika, kufuatia tathmini iliyofanyika ya athari zinazotokana na COVID-19
na kufuatilia mwenendo wa maambukizi nchini, Serikali imechukua hatua zifuatazo
kwa lengo la kutegemeza uchumi na kusaidia sekta zilizopata athari zaidi:
(a)
Kutoa unafuu wa kodi kama nitakavyoeleza hivi
punde katika sehemu ya maboresho ya kodi ya hotuba hii. Lengo ni kuwezesha
upatikanaji vifaa, vifaa tiba, dawa na vitendanishi kwa gharama nafuu na
kuhamasisha uzalishaji wa vifaa hivyo na bidhaa nyingine hapa nchini;
(b)
Kuingia makubaliano maalum na baadhi ya mashirika
ya ndege ili kukodi ndege kwa ajili ya kusafirisha maua, mbogamboga na minofu
ya samaki nje ya nchi moja kwa moja kutoka Tanzania (Uwanja wa ndege wa Mwanza
na KIA);
(c)
Kugharamia mahitaji ya Taasisi za sekta ya
utalii za Shirika la Hifadhi ya Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro (NCAA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ambazo
ziliathiriwa na COVID-19 pamoja na uharibifu wa miundombinu ya uhifadhi
na utalii kutokana na mvua. Taasisi hizo zitapatiwa fedha za uendeshaji kupitia
bajeti ya Serikali kwa ajili ya kulipa mishahara ya watumishi, matumizi
mengineyo na matumizi ya maendeleo;
(d)
Kufungua rasmi anga ya Tanzania na kuruhusu
ndege zote za kibiashara, misaada, diplomasia na za dharura kuweza kutua na
kuruka kama ilivyokuwa hapo awali;
(e)
Kufungua na kutangaza sekta ya utalii na kutoa
mwongozo wa utalii ambapo tayari watalii wameanza kuingia nchini kwa ndege
binafsi na kwa kupitia baadhi ya kampuni za ndege;
(f)
Kuongeza kasi ya kulipa madeni na malimbikizo ya
madai ya makandarasi, watumishi, wazabuni na watoa huduma ambapo kiasi cha
shilingi trilioni 1.145 kililipwa katika kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili
2020. Kati ya kiasi hiki, shilingi bilioni 916.4 zililipwa mwezi Machi 2020.
Vile vile, malipo ya marejesho ya kodi ya ongezeko la thamani yaliyolipwa hadi
Aprili 2020 yalifikia shilingi bilioni 173.7 sawa na asilimia 148 ya lengo la
kulipa shilingi bilioni 117.4 kwa kipindi hicho. Lengo la hatua hizi ni
kuongeza mzunguko wa fedha katika uchumi ili kuwawezesha wakandarasi,
wafanyabiashara na watoa huduma kuendelea kufanya biashara au kutoa huduma
katika kipindi cha janga la COVID-19;
(g)
Kushusha kiwango cha riba kinachotozwa kwa benki
kukopa Benki Kuu (discount rate) kutoka asilimia 7 hadi asilimia 5.
Hatua hii inalenga kuongeza wigo wa benki kukopa kutoka Benki Kuu kwa riba
nafuu kwa kutarajia benki nazo zitapunguza riba ya mikopo kwa wateja;
(h)
Kushusha kiwango cha chini cha kisheria cha
sehemu ya amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu ya Tanzania (Statutory
Minimum Reserve Requirement) kutoka asilimia 7 hadi asilimia 6. Hatua hii
inatarajiwa kuongeza ukwasi katika sekta ya benki na hivyo kuwezesha benki
kutoa mikopo kwa sekta binafsi;
(i)
Kuyataka makampuni yanayotoa huduma za fedha kwa
njia ya mtandao kupunguza gharama za kufanya miamala kwa wateja ili kuongeza
kiwango cha miamala kwa siku kwa mteja kutoka shilingi milioni 3.0 hadi
shilingi milioni 5.0 na kiwango cha akiba kwa siku kwa mteja kutoka shilingi
milioni 5.0 hadi shilingi milioni 10.0. Hatua hii inalenga kuhamasisha matumizi
ya huduma za kifedha za kidigitali katika kufanya miamala mbalimbali na hivyo
kupunguza ulazima wa wateja kwenda benki;
(j)
Serikali imeagiza benki na taasisi za fedha
kutathmini kwa kina athari zinazotokana na mlipuko wa COVID-19 kwenye
urejeshaji wa mikopo, kujadiliana (re-negotiation) na kukubaliana na
wakopaji namna ya kurejesha mikopo na kutoa unafuu wa urejeshaji wa mikopo (loan
rescheduling). Serikali kupitia
Benki Kuu itatoa unafuu kwa benki na taasisi za fedha zitakazotoa unafuu katika
urejeshwaji wa mikopo hiyo kwa kuzingatia uwazi na bila upendeleo. Katika hili,
napenda kuzipongeza baadhi ya benki kama Exim ambazo tayari zimetangaza
kuongeza muda wa urejeshaji wa mikopo ili kusaidia wateja wao katika sekta ambazo
biashara zao zimeathiriwa na COVID-19 na naziomba benki nyingine zifuate mfano
huo;
(k)
Taasisi za umma na binafsi zimesisitizwa kutumia
mifumo ya kielektroniki katika kufanya shughuli mbalimbali kama vile mikutano
kwa njia ya mtandao; ukusanyaji wa takwimu; mafunzo; miamala ya fedha; na
mifumo ya huduma za afya;
(l)
Serikali itaimarisha zaidi Mfuko wa Maendeleo ya
Jamii (TASAF) na kuongeza wigo wa upatikanaji wa mikopo ya gharama nafuu
kwa wajasiriamali wadogo na wa kati (SME financing) pamoja na kuhakikisha
halmashauri zinatenga fedha asilimia 10 ya mapato kwa ajili ya wanawake, vijana
na watu wenye ulemavu kama Sheria inavyotaka;
(m)
Kufuatia kupungua kwa maambukizi ya COVID-19
nchini, Serikali imeruhusu vyuo na shule za sekondari (kwa wanafunzi wa kidato
cha sita) zifunguliwe kuanzia tarehe 1 Juni 2020; na
(n)
Serikali imeruhusu shughuli zote za michezo
kuanza tena kama ilivyokuwa awali.
Fursa Zilizojitokeza Kutokana na COVID-19
58.
Mheshimiwa
Spika, pamoja na athari zilizojitokeza, zipo pia fursa kadhaa zilizoambatana
na janga hili zikijumuisha: kuongezeka kwa matumizi ya njia za mtandao katika
shughuli mbalimbali ikiwemo mikutano (pamoja na ya
Bunge); miamala ya fedha kwa njia za kielektroniki; matumizi ya tiba asili;
fursa za kuongeza uzalishaji viwandani na kuuza mazao ya chakula katika masoko
ya kikanda; na kupungua kwa gharama za usafirishaji na uzalishaji viwandani
kutokana na kuendelea kushuka kwa bei za mafuta. Aidha, janga hili limetupa
fundisho la umuhimu wa kutumia mikakati inayoendana na mazingira yetu katika
kukabiliana na majanga badala ya kuiga mikakati ya nchi nyingine. Vile vile, COVID-19
imetukumbusha umuhimu wa kuhakikisha kuwa tunajitosheleza kwa uzalishaji wa
mahitaji ya bidhaa muhimu hapa nchini.
59.
Mheshimiwa
Spika, licha ya athari za COVID-19 ambazo zimeonekana kwenye
uchumi wa Taifa hadi sasa na hatua ambazo zimechukuliwa, napenda pamoja na
mwenendo mzuri wa kupungua kwa COVID-19 nchini, nami niwaombe Watanzania
kuendelea kuzingatia ushauri wa wataalam wetu wa afya kuhusu kujikinga na COVID-19.
Aidha, niwahakikishie watanzania kwamba fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo
kwa mwaka ujao wa fedha 2020/21 hazitapunguzwa kwa sababu ya COVID-19.
IV.
SERA ZA BAJETI KWA MWAKA 2020/21
Shabaha za Uchumi Jumla
60.
Mheshimiwa Spika, huu ni mwaka
wa mwisho wa utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka
Mitano (FYDP II) 2016/17-2020/21 wenye dhima ya “kujenga uchumi wa viwanda
utakaochochea ajira na ustawi endelevu wa jamii”. Hivyo, bajeti hii
imeandaliwa kwa kuzingatia lengo hilo kuu ambalo linaitaka Serikali iendelee kuimarisha
mazingira wezeshi ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini. Hii ni pamoja na
kuhakikisha miundombinu ya kiuchumi inaboreshwa, panakuwepo na sera rafiki za
kikodi na fedha, mfumo rekebu mzuri, upatikanaji mzuri wa ardhi, vibali vya
kazi na nguvu kazi yenye ujuzi pamoja na kuendelea kutilia mkazo nafasi muhimu
ya kilimo katika ujenzi wa uchumi wa viwanda. Aidha, bajeti hii imeandaliwa kwa
kuzingatia kwamba ni muhimu kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani ili
kuwezesha ujenzi na ukarabati wa miundombinu, kuendelea kugharamia mahitaji
mengine ya msingi na uendeshaji wa Serikali. Aidha, kama ilivyo kwa nchi zote
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, dhima ya bajeti ya 2020/21 ni kuchochea
ukuaji wa uchumi ili kulinda na kuboresha maisha ya wananchi, ajira na biashara
pamoja na kufufua viwanda.
61.
Mheshimiwa Spika, maandalizi
ya bajeti hii yamezingatia pia mazingira tuliyonayo hivi sasa ikiwemo athari za
ugonjwa wa homa kali ya mapafu katika sekta mbalimbali na mvua nyingi ambazo
zimeharibu miundombinu ya usafiri na usafirishaji mijini na vijijini na hata
mazao kama vile zabibu. Licha ya athari hizo, bajeti hii imezingatia fursa
zilizoibuka ikiwemo kushuka kwa bei za mafuta, kuongezeka kwa bei za dhahabu na
mwanya wa kuzalisha vifaa na vifaa tiba katika viwanda vya ndani ili
kukabiliana na COVID-19. Janga la COVID-19 pia limeilazimu bajeti
hii kuweka msukumo zaidi kwenye utafiti upande wa dawa, virusi na maendeleo ya
viwanda.
62.
Mheshimiwa Spika, ni
wazi pia kwamba maandalizi ya bajeti hii
yamezingatia kuwa mwaka huu 2020 ni mwaka wa uchaguzi mkuu. Hivyo, bajeti hii imetilia
maanani umuhimu wa kuwezesha zoezi hili muhimu kibajeti kwa lengo la kuimarisha
demokrasia na utawala bora nchini. Aidha, bajeti hii itaimarisha na kuendeleza
mafanikio makubwa yaliyopatikana upande wa huduma za jamii na miundombinu ya
kiuchumi, hususan kuhakikisha kwamba miradi ya kitaifa ya kimkakati inaendelea
kutekelezwa kama ilivyopangwa.
63.
Mheshimiwa Spika, kutokana na mambo ya msingi yaliyozingatiwa katika kuandaa bajeti hii kama
nilivyoeleza hapo awali, shabaha za uchumi jumla katika kipindi cha mwaka 2020/21
ni kama ifuatavyo: -
(i)
Ukuaji wa Pato Halisi la Taifa
unatarajiwa kupungua kutoka maoteo ya awali ya asilimia 6.9 na kufikia asilimia
5.5 mwaka 2020 ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2019. Hii ni kutokana na
mvua nyingi ambazo zimeharibu miundombinu ya usafirishaji nchini na athari za
ugonjwa wa COVID–19 ulioenea katika nchi nyingi ambazo ni washirika wetu
wakubwa wa kibiashara;
(ii)
Mfumuko wa bei unatarajiwa
kuendelea kubaki katika wigo wa tarakimu moja kati ya wastani wa asilimia 3 hadi
5 kwa mwaka 2020/21;
(iii)
Mapato ya ndani yanakadiriwa
kuwa asilimia 14.7 ya Pato la Taifa mwaka 2020/21 kutoka matarajio ya asilimia 14.0
mwaka 2019/20;
(iv)
Mapato ya kodi yanatarajiwa kufikia
asilimia 12.9 ya Pato la Taifa mwaka 2020/21 kutoka matarajio ya asilimia 12.1 mwaka
2019/20;
(v)
Matumizi ya Serikali
yanatarajiwa kuwa asilimia 22.1 ya Pato la Taifa mwaka 2020/21;
(vi)
Nakisi ya bajeti (ikijumuisha
misaada) inakadiriwa kuwa asilimia 2.6 ya Pato la Taifa mwaka 2020/21 ikiwa ni
chini ya asilimia 3.0 iliyokubaliwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki; na
(vii) Kuwa na
akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa
na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne (4).
Sera na Mikakati ya Kuongeza Mapato
64.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/21, Serikali
itaendelea kuweka kipaumbele katika ukusanyaji wa mapato ya ndani. Masuala
muhimu yatakayozingatiwa ni pamoja na kuimarisha zaidi usimamizi wa ukusanyaji
wa mapato kwa kutekeleza hatua zifuatazo:
(i)
Kuendelea na utekelezaji wa mpango
wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuwianisha na kupunguza viwango vya kodi, tozo
na ada mbalimbali;
(ii)
Mamlaka ya Mapato Tanzania
kuchukua hatua za kupanua wigo wa kodi na kujenga mahusiano na mazingira rafiki
kwa mlipakodi;
(iii)
Kuimarisha Ofisi ya Msajili wa
Hazina na kuiwezesha kukusanya gawio na michango ya Mashirika kwenye Mfuko Mkuu
wa Serikali;
(iv)
Kuwezesha na kuimarisha Baraza
la Rufaa za Kodi (TRAT) na Bodi ya Rufaa za Kodi (TRAB) kushughulikia pingamizi
na rufaa za kodi kwa haraka;
(v)
Kuimarisha usimamizi wa sheria
za kodi ili kutatua changamoto za ukwepaji kodi na kupunguza upotevu wa mapato;
na
(vi)
Kuhimiza matumizi ya mifumo ya
TEHAMA ili kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani yakijumuisha
mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa.
65.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hatua hizo za
kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, Serikali itaendelea kutoa
elimu kwa umma ili kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika kuwekeza kwenye
Hatifungani na Dhamana za Serikali na kuorodhesha Hatifungani za Serikali
katika Soko la Hisa la Dar es Salaam. Aidha, Serikali itaendelea kutekeleza Mwongozo wa Ushirikiano
wa Maendeleo (Development Cooperation Framework - DCF) ili kuwezesha
upatikanaji wa misaada na mikopo ya masharti nafuu na kukopa kwa utaratibu wa
udhamini kutoka taasisi za udhamini
wa mikopo (Export Credit Agencies -ECA), ambayo masharti yake yana
unafuu.
Sera za
Matumizi
66.
Mheshimiwa Spika, Sera za Matumizi
katika mwaka 2020/21 zitajumuisha yafuatayo:
(i)
Kuendelea kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma na
kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima;
(ii)
Kuhakikisha kuwa nakisi ya bajeti haizidi asilimia 3.0 ya
Pato la Taifa kuendana na vigezo vya Jumuiya ya Afrika Mashariki;
(iii)
Kuelekeza fedha kwenye maeneo ya kipaumbele yatakayochochea
ukuaji wa uchumi;
(iv)
Kuhakikisha kuwa miradi inayoendelea inapewa kipaumbele
kabla ya miradi mipya;
(v)
Kudhibiti ulimbikizaji wa madai; na
(vi)
Kuongeza kasi ya matumizi ya TEHAMA katika miamala na shughuli
za Serikali.
Maeneo ya Vipaumbele kwa Mwaka 2020/21
67.
Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka 2020/21 ni ya tano na ya mwisho katika utekelezaji wa
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21. Hivyo,
utekelezaji wa bajeti hii utajikita zaidi katika maeneo mbalimbali ya
vipaumbele yenye kuchochea mageuzi ya uchumi na maendeleo ya watu.
