HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 01, 2020

Serikali Yaziunganisha TPB NA TIB Kuongeza Ufanisi

Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka, akiwahakikishia wateja wa Benki ya TIB na TPB kuwa huduma hazitaathirika kutokana na kuunganishwa kwa Benki hizo, wakati wa Mkutano na vyombo vya Habari, katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jijini Dodoma.
Msajili wa Hazina, Bw. Athumani Mbuttuka (wa pili kulia), wakiangalia baadhi ya nyaraka zinazohusu kuunganishwa kwa Benki ya TIB na TPB Corporate, katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dodoma. (Picha na Ramadhani Kissimba, WFM, Dodoma).
 Msajili wa Hazina, Bw. Athumani Mbuttuka, wa tatu kushoto na Mtendaji Mkuu wa Benki ya TPB, Bw. Sabasaba Moshingi, wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi baada ya kutangazwa kuunganishwa kwa Benki ya TIB na TPB Corporate, katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dodoma.


Na Immaculate Makilika – MAELEZO

Serikali imeziunganisha  benki zake mbili za biashara, Benki ya Posta Tanzania (TPB Bank Plc) na Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB Corporate Limited) ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji.

Akizungumza leo (Jumatatu Juni 1, 2020) jijini  Dodoma, Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka, alisema kuwa Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali zenye lengo la kuboresha utendaji wa mashirika na taasisi za umma ikiwemo kuunganisha taasisi zinazotekeleza majukumu yanayofanana, ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji.

“Kwa muktadha huu, Serikali imeamua kuunganisha benki zake mbili za biashara, yaani Benki ya TPB na Benki ya TIB Corporate kuanzia tarehe 01 Juni 2020. Kwa hatua ya awali, Benki ya TPB itachukua mali na madeni ya Benki ya TIB Corporate na muunganiko huu utafanya benki kuwa na mali takribani trilioni moja”, alisema Mbuttuka.

Alifafanua Mbuttuka amesema Serikali imechukua uamuzi huu kwa lengo la kuboresha utendaji wa benki inazozimiliki ili kuwa na benki moja ya biashara ambayo ni imara. Aidha, muungano huu unalenga kuleta mageuzi makubwa ya kiutendajii, kimfumo, kimuundo, na kitaswira ili benki hii iweze kuhimili ushindani wa kibiashara kwenye sekta ya fedha. 

 “Muunganiko huo hautakuwa na athari katika huduma za kibenki, wala hakuna mfanyakazi atakayepoteza ajira. Aidha,  Serikali inapenda kuuhakikishia umma kuwa itaendelea kuhakikisha utendaji wa benki zake unaimarika na maslahi ya wenye amana na wateja wote yanalindwa kwa mujibu wa sheria, kanuni, na taratibu za usimamizi wa benki na taasisi za fedha”, alioneza Mbuttuka. 

Kwa mujibu wa Msajili wa Hazina, wateja wote wa Benki ya TPB na Benki ya TIB Corporate wataendelea kuhudumiwa kwenye matawi yao ya sasa hadi hapo watakapotaarifiwa vinginevyo.

No comments:

Post a Comment

Pages