Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akishuhudia wakati Mkurugenzi Mtendaji wa
Benki ya Maendeleo ya Kilimo, Japhet Justine (kulia) alipomkabidhi Mkuu
wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa hundi ya Sh. 9,050,846,030/= ikiwa
ni malipo ya madeni ya wakulima, waendesha maghala, wasafirishaji na
wapuliza madawa wa zao la korosho wilayani Tandahimba katika mkutano
aliouhutubia kwenye viwanja vya AMCOS ya Matogoro, Tandahimba, Julai
19, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Serikali imetoa sh. bilioni 20 za kulipa madeni ya wakulima,
wasafirishaji, wapuliziaji dawa na waendesha maghala ya korosho.
"Rais
Magufuli ametoa fedha hizi kwa ajili ya Tandahimba, Masasi, Mtwara na
Kibiti kwa ajili ya waliokuwa wamelipwa nusu, waliolipwa kiasi na
wasiolipwa kabisa. Fedha hizi zitaanza kulipwa kesho asubuhi," amesema.
Ametoa
kauli hiyo leo (Jumapili, Julai 19, 2020) wakati akizungumza na
wanachama wa Chama cha Msingi (AMCOS) cha Matogoro na wakazi wa
Tandahimba mkoani Mtwara alikoenda kuhamasisha maandalizi ya msimu wa
ununuzi wa korosho.
Amesema
uhakiki uliofanywa kwa wakulima wa Kibiti, Rufiji, Mkuranga, Ruangwa,
Liwale, Lindi, Tunduru na wilaya zote za mkoa wa Mtwara ulibaini kuwa
wakulima na watoa huduma wote walikuwa wakidai zaidi ya sh. bilioni 23.
“Katika
hao, Tandahimba wanadai zaidi ya sh. bilioni 9, Masasi wanadai sh.
bilioni 2.3 na Mtwara Vijijini wanadai sh. milioni 884. Nyingine ni za
Pwani na Lindi," amefafanua.
Waziri
Mkuu amesema fedha hizo zimetokana na mfumo uliotengenezwa na wanunuzi
ili kumnyonya mkulima katika msimu wa 2018/2019 kwa kununua kilo ya
korosho kwa sh. 1,500 badala ya sh. 3,000 hali iliyolazimu Serikali
kuingilia kati na kuamua kuzinunua korosho zote.
Waziri
Mkuu alishuhudia Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Kilimo (TABD), Bw.
Japhet Justine akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Bw. Gelasius Byakanwa
hundi ya sh. 9,050, 846,030 ambaye pia aliikabidhi kwa viongozi wa
Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba na Newala (TANECU) na AMCOS ya
Matogoro.
Awali,
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mtwara, Bw. Yusuph Nanila alimuomba Waziri
Mkuu atoe majibu ya lini wakulima wa Tandahimba watalipwa fedha zao,
ambazo zimefikia zaidi ya sh. bilioni 9.
Wakati huohuo, Waziri
Mkuu amevitaka Vyama Vikuu vya Ushirika na AMCOS waweke kipaumbele cha
kununua mashine ndogo ndogo za kubangulia korosho ili waache mtindo wa
kuuza korosho ghafi.
"Ukibangua
kilo tatu za korosho yenye maganda, unapata kilo moja ya korosho
zilizobanguliwa. Kilo moja ya korosho yenye maganda inauzwa sh. 2,400
kwa hiyo kilo tatu ni sh.7,200, lakini ukizibangua, kilo moja inauzwa
sh.25,000. Ninawasihi tuanzishe viwanda vidogo vya kubangua korosho ili
tupate fedha zaidi kwenye vyama vya msingi."
"Matogoro
mnaweza kununua hata mashine 100 kutoka SIDO ili mzibangue hapahapa na
kuongeza pato la wakulima wenu. Tena mashine za viwanda vidogovidogo
zinatoa korosho nzuri zenye ubora sawa na zilizotoka kwenye mashine
kubwa," aliongeza.
Kuhusu
msimu wa ununuzi wa korosho, Waziri Mkuu alisema msimu mpya unaanza
Septemba hadi Desemba na akawataka viongozi wa ushirika wasimamie
ununuzi wa korosho mapema.
Aliwataka
wakulima wa korosho wa wilaya hiyo wabadili mfumo wa kilimo cha zao
hilo kwa kuanza kupanda miche mipya ambayo inazaa kwa wingi na inachukua
muda mfupi kukomaa. “Pandeni miche mipya kwa sababu inazaa ndani ya
mwaka mmoja na nusu, ondoeni mikorosho iliyozeeka.”
Pia
aliwataka wanachama hao walime mazao mbadala kama chikichi na alizeti
ambayo yanakubali kwenye ardhi yao ili waongeze wigo wa sgughuli za
kiuchumi kwenye wilaya hiyo. “Michikichi inakubali sana kwenye ukanda wa
pwani, kwa hiyo jaribuni muone ukuaji wake.”
Kuhusu
malipo ya wasafirishaji, Waziri Mkuu alisema kati ya fedha zilizolipwa,
wasafirishaji wametengewa sh. bilioni 3.3. Alikuwa akijibu swali la
Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji wilayani Tandahimba, Bw. Maulid
Mussa ambaye alisema walisafirisha korosho kutoka kwa wakulima hadi
kwenye maghala na madai yao yaliyofikia sh. milioni 600 yamekuwa
yakiwanyima usingizi kwa muda mrefu.
Kuhusu
bei dira ya korosho, Waziri Mkuu amewaelekeza viongozi wa vyama vya
msingi na vyama vikuu nchini kote wakae na kuandaa gharama ambazo
mkulima anakuwa amezitumia na gharama zitakazokubaliwa ndiyo iwe msingi
wa bei dira.
“Vyama
vikuu vifanye hiyo kazi kabla msimu haujaanza Septemba 2020. Mniletee
ofisni kwa maandishi ili tumshirikishe Waziri wa Kilimo na kisha
tutangaze kitaifa bei dira ni ipi,” amesema.
No comments:
Post a Comment