Kukarabati Miundombinu Iliyoharibiwa
na Mvua Nyingi/Mafuriko na Kupambana na Homa Kali ya Mapafu (COVID-19)
68.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tunamaliza mwaka 2019/20 katika hali isiyo ya kawaida kutokana na uharibifu
mkubwa wa miundombinu ya usafirishaji nchi nzima uliosababishwa na mvua
nyingi/mafuriko pamoja na athari za ugonjwa wa homa kali ya mapafu
inayosababiswa na virusi vya CORONA, Serikali italazimika kuelekeza
rasilimali zaidi kukarabati barabara, madaraja, reli na miundombinu mingine
iliyoharibiwa na mafuriko pamoja na kuendelea kupambana na athari za janga la COVID-19
ikiwa ni pamoja na kusaidia sekta zilizoathirika zaidi.
Miradi ya Kielelezo
69.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kugharamia utekelezaji wa miradi ya Kitaifa ya
kimkakati ikiwemo: Ujenzi wa Reli ya Kati ya Standard Gauge; Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere - MW
2,115; Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania; kuwezesha Mradi wa Ujenzi wa Bomba
la Mafuta Ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga; na Kuendelea na ujenzi na
ukarabati wa reli, barabara, madaraja, viwanja vya ndege, bandari, meli katika
maziwa makuu na vivuko; kuimarisha miundombinu ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji
wa umeme na gesi; Uendelezaji wa Kanda Maalum za Kiuchumi; na Kusomesha kwa wingi
Wataalamu kwenye Fani na Ujuzi Adimu/Maalum.
Huduma za Jamii
70.
Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la huduma za jamii miradi
itakayotekelezwa inalenga kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, elimu na ujuzi na huduma za maji safi na majitaka. Kwa upande wa
elimu, shughuli zitakazotekelezwa ni pamoja na kuendelea kugharamia utoaji wa
elimumsingi bila ada, kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika
shule za msingi, sekondari, vyuo vya ualimu, vyuo vya ufundi na vyuo vya elimu
ya juu ikijumuisha mifumo ya TEHAMA, kuimarisha elimu ya ufundi na mafunzo ya
ufundi stadi na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kuboresha
huduma ya maji, elimu ya afya na usafi wa mazingira shuleni.
71.
Mheshimiwa Spika, katika uboreshaji wa huduma za afya, shughuli zitakazotekelezwa ni pamoja
na ununuzi na usambazaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi, ujenzi wa
hospitali za rufaa za mikoa na kanda, hospitali za wilaya, vituo vya afya na
zahanati, kuimarisha huduma za afya kwa watu wote kupitia bima ya afya na
kuajiri wataalam mbalimbali katika sekta ya afya.
72.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha huduma za maji safi na salama mijini na
vijijini. Shughuli zitakazotekelezwa ni kuimarisha Mfuko wa Maji Vijijini, kuendelea
kujenga na kukarabati miundombinu ya usambazaji maji, kuendeleza rasilimali za
maji, kuimarisha huduma za ubora wa maabara za maji, kuimarisha huduma za
majitaka na kuimarisha usimamizi wa mazingira ili kupunguza athari za mabadiliko
ya tabianchi;
Kilimo na Viwanda
73.
Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda, miradi itakayotiliwa
mkazo ni ujenzi wa viwanda vinavyotumia kwa wingi malighafi zinazopatikana hapa
nchini zikiwemo za kilimo, madini na gesi asilia ili kukuza mnyororo wa
thamani. Miradi hiyo ni pamoja na Ujenzi wa Kiwanda cha Kuchakata Gesi Asilia;
Uanzishwaji na Uendelezaji wa Kanda Maalum za Kiuchumi na Kongane za
Viwanda; viwanda vya kuongeza thamani mazao ya kilimo, mifugo na
uvuvi; kuongeza thamani ya madini; kuimarisha masoko ya madini na usimamizi
endelevu wa rasilimali za misitu. Katika eneo hili, Serikali itaendelea kutekeleza
Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) ikijumuisha
kuboresha miundombinu ya umwagiliaji na masoko na upatikanaji wa pembejeo za
kilimo na huduma za ugani, kuimarisha Ushindani katika Soko kwa kuzingatia
Sheria na Kanuni za Ushindani Sawa na kusimamia Sheria ya Mapitio na Majadiliano
Kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Utajiri na Maliasili za Nchi ya mwaka
2017.
74.
Mheshimiwa Spika, mikakati mingine
katika sekta ya kilimo ni pamoja na: kuhimiza matumizi ya TEHAMA kwa ajili ya
huduma za kilimo zikiwemo masoko, pembejeo na ugani; kuimarisha mfumo wa
usimamizi wa ushirika ikiwa ni pamoja na kuboresha mifumo ya ushirika katika
malipo ya fedha za wakulima; na kuanzisha mfumo wa kulinda wazalishaji wa ndani
wa mazao ya kilimo, dhidi ya mazao na bidhaa zinazoagizwa nje ya nchi kama
ngano, shayiri na mchuzi wa zabibu ili kuwahakikishia wakulima soko na kuwa na
uzalishaji endelevu na wenye tija.
Maeneo Mengine Muhimu
75.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha maisha ya wananchi wanyonge kwa kuendelea na
utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya
Jamii (TASAF), ambapo katika Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu (2020-2023) jumla
ya shilingi trilioni 2.03 zitatumika. Katika
awamu hii, utekelezaji utafanyika katika Halmashauri zote 185 za
Tanzania Bara na Wilaya zote 11 za Zanzibar.
Kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 1.22, sawa na asilimia 60
zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye vijiji na mitaa 16,596
Tanzania bara na shehia 388 Zanzibar. Kipaumbele kitatolewa kwa watu wenye
nguvu wanaotoka kwenye kaya maskini ambapo ajira milioni 1.2 zitazalishwa na
kuwapatia walengwa ujuzi pamoja na stadi za kazi.
76.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa uboreshaji wa
mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji, Serikali itaendelea
kutenga na kuendeleza maeneo ya uwekezaji kwa kujenga miundombinu wezeshi. Aidha,
Serikali itaendelea kutekeleza Mpango Kazi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara
na Uwekezaji kwa kuendelea kupunguza tozo na kodi kero na kuondoa mwingiliano
wa majukumu miongoni mwa taasisi za Serikali zinazohusika na masuala ya
biashara na uwekezaji.
77.
Mheshimiwa Spika, ukiacha utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini katika Awamu ya
Tatu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF III), ipo pia miradi mingine itakayotekelezwa
kwa pamoja kati ya Tanzania bara na Zanzibar ikiwemo Mradi wa Kikanda wa
Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya
Hindi (SWIOFish), programu ya mabadiliko ya tabianchi ambayo inalenga
kulinda mazingira ya fukwe katika ukanda wa bahari kuu na mradi wa Kupitia
Mifumo ya Ikolojia kwa lengo la kuongeza uwezo wa jamii kuhimili mabadiliko ya
tabianchi katika ngazi ya vijiji kwa kuimarisha mifumo ikolojia katika Wilaya
za Mvomero (Morogoro), Simanjiro (Manyara), Kishapu (Shinyanga), Mpwapwa
(Dodoma) na Kaskazini A, (Kaskazini Unguja).
Shehia zitakazonufaika na mradi kutoka Kaskazini A ni pamoja na Shehia
ya Matemwe Kijijini, Matemwe Jugakuu na Matemwe Mbuyutende.
78.
Mheshimiwa Spika, Mpango wa maendeleo wa Taifa wa mwaka 2020/21 niliouwasilisha leo asubuhi,
umeainisha kwa kina maeneo ya kipaumbele ambayo Serikali itayatekeleza katika
bajeti ya mwaka 2020/21.
V. MABORESHO YA MFUMO
WA KODI, ADA NA TOZO MBALIMBALI
79.
Mheshimiwa Spika, napenda sasa kuwasilisha
mbele ya Bunge lako Tukufu mapendekezo ya kufanya marekebisho ya mfumo wa kodi,
ikiwemo baadhi ya viwango vya kodi, tozo na ada zinazotozwa chini ya Sheria
mbalimbali na kurekebisha taratibu za
ukusanyaji na usimamiaji wa mapato ya Serikali. Marekebisho haya yamezingatia
dhamira ya Serikali ya kuendelea kuwa na mfumo wa kodi ambao ni tulivu na wa
kutabirika. Aidha, marekebisho yanalenga kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi
hususan katika sekta ya kilimo na viwanda, kuongeza kipato kwa waajiriwa na kuongeza mapato ya Serikali. Vile vile, maboresho haya yamezingatia uhitaji wa kuwekeza nguvu katika kuongeza upatikanaji wa vifaa tiba na dawa. Serikali pia
inaendelea kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Kufanya Biashara (BluePrint)
ulioidhinishwa mwaka 2017/18 kwa kupitia mfumo wa tozo na ada mbalimbali
zinazotozwa na Wizara na Mamlaka za Udhibiti kwa lengo la kupunguza au kuzifuta
baadhi ya tozo na ada hizi. Hadi sasa, jumla ya tozo na ada 114 zimefutwa. Marekebisho
yanayopendekezwa yanahusu maeneo 16 yafuatayo:
(a)
Sheria ya Kodi ya
Ongezeko la Thamani, SURA 148
80.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la
Thamani, Sura 148 kama ifuatavyo:
(i)
Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye bima ya kilimo
cha mazao. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama na kutoa unafuu katika bima
za kilimo ili kuwawezesha wakulima kuziwekea bima shughuli za kilimo na kuvutia
wananchi kutumia huduma za bima kwa ajili ya kujikinga na majanga mbalimbali
yanayoathiri shughuli zao za kilimo mfano ukame, mafuriko n.k; na
(ii)
Kufanya marekebisho ya kuwawezesha wauzaji wa bidhaa ghafi
nje ya nchi kuendelea kujirudishia Kodi ya Ongezeko la Thamani iliyolipwa
kwenye gharama za huduma au bidhaa katika shughuli hizo ili bidhaa hizo ziweze
kushindana katika masoko ya nje. Hatua hii pia inalenga kuendana na msingi wa
utozaji VAT kwa kuzingatia mahali bidhaa inapotumika (destination
principle).
Hatua zote za Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa ujumla wake
zinatarajiwa kupunguza mapato ya
Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni
46.
(b)
Sheria ya Kodi ya
Mapato, SURA 332
81.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya
Mapato, Sura 332 kama ifuatavyo:
(i)
Kupandisha kiwango cha mapato ya waajiriwa ili kuongeza
kiwango cha mapato yasiyotozwa kodi (threshold) kutoka shilingi 170,000
kwa mwezi hadi shilingi 270,000 kwa mwezi (sawa na kutoka shilingi 2,040,000/=
kwa mwaka hadi shilingi 3,240,000/= kwa mwaka) na kubadilisha makundi mengine
kwa viwango kama vilivyobainishwa katika Jedwali Na. 1b. Lengo la
mabadiliko haya ni kutoa unafuu wa Kodi ya Mapato kwa wafanyakazi. Hatua hii
pekee inatarajiwa kupunguza mapato kwa shilingi milioni 517.2;
(ii)
Kuongeza kiwango cha Mapato ghafi ya Vyama vya Ushirika vya
Msingi yasiyotakiwa kutozwa Kodi ya Mapato kutoka shilingi milioni hamsini
(50,000,000/=) hadi shilingi milioni mia moja (100,000,000/=) kwa mwaka. Lengo
la hatua hii ni kutoa nafuu ya kulipa Kodi ya Mapato kwa Vyama vya Ushirika vya
Msingi zikiwemo SACCOS kutokana na kuwa na mitaji midogo ili kuwanufaisha
wanachama wake kwa njia ya gawio na mikopo;
(iii)
Kufuta msamaha wa Kodi ya Mapato kwa wazalishaji walio
ndani ya maeneo maalum ya kiuchumi (Special Economic Zones) wanaozalisha
bidhaa na kuuza ndani ya nchi kwa asilimia 100. Hatua hii inalenga kuweka usawa
katika utozaji wa kodi ya mapato baina ya wazalishaji wa bidhaa walio nje na
walio ndani ya maeneo maalum ya Kiuchumi;
(iv)
Kuruhusu michango ya wadau kwenye Mfuko wa Ukimwi isitozwe
kodi ya Mapato (allowable deduction). Aidha, napendekeza pia michango
iliyotolewa na wananchi kwa Serikali na itakayoendelea kutolewa katika kipindi
hiki cha mapambano dhidi ya ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu (COVID 19)
isitozwe kodi hadi hapo Serikali itakapotangaza kuisha kwa ugonjwa huu. Lengo
la mabadiliko haya ni kuhamasisha uchangiaji wa hiari katika Mfuko wa Ukimwi na
kwa Serikali ili kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Ukimwi na COVID
19;
(v)
Kumpa Mamlaka Waziri wa Fedha kutoa msamaha wa Kodi ya
Mapato kwenye Miradi ya Kimkakati yenye jumla ya Kodi ya Mapato isiyozidi
shilingi bilioni moja kwa kipindi chote cha mradi (1,000,000,000/=) bila
kuwasilisha mapendekezo hayo kwenye Baraza la Mawaziri. Lengo la hatua hii ni
kuwezesha miradi yenye kiwango kidogo cha kodi ya mapato kutekelezwa kwa
haraka. Waziri mwenye dhamana ya fedha atafanya mashauriano na Mamlaka ya
Mapato kabla ya kutoa msamaha wa kodi husika;
(vi)
Kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani ya Mtaji (Capital
Gains) kwenye mapato yatokanayo na ubadilishaji wa leseni (concessional
right) katika ardhi iliyohodhiwa (reserved land) na kupangishwa kwa
mwekezaji mwingine. Lengo la hatua hii ni kupanua wigo wa kodi na kuongeza mapato
ya Serikali;
(vii)
Kutoza kodi ya zuio ya asilimia 10 kwenye malipo ya uwakala
inayolipwa kwa mawakala wa Benki kama ilivyo kwa mawakala wa huduma za uhamishaji
fedha za kieletroniki. Lengo la hatua hii ni kuweka usawa katika utozaji wa
kodi ya mapato kwa watoa huduma za kibenki, kielektroniki na huduma za usafirishaji
fedha kwa njia ya mitandao ya simu; na
(viii)
Kufanya marekebisho kwenye vifungu vya 3, 4, 6 na 69 vya
Sheria ya Kodi ya Mapato ili kuongeza tafsiri ya maneno “beneficial owner”; “representative
assessee” na “business connection”.
Lengo la maboresho haya ni kutekeleza matakwa ya nchi kujiunga kwenye Jukwaa la
Kimataifa la kubadilishana taarifa za kikodi ili kukabiliana na ukwepaji kodi
unaofanywa na kampuni za kimataifa. Aidha, maboresho haya yanalenga kuziba
mianya ya ukwepaji kodi ya mapato unaofanywa na makampuni yenye mahusiano
mbalimbali ya kibiashara kupitia matawi ya kampuni hizo kwenye nchi mbalimbali.
Hatua hizi za Kodi ya Mapato kwa ujumla wake zinatarajiwa
kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi bilioni 514.0.
(c)
Sheria ya Ushuru
wa Bidhaa, SURA 147
82.
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Sheria ya Ushuru wa bidhaa kifungu cha 124(2), marekebisho ya
viwango maalum vya ushuru wa bidhaa
(specific duty rates) kwa bidhaa zote zisizo za petroli yanaweza kufanyika
kila mwaka ili kuviwianisha na mfumuko wa bei na viashiria vingine vya uchumi
jumla. Hata hivyo, kutokana na biashara za bidhaa hizi kuzorota kutokana na
athari za kiuchumi zilizosababishwa na COVID-19, napendekeza kutofanya mabadiliko ya viwango maalum vya Ushuru wa Bidhaa
kwa bidhaa zote. Aidha, hatua hii inazingatia kiwango kidogo cha mfumuko wa
bei nchini na azma ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda, na hivyo
kuhamasisha uwekezaji kwenye sekta ya viwanda, kuvilinda na hatimaye kukuza
ajira na mchango wa sekta hiyo kwenye pato la Taifa.
