Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akizungumza na mmiliki wa lori lililozama katika daraja la sasa la Wami, Mwajuma Selemani, wakati wa ziara yake mkoani Pwani na kutembelea eneo lilipozama lori hilo. (Na Mpiga Picha Wetu).
NA MWANDISHI WETU
SERIKALI
imesema ukamilishaji wa ujenzi wa Daraja jipya la Wami lenye urefu wa
mita 510 linalounganisha nchi yetu kupitia mikoa ya Kaskazini na nchi
jirani za Afrika Mashariki litaongeza fursa nyingi za kiuchumi kwa Taifa
kupitia usafiri na usafirishaji wa abiria na mazao.
Aidha imemtaka mkandarasi Power Construction Corporation anayejenga
Daraja hilo kutumia muda uliopo kufidia kazi zilizosimama kufanyika hasa nyakati za mvua nyingi.
Hayo
ameyasema Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, katika ziara yake
mkoani Pwani ambapo amekagua hatua zilizofikiwa za mradi huo na
kuridhishwa na kasi ya mkandarasi ambapo kwa ujumla mpaka sasa ujenzi
umefikia asilimia 40.
"Watanzania
niwahakikishie kuwa mradi huu utakamilika mapema kwa kuwa Serikali
inahitaji daraja hili litumike haraka sana kwani litapunguza shida na
adha nyingi ambazo watumiaji wa barabara hii wanapata ikiwemo upotevu
wa mali nyingi,"alisema Naibu Waziri huyo.
Alisisitiza
kuwa mradi huo hautakuwa na sababu yoyote ya kutoendelea kwa kuwa fedha
zimetolewa kwa mkandarasi na ataendelea kulipwa kwa wakati ili
kuhakikisha watanzania wanapata manufaa makubwa kwa nchi yao na
rasilimali zao.
Kuhusu
daraja la sasa linalotumika, Naibu Waziri huyo alisema kuwa mkandarasi
anayejenga daraja jipya atafanya ukarabati wa daraja hilo baada ya
kufanyiwa ukaguzi wa kina na wataalamu wa madaraja ili kuhakikisha
daraja hilo linaendelea kuwa imara kila wakati.
Naibu
Waziri huyo aliongeza kuwa zaidi ya kiasi cha shilingi bilioni 723
zimelipwa kwa wakandarasi wote nchini wanaoendelea na miradi ya ujenzi
ya miundombinu ili kuhakikisha hakuna miradi itakayosimama na wala kuwa
na changamoto yoyote ya malipo.
"Tunamshukuru
Rais John Magufuli kwa kutuamini kusimamia miradi hii mikubwa ya
Kitaifa na sisi kama Sekta ya Ujenzi kazi yetu ni moja ya kuwezesha
watanzania wawe na miundombinu sahihi ya kuwafanya waweze kutoa mchango
wao wa kiuchumi," alifafanua Kwandikwa.
Katika
hatua nyingine Naibu Waziri huyo amekutana na mmiliki wa lori
lililozama katika daraja hilo majuma mawili yaliyopita Mwajuma Selemani,
na kutoa pole kwa uharibifu wa mali na kifo cha dereva wake.
Naye,
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Pwani Mhandisi Yudas
Msangi, alieleza kuwa kazi ya upimaji na uchimbaji wa msingi ya nguzo za
daraja zimekamilika kwa asilimia 100 huku kazi zingine zikiendelea
vizuri na wanaendelea kumsiamamia na kushirikiana na mkandarasi kwa
karibu ili asicheleweshe mradi huo.
Aliongeza
kuwa mpaka sasa kilometa 3 kati ya 4.3 ya barabara unganishi
zimeshafanyiwa usafishaji na ufukuaji kwacha asilimia 70 ya barabara
unganishi na kazi ya kukata vilima ili kupata usawa wa barabara nayo
inaendelea vizuri kwa pande zote za daraja.
Ujenzi
wa daraja jipya la wami ni mkakati wa Serikali wa kuondoa adha
wanaoipata wasafirishaji na wasafiri wanaopita katika daraja hilo
lililojengwa toka mwaka 1959 na kuonesha kutokidhi mahitaji ya magari
yanayopita na kuwa jembamba na lenye njia ya kuwezesha kupitisha gari
moja tu.
No comments:
Post a Comment