WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameiagiza Kampuni ya Xiamen
Ongoing Construction Group inayojenga Bandari ya Karema kwa gharama za zaidi ya sh. bilioni
47 ifanye kazi usiku na mchana na kukamilisha ujenzi huo kwa wakati ili kuimarisha
biashara kati ya Tanzania na Congo.
Pia,
Waziri Mkuu ametoa muda wa siku 21 kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA),
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Polisi, Wizara ya
Madini na wawe wameanza kutoa huduma katika eneo la Ikola ili kuhudumia wageni
wanaotoka Congo.
Alitoa
agizo hilo jana jioni (Jumamosi, Julai 04, 2020) baada ya kuweka jiwe la msingi
la ujenzi wa Bandari ya Karema
inayojengwa kwenye ziwa Tanganyika katika kata ya Karema wilayani Tanganyika,
Katavi. Alisema mkandarasi anatakiwa ahakikishe mradi huo unakamilika haraka.
Waziri
Mkuu alisema mradi huo unalenga kuongeza tija katika shughuli za kibandari
kwenye ukanda wa Ziwa Tanganyika ndani na nje ya nchi na kwamba utaongeza fursa
za kibiashara nchini na pia utakuwa chachu ya kukuza uchumi pamoja na kuboresha
huduma za usafiri kwa wananchi.
“Tumeamua
kujenga bandari hii ambayo itawezesha meli zaidi ya moja kupakia na kushusha
abiria na mizigo kwa wakati mmoja. Hii ni Serikali ya kuahidi na kutekeleza na
ni Serikali ya kusikia na kutenda na ndio maana halisi ya falsafa ya Rais Dkt.
John Pombe Magufuli ya Hapa Kazi Tu.”
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TPA Mhandisi Dkt. Baraka
Mdima alisema mradi huo unahusisha ujenzi wa gati kubwa la kufungia meli lenye
urefu wa mita 150 pamoja na kingo ya kuzuia mawimbi makali, uchimbaji wa
kuongeza kina cha lango la kuingilia bandarini na sehemu ya kugeuzia meli.
Alisema
eneo jinguine ni ujenzi wa miundombinu ya bandari ikiwemo mgahawa, jengo la
kupumzikia abiria, majengo ya ofisi, eneo la sakafu ngumu kwa ajili ya
kuhifadhia makasha pamoja na miundombinu ya Zimamoto na Tehama. Mradi huo
utazingatia ujumuishi wa Reli ya Kisasa (SGR).
“Mradi
unajengwa kwa miezi 24 na kukamilika kwa bandari ya kisasa ya Karema,
kutaboresha shughuli za kiuchumi katika mkoa wa Katavi na Tanzania kama
kusafirisha watu na bidhaa katika maeneo ya mwambao wa Ziwa Tanganyika na nchi
jirani za Congo, Burundi na Zambia.”
Kadhalika, Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Katavi,
Juma Homera aendelee na operesheni ya kuwasaka watu wote wanaomiliki silaha
kinyume cha sheria.“Watu wote wanaomiliki silaha bila ya kuwa na vibali
watafuwe popote walipo na wachukuliwe hatua za kisheria.”
Awali,
Waziri Mkuu alizungumzia upatikanaji wa umeme katika wilaya ya Tanganyika, alisema
Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli
imedhamiria kufikisha huduma ya umeme katika vijiji vyote nchini, hivyo
waendelee kuwa na subira.
“Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John
Pombe Magufuli anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inawaka umeme na
amepunguza gharama za kuunganisha umeme kutoka sh. 380,000 hadi sh. 27,000 ili
kila mwananchi aweze kumudu gharama hizo.”
Waziri Mkuu aliongeza kuwa licha
ya gharama za kuunganishiwa umeme kupunguzwa, pia wananchi hatolazimika kulipia
gharama za nguzo pamoja na gharama za fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme
kwani tayari zimeshalipiwa na Serikali.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata
utepe wakati alipoweka jiwe la msinngi la ujenzi wa bandari ya Karema
wilayani Tanganyika Julai 4, 2020. Wengine kutoka kushoto ni Mbunge wa
Mpanda Vijijini,Moshi Kakoso, Mkuu wa Mkoa wa katavi, Juma Homela,
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandii Isack Kamwelwe,
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzani, Masanja Kadogosa na kulia
ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo.(Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu).
No comments:
Post a Comment