83.
Mheshimiwa Spika, napendekeza pia kufanya marekebisho ya Ushuru wa Bidhaa kwenye bidhaa
zifuatazo:
(i)
Kutoza Ushuru wa
Bidhaa kwenye
bia za unga (powdered beer) zinazotambulika kwa HS Code 2106.90.99 kwa kiwango cha shilingi 844 kwa kilo ya bia ya unga inayoagizwa kutoka nje ya nchi. Lengo
la mabadiliko haya ni kupanua wigo wa kodi kwa kuwa bidhaa hizi kwa sasa
zinaagizwa toka nje ya nchi; na
(ii)
Kutoza Ushuru wa Bidhaa
kwenye
juisi za unga zinazotambulika kwa HS Code
2106.90.99 kwa kiwango cha shilingi 232/= kwa kilo ya juisi ya unga inayoagizwa
kutoka nje ya nchi. Lengo la mabadiliko haya ni kupanua wigo wa kodi kwa kuwa
bidhaa hizi kwa sasa zinaagizwa toka nje ya nchi.
Hatua za kutoza Ushuru wa Bidhaa kwenye bidhaa zisizo za
petroli kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha
shilingi bilioni 45.8.
(d)
Sheria ya
Usimamizi wa Kodi, SURA 438
84.
Mheshimiwa Spika; napendekeza kufanya maboresho kwenye
Sheria ya Usimamizi wa Kodi Sura 438, ili kumwezesha Kamishna Mkuu wa Mamlaka
ya Mapato Tanzania kutatua mapingamizi ya kodi kwa ufanisi na haraka.
Marekebisho haya ni pamoja na kuweka ukomo wa muda wa siku 30 za kuwasilisha
nyaraka zitakazotumika kwenye utatuzi wa pingamizi. Aidha marekebisho haya
yataweka ukomo wa miezi 6 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania kufanya maamuzi ya
mapingamizi ya kodi. Kwa sasa, sheria haitoi ukomo kwa walipakodi kuwasilisha
nyaraka zitazoisaidia Mamlaka ya Mapato kufanya uamuzi kuhusu pingamizi. Vile
vile, kwa sasa sheria haitoi muda wa ukomo kwa Kamishna Mkuu kwa Mamlaka ya
Mapato kufanya uamuzi kuhusu pingamizi.
(e)
Sheria ya Fedha za
Serikali za Mitaa, SURA 290
85.
Mheshimiwa Spika, napendekeza
kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290, ili
kumpa mamlaka Waziri mwenye dhamana ya masuala yanayohusu Serikali za Mitaa kukusanya tozo ya huduma (Service
Levy) ya asilimia 0.3 ya mapato ghafi kwenye Sekta ya Mawasiliano kwa niaba
ya Halmashauri, na kuyagawa mapato hayo kwa Halmashauri zote ndani ya siku 14
baada ya kukusanywa. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- TAMISEMI ataandaa kanuni
ambazo zitaweka utaratibu wa ukusanyaji na ugawaji wa mapato hayo kwa kutumia
kikokotoo maalum kwa kuzingatia kiasi cha Tozo ya Huduma kutoka Sekta ya
Mawasiliano kwa kila Halmashauri. Hatua hii itasaidia kuziondolea kero baadhi
ya Halmashauri ya kukosa mapato kutoka kwenye chanzo hiki na kupunguza usumbufu
wa ufuatiliaji wa kila Halmashauri kwenye Makao Makuu ya Makampuni yanayotoa huduma
za mawasiliano nchini.
(f)
Sheria ya Fedha za
Umma, Sura 348
86.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye
Sheria ya Fedha za Umma Sura 348 ili
kuziongeza Taasisi za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC); Mamlaka ya Udhibiti
wa Mbolea (TFRA); Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA); na Mamlaka ya
Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwenye orodha ya taasisi zinazochangia gawio au asilimia
15 ya Mapato ghafi kwenye Mfuko wa Hazina.
Hatua hiyo ya marekebisho ya Sheria ya Fedha za Umma
inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi bilioni 5.89.
(g)
Sheria ya Msajili
wa Hazina, Sura 370
87.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya Marekebisho ya Kifungu cha 10A
(1) cha Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370 kwa kuondoa maneno “not financed through Government Budget” ili kuruhusu Ofisi ya
Msajili wa Hazina kukusanya asilimia 70 ya fedha za ziada kutoka kwenye
Mashirika, Taasisi au Wakala yoyote itakayoonekana kuwa na ziada. Lengo la
hatua hizi ni kuongeza udhibiti wa fedha za Serikali.
(h)
Sheria ya Usajili
wa Magari, Sura 124
88.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Usajili wa Magari
Sura 124, ili kuanzisha usajili wa magari kwa kutumia namba maalum (mfano T.
777 DDD) kwa ada ya shilingi laki tano (500,000/=). Ili kuwezesha wateja
kuchagua namba ya usajili wa gari katika namba zilizopo katika regista ya namba
za magari katika muda husika.
Hatua hizi za marekebisho ya Sheria ya Usajili wa Magari
inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 200.
(i)
Sheria ya Madini,
SURA 123
89.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Madini, Sura 123 ili kuweka vipengele vinavyomtaka mwombaji wa leseni au
anayetaka kuhuisha leseni za uchimbaji madini kuwa na Namba ya Utambulisho wa
Mlipakodi na Cheti cha Kodi (Tax Clearance) kutoka Mamlaka ya Mapato.
Lengo la hatua hii ni kuchochea uwajibikaji wa hiari.
(j)
Sheria ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi Stadi, SURA 82
90.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kupunguza kiwango
cha tozo kwa ajili ya maendeleo ya ufundi stadi (Skills Development Levy)
kutoka asilimia 4.5 hadi asilimia 4. Lengo la marekebeisho haya ni kuwapunguzia
waajiri mzigo na gharama za uendeshaji wa shughuli zao na kutimiza azma ya
kupunguza tozo hizi hatua kwa hatua bila kuathiri mapato kwa kiasi kikubwa.
Marekebisho haya yanategemea kupunguza Mapato ya Serikali kwa kiasi cha
shilingi bilioni 42.07.
(k)
Sheria ya Posta na
Mawasiliano ya Kielektroniki, SURA 306
91.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye
Sheria ya Posta na Mawasiliano ya Kielektroniki Sura 306 ili kuziondoa kampuni
zinazomilikiwa na Serikali na ambazo Serikali inamiliki hisa asilimia 25 na
zaidi katika takwa la kuorodheshwa kwenye soko la hisa. Hatua hii inalenga
kutokusababisha kupungua kwa hisa zinazomilikiwa na Serikali baada ya Kampuni
kuorodheshwa kwenye soko la hisa. Aidha, napendekeza kuondoa kampuni
zinazokodisha minara ya mawasiliano zisiwe sehemu ya makampuni ya mawasiliano
zinazotakiwa kuorodheshwa kwenye soko la hisa.
(l)
Sheria ya Ardhi,
Na. 4 ya Mwaka 1999
92.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya
marekebisho ya Sheria ya Ardhi, Na. 4 ya Mwaka 1999 ili kuweka ulazima wa
mwananchi yeyote ambaye ardhi yake imefanyiwa upimaji (survey) na
michoro yake kuidhinishwa na Wizara yenye dhamana ya masuala ya ardhi kupeleka
maombi kwa Kamishna wa Ardhi kupatiwa hati ya kumiliki ardhi ndani ya siku
tisini (90) kuanzia tarehe ya kuidhinishwa kwa michoro ya upimaji. Lengo la
marekebisho haya ni kuwafanya wananchi wanaohodhi ardhi bila umiliki wafanye
taratibu za kuomba umiliki.
(m) Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya
mwaka 2004
93.
Mheshimiwa Spika, kikao cha
Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki cha Maandalizi ya Bajeti
kilichofanyika tarehe 13 Mei, 2020 kwa njia ya mtandao (Video Conference), kilipendekeza kufanya marekebisho ya Viwango vya
Ushuru wa Pamoja wa Forodha (EAC – Common External Tariff “CET”) na
Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Customs Management
Act, 2004) kwa mwaka wa fedha 2020/21.
94.
Mheshimiwa Spika, mapendekezo ya Mawaziri wa
Fedha ya kufanya marekebisho kwenye Viwango vya Pamoja vya Ushuru wa Forodha
yanahusisha hatua mpya na zinazoendelea ambazo zimekuwa zikitekelezwa katika
mwaka 2019/20.
(i)
Mapendekezo ya
hatua mpya za viwango vya Ushuru wa Forodha ni kama ifuatavyo: -
(a)
Kupunguza Ushuru wa Forodha hadi asilimia 0 kutoka viwango vya awali vya
asilimia 10 na asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye malighafi zinazotumika
katika uzalishaji wa vifaa maalum vinavyotumika katika kupambana na ugonjwa wa
homa kali ya mapafu (COVID-19) vikiwemo Barakoa (Masks), kipukusi (sanitizer), mashine za kusaidia kupumua (ventilators),
na mavazi maalum ya kujikinga
yanayotumiwa na madaktari na wahudumu wa afya (PPE). Msamaha huu
utatolewa kwa utaratibu wa “duty
remission”. Hatua hii inalenga kutoa unafuu wa uzalishaji wa vifaa hivyo
hapa nchini ili kuongeza kasi katika kupambana na ugonjwa huo;
(b)
Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 10 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye mashine za
kielektroniki zinazotumika kukusanya mapato ya Serikali (Cash registers,
Electronic Fiscal Device (EFD) Machines and Point of Sale (POS) machines zinazotambulika
katika HS Code 8470.50.00 na 8470.90.00;
(c)
Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye vifungashio
vinavyotumiwa na wazalishaji wa maziwa kwa joto la juu yanayodumu kwa muda
mrefu (UHT Milk) vinavyotambulika kwa
HS codes 4819.50.00. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa wazalishaji wa
maziwa hapa nchini. Aidha utaratibu utakaotumika kutoa unafuu huo ni wa “Duty Remission”;
(d)
Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka kiwango cha asilimia 10 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja
kwenye vifuniko vya chupa za mvinyo (corks)
vinavyotambulika kwa HS Codes 4503.10.00 kwa kuzingatia kuwa hazizalishwi hapa
nchini. Hatua hii inalenga kuwapunguzia gharama wazalishaji wa mvinyo ili
kuhamasisha na kuendeleza kilimo cha zao la zabibu nchini pamoja na ajira.
Aidha utaratibu utakaotumika kutoa unafuu huo ni wa “Duty Remission”;
(e)
Kuongeza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35 kwa mwaka mmoja
kwenye
bidhaa za marumaru zinazotambulika kwa HS Code 6907.21.00; 6907.22.00; na
6907.23.00 zinazoingizwa kutoka nje. Lengo la hatua hii ni kulinda na kukuza
viwanda vya ndani vinavyozalisha marumaru pamoja na kuongeza ajira;
(f)
Kuongeza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35 kwa mwaka mmoja
kwenye
chai inayotambulika kwa HS Code 09.02 inayoagizwa kutoka nje. Lengo la
pendekezo hili ni kulinda viwanda vya ndani na kuhamasisha kilimo cha chai hapa
nchini pamoja na kuongeza ajira katika sekta ya kilimo.
(g)
Kuongeza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye magunia (sacks
and bags of jute or other textile bast fibers of heading 53.03)
yanayotambulika kwa HS Code 6305.10.00 yanayoagizwa kutoka nje. Lengo la hatua
hii ni kulinda viwanda vya ndani vinavyotengeneza magunia ya mkonge, kukuza na
kuendeleza kilimo cha zao la mkonge hapa nchini pamoja na kuongeza ajira na
mapato ya Serikali;
(h)
Kuongeza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 0 hadi asilimia 10 kwa mwaka mmoja
kwenye
kakao inayoingizwa kutoka nje inayotambulika kwa HS Code 1805.00.00. Lengo ni
kuchochea na kuhamasisha kilimo cha zao la kakao nchini pamoja na kuongeza
mapato ya Serikali;
(i)
Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja
kwenye vifungashio vya kuhifadhia kahawa vinavyotumiwa na viwanda vya kusaga
kahawa
nchini. Vifungashio vitakavyohusika ni vile vinavyotambulika katika HS codes
7310.21.00; 6305.10.00; 3923.50.10; 3923.50.90; 3920.30.90 na 48.19. Hatua hii
inalenga kuongeza thamani kwenye zao la kahawa na kuvipa unafuu wa gharama
viwanda vinavyosaga kahawa hapa nchini. Aidha utaratibu wa “Duty Remission” utatumika katika kuagiza vifungashio hivyo;
(j)
Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja
kwenye vifungashio vya kuhifadhia korosho. Vifungashio vitakavyohusika
ni vile vinavyotambulika katika HS codes 3923.21.00. Hatua hii inatarajiwa
kuongeza thamani kwenye zao la korosho na kuzipa unafuu wa gharama taasisi
zinazohusika na kuchakata korosho hapa nchini. Aidha utaratibu wa “Duty Remission” utatumika katika
kuagiza vifungashio hivyo; na
(k)
Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye
vifungashio vya kuhifadhia pamba. Vifungashio vitakavyohusika ni vile
vinavyotambulika katika HS codes 3920.30.90; 6305.39.00 na 7217.90.00. Hatua
hii inalenga kuvutia uwekezaji ili kuongeza thamani ya zao la pamba nchini.
