HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 20, 2020

Shilingi trilioni 23 zatumika kujenga miundombinu nchini

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale, akimuelezea Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Selander lililopo Kinondoni jijini Dar es Salaam, mwishoni mua wiki. (Picha na Suleiman Msuya).
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe akizungumza na Mhandisi wa Daraja la Selander upande wa Mhandisi Mshauri, Lulu Dunia.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe akizungumza na Mhandisi wa Daraja la Selander upande wa Mhandisi Mshauri, Lulu Dunia.


NA SULEIMAN MSUYA

WIZARA ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imetumia shilingi trilioni 23 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali miundombinu nchini kote.

Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Wizara hiyo Mhandisi Isack Kamwelwe wakati akizungumza na waandishi wa habari alipotembelea mradi wa ujenzi wa Daraja la Selander linalojengwa wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Alisema Serikali kupitia Wizara hiyo imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya miradi ya barabara, madaraja, vivuko, barabara za juu na ujenzi wa meli mbalimbali lengo likiwa ni kumaliza adha ya usafiri nchini.

Mhandisi Kamwelwe alisema Daraja la Selander limejengwa ili kupunguza foleni ambayo ipo barabara ya Ally Hassan Mwinyi ambapo kwa siku zaidi ya magari 60,000 yanapita.

Alisema idadi hiyo ya magari pamoja na kusababisha foleni pia ni chanzo cha kusimamisha shughuli za uchumi na uharibifu wa mazingira.

"Tunatekeleza miradi mingi ya barabara, madaraja, vivuko, meli na mingine ikiwemo Daraja la Selander ambalo pamoja na barabara za nje litakuwa na urefu wa kilometa 6.53.

Pia daraja hili la kisasa hadi linakamilika litagharimu zaidi ya shilingi bilioni 243 ambapo fedha hizo dola milioni 91 zinatolewa na nchi ya Korea ya Kusini na dola milioni 21 zikitolewa na Serikali ya Tanzania," alisema.

Waziri Kamwelwe alisema matarajio ya Serikali ifikapo Oktoba 2021 watakuwa wamekabidhiwa daraja hilo la kisasa ambalo lenyewe lina urefu wa kilomita 1.3.

"Hadi kufikia sasa ujenzi umefikia zaidi asilimia 40 ambapo lengo lilikuwa wafikie asilimia 44 lakini kuna changamoto zilitokea kama virusi vya corona na baadhi ya maeneo kuhitaji ufuatiliaji zaidi," alisema.

Mhandisi Kamwelwe alisema kwa miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Magufuli wameweza kujenga zaidi ya madaraja 13 huku miradi mingine inaendelea.

Alisema dhamira ya Serikali ni kuibadilisha Tanzania ili iwe kwenye hadhi ya nchi nyingine ambazo zimeendelea.

Kwa upande mwingine Waziri Kamwelwe alisema kuanzia kesho Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Dar es Salaam wataanza kulipa fidia watu ambao barabara inapita.

Alisema shilingi bilioni 2.4 zitalipwa kwa wahusika ili kupisha eneo ambalo barabara itajengwa kuunganisha na Daraja la Selander.

Waziri Kamwelwe alisema Serikali itahakikisha inatekeleza ilani ya Chama Cha  Mapinduzi (CCM) ambayo inataka huduma za kijamii ikiwemo barabara na madaraja yanajengwa.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale amesema miradi huo utakamilika kama ulivyopangwa na kuweka bayana kuwa asilimia 4 ambayo wapo nyuma watahakikisha inazibwa.

Mfugale alisema hadi sasa wememlipa mkandarasi zaidi ya shilingi bilioni 121 kati ya shilingi bilioni 243 anazopaswa kulipwa.

"Ujenzi unaendelea vizuri kupitia kampuni ya GS Engineering Corporation kutoka Korea ya Kusini na Mhandisi Mshauri ni Yooshin Engineering Corporation ya Korea Kusini na Afrisa Consulting Limited ya Tanzania,"alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages