Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasili
katika Jengo la Mamlaka ya Mkonge, Mkoani Tanga kabla ya kulizindua
rasmi, akiwa katika ziara ya siku moja ya Mkoa huo, kukagua maendeleo ya
zao la mkonge, Juni, 1, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka jiwe la msingi wa Jengo la Mamlaka ya Mkonge, akiwa katika ziara ya siku moja, kukagua maendeleo ya zao la mkonge, mkoani Tanga, Juni, 1, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifafanuliwa jambo na Naibu Waziri Wizara ya Kilimo, Omar Mgumba, wakati akikagua shamba katika kituo cha utafiti wa zao la mkonge TARI Mlingano, akiwa katika ziara ya siku moja ya Mkoa huo, kukagua maendeleo ya zao la mkonge, Juni, 1, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli itahakikisha mali zote za wakulima wa zao la mkonge nchini zinarudishwa mikononi mwao na hakuna mtu yeyote atakayeonewa.
“Tutarudisha mali zote za wakulima na
ninawahakikishia hakuna mtu yoyote atakayeonewa, kama tulivyorudisha hizi mali za Bodi ya
Mkonge Tanzania tutafanya hivyo hivyo kote bila kumuonea yeyote na kuanzia leo
Bodi hii ya Mkonge imethibitishwa kuwa bodi kamili.”
Waziri Mkuu ametoa
kauli hiyo leo (Jumatatu, Juni 1, 2020) wakati akifungua jingo la Bodi ya
Mkonge Tanzania zilizopo jijini Tanga. “Mkonge ni fedha Halmashauri
wekeni vitalu mzalishe mbegu muwape wananchi bure. Kama unashamba kubwa
hujaliendeleza, kulingana na muda uliowekwa, tutalichukua.”
Amesema Serikali imedhamiria kulirudisha zao
hilo, hivyo ametoa wito kwa wananchi hususani wa mkoa wa Tanga wajipange katika
kuyafufua mashamba yao na kuanzisha mapya na Serikali itawasaidia kuhakikisha
mbegu bora na pembejeo zinapatikana.
Kadhalika,
Waziri Mkuu ametoa rai kwa wananchi katika kila mkoa wenye ardhi nzuri ambayo
inastawi zao hilo waanzishe kilimo cha zao mkonge walime na Serikali itawasaidia
bila kujali ni mtu mmoja mmoja, wakulima wa kati na wakubwa.
“Wakuu
wa wilaya waondoeni Maafisa Kilimo waliopo Ofisini waende vijijini wakawasaidie
wakulima namna nzuri ya kulima zao hili kwa faida, mkonge ni pesa, Serikali
yenu itasimamia. Tunataka mkonge urudi kwenye nafasi yake. Endeleeni kuwahamasisha
walime mkonge, tunataka kila tunapopita tuone mashamba ya mkonge.”
Ameiagiza
Bodi ya Mkonge kufanya utambuzi wa mashamba na wayarudishe kwa watu walime. Pia
mapori yote makubwa yaliyoko kwenye halmashauri ambayo hayatumiki nayo
wayatambue na waishauri Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili nao
wamshauri Rais Dkt. Magufuli kwa ajili ya kugawiwa kwa wananchi waweze kulima.
Katika
mkutano huo, Waziri Mkuu amesema amewahusisha wadau kutoka taasisi mbalimbali za
kifedha na kwamba Serikali imeweka utaratibu utakaowawezesha wakulima wanaotaka
kuboresha mashamba yao waweze kukopa. “Nendeni Benki ya Kilimo mkachukue mikopo.”
“Zao la mkonge ni
muhimu nchini kwani linawanufaisha wakulima wadogo, wa kati na wakubwa. Mkonge
kwa Tanga ni uchumi kwa wananchi na ni mkombozi kwa sababu unawawezesha kupata
riziki zao. Zao hili hapo katikati halikuwa na tija, zao hili lilikuwa
linalimwa na mikoa zaidi ya 12 lakini sasa limeachwa kwenye mikoa minne tu.”
Waziri Mkuu amesema kwenye miaka ya 60
Tanzania ilikuwa inaongoza kwa uzalishaji wa mkonge duniani, ambapo ilikuwa
inazalisha tani 235,000 huku mahitaji ya mkonge duniani yakiwa tani 550,000.
“Tulikuwa tunazalisha zaidi ya nusu ya mahitaji ya dunia, leo hii mchango wake
haupo ukiuliza kwa nini hakuna sababu. Serikali imeagizwa na CCM kuwa ni lazima
zao hili lirudi kwenye hadhi yake na litarudi.”
Kufuatia hali hiyo, Waziri Mkuu ameagiza
mikoa yote inayolima zao la mkonge kuanzia sasa ijipange kwa sababu Serikali
imeamua kulifufua zao hilo na inataka kulirudisha katika nafasi yake, hivyo
viongozi wahakikishe wanaendelea kuwahamasisha wananchi walime kwa wingi.
“Tunataka mkonge ushamiri, Bodi tumieni vyombo vya habari
kuhamaisha wananchi walime zao hili pamoja na kuwaeleza fursa zitokanazo na zao
hilo. Wawekezaji wetu panueni mashamba, leteni mitambo ya kuchakata mkonge
pamoja na vyote vitokanavyo na mkonge. Nampongeza Mkuu wa Mkoa wa Tanga
amefanya kazi kubwa katika hili.”
Naye, Naibu Waziri
Kilimo, Omar Mgumba, ametumia fursa hiyo kumshukuru Waziri Mkuu kwa jitihada
kubwa anazozifanya katika kusimamia sekta ya kilimo likiwemo zao la mkonge. “Uadilifu
wako na uzalendo wako ulikufanya uunde kamati ya kuchunguza mali za Bodi ya Mkonge
Tanzania na leo hii mali zao zimerudi.”
“Mheshimiwa Waziri Mkuu utaingizwa kwenye
kumbukumbu za Tanzania kwa kujitoa kwako katika kuhakikisha zao hili linarudi
kama ilivyokuwa awali. Tutafufuka katika mikoa yote ambayo imeonesha inaweza
kulima zao hili la mkonge, lengo ni kuhakikisha zao hili linarudi kwenye hadhi
yake.”
Kwa upande wake,
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
amemshukuru Waziri Mkuu kwa kusimamia ajenda za maendeleo katika mkoa wa Tanga,
hususani zao la mkonge.
“Tunashukuru
uliporejesha hadhi ya zao hili.Tutawahimiza wananchi kulima mkonge kwani
tunaona muelekeo na maono ni makubwa sana, Tanga tunajivunia jitihada hizi za
maendeleo, uchumi wa Tanga utakuwa kwa kasi sana.”
Awali, Mbunge wa Lushoto
Rashidi Shangazi alisema wanaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuweza kuwarejeshea wananchi
mashamba yao.
Nao, Wakuu wa Mikoa ya Pwani,
Morogoro na Kilimanjaro waliishukuru Serikali kwa kulifufua zao hilo na kwamba wameshaweka mipango ya kuendeleza zao hilo na wameiomba Wizara ya Kilimo ishirikiane
nao kwa kuwasaidia wakulima katika kuendeleza zao hilo, ikiwemo uandaaji wa mashamba,
uendelezaji pamoja na utafutaji wa masoko. “Wizara ya Kilimo na Wizara ya Ardhi
zitusaidie kutenga maeneo makubwa ya ardhi kwa ajili ya uzalishaji.”
No comments:
Post a Comment