(ii)
Mapendekezo ya
kuendelea na utekelezaji wa viwango vya Ushuru wa Forodha vya mwaka 2019/20 ni
kama ifuatavyo; -
(a)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 0 kwa mwaka mmoja kutoka
kiwango cha awali cha asilimia 25 kwenye malighafi za kutengeneza taulo za
watoto (Baby Diapers) zinazotumbulika kwa HS code 3506.91.00 Hot Melt
Adhesive; PE film HS Code 3920.10.90, Empty bag for Baby Diapers
HS Code 6305.33.00, Plastic cask HS Code 3926.90.90; na kiwango cha
awali cha asilimia 10 kwenye Super
Absorbent Polymer HS Code 3906.90.00, Wet strength paper HS Code
4803.00.00, Non-woven HS Code 5603.11.00, Polyethylene laminated
Nonwovens HS Code 5903.90.00, Spandex HS Code 5402.44.00 na Dust
free paper HS Code 4803.00.00. Aidha, msamaha huu utatolewa kwa utaratibu
wa “Duty Remission”. Hatua hii
inatarajiwa kutoa unafuu wa gharama za uzalishaji, kuongeza ajira na mapato ya
Serikali;
(b)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 0 kwa mwaka mmoja kutoka kiwango cha
awali cha asilimia 25 kwenye vifaa vinavyotumika katika kukata, kung’arisha na
kuongeza thamani ya madini ya vito vinavyotambulika kwa HS Codes 6804.10.00;
7018.90.00; 7020.00.99; na kiwango cha awali cha asilimia 10 kwenye HS Codes
3606.90.00; 6813.20.00; 8202.20.00; 8202.99.00; 8203.20.00; 8205.10.00;
8423.89.90; 8513.10.90; na 9002.19.00. Hatua hii itawanufaisha wanaofanya
shughuli hizo na utaratibu wa “Duty
Remission” ndio utatumika katika kuagiza vifaa hivyo;
(c)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia
0 kwa mwaka mmoja kutoka
kiwango cha awali cha asilimia 10 kwenye makaratasi (HS Code 4805.11.00 na 4805.19.00)
pamoja na asilimia 25 hadi 10, kwa mwaka mmoja kwenye makaratasi (HS Code 4805.24.00
na 4805.25.00) yanayotumika kama malighafi ya kutengeneza vifungashio vya mboga
mboga kwa ajili ya kuuza nje ya nchi. Utaratibu wa “Duty Remission” utatumika ambapo viwanda vinavyotengeneza
vifungashio hivyo tu ndivyo vitakavyonufaika. Aidha, karatasi hizi hazizalishwi
na kiwanda chetu cha Mufindi hapa nchini. Lengo la hii ni kuwapa unafuu wazalishaji
wa vifungashio vya mbogamboga hapa nchini pamoja na kuwawezesha wakulima kupata
vifungashio hapa nchini ambapo kwa sasa vinaagizwa kutoka nje kwa gharama
kubwa;
(d)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia
0 kwa mwaka mmoja kutoka
kiwango cha awali cha asilimia 25 kwenye vifungashio vya mbegu vinavyotambulika katika HS codes
3923.29.00; 6305.10.00; 4819.40.00; 7310.29.90; 6305.33.00; 6305.20.00;
6304.91.90; 7607.19.90. Utaratibu utakaotumika kutoa unafuu huo ni wa “duty
remission”. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa wazalishaji wa mbegu
hapa nchini;
(e)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja
kwenye kahawa inayotambulika kwa HS Code 09.01 inayoagizwa kutoka nje ya nchi
za EAC. Lengo la pendekezo hili ni kulinda viwanda vya ndani na kuhamasisha
kilimo cha kahawa hapa nchini pamoja na kuongeza ajira katika sekta ya kilimo;
(f)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 au dola za kimarekani 125 kwa kila tani
moja ya ujazo (Metric ton) kwenye bidhaa za chuma kwa mwaka mmoja
kutegemea kiwango kipi ni kikubwa. Bidhaa hizo ni “Flat -rolled products of
iron or Non-alloy steel na Flat –rolled products of other alloy steel.” Bidhaa hizi hutambulika katika HS Codes
7209.16.00; 7209.17.00; 7209.18.00; 7209.26.00; 7209.27.00; 7209.28.00;
7209.90.00; 7211.23.00; 7211.90.00; 7225.50.0 na 7226.92.00. Lengo la kuendelea
kutoza viwango hivyo ni kulinda viwanda vya hapa nchini, kukuza ajira pamoja na
kudhibiti udanganyifu wa thamani halisi ya bidhaa hizo kutoka nje;
(g)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au dola za kimarekani 250 kwa kila tani moja ya
ujazo (metric ton) kwenye bidhaa za mabati zinazotambulika kwa HS codes
7210.41.00; 7210.49.00; 7210.61.00; 7210.69.00; 7210.70.00 na 7210.90.00 kutegemea
kiwango kipi ni kikubwa badala ya ushuru wa asilimia 25 au dola za kimarekani
200 kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton), kwa mwaka mmoja. Lengo la hatua
hii ni kuwalinda wazalishaji wa bidhaa hizo hapa nchini kutokana na ushindani
wa nje;
(h)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 au dola za kimarekani 250 kwa kila tani moja ya
ujazo (Metric ton) kwa mwaka mmoja kutegemea kiwango kipi ni kikubwa
kwenye bidhaa za mabati zinazotambulika katika HS Code 7212.60.00 badala ya
ushuru wa asilimia 10 pekee. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani
kutokana na udanganyifu wa thamani halisi ya bidhaa hizo zinapoingizwa kutoka
nje (under-invoicing and under valuation), na kulinda ajira na mapato ya
Serikali;
(i)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au dola za kimarekani 250 kwa kila tani moja ya
ujazo (Metric ton) kwenye bidhaa za mabati kwa mwaka mmoja kutegemea
kiwango kipi ni kikubwa. Ushuru huo unahusu bidhaa zinazotambulika katika HS
Code 7212.30.00; 7212.40.00 na 7212.50,00. Hatua hii ina lengo la kulinda
viwanda vya ndani kutokana na udanganyifu wa thamani halisi ya bidhaa hizo
zinapoingizwa kutoka nje (under-invoicing and under valuation), na
kulinda ajira na mapato ya Serikali;
(j)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au dola
za kimarekani 250 badala ya kiwango cha asilimia 25 au dola za kimarekani 200
kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kwenye bidhaa za chuma kwa
mwaka mmoja kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwenye nondo kwa mwaka mmoja. (Reinforment
bars and hallow profile). Hatua hii inahusu bidhaa zinazotambulika katika Hs
codes 7213.10.00; 7213.20.00; 7213.99.00; 7214.10.00; 7214.20.00; 7214.30.00;
7214.90.00; 7214.99.00; 7215.10.00; 7215.50.00; 7215.90.00; 7225.90.00;
7225.92.00; 7225.99.00; 7306.30.00; 7306.50.00; 7306.61.00; 7306.69.00; na
7306.90.00. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vinavyozalisha nondo hapa
nchini na kuongeza ajira;
(k)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya
asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye bidhaa za mboga mboga (horticultural
products) zinazotambulika kwa HS codes 0603.11.00; 0603.12.00; 0603.13.00;
0603.14.00; 0603.19.00; 0604.20.00; 0604.90.00; 0701.90.00; 0702.00.00;
0703.10.00; 0703.20.00; 0706.10.00; 0710.10.00; 0710.21.00; 0710.22.00;
0710.30.00; 0714.10.00; 0714.20.00; 0804.30.00; 0804.40.00; 0804.50.00;
0805.10.00; 0805.40.00; 0805.50.00; 0806.10.00; 0807.11.00; 0807.20.00;
0808.10.00; 0808.20.00. Hatua hii ni katika kulinda wakulima wa ndani ili
kuendeleza kilimo cha mbogamboga na maua hapa nchini;
(l)
Kuendelea kutoza ushuru wa forodha kwa kiwango cha asilimia
10 badala ya asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye bidhaa za fito za plastiki
zijulikanazo kama PVC Profiles HS
Code 3916.10.00; 3916.20.00; 3916.90.00 ambazo hutumika kwa ajili ya
kutengenezea fremu za milango, madirisha n.k. Lengo la hatua hii ni kuongeza
mapato ya Serikali;
(m)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya asilimia 10 kwa mwaka
mmoja kwenye karatasi zinazozalishwa na kiwanda cha mufindi hapa nchini ambazo
zinazotambulika kwa HS codes 4804.11.00; 4804.21.00; 4804.29.00; 4804.31.00 na
4804.41.00.
Lengo
la hatua hii ni kuendelea kulinda kiwanda cha mufindi na kuongeza uzalishaji wa
karatasi hapa nchini;
(n)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia
10 kwa mwaka mmoja kutoka kiwango cha awali cha asilimia 35 kwenye ngano inayotambulika
kwa HS Code 1001.99.10 na HS Code 1001.99.90 kwa utaratibu wa “Duty Remission” ambapo wanaonufaika na
unafuu huu ni wenye viwanda vya kusaga ngano. Hatua hii imezingatia makubaliano
na Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kutokana na kwamba uzalishaji wa ngano
katika nchi hizi hautoshelezi mahitaji, na bidhaa hii ni muhimu katika
kutengeneza vyakula mbalimbali. Lengo la Serikali ni kuwezesha Viwanda na
walaji wa vyakula vilivyotengenezwa kwa ngano waweze kupata vyakula husika kwa
bei nafuu na tulivu;
(o)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia
0 kwa mwaka mmoja kutoka kiwango cha awali cha asilimia 25 kwa utaratibu wa duty remission kwenye bidhaa ijulikanayo
kama “Printed Alluminium Barrier
Laminates” (ABL) HS Code 3920.10.90 ambayo hutumika kama malighafi ya
kutengeneza vifungashio vya dawa ya meno kwenye viwanda vya ndani, kwa mwaka
mmoja;
(p)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia
0 kwa mwaka mmoja kutoka kiwango cha awali cha asilimia 10 kwa utaratibu wa “Duty Remission” kwenye malighafi ya
kutengeneza sabuni ijulikanayo kama RBD Palm Stearin (HS Code
1511.90.40) kwa viwanda vinavyotengeneza sabuni nchini. Lengo la hatua hii ni
kutoa unafuu kwa viwanda vya kuzalisha sabuni nchini;
(q)
Kuendelea kutoza kwa mwaka mmoja Ushuru wa Forodha wa
asilimia 25 au dola za kimarekani 1.35 kwa kilo moja ya viberiti (safety
match boxes) vinavyotambuliwa kwenye HS code 3605.00.00 kutegemea kiwango
kipi ni kikubwa badala ya asilimia 25 pekee;
(r)
Kuendelea kutoza kwa mwaka mmoja Ushuru wa Forodha wa
asilimia 25 au dola za kimarekani 350 kwa kila tani moja ya ujazo (Metric
ton) kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwenye bidhaa za chuma za misumari
zinazotambulika kwa HS code 7317.00.00 (nails, tacks, drawing pins,
corrugated nails, and staples other than those of heading 83.05) badala ya
asilimia 25 pekee;
(s)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya
asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye soseji (sausages) na bidhaa za aina
hiyo zinazotambulika kwa HS code 1601.00.00. Lengo ni kuendelea kulinda
wajasiliamali wa ndani wanaozalisha bidhaa hizo;
(t)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya
asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye chingamu (chewing gum)
zinazotambulika kwa HS code 1704.10.00 zinazoagizwa kutoka nje. Lengo ni
kuendelea kulinda viwana vya ndani;
(u)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya
asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye peremende zinazotambulika kwa HS code
1704.90.00 zinazoagizwa kutoka nje. Lengo ni kuendelea kulinda viwanda vya
ndani na kukuza ajira;
(v)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya
asilimia 25 kwenye chokoleti (chocolates) HS code 18.06 kwa mwaka mmoja.
Lengo ni kulinda viwanda vya ndani na kukuza ajira;
(w)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya
asilimia 25 kwenye biskuti (HS code 1905) kwa mwaka mmoja;
(x)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya
asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye nyanya zilizosindikwa (tomato sauces)
zinazotambulika katika HS code 2103.20.00;
(y)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 60 badala ya
asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye maji (mineral water) yanayotambulika
katika HS code 2201.10.00;
(z)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya
asilimia 25 kwenye nyama zilizoainishwa katika sura ya 2 katika Viwango vya
pamoja vya ushuru wa forodha (meat and edible meat offal in chapter 2) kwa
mwaka mmoja. Lengo la hatua hii ni kuendelea kulinda na kuchochea sekta ya
ufugaji nchini;
(aa)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia
25 kwa mwaka mmoja kutoka kiwango cha awali cha asilimia 0 kwenye mafuta Ghafi
ya kula (mfano alizeti, mawese, soya, mizeituni, nazi, karanga, mahindi n.k)
yanayotambulika kwa HS code 1507.10.00; 1508.10.00; 1511.10.00; 1513.11.00;
1514.11.00; 1514.91.00; 1515.11.00; na kiwango cha awali cha asilimia 10 kwenye
HS Codes 1512.11.00, 1515.21.00; na 1515.30.00. Hatua hii inalenga katika
kuendelea kulinda na kuhamasisha uzalishaji wa mbegu za mafuta na mafuta ya
kula hapa nchini pamoja na kuongeza ajira mashambani, viwandani na pia kulinda
fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta hayo nje ya nchi;
(bb)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya
asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye mafuta ya kula yaliyochakatwa kwa kiwango
cha kati na mwisho (semi-refined, refined/double refined oil) mfano
alizeti, mawese, soya, mizeituni, karanga, nazi, mahindi n.k zinazotambulika
kwa HS codes 1507.90.00; 1508.90.00; 1509.90.00; 1510.00.00; 1511.90.10;
1511.90.30; 1511.90.90; 1512.19.00; 1512.29.00; 1513.19.00; 1513.29.00;
1514.19.00; 1514.99.00; 1515.19.00; 1515.29.00; 1515.50.00; 1515.90.00. Lengo
ni kuhamasisha uchakataji wa mbegu za mafuta hapa nchini na kuongeza ajira
viwandani na mashambani pamoja na kulinda fedha za kigeni zinazotumika kuagiza
mafuta hayo nje ya nchi;
(cc)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 badala ya
asilimia 0 kwenye “Gypsum Powder” HS code 2520.20.00 kwa mwaka mmoja;
(dd)
Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia
35 kwa mwaka mmoja kutoka kiwango cha asilimia 100 kwenye sukari ya matumizi ya
kawaida (consumption sugar) inayoagizwa kutoka nje ya nchi kwa vibali
maalum kwa lengo la kuziba pengo (gap sugar) la uzalishaji hapa nchini;
(ee)
Kuendelea kutoza kwa mwaka mmoja Ushuru wa Forodha wa
asilimia 35 kwenye mitumba inayoingia kutoka nje (badala ya asilimia 35 au dola za marekani 0.40 kwa kilo moja
kutegemea kiwango kipi kikubwa); na
(ff)
Kuendelea kusamehe Ushuru wa Forodha kwenye malighafi,
vipuri na mashine vinavyotumika katika kutengeneza viatu vya ngozi na nguo.
Aidha, sambamba na pendekezo hilo, Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki wanaendelea kutoa unafuu wa ushuru wa forodha kwa pamoja kwenye
orodha iliyooanishwa (harmonized list) ya malighafi na vipuri ili nchi
hizo ziweze kufanya biashara kwa bidhaa za nguo na viatu vya ngozi
vitakavyozalishwa ndani ya Jumuiya bila kutozana ushuru.
95.
Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa Fedha wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya pia marekebisho
kwenye Sheria ya Usimamizi wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Customs Management Act, 2004) kama ifuatavyo:
(i)
Kufanya marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Forodha ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACCMA, 2004) ili kutoa msamaha kwenye madawa na
vifaa muhimu vinavyotumika kupima, kukinga, kutibu na kupambana na mlipuko wa
magonjwa (supplies for diagnosis, prevention, treatment, and management of
epidemics, pandemics and health hazards) kama vile ugonjwa wa homa kali ya
mapafu (COVID- 19). Hatua hii inalenga kutoa unafuu wa bidhaa hizo ili
kurahisisha mapambano na udhibiti wa magonjwa hayo pindi yanapojitokeza;
(ii)
Kufanya marekebisho katika Jedwali la Tano la Sheria ya
Usimamizi wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACCMA, 2004) ili kusamehe
ushuru wa forodha kwenye zana (implements) zinazoingizwa nchini na watu
au taasisi zinazohusika katika kilimo, kilimo cha mbogamboga, kilimo cha maua
pamoja na ufugaji wa samaki. Lengo la kutoa msamaha huo ni kuchochea na
kuhamasisha ukuaji wa sekta ya kilimo pamoja na kuvutia uwekezaji mpya katika
sekta ndogo ya ufugaji wa samaki nchini; na
(iii)
Kufanya marekebisho katika Jedwali la Tano la Sheria ya
Usimamizi wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACCMA, 2004) ili kutoa
msamaha wa ushuru wa forodha kwenye Mayai ya kutotolesha vifaranga vya kuku (fertilized eggs for incubation) yanayoingizwa
na watu au taasisi zinazohusika na ufugaji wa kuku. Lengo ni kukuza na
kuhamasisha ufugaji wa kuku nchini.
Hatua hizi za Ushuru wa Forodha kwa pamoja zinatarajiwa
yatapunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi bilioni 208.04.
96.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kuongeza uthaminishaji wa vitenge
vinavyoingizwa nchini kutoka uthaminishaji wa sasa wa dola za Marekani 0.40 kwa
kila mita moja hadi dola za Marekani 1 kwa kila mita moja ya kitenge. Lengo la
hatua hii ni kuzuia udanganyifu wa thamani unaofanywa na baadhi ya
wafanyabiashara wasio waaminifu kwenye ankara wanazowasilisha Mamlaka ya Mapato
Tanzania.
(n)
Utekelezaji wa
Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Kufanya Biashara (Blueprint) kwa kurekebisha
Ada na Tozo mbalimbali.
97.
Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufuta au
kupunguza ada na tozo sitini (60) zinazotozwa na Wizara, Idara na Taasisi
zinazojitegemea ili Kuondoa kero na urasimu kwa wafanyabiashara na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji hasa katika kipindi hiki
cha mlipuko wa janga la homa kali ya mapafu duniani. Hatua hizi ni
sehemu ya mwendelezo wa utekelezaji wa Mpango wa kuboresha Mfumo wa udhibiti wa
Biashara (Blueprint for Regulatory Reforms to Improve the Business
Environment). Marekebisho hayo yatajumuisha:
(i)
Tume ya Ushindani
Napendekeza kufanya marekebisho ya kifungu cha 60
cha Sheria ya Ushindani kinachohusu adhabu ya makosa ya ushindani ili ihusishe
tu pato ghafi lililopatikana ndani ya Tanzania Bara pekee na si duniani kote.
Lengo la mabadiliko haya ni kuifanya Sheria hii itekelezeke kwa kuwa adhabu
inayotokana na pato ghafi la Kampuni za nje ni kubwa mno na hivyo kutolipika.
(ii)
Wakala wa Usajili
wa Biashara na Leseni (BRELA)
Napendekeza kufuta kipengele cha 16(2) cha Sheria ya
makampuni ili kuondoa takwa la kugongewa muhuri na Kamishna wa Viapo ili
kuonyesha umetimiza matakwa ya Sheria hiyo wakati unafungua kampuni au kuhuisha
usajili. Aidha, Kifungu cha 14(4) kinatosheleza matakwa yote hayo na hivyo hatua
hii itapunguza urasimu na gharama za kupata tamko la kutimiza matakwa ya
kisheria (Declaration of Competence).
(iii)
Bodi ya Sukari
Napendekeza kupunguza tozo inayotozwa na Bodi ya
Sukari kutoka asilimia 2 ya thamani ya mzigo au asilimia 2 ya dola za Marekani
mia nne na sitini (460) sawa na takriban dola za Marekani 9 kwa tani, chochote
kitakachokuwa kikubwa hadi dola 7.5 kwa tani moja.
(iv)
OSHA
(a)
Napendekeza kufuta tozo ya
mafunzo ya elimu kwa umma iliyokuwa inatozwa kiasi cha shilingi laki mbili na
nusu (250,000/=) kwa kila mshiriki kwa kuwa hili ni jukumu la msingi la OSHA
kuelimisha umma;
(b)
Napendekeza kufuta ada ya ukaguzi
iliyokuwa inatozwa kwa kiwango cha asilimia 80 ya ada ya usajili, ada hii
inaleta mkanganyiko kwa kuwa tozo ya usajili ilishafutwa; na
(c)
Napendekeza kupunguza ada ya
uchunguzi wa ajali iliyokuwa ikitozwa kiasi cha shilingi laki tano (500,000/=)
kwa kila mtaalamu anayefanya uchunguzi hadi shilingi laki moja na elfu ishirini
(120,000/=) kwa kila mtaalamu lakini si zaidi ya shilingi milioni moja
(1,000,000/=).
(v)
Jeshi la Zimamoto
na Uokoaji
Napendekeza
kufanya marekebisho ya Sheria ya Jeshi ya Zimamoto na Uokoaji Sura 427 kwa
kupunguza ada na tozo zifuatazo:
(a)
Kupunguza tozo ya Cheti cha Umahiri (Certificate of
Competence) inayotozwa kwa wauzaji wa vifaa vya zimamoto na uokoaji kutoka
shilingi laki tano (500,000/=) hadi shilingi laki mbili (200,000/=);
(b)
Kupunguza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto
kwenye maeneo ya uchimbaji madini yenye ukubwa usiozidi mita za mraba 2,000
kutoka shilingi milioni sita (6,000,000/=) hadi shilingi laki moja (100,000/=);
(c)
Kupunguza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto
kwenye maeneo ya uchimbaji madini yenye ukubwa kati ya mita za mraba 2001 hadi
4000 kutoka shilingi milioni sita (6,000,000/=) hadi shilingi laki moja na elfu
hamsini (150,000/=);
(d)
Kupunguza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto
kwenye maeneo ya uchimbaji madini yenye ukubwa kati ya mita za mraba 4001 hadi
9000 kutoka shilingi milioni sita (6,000,000/=) hadi shilingi laki mbili
(200,000/=);
(e)
Kupunguza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto
kwenye mitungi ya gesi yenye ujazo wa gesi kati ya tani 1 hadi tani 10 kutoka
shilingi milioni mbili (2,000,000/=) hadi shilingi milioni moja na laki tano
(1,500,000=/);
(f)
Kupunguza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto
kwenye maduka yanayouza mitungi ya gesi yasiyozidi ukubwa wa mita za mraba 100
kutoka shilingi laki moja (100,000/=) hadi shilingi elfu arobaini (40,000/=);
(g)
Kupunguza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto
kwenye maduka ya rejareja na maduka ya jumla kutoka shilingi elfu arobaini (40,000)
hadi shilingi elfu ishirini (20,000/=);
(h)
Kupunguza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto
kwenye vituo vidogo vya kuzalisha na kugawa umeme chini ya Megawatt 10 kutoka
shilingi milioni sita (6,000,000/=) hadi shilingi laki mbili (200,000/=);
Aidha,
napendekeza pia kufanya marekebisho ya Sheria ya Jeshi ya Zimamoto na Uokoaji
Sura 427, ili kuanzisha viwango vipya vya tozo kama ifuatavyo:
(a)
Kutoza tozo ya ukaguzi wa
kinga na tahadhari ya moto ya shilingi milioni
mbili (2,000,000/=) kwenye mitungi ya gesi yenye ujazo wa gesi kati ya tani 11
hadi tani 20; na
(b)
Kutoza tozo ya ukaguzi wa
kinga na tahadhari ya moto kati ya
shilingi elfu arobaini (40,000/=) hadi shilingi milioni tano (5,000,000/=)
kwenye taasisi ndogo za mikopo kutegemea na ukubwa wa eneo.
Lengo la hatua hizi ni kuweka mazingira rafiki ya
kibiashara na uwekezaji ili kuchochea uzingatiaji wa sheria kwa hiari na
kuongeza wigo wa wadau wanautumia huduma za Jeshi la Zimamoto.
(vi)
Wizara ya Mifugo
na Uvuvi
(a)
Sekta ya Mifugo
98.
Mheshimiwa Spika, napendekeza
kufanya marekebisho kwenye tozo mbalimbali kwenye Sekta ya Mifugo kama
ifuatavyo:
(i)
kufuta tozo ya kibali cha kusafirisha ngozi ndani na nje ya
wilaya iliyokuwa ikitozwa shilingi elfu tano (5000/=) kwa kibali; na
(ii)
Kupunguza tozo mbalimbali kwenye sekta ya mifugo na mazao
kama zilivyoanishwa kwenye Jedwali Na 2
na Na.3: -
Jedwali Na. 2:
Tozo za Vibali vya Kusafirisha Mifugo na Mazao Yake kwenda Nje ya Nchi
(shilingi)
Na.
|
Aina ya Mfugo/Zao
|
Kipimo
|
Tozo za Zamani
|
Tozo Pendekezwa
|
1
|
Ng’ombe
|
Kila mmoja
|
30,000
|
25,000
|
2
|
Kondoo/Mbuzi
|
Kila mmoja
|
7,500
|
5,000
|
3
|
Nyama ya ng’ombe
|
Kilo moja
|
150
|
100
|
4
|
Chakula cha wanyama
|
Tani
|
20,000
|
10,000
|
5
|
Mayai ya kula
|
Trei 1 (mayai 30)
|
1,000
|
100
|
Jedwali Na. 3: Tozo za Vibali vya Kuingiza Mifugo
na Mazao yake ndani ya Nchi (shilingi)
Na.
|
Aina ya
Mfugo/Zao
|
Kipimo
|
Tozo za
zamani
|
Tozo mpya
|
1
|
Punda
|
Kila mmoja
|
10,000
|
5,000
|
2
|
Ngamia
|
Kila mmoja
|
10,000
|
5,000
|
3
|
Nyama ya
ng’ombe
|
Kilo moja
|
5,000
|
4,000
|
4
|
Chakula cha
wanyama
|
Tani
|
20,000
|
10,000
|
Jedwali Na. 4: Tozo za Vibali vya
Kusafirisha Mifugo na Mazao yake kwenda Nje ya Nchi (shilingi)
Na.
|
Aina ya Mfugo/Zao
|
Kipimo
|
Tozo za Zamani
|
Tozo Pendekezwa
|
1
|
Farasi
|
Kila mmoja
|
30,000
|
50,000
|
2
|
Mbwa/paka
|
Kila mmoja
|
20,000
|
50,000
|
3
|
Ngamia
|
Kila mmoja
|
30,000
|
50,000
|
4
|
Wanyama pori
|
Kila mmoja
|
30,000
|
50,000
|
5
|
Mbegu
|
Kwa mrija
|
1,000
|
2,000
|
Jedwali Na. 5: Tozo za Vibali vya Kuingiza Mifugo na
Mazao yake ndani ya Nchini (shilingi)
Na.
|
Aina ya Mfugo/Zao
|
Kipimo
|
Tozo za zamani
|
Tozo Pendekezwa
|
1
|
Farasi
|
Kila mmoja
|
10,000
|
50,000
|
2
|
Mbwa/paka
|
Kila mmoja
|
30,000
|
50,000
|
3
|
Mayai ya kula
|
Trei (Mayai 30)
|
2,500
|
5,000
|
(iv)
Kuongeza ada ya kutunza mbuzi au kondoo kwenye vituo vya karantini,
kupumzishia mifugo na ukaguzi kwa kila mmoja kutoka shilingi mia mbili (200/)
hadi shilingi mia tano (500);
(v)
Kutoza tozo mpya za vibali vya kusafirisha nje ya nchi na kuingiza ndani ya
nchi mifugo na mazao yake kama ilivyoainishwa kwenye Kiambatisho Na. 5
(vi)
Kutoza shilingi elfu ishirini (20,000/=) kwa kibali cha kusafirisha pembe za ng'ombe, mbuzi na
kondoo pamoja na kwato na mifupa ndani na nje ya Wilaya;
(vii) Kutoza shilingi elfu tano 5,000/= kwa
kila kibali cha kusafirisha chakula cha Wanyama ndani na nje ya Wilaya;
(viii) Kutoza kibali kwa ajili ya huduma kwa mifugo na mazao yake wanaopita nchini kwenda nchi nyingine kama zilivyoainishwa
kwenye Kiambatisho Na. 6.
(b)
Sekta ya Uvuvi
99.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufuta tozo mbalimbali
kwenye Sekta ya Uvuvi kama ifuatavyo:
(i)
Kufuta tozo ya mrabaha wa dola za Marekani 0.4 kwa kilo ya
samaki katika uvuvi wa bahari kuu;
(ii)
Kupunguza ada za leseni ya kuuza samaki na mazao ya uvuvi
yanayovuliwa kwenye maji baridi (maziwa, mabwawa na mito) nje ya nchi kama
zilivyoainisha kwenye Jedwali Na. 6.
Jedwali Na: 6: Mapendekezo ya Kupunguza Ada ya Leseni
ya kuuza Samaki na Mazao ya Uvuvi yanayovuliwa kwenye Maji baridi Nje ya Nchi
(US$)
(iii)
Kupunguza ada za leseni ya kuuza samaki na mazao ya uvuvi
yanayovuliwa kwenye maji chumvi (bahari) nje ya nchi kama zilivyoainisha kwenye
Jedwali Na. 7.
Jedwali Na. 7:
Mapendekezo ya
Kupunguza ada ya Leseni ya kuuza Samaki
na Mazao ya Uvuvi yanayovuliwa kwenye Maji chumvi Nje ya Nchi (USD)
(iv)
Kupunguza tozo za mrabaha wa kusafirisha samaki nje ya
nchi kama ilivyoainishwa kwenye Kiambatisho Na. 7.
(v)
Kuongeza ada ya
leseni ya kuuza Mapezi /taya za papa nje ya nchi kutoka dola za kimarekani
2,700 hadi dola za kimarekani 5,000 kwa ajili ya kuendelea kuhifadhi papa na
jamii zake ambao wako hatarini kutoweka;
(vi)
Kutoza ada ya leseni ya kusafirisha aina nyingine ya mabondo na makome nje ya nchi kama
ilivyoainishwa kwenye Jedwali Na. 8.
Jedwali Na 8: Mapendekezo ya Kutoza Ada ya Leseni
ya Kusafirisha Samaki na Mazao Yake Nje
|
(vii)
Kutoza ada ya cheti cha afya ya samaki na
mazao yake yanayosafirishwa nje ya nchi (QA/APP/02) shilingi 30,000/= kwa ajili ya kukidhi matakwa ya soko la nje na afya ya mlaji;
(viii) Kutoza tozo za vibali vipya vya kusafirisha samaki na mazao yake kama
ilivyoainishwa kwenye Jedwali Na. 9 kwa ajili ya
kuendeleza uhifadhi wa mazao hayo.
Jedwali Na. 9: Mapendekezo ya Kutoza vibali
vipya vya kusafirisha samaki na mazao yake
Na.
|
Aina
ya Samaki/Zao
|
Idadi
|
Tozo Pendekezwa (Shilingi)
|
1
|
Kaa hai
|
Kilo moja
|
100
|
2
|
Kamba kochi hai
|
Kilo moja
|
100
|
3
|
Samaki hai wa mapambo waliokamatwa maji ya asili
|
Kipande kimoja
|
200
|
(vii) Wizara ya Maliasili na Utalii
100.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya mabadiliko ya
tozo za viingilio na huduma mbalimbali zinazotolewa na Makumbusho ya Taifa kama
zilivyoainishwa kwenye Kiambatisho Na. 8.
Lengo la mabadiliko haya ni kuongeza Mapato ya Serikali kwa kuwa viwango
vinavyotumika sasa ni vya toka mwaka 2002.
(viii) Mabango na Matangazo
101.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho
kwenye Jedwali la viwango vya tozo chini ya Kanuni za Ada ya Mabango na
Matangazo [Local Government Finance (fees for Billboards, Posters and
Hoarding) Order 2019], ili kupunguza kiwango cha tozo ya matangazo kwenye
magari ya wazalishaji wa bidhaa yanayotumika kusafirisha bidhaa hizo toka
viwandani kwenda kwa wasambazaji kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 10,000
hadi shilingi 4,000. Lengo la mabadiliko haya ni kukidhi maombi ya wazalishaji
dhidi ya tozo hii iliyosababisha wazalishaji wa bidhaa kuondoa matangazo kwenye
magari hayo hivyo kupunguza mapato ya Serikali kutoka kwenye chanzo hicho.
Hatua hii inatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa
kiasi cha shilingi bilioni 1.25
(o)
Mfumo wa
ukusanyaji wa maduhuli yanayotokana na sekta ya utalii
102.
Mheshimiwa Spika, katika kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa maduhuli yanayotokana na sekta ya
utalii na mazao ya misitu, Serikali inapendekeza ukusanyaji wa maduhuli
hayo ufanywe na Mamlaka ya Mapato Tanzania na mapato hayo yaingie katika Mfuko
Mkuu wa Hazina. Utekelezaji wa hatua hii utahusisha marekebisho katika Sheria
ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, Sura 399, Sheria ya Hifadhi ya Mamlaka ya
Ngorongoro, Sura 284, Hati ya Kuanzisha Mamlaka ya
Hifadhi ya Wanyamapori ya mwaka 2014, na Sheria ya Hifadhi za Taifa, Sura
282 kupitia Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2020 (The Finance Bill, 2020) ili:
(i)
Kuipa TRA mamlaka kisheria ya kukusanya
maduhuli yanayokusanywa hivi sasa na Shirika la Hifadhi za
Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), na Mamlaka ya Hifadhi
ya Wanyamapori (TAWA);
(ii)
Kuweka sharti la kisheria ili kuwezesha
maduhuli yatakayokusanywa na TRA yahifadhiwe Mfuko Mkuu wa Hazina badala ya
utaratibu wa sasa unaoruhusu taasisi hizi kubaki na mapato yake;
(iii)
Kuweka utaratibu wa kisheria kwa taasisi hizo
kutumia utaratibu wa bajeti ya Serikali na kuondoa mfumo wa kibajeti unaotumiwa
na taasisi hizo kwa sasa.
(p)
Marekebisho madogo
madogo katika baadhi ya Sheria za Kodi na
Sheria nyingine mbalimbali.
103. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho mengine madogo madogo yasiyo ya kisera katika sheria mbalimbali za kodi pamoja na sheria nyingine ili ziwe sanjari na azma ya kurahisisha
utekelezaji wake.
(q)
Tarehe ya Kuanza
Kutekeleza Hatua Mpya za Kodi.
104.
Mheshimiwa Spika, hatua hizi za kikodi zinazopendekezwa zitaanza kutekelezwa tarehe 1 Julai,
2020, isipokuwa pale itakapoelezwa vinginevyo. Aidha, Marekebisho hayo yataainishwa katika Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2020 na Matangazo ya Serikali (Government Notices).
VI. SURA YA BAJETI KWA
MWAKA 2020/21
105.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia shabaha, malengo
pamoja na sera za bajeti kwa mwaka 2020/21, Sura ya Bajeti inaonesha kuwa jumla
ya shilingi trilioni 34.88 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika kipindi
hicho. Jumla ya mapato ya ndani (ikijumuisha mapato ya Halmashauri)
yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 24.07, sawa na asilimia 69.0 ya bajeti
yote. Kati ya mapato hayo, Serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla
ya shilingi trilioni 20.33; mapato yasiyo ya kodi ya shilingi trilioni 2.92 na
mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri shilingi bilioni 815.0.
106.
Mheshimiwa
Spika, Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 4.90 kutoka soko la
ndani. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 3.32 ni kwa ajili ya kulipia
hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na kiasi cha Shilingi trilioni
1.59 sawa na asilimia 1.0 ya Pato la Taifa ni mikopo mipya kwa ajili ya
kugharamia miradi ya maendeleo. Aidha, shilingi trilioni 3.04 zinatarajiwa
kukopwa kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara kwa lengo la kuongeza
kasi katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu.
107.
Mheshimiwa Spika, Washirika wa Maendeleo wanatarajia
kuchangia misaada na mikopo nafuu yenye jumla ya shilingi trilioni 2.87 ambayo
ni asilimia 8.2 ya bajeti. Kati ya kiasi hicho, miradi ya maendeleo ni shilingi
trilioni 2.46; Mifuko ya Pamoja ya Kisekta shilingi bilioni 138.3; na Misaada
na Mikopo nafuu ya Kibajeti (General Budget Support-GBS) shilingi
bilioni 275.5.
108.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2020/21, Serikali
inapanga kutumia jumla ya shilingi trilioni 34.88 kwa matumizi ya kawaida na
maendeleo. Kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 22.10 zimetengwa kwa ajili ya
matumizi ya kawaida sawa na asilimia 63 ya bajeti na shilingi trilioni 12.78
kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Fedha zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya
kawaida zinajumuisha shilingi trilioni 10.48 kwa ajili ya ulipaji wa deni la
Serikali, shilingi trilioni 7.76 kwa ajili ya mishahara na shilingi trilioni
3.74 kwa ajili ya Matumizi Mengineyo (OC) ambayo yanajumuisha shilingi bilioni
481.9 kwa ajili ya matumizi yatokanayo na vyanzo vya ndani vya Halmashauri.
109.
Mheshimiwa Spika, matumizi ya maendeleo ni shilingi
trilioni 12.78, ambayo ni sawa na asilimia 37 ya bajeti yote na yanajumuisha fedha
za ndani shilingi trilioni 10.04 na fedha za nje shilingi trilioni 2.74. Kati
ya fedha hizo, shilingi trilioni 2.10 ni kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa reli
kwa kiwango cha Standard Gauge; shilingi trilioni 1.60 ni kwa ajili ya
mradi wa kufua umeme Mto Rufiji; shilingi bilioni 823.7 ni kwa ajili ya mifuko ya Reli, Maji na
REA; shilingi bilioni 490 ni kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu;
na shilingi bilioni 298.1 kwa ajili ya elimumsingi bila ada. Aidha, Serikali
imetenga jumla ya shilingi bilioni 600.0 kwa ajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa
ya watumishi, watoa huduma na makandarasi wa barabara, maji na umeme.
110. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia
mfumo wa bajeti kama nilivyoeleza, sura ya bajeti kwa mwaka 2020/21 ni kama
inavyooneshwa katika Jedwali A.
Jedwali A: Mfumo wa Bajeti ya Mwaka
2020/21
Chanzo:
Wizara ya Fedha na Mipango
VII.
SHUKRANI
111. Mheshimiwa Spika, tofauti na ilivyozoeleka naomba nianze salamu
za shukrani kwa kutoa pole kwa Watanzania waliopatwa na majanga mbalimbali na
misiba, nikianza na Bunge ambalo liliwapoteza wenzetu, Mheshimiwa Rashid Ajali
Akbar, aliyekuwa Mbunge wa Newala vijijini (CCM), Mheshimiwa Mchungaji Dkt.
Getrude Pangalile Rwakatare, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mheshimiwa
Richard Mganga Ndasa aliyekuwa Mbunge wa Sumve (CCM) na Mheshimiwa Balozi Dkt.
Augustine Philip Mahiga, aliyekuwa Mbunge wa kuteuliwa (CCM) na Waziri wa
Katiba na Sheria. Ninawashukuru wote hawa kwa mchango wao mkubwa kwa Taifa na
tunamwomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu wote mahali pema peponi.
Amina! Aidha, natoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza
wapendwa wao kutokana na majanga mbalimbali ikiwemo homa kali ya mapafu
inayosababishwa na virusi vya CORONA. Natumia nafasi hii kuwashukuru
watu wote walio katika mstari wa mbele kupambana na ugonjwa huu ikiwa ni pamoja
na: Madaktari na wahudumu wa afya; timu ya Serikali ya uratibu; na wadau
mbalimbali ambao kwa namna moja au nyingine wamechangia fedha na vifaa kusaidia
katika mapambano haya. Aidha, napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru viongozi
wote wa dini zetu zote kwa kuendelea kuiombea nchi yetu amani, umoja na
mshikamano wa Kitaifa.
112. Mheshimiwa Spika, niwashukuru pia wananchi
wenzangu wa Wilaya za Buhigwe na Kasulu na mkoa wetu wa Kigoma kwa ujumla ambao
walinilea na kunifunda kufanya kazi kwa bidii. Pia naendelea kuwashukuru
wananchi wa vijiji vya Nzinje (Zuzu) na Mayamaya hapa Dodoma kwa kunipokea mimi
na familia vizuri sana. Aidha, naishukuru familia yangu, hususan mke wangu
Mbonimpaye kwa kuniombea na kunipa raha na utulivu nyumbani na hivyo kuniwezesha
kutekeleza majukumu yangu ipasavyo. Shukrani zangu pia, kwa wanangu, wajukuu,
ndugu zangu, majirani na marafiki wote wa familia kwa kunivumilia, kunibariki
na kunitia moyo.
113. Mheshimiwa Spika, ninawashukuru viongozi na
watumishi wenzangu wa Wizara ya Fedha na Mipango, kwa ushirikiano mkubwa
walionipa na kwa kujituma katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara na
maandalizi ya bajeti hii ya Watanzania. Kipekee ninamshukuru Mheshimiwa Dkt.
Ashatu K. Kijaji, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Jimbo la Kondoa.
Nawasihi wananchi wa Kondoa wamrudishe mama huyu kwa kura za kishindo katika
Bunge lijalo; Ninamshukuru sana Katibu Mkuu HAZINA na Mlipaji Mkuu wa Serikali,
Doto M. James, pamoja na Naibu Makatibu Wakuu, Amina Kh. Shaaban, Adolf H.
Ndunguru na Mary N. Maganga pamoja na watumishi wa kada zote wa Wizara ya Fedha
na Mipango. Nawakumbusha mwendelee kuchapa kazi. Ninawapenda na Mungu
awabariki. Aidha, ninamshukuru Profesa Florens D. Luoga, Gavana wa Benki Kuu ya
Tanzania kwa kusimamia sekta ya fedha kwa ustadi pamoja na Naibu Gavana wote
watatu (Dkt. Yamungu Kayandabila, Dkt. Bernard Kibesse na Bw. Julian R. Banzi).
Pia namshukuru Dkt. Edwin Mhede Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) na Naibu wake Bw. Msafiri Mbibo kwa kuvunja rekodi ya ukusanyaji wa
mapato ya Serikali. Vile vile,
namshukuru CPA Charles E. Kichere, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali kwa kazi nzuri ikiwa ni pamoja na kukagua mashirika yetu makubwa kwa
kutumia wataalam wa ndani kwa mara ya kwanza na CPA Athumani S. Mbuttuka, Msajili
wa Hazina kwa kuvunja rekodi ya ukusanyaji wa gawio na michango ya mashirika
kwenye Mfuko Mkuu. Ninamshukuru pia Dkt. Albina A. Chuwa, Mtakwimu Mkuu wa
Serikali kwa kusimamia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) vizuri.
114. Mheshimiwa Spika, kwa dhati kabisa, napenda
kuchukua fursa hii kuwashukuru Washirika wetu wa Maendeleo kwa misaada na
mikopo nafuu wanayoendelea kutupatia katika kutekeleza miradi na programu
mbalimbali za maendeleo nchini. Katika bajeti ya mwaka 2020/21, Washirika wa Maendeleo
kwa pamoja wanatarajia kuchangia jumla ya shilingi trilioni 2.87. Washirika
wanaotarajiwa kuchangia bajeti ya Serikali ni pamoja na: nchi wahisani
ikijumuisha Canada, China, Denmark, Finland, India, Ireland, Italia, Japan,
Korea ya Kusini, Marekani, Norway, Poland, Sweden, Ubelgiji, Ufaransa,
Uholanzi, Ujerumani, Uingereza, na Uswisi. Aidha,
yapo mashirika ya fedha ya kimataifa yakiwemo: Benki ya Maendeleo ya Afrika
(AfDB), Benki ya Dunia, Arab Bank for Economic Development in Afrika (BADEA),
Global Fund, Kuwait Fund, Abu Dhabi Fund, Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU), Benki
ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB), OPEC Fund, Global Environmental Facility (GEF),
Shirika la Mapinduzi ya Kijani Afrika (AGRA), Mfuko wa kukinga Hatari ya
Kimazingira (GRMF), Climate Development Special Fund, African Legal Support
Facility (ALSF), Dignity, Global Agriculture and Food Security Program
(GAFSP),na Mashirika ya Umoja wa Mataifa yakiwemo UNICEF, IFAD, UNDP, UNFPA,
Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), na United Nations Environment Programme
(UNEP). Napenda pia kutambua ushirikiano mzuri tulionao na Shirika la Fedha la
Kimataifa (IMF). Ni matarajio yetu kuwa misaada ya kiufundi na fedha
zilizoahidiwa na marafiki zetu hawa zitatolewa kwa wakati na kwa kiasi
kilichoahidiwa. Nasi, kwa upande wa Serikali tunaahidi kusimamia ipasavyo
matumizi ya fedha hizo kama ilivyokusudiwa.
115. Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii
kutoa shukrani za dhati kwa Katibu Mkuu Kiongozi Mheshimiwa Balozi Mhandisi
John William Kijazi, Waheshimiwa Mawaziri wa SMT na SMZ, Mheshimiwa Mwanasheria
Mkuu wa Serikali Prof. Adelardus Kilangi, Naibu Mawaziri, Wakuu wa Mikoa,
Makatibu Wakuu, Katibu wa Bunge Bw. Stephen Kagaigai, Mtendaji Mkuu wa Mahakama
Bw. Mathias Kabunduguru, Naibu Makatibu Wakuu pamoja na watumishi wote wa
Wizara, Idara Zinazojitegemea, Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Taasisi na
Mashirika ya Umma kwa kazi zao nzuri za kuwatumikia wananchi katika maeneo yao
na kwa ushirikiano mkubwa sana walionipa mimi na watumishi wenzangu wa Wizara
ya Fedha na Mipango katika kutekeleza majukumu ya msingi ya Wizara hii.
116. Mheshimiwa Spika, Napenda pia nitumie fursa
hii kumpongeza na kumshukuru kwa dhati Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Bajeti Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Jimbo la Maswa
Magharibi, kwa kuongoza shughuli za Kamati hii muhimu kwa umahiri mkubwa. Ninawashukuru
wajumbe wote wa Kamati ya Bajeti. Ninakiri kuwa wakati wote wametupatia maoni
na ushauri makini ambao umeisadia Serikali katika kuimarisha utekelezaji wa
bajeti na mpango wa maendeleo wa Taifa na katika kuboresha mapendekezo ya
bajeti hii. Kati yao ninawaombea wale wenye sare za kijani wapate ushindi usio
na shaka katika majimbo yao ili warejee katika Bunge lijalo.
117. Mheshimiwa Spika, napenda niwapongeze na
kuwashukuru kwa dhati wakuu wote wa vyombo vya ulinzi na usalama, makamanda na
askari wote kwa uzalendo na nidhamu ya hali ya juu. Naomba niwataje Mkuu wa
Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo; Inspekta
Jenerali wa Polisi, Simon Nyakoro Sirro; Kamishna Jenerali wa Magereza,
Suleiman Mungiya Mzee; Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Peter Makakala;
Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji, John William Hasunga; Mkurugenzi wa
Usalama wa Taifa, Diwani Athuman Msuya; Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa, Brigedia John Julius Mbungo; na Kaimu Kamishna Jenerali wa
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, James Wilbert Kaji. Hakika,
Watanzania tunatembea kifua mbele na kutekeleza shughuli mbalimbali za kijamii na
kiuchumi bila wasiwasi kutokana na umahiri wa vyombo vyetu vya ulinzi na
usalama.
118. Mheshimiwa Spika, nampongeza Dkt. Bashiru Ally
Kakurwa, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa utendaji wake makini
hususan katika kusimamia misingi ya Chama Cha Mapinduzi, kuimarisha umoja,
mshikamano na kutetea haki za wanyonge. Aidha, naipongeza Sekretarieti ya
Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa kuendelea kusimamia na kufuatilia utekelezaji
wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 uliozaa matokeo ya kishindo niliyoeleza
hapo awali.
119. Mheshimiwa Spika, napenda kutumia nafasi hii
kuwapongeza waheshimiwa Marais wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa mzee Ally Hassan Mwinyi, Mheshimiwa mzee Benjamin William Mkapa na
Mheshimiwa mzee Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na wenzi wao kwa mchango
mkubwa waliotoa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Taifa letu na
tunaendelea kunufaika na busara na hekima za wazee hawa katika kusukuma mbele
gurudumu la maendeleo.
120. Mheshimiwa Spika, nakushukuru pia wewe binafsi
Mhe. Job Yustino Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Mbunge wa Jimbo la Kongwa bila kumsahau Naibu Spika Mheshimiwa Dkt. Tulia
Ackson kwa kuendesha Bunge kwa umahiri mkubwa wakati wote na kwa ubunifu wako
hadi kulifikisha Bunge kuwa la kidigitali. Kadhalika, ninampongeza sana
Mheshimiwa Profesa Ibrahim Hamisi Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania pamoja na
Mheshimiwa Dkt. Eliezer Feleshi, Jaji Kiongozi kwa uongozi makini na mahiri wa mhimili wa
Mahakama.
121. Mheshimiwa Spika, kwa umuhimu wa kipekee
nawapongeza na kuwashukuru waheshimiwa wenzi wa viongozi wakuu wa kitaifa,
Mwalimu Janet Magufuli, Bwana Ameir Hafidh Ameir, Mama Mwanamwema Shein,
Mwalimu Mary Majaliwa, Dkt. Fatuma Ramadhani Mganga, na Mama Marina
Papadopoulos Juma kwa kuwawezesha viongozi wetu wakuu wa kitaifa kutekeleza
vizuri majukumu yao kwa utulivu.
122. Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza na kumshukuru
Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Mbunge wa Jimbo la Ruangwa kwa kusimamia bila kuchoka shughuli za Serikali. Ni
mchapa kazi, muungwana na mnyenyekevu ambaye kwenye vikao anavyoviongoza vya
Baraza la Kazi anajishusha kwa kutuita sisi “Mawaziri wenzangu’’. Kwa heshima
na taadhima rai yangu kwa wananchi wa Ruangwa ni kuwa wampitishe Mheshimiwa
Kassim Majaliwa bila kupingwa katika Uchaguzi Mkuu ujao. Aidha, napenda
kumshukuru Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
kwa kazi nzuri na ushauri wake kwa Rais wa Zanzibar. Naomba pia nimpongeze kipekee
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi kwa kuendelea kuiongoza Zanzibar kwa hekima na uadilifu, hali ambayo
imewaletea wananchi wa Zanzibar umoja, utulivu na maendeleo ya kijamii na
uchumi katika kipindi chote cha uongozi wake. Tunamwombea maisha ya amani baada
ya kukabidhi kijiti kwa Rais wa Zanzibar atakayefuata. Vile vile, natoa
shukrani za kipekee kwa Mheshimiwa mama Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hekima na mfano maridhawa wa uwezo mkubwa
wa wanawake katika uongozi ambao umechangia mafanikio tuliyoyapata katika
kujenga nchi yetu na kuimarisha Muungano wetu.
123.
Mheshimiwa Spika, kabla ya kuhitimisha
hotuba hii, naomba kutoa ushuhuda wangu juu ya Mhe. Dkt John Pombe Joseph Magufuli,
Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Natanguliza kuomba msamaha wake kama baadhi
ya haya nitakayosema asingependa niyaseme hapa. Nimeamua niyaseme kwa ajili ya
kumbukumbu lakini zaidi ili watanzania wajue waziwazi mkuu wa nchi tuliyenaye
hivi sasa ni kiongozi wa namna gani ili itusaidie wote kutambua na kutimiza
wajibu wetu kwa Taifa letu la Tanzania.
124.
Mheshimiwa Spika,
Baba huyu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ni kiongozi mwenye maono
na uwezo mkubwa. Aidha, ana kipaji cha hali ya juu cha kufanya yasiyowezekana (ability
to make the impossible happen)! Ni kiongozi ambaye anafahamu vema kuwa ili
nchi ifanikiwe kuleta mabadiliko chanya ni lazima kuvunja kabisa utaratibu wa
kufanya kila kitu kwa mazoea (break the status quo in order to break
through). Ni jemadari anayetambua vema kwamba bila jasho hakuna tuzo (no
pain, no gain) na huu ndiyo msingi wa kauli mbiu ya HAPA KAZI TU! Ni
kiongozi jasiri ambaye anajiamini na ana ndoto kubwa kwa maendeleo ya nchi (has
no room for small dreams), tena hana woga wa kushindwa (has guts to
conquer the fear of failure). Kwa sababu hizo amekuwa akituasa watanzania
tubadilike na kujiamini. Kwa maneno yake mwenyewe amekuwa akituambia
"watanzania tunaweza, Tanzania siyo masikini".
125.
Mheshimiwa Spika,
tangu mwanzo wa utawala wake Rais Magufuli amepambana na rushwa na ufisadi bila
kigugumizi. Amevunjavunja mazoea ya udanganyifu uliokuwa umekithiri kila kona
kama vile watumishi hewa, mishahara na posho kwa watumishi vizuka, mikopo kwa
wanafunzi ambao hawapo, madai ya kugushi ya pembejeo na marejesho ya kodi ya
ongezeko la thamani. Rais huyu ni mfuatiliaji makini, tena kwa takwimu, wa kila
kinachoendelea katika kila eneo la utawala. Rais Magufuli alijipa kazi ya
kutumbua majipu na ameifanya kazi hiyo bila kupepesa macho ndani ya Serikali na
hata ndani ya CCM. Ni dhahiri kwangu kuwa Rais Magufuli ni muumini wa
mafundisho ya uongozi ya Peter Ferdinand Drucker (ingawa sina hakika kama Rais
wetu alisoma maandishi ya mtaalam huyo mashuhuri) kwamba, naomba kunukuu kwa
Kiingereza "It is the duty of the executive to remove ruthlessly anyone
- and especially any manager - who consistently fails to perform with high
distinction. To let such a man stay on corrupts others". Tafsiri yake
ni kuwa ni wajibu wa mtendaji mkuu kumuondoa bila huruma mtumishi yeyote - na
hasa meneja yeyote - ambaye daima anashindwa kutekeleza kazi zake kwa kiwango
cha kupata nishani. Kuacha mtu kama huyo aendelee kazini inashawishi wengine
kufanya vibaya!
126.
Mheshimiwa Spika,
kiongozi wetu mkuu amesimamia kwa karibu nidhamu ya matumizi katika wizara,
idara na taasisi za Serikali Kuu na Mamlaka za Serikali za Mitaa ikiwa ni
pamoja na kudhibiti safari za watumishi wa umma nje ya nchi, hata yeye mwenyewe
hajasafiri nje ya Bara la Afrika tangu alipochukua hatamu za uongozi wa nchi
hadi sasa; amefuta baadhi ya sherehe za kitaifa na kuelekeza fedha zilizokuwa
zimepangwa zitumike kwenye maeneo mengine yenye uhitaji mkubwa; na alipiga
marufuku "MKUKUBI". Kwa wasiofahamu MKUKUBI ni kifupi cha kilichokuwa
kinaitwa kininja kama 'Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Binafsi'
kupitia posho za kwenye makongamano, semina na warsha zilizokuwa zinafanyika
kwenye kumbi za kukodi na hoteli. Aidha, alipunguza misafara mirefu ya
kusindikiza viongozi kwenda kwenye matibabu au kupima afya zao nje ya nchi huku
wakiacha hospitali ya Taifa ya Muhimbili na hospitali za rufaa nchini zikiwa
zinadidimia. Mtakumbuka pia alichukua hatua isiyotarajiwa ambayo iliduwaza watu
wengi na hata kupelekea wengine kumlaumu pale alipoamua kumpeleka mke wake (First
Lady) hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu ambapo alilazwa kwa siku
kadhaa badala ya kumpeleka nje!
127.
Mheshimiwa Spika,
Rais Magufuli ni Jemadari mwenye msimamo usiotetereka hata kwenye kilele cha
hatari (crisis) kama wakati wa malalamiko kuwa "vyuma
vimebana", pia katika kipindi cha uhaba wa mafuta ya kula na hivi karibuni
wakati watawala wengine wakilazimisha wananchi wao kubakia majumbani (Lock
down) ili kukabiliana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu (COVID - 19),
kwa mshangao wa wengi Rais Magufuli aliagiza watanzania waendelee kuchapa kazi,
na wazingatie maelekezo ya wataalam wa afya kujikinga na CORONA huku
wakiendelea kumwomba Mungu! Aidha, katika nafasi yake ya Amiri Jeshi Mkuu,
ameendelea kiliamini Jeshi, kulijengea uwezo na kulishirikisha katika miradi
mbalimbali ya kimkakati ya ujenzi wa uchumi wa nchi yetu.
128.
Mheshimiwa Spika,
katika kipindi cha utawala wake Rais Magufuli ameendelea kumtanguliza Mungu
katika kazi zake na kuwaelekeza viongozi anaowateua na wananchi kwa ujumla nao
wafanye hivyo hivyo. Ameonesha
unyenyekevu na ukarimu sehemu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuenzi mchango wa
awamu za uongozi zilizotangulia, kuchangia ujenzi wa nyumba za ibada (misikiti
na makanisa), kukusanya sadaka kanisani yeye mwenyewe, kushiriki misiba ikiwa
pamoja na ile inayogusa viongozi wa vyama vya upinzani, kutembeza sinia lenye
vitafunio vya chai pale ikulu Dar es Salaam na Chamwino kwa ajili ya wageni
wake, na kunywa kahawa au kununua bidhaa na matunda kutoka kwa wajasiriamali
wadogo. Rais Magufuli ana huruma na anaumizwa na kilio na machozi ya wanyonge
au waliodhulumiwa na hasiti kuwafuta machozi hapo hapo. Ni kwa mantiki hiyo
kiongozi wetu huyu amewatembelea wafungwa magerezani kujionea hali halisi na
kuongea nao na kufanya uamuzi wa kusamehe idadi kubwa sana ya wafungwa na
mahabusu. Kama hiyo haitoshi, baba huyu ameendeleza moyo wake wa msamaha hata
kwa waliombeza na kumtusi!
129.
Mheshimiwa Spika,
Kiongozi wetu mkuu ni mzalendo namba moja ambaye amevaa koti la Baba wa Taifa
hayati Mwalimu Julius K. Nyerere na kufufua ndoto zake za maendeleo ya Taifa
letu. Alianza kwa kupiga vita rushwa na ukwepaji kodi vilivyokuwa vimekithiri
bandarini na TRA na kufanikiwa kuongeza ukusanyaji wa mapato ya kodi kutoka
wastani wa shilingi bilioni 825 kwa mwezi kabla ya utawala wake hadi wastani wa
shilingi trilioni 1.5 kwa mwezi katika mwaka 2019/20; Aidha alielekeza mikataba
ya madini na huduma muhimu kama mawasiliano ipitiwe upya na kutunga Sheria ya
Mamlaka ya Nchi Kuhusiana na Umiliki wa Maliasili ya mwaka 2017 ili kulinda
rasilimali za Taifa na kuhakikisha watanzania wananufaika, na kujenga uzio
wenye urefu wa kilometa 24.5 kuzunguka mgodi wa madini ya tanzanite Mirerani na
kuanzisha masoko ya madini; Aidha, aliamua kutekeleza maamuzi ya kikao cha
Halmashauri Kuu ya Chama cha TANU kilichofanyika tarehe 30 Agosti hadi tarehe 1
Septemba mwaka 1973 kuhamisha makao makuu ya Serikali kutoka Dar es Salaam kuja
hapa Dodoma.
130.
Mheshimiwa Spika,
Rais wetu Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli amethubutu kutekeleza miradi
mikubwa ya kielelezo iliyobuniwa na Baba wa Taifa ikiwa ni pamoja na bwawa la
Nyerere la kuzalisha umeme wa MW 2,115 katika mto Rufiji; kujenga uchumi wa viwanda;
kujenga reli ya kati ya kisasa (Standard Gauge Railway); kufufua Shirika
la Ndege la Tanzania kwa kununua ndege mpya 11 na kujenga viwanja vya ndege;
kuendeleza ujenzi wa barabara kuu na za mikoa kwa kiwango cha lami na madaraja
makubwa; kununua meli mpya za abiria na mizigo na kukarabati zile za zamani na
vivuko pamoja na kupanua au kuboresha bandari katika ukanda wa bahari na maziwa
makuu; kutoa elimumsingi (shule ya msingi hadi kidato cha nne) bila ada na
kuongeza mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu;
mradi kabambe wa kupeleka umeme vijijini (REA) ambapo hadi sasa vijiji
9,112 kati ya vijiji 12,268 vya Tanzania Bara (asilimia 74.3) vimeunganishiwa
umeme; ameendelea kupiga vita adui maradhi kwa kuimarisha huduma za afya nchini
kama ilivyoelezwa kwa kirefu katika taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa
niliyosoma leo asubuhi.
131.
Mheshimiwa Spika,
Rais wetu huyu ana akili ya kisayansi ya kudadisi na kuhoji kila jambo ikiwa ni
pamoja na usahihi wa vipimo vya mafuta ghafi ya kula na hata ugonjwa wa CORONA.
Rais Magufuli amekuwa mfano bora wa kutumia na kuenzi lugha ya kiswahili hata
kufikia kuwa moja ya lugha zilizokubalika kutumika katika Jumuiya ya Nchi za
Kusini mwa Afrika SADC.
132.
Mheshimiwa Spika,
Rais Magufuli ni kiongozi anayetuhimiza watanzania kuwa wamoja na kusisitiza
kuwa maendeleo hayana chama. Mheshimiwa Rais Magufuli ana nidhamu kubwa ya
kufanya kazi (relentless work ethic). Waheshimiwa mawaziri wenzangu
wanafahamu vizuri simu zake za usiku wa manane kuanzia saa 8 hadi saa 11
alfajiri! Kwa sababu hiyo baadhi yetu ilitubidi kubadilisha hata muda wa kulala
usingizi! Hii ilinikumbusha maneno ya Shimon Peres aliyekuwa Waziri Mkuu wa
Israel kwa mawaziri wake kwamba wakati wa vita, waziri wa Israel hana budi
kutosinzia... Ni wajibu wake kubaki macho! (An Israel Minister shouldn’t
sleep ... It is a minister's duty to stay awake).
133.
Mheshimiwa Spika,
mwisho, japo si kwa umuhimu Rais wetu ni mkakamavu na mpenzi wa maendeleo ya
michezo nchini. Mnafahamu katika ubora wake, mazoezi ya push-ups
anazopiga usiige! Mtakumbuka pia jinsi alivyowaalika ikulu Dar es Salaam vijana
wetu wa timu ya Taifa wenye umri chini ya miaka 17 na makocha wao ili
kuwajengea ari ya utaifa na kushinda. Aidha, naamini hamjasahau siku Mhe. Magufuli
alipokwenda uwanja wa Taifa kujionea mpambano wa watani wa jadi Yanga na Simba
na kushuhudia mnyama akipigwa mkuki mmoja wa sumu kali na Benard Morrison!
Inaonekana Mheshimiwa Waziri Mkuu, na wewe Mheshimiwa Spika na hata Mheshimiwa
Naibu Spika machale yaliwacheza mapema siku hiyo hamkuonekana uwanjani!!
134.
Mheshimiwa Spika,
huo ndio ushuhuda wangu juu ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais
wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha
Mapinduzi Taifa, na ushuhuda wangu ni wa kweli. Swali ambalo napenda kila
Mtanzania ajiulize ni: Je, mimi na wewe tunatimiza kikamilifu wajibu wetu kwa
nchi yetu? Kisha achukue hatua. Mojawapo ya suala ambalo nataka kuwaomba kwa
unyenyekevu mkubwa, ni kwamba watanzania wote tuliojiandikisha kupiga kura
katika uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba 2020 tumpe zawadi ya kura ya NDIYO Rais
huyu ambaye amekuwa mfano wa kuigwa na wa kipekee katika bara la Afrika kama
shukrani yetu kwake kwa kazi yake iliyotukuka ili aendelee kuipaisha nchi yetu
ya Tanzania kwa kipindi cha pili cha miaka mitano. Watanzania msisahau pia
kumpatia Rais wetu wabunge na madiwani wanaomudu maadili na mwendo wa HAPA KAZI
TU, na kama itawapendeza wananchi wenzangu wa Buhigwe na Chama chetu, basi iwe
pamoja na mimi mtumishi wenu! Nawaambia kweli watanzania wenzangu, Rais huyu ni
tunu ya thamani kubwa kwa Tanzania na utawala wake ni fursa kubwa ambayo kama
hatutaitumia vizuri, basi mjue itachukua miaka mingi ijayo kuifikia Tanzania mpya
tunayoitamani. Na kwa mheshimiwa Rais, najua unafuatilia hotuba hii, sina
maneno mazuri ya kukushukuru kwa kuniinua, kunipa heshima kubwa ya kulitumikia
Taifa katika Serikali yako na kwa kuniongoza vizuri katika utumishi huu.
Mwenyezi Mungu akubariki, akulinde, akufadhili na kukupa amani wewe na familia
yako.
VIII.
HITIMISHO
135.
Mheshimiwa Spika, hii ni
hotuba yangu ya mwisho katika Bunge hili ambayo imeeleza mwenendo wa
utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/20, mafanikio ya kishindo
yaliyopatikana na hatua muhimu ambazo Serikali inakusudia kutekeleza katika
mwaka 2020/21.
136. Mheshimiwa Spika, kwa kipindi hiki cha miaka 4 na
miezi 5 ambacho nimepewa heshima na dhamana kubwa wa kuwa Waziri wa Fedha na
Mipango wa nchi yetu, nina jambo moja tu la kusema kwa watanzania: ASANTENI
SANA!
Ninasema asanteni sana kwa sababu
watanzania wengi nje na ndani ya Serikali wamekuwa wakinitia moyo na
kuniongezea ujasiri wa kufanya kazi hii kwa manufaa ya Tanzania. Hata hivyo,
mimi ni binadamu na kwa hakika siyo mkamilifu. Ninawashukuru kwa dhati wote
walionikosoa kuhusu sera za uchumi na utekelezaji wa bajeti kwa nia ya kujenga
na ninawaomba radhi pale ambapo niliwakwaza katika kutekeleza majukumu yangu lakini
kwa wale wenye maslahi binafsi walioniona mimi ni kikwazo kwao, natumaini sasa
wamenielewa na Mungu awasamehe! Na kwa yale niliyoweza kufanya vizuri sistahili
kupewa sifa peke yangu kwa sababu tuliyafanya pamoja. Napenda niseme mambo
mawili tu ya kuwaaga:
(i)
Kwa yeyote atakayeteuliwa katika nafasi hii baada yangu ajitahidi
kujinyenyekeza kwa kuwa na hofu ya Mungu, asimamie maslahi ya Taifa na haki za
wananchi wanyonge, ashinde vishawishi vya rushwa, azingatie sheria, kanuni na
taratibu zinazo ongoza ukusanyaji wa mapato, ukopaji wa mikopo, upokeaji wa
misaada, ugawaji wa rasilimali fedha na kusimamia matumizi ya Serikali ili yawe
yenye tija na afanye hivyo bila kuyumba. Aidha, ajitahidi kuwa makini
kufuatilia mwenendo wa uchumi wa Taifa na Dunia ili kushauri ipasavyo juu ya
sera na mipango ya kiuchumi na hatua za kuipeleka Tanzania mbele. Katika hili,
atumie ujuzi na uzoefu alio nao lakini pia ashirikiane na kuthamini ushauri wa
wataalam ndani ya Serikali na taasisi zake. Aidha, ni muhimu sana afungue
masikio yake kwa mahitaji ya sekta binafsi na ushauri wa Bunge.
(ii)
Tanzania tuko katika vita ya kiuchumi ambayo ni lazima
tushinde. Hakuna mbadala wa ushindi! Jambo la muhimu ni kwamba hatuna budi
kujitambua, tuwajue vema maadui zetu wa ndani na nje na mbinu wanazotumia na
tujipange kimkakati ikiwa ni pamoja na kuwahi kutumia vema fursa zinazoibuka na
vile vile kuingia ubia na marafiki zetu ambao unanufaisha pande zote. Uwezo wa
kupambana na kushinda vita hivyo tunao, sababu tunazo na nia tunayo. Hata
hivyo, ili tushinde sharti la kwanza: lazima tuendelee kuwa wamoja na kuwa na
uaminifu wa hali ya juu kwa Taifa hususan kulinda maslahi ya Taifa. Sharti la
pili: Kuanzia muhula unaofuata wa Serikali ya Awamu ya Tano na kuendelea ni
lazima pawepo ujasiri na kufanya maamuzi ya kuwekeza kwa kiasi kikubwa kibajeti
kwenye sayansi na teknolojia mpya na ya kisasa kabisa kwa kuibua, kujenga,
kulea na kuthamini vipaji na utaalamu na kwa kipekee kabisa ndani ya majeshi
yetu na vile vile kwenye taasisi za utafiti na ufundi stadi na vyuo vikuu.
Wakati umefika sasa Taifa letu liweke msukumo mahsusi kuamsha fikra bunifu za
watanzania hasa vijana ambazo hazijatumika ipasavyo. Aidha, ni muhimu sekta
binafsi ishiriki kuwekeza katika maendeleo ya sayansi na teknolojia na
ichangamkie fursa zinazoambatana na uwekezaji huo katika sekta zote za
uzalishaji na huduma. Nina hakika pia kuwa Mungu yuko upande wetu kama
tutaendelea kumtegemea. Kwa upande wangu nawahakikishia kwamba nitaona fahari
kuendelea kulitumikia Taifa letu katika Sekta ya umma au Sekta binafsi kadri
Mungu atakavyonituma.
137.
Mheshimiwa Spika,
napenda kumalizia kusoma hotuba yangu ya mwisho ya bajeti kuu ya Serikali kwa
kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa moyo wangu wote kwa ajili ya fadhili zake na
uaminifu wake. Siku niliyomuita aliniitikia, akanifariji kwa kunitia nguvu.
Nitaendelea kumhimidi kila wakati. Mtukuzeni Mungu pamoja nami.
MUNGU IBARIKI
AFRIKA, MUNGU IBARIKI TANZANIA
138.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
Mapendekezo ya Tozo
Mpya za Vibali vya Kusafirisha Nje ya Nchi na Kuingiza Ndani ya Nchi Mifugo na
Mazao (shilingi)
Na.
|
Aina ya Mfugo/Zao
|
Kipimo
|
Kuingiza ndani ya Nchi
|
Kusafirisha nje ya Nchi
|
1
|
Sungura
|
Kila mmoja
|
500
|
5,000
|
2
|
Mbegu
zilizochambuliwa kijinsia
|
Mrija
|
2,000
|
2,000
|
3
|
Sampuli za kibailojia
|
Kwa kibali
|
5,000
|
100,000
|
4
|
Nyama ya kondoo/mbuzi
|
Kilo moja
|
4,000
|
50
|
5
|
Nyama ya
nguruwe
|
Kilo moja
|
4,000
|
20
|
6
|
Nyama ya Wanyama pori
|
Kilo moja
|
4,000
|
500
|
7
|
Nyama ya punda
|
Kilo moja
|
5,000
|
1,000
|
8
|
Soseji
|
Kilo moja
|
4,000
|
50
|
9
|
mjeledi/misuli
|
Kilo moja
|
150
|
150
|
10
|
Bidhaa
zingine za nyama
|
Kilo moja
|
1,000
|
150
|
11
|
Vifungashio
vya soseji
|
Kibali
|
50,000
|
0
|
12
|
Maziwa condensed
|
Lita moja
|
2000
|
100
|
13
|
Maziwa
yaliyotolewa mafuta
|
Lita moja
|
2,000
|
100
|
14
|
Maziwa mtindi
|
Lita moja
|
2,000
|
50
|
15
|
Maziwa ya
unga
|
Kilo moja
|
2,000
|
100
|
16
|
Jibini / siagi
|
Kilo moja
|
2,000
|
20
|
17
|
Nyongo
|
Kibali
|
100,000
|
300,000
|
18
|
Mbolea ya
asili
|
Tani moja
|
5,000
|
5,000
|
19
|
Kemikali na
vifaa vya maabara
|
Kibali
|
100,000
|
100,000
|
20
|
Kitotoleshi
|
Kibali
|
50,000
|
10,000
|
21
|
Vitamini/mawe ya madini/amino
acids/ vyakula vilivyoongezewa virutubisho
|
Tani moja
|
10,000
|
10,000
|
22
|
Vifaa vya
utambuzi hereni za sikoni)
|
Kibali
|
50,000
|
NIL
|
23
|
Mawe ya
kwenye nyongo
|
Kibali
|
10,0000
|
300,000
|
24
|
Kuongeza muda
ya leseni ambayo imepita muda
|
Kibali
|
50,000
|
50,000
|
25
|
Mikojo ya
wanyama
|
Kibali
|
5,000
|
5,000
|
26
|
Asali
|
Kibali
|
200,000
|
100,000
|
27
|
Mbwa na paka
kwa ajili ya vinasaba kwa ajili ya utafiti
|
Kila mmoja
|
5,000
|
3,000
|
28
|
Kuku au ndege
wafugwao kwa ajili ya vinasaba na utafiti
|
Kila mmoja
|
200
|
1,000
|
29
|
Wanyama kwa
ajili ya mapambo
|
Kibali
|
20,000
|
20,000
|
Kiambatisho Na.6
Mapendekezo ya Kutoza
Kibali kwa Ajili ya Huduma kwa Mifugo na Mazao Yake Wanaopita Nchini Kwenda Nje
ya Nchi (shilingi)
S/N
|
Aina ya Mfugo/zao
|
Kipimo
|
Tozo (Tshs)
|
1
|
Ng’ombe
|
Kila mmoja
|
2,500
|
2
|
Kondoo/mbuzi
|
Kila mmoja
|
1,500
|
3
|
Nguruwe
|
Kila mmoja
|
1,500
|
4
|
Farasi / Mule
/ Punda
|
Kila mmoja
|
2,500
|
5
|
Mbwa/paka
|
Kila mmoja
|
1,000
|
6
|
Ngamia
|
Kila mmoja
|
2,500
|
7
|
Kuku / Kanga
|
Kila mmoja
|
200
|
8
|
Vifaranga
|
100
|
1,000
|
9
|
Zaidi ya trei
100 za mayai ya kula
|
Trei la mayai
30
|
500
|
10
|
Zaidi ya trei
10 za mayai ya kutotolea
|
Kila mmoja
|
1,000
|
11
|
Bata mzinga
|
Kila mmoja
|
1000
|
12
|
Kasuku/falcon/Mbuni
|
Kila mmoja
|
15,000
|
13
|
Ndege wa
porini
|
Kila mmoja
|
500
|
14
|
Sungura
|
Kila mmoja
|
500
|
15
|
Vyura/ mijusi
/ wadudu
|
Kibali
|
20,000
|
16
|
Wanyama wa
maabara
|
Kibali
|
30,000
|
17
|
Wanyama wa
porini
|
Kila mmoja
|
1,000
|
18
|
Nyara za
Serikali
|
Kibali
|
30,000
|
19
|
Nyama na
mazao yake zaidi ya kilo 50
|
Kilo
|
50
|
20
|
Soseji /
nyama ya kusaga/ bidhaa zingine za nyama
|
Kilo
|
50
|
21
|
Nyongo
|
Kibali
|
50,000
|
22
|
Korodani/tendons
|
Kibali
|
200,000
|
23
|
Maziwa
|
Lita
|
500
|
24
|
Mtindi
|
Lita
|
2,000
|
25
|
Maziwa ya
unga
|
Kilo
|
4,000
|
26
|
Jibini /
siagi
|
Kilo
|
2,000
|
27
|
Ngozi ya
ng’ombe
|
Kipande
|
500
|
28
|
Ngozi ya
mbuzi/kondoo
|
Kipande
|
100
|
29
|
Pembe za
ng'ombe, Mbuzi, kondoo, kwato na mifupa
|
Tani
|
10,000
|
30
|
Manyoya /
sufu
|
Kibali
|
20,000
|
31
|
Chakula cha
wanyama
|
Tone
|
10,000
|
32
|
Mbolea ya
kiboni
|
Ton
|
5,000
|
33
|
Embryos
|
Each
|
500
|
34
|
Semen
|
Straws
|
50
|
35
|
Specimen
|
Permit
|
20,000
|
36
|
Maunzi /
vifaa vya maabara
|
Permit
|
300,000
|
37
|
Vifaa vya
utambuzi (mfano hereni za sikioni)
|
Permit
|
200,000
|
Kiambatisho Na. 7
Mapendekezo ya
Kupunguza Tozo za Mrabaha wa kusafirisha samaki nje
No.
|
Aina ya Samaki/Zao
|
Tozo ya Sasa (US$)
|
Tozo Pendekezwa (US$)
|
1
|
Minofu ya
samaki
|
0.24
|
0.2
|
2
|
Sangara aliyetolewa kichwa na matumbo
|
0.25
|
0.21
|
3
|
Sangara nzima aliyetolewa matumbo
|
|
0.25
|
4
|
Ngozi ya samaki
|
|
0.15
|
5
|
Dagaa-Victoria
|
0.2
|
0.16
|
6
|
Dagaa-Tanganyika
|
1
|
0.5
|
7
|
Dagaa-Nyasa
|
0.3
|
0.16
|
8
|
Furu
waliokaushwa
|
0.16
|
0.16
|
9
|
Samaki wakavu
|
0.3
|
0.3
|
10
|
Kayabo,
Ng'onda
|
|
0.3
|
11
|
Migebuka
wabichi
|
0.5
|
0.3
|
12
|
Migebuka
wakavu
|
0.4
|
0.2
|
13
|
Vipande vya
minofu ya sangara
|
0.24
|
0.2
|
14
|
Sangara Wakavu
|
0.3
|
0.2
|
15
|
Makome ya Baharini
|
|
0.075
|
16
|
Kamba miti wasiokuwa na vichwa
|
|
0.9
|
17
|
Kamba miti wenye vichwa
|
|
1.2
|
18
|
Aina ya samaki wengine
|
1
|
0.2
|
19
|
Makome ya Maji baridi
|
|
0.01
|
20
|
Makome (Nyumba za Konokono)
|
|
0.3
|
21
|
Mabondo mabichi
|
5% ya bei ya soko
|
4% ya bei ya
soko
|
22
|
Mabondo
makavu
|
5% ya bei ya
soko
|
4% ya bei ya
soko
|
23
|
Mabondo
mengineyo mabichi/makavu
|
|
0.5
|
Kiambatisho Na 8
Tozo za Viingilio na huduma mbalimbali za makumbusho.
Na.
|
Huduma
|
Kiingilio/Tozo zaa Sasa (Shilingi)
|
Kiingilio
/Tozo Pendekezwa
(Shilingi)
|
Kwa
Watanzania na Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
|
|||
|
|
|
|
1.
|
Kiingilio katika makumbusho
|
|
|
|
i) Mtu mzima
|
1,500
|
2,500
|
|
ii) Mwanafunzi
|
500
|
1,000
|
2.
|
Kiingilio kwa makundi (Group)
|
|
|
|
i)
1-15
|
5,000
|
10,000
|
|
ii)
15-30
|
7,000
|
15,000
|
|
iii)
30-50
|
10,000
|
20,000
|
3.
|
Kazi Miradi (school project)
|
2,000
|
2,500
|
4.
|
Tozo za Tafiti (Research
fee)
|
9,000
|
15,000
|
5.
|
Maktaba /kusoma (studying)
|
1,000
|
2,000
|
6.
|
Picha Mnato (still picture /Video
shooting – educational)
|
130,000
|
300,000
|
7.
|
Picha Mnato (commercial still picture
/Video shooting)
|
260,000
|
500,000
|
8.
|
Huduma za Maktaba (Library services /
Archival pictures)
|
2,000
|
5,000
|
9.
|
Majengo ya maonesho ya muda (Temporary
Exhibition Halls)
|
500,000
|
600,000
|
10.
|
Mifumo ya matangazo kwa umma (Public
Adressing System - PA)
|
250,000
|
300,000
|
11.
|
Jopo la maonesho (Exhibition Panel)
|
10,000
|
20,000
|
12.
|
Maeneo tengefu ya kuona viumbe vya
kale(Special reservation to see original hominids)
|
|
20,000
|
13.
|
Vyumba vya mikutano (Conference Room)
|
700,000
|
750,000
|
kwa
wageni wa kutoka Nje ya Nchi za EAC
|
|||
1.
|
Kiingilio katika makumbusho
|
|
|
|
i) Mtu mzima
|
6,500
|
12,000
|
|
ii) Mwanafunzi (student)
|
2,600
|
6,300
|
2.
|
Kiingilio kwa makundi (Group)
|
|
|
|
i) 1 - 15
|
19,500
|
30,000
|
|
ii) 15 - 30
|
20,000
|
35,000
|
|
iii) 30-50
|
30,000
|
55,000
|
3.
|
Tozo za tafiti (Research fee)
|
$200
|
$300
per month
|
4.
|
Huduma za Maktaba (Library services /
Archival pictures)
|
|
20,000
|
5.
|
Mfumo wa muziki (Music system)
|
250,000
|
300,000
|
6.
|
Kutembelea viumbe wa kale (Visit Original
Homide (zinj)
|
$15
|
$30
per head
|
No comments:
Post a Comment