HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 18, 2020

WAZIRI MKUU: VIJANA, AKINAMAMA, NENDENI MKALIME

 *Asema anayetaka fedha, ataipata shambani
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa soko la mbogamboga na matunda katika kijiji cha Namahema linalojengwa na serikali kwa ajili ya wakulima wadogowadogo wa bonde la  Mnindu wilayani Ruangwa, Julai 18, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa soko la mbogamboga na matunda katika kijiji cha Namahema linalojengwa na serikali kwa ajili ya wakulima wadogowadogo wa bonde la  Mnindu wilayani Ruangwa, Julai 18, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Bibi Asumini  Milanzi (kulia) baada ya kukagua ujenzi wa soko la mbogamboga na matunda  katika kijiji cha Namahema linalojengwa na serikali  kwa ajili ya wakulima wadogowadogo wa bonde la  Mnindu wilayani Ruangwa, Julai 18, 2020.  Wa pili kushoto ni Mzee Abdallah Said na wa tatu kushoto ni  Mwanahamis Mohamed. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka vijana wa wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi waache kukaa vijiweni na badala yake waanzishe bustani ili kujiongezea kipato.

“Biashara ya bustani inalipa sana, yeyote anayetaka fedha, ataipata shambani. Nataka niwasisitize sana twende tukalime, twende shambani. Shamba siyo lazima ulime mahindi, mpunga pekee ama muhogo. Bustani ya nyanya, vitunguu, karoti na mchicha inalipa sana.”

Waziri Mkuu ametoa wito huo leo mchana (Jumamosi, Julai 18, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Namahema alipokwenda kukagua mradi wa ujenzi wa soko la mbogamboga na matunda katika bonde la Mnindu unaolenga kuongeza uzalishaji na masoko kwa wakulima wadogo.

Amesema Serikali imetoa sh. milioni 600 ili zijenge masoko na kuongeza uzalishaji huko Mpumbe, Mnindu, Chiepo na Chikalala. “Serikali imewaandalia mradi huu ili mlime wakati wote, iwe masika au kiangazi. Rais wetu ametoa fedha hizi ili vijana na akinamama walime bustani na kujipatia kipato zaidi,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameagiza kamati ya ujenzi ya mradi huo irekebishe mara moja kasoro zilizosababishwa na ukiukaji wa taratibu wa ujenzi wa majengo ya Serikali kwenye soko hilo.

Amemtaka msimamizi wa mradi huo, Bw. Kalistus Mnunduma ambaye ni mkufunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Nkowe ahakikishe anatoboa milango ya ziada kwenye jengo ili kuongeza usalama wa watumiaji wakati wa kutoka na kuingia kwenye soko hilo.

Waziri Mkuu alifikia hatua hiyo baada ya kubaini ujenzi wa soko hilo ulianza kwa kutumia michoro ya awali (sketch) badala ya kutumia ramani za ujenzi na matokeo yake wakajenga jengo lenye vyumba vya baridi vya kuhifadhia mazao, eneo la wazi la kupokelea mazao na kuweka mlango mmoja tu wa kuingilia na kutokea.

“Nimetoa maagizo manne. Kwanza, toboa milango, pili weka vizimba ili wananchi wauze bidhaa zao mahali pasafi, usiruhusu watu wauze bidhaa zao chini, siyo sawa kiafya. Tatu, chimba visima, weka mnara, tanki na mipira ya kumwagilia ya kutosha ili wakulima wasipate taabu ya kusomba maji. Weka mashine ya kusukumia maji ili uweze kuyasambaza katika eneo kubwa. Nne, tenga eneo la kuuza bidhaa kwa rejereja ili wananchi wa hapa jirani wanufaike na mradi huu,” amesema.

Pia alimwagiza Afisa Kilimo wa Wilaya hiyo, Bw. Harun Ibrahim Kiara ahakikishe wanatoa elimu ya kilimo cha bustani kwa vijana ili waanze na matuta machache. “Pia anzisheni programu ya kukutana na vijana na akinamama na muwaeleze bonde la Mnindu linatumikaje kwa kilimo hicho,” amesema.

Mapema, akitoa taarifa ya mradi huo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo, Bw. Selemani Mrope alisema mradi huo unatarajiwa kutumia sh. milioni 127 hadi kukamilika kwake na mpaka sasa wamekwishapokea sh. milioni 50.8 ambazo ni sawa na asilimia 40.

Alisema ujenzi wa soko ambao ulianza Mei 25, 2020 ulikadiriwa kugharimu sh. milioni 25 na mpaka sasa wameshatumia sh. milioni 18.2 ambapo ujenzi umefikia hatua ya uinuaji wa nguzo. Mradi huo unatarajia kukamilika Agosti 30, mwaka huu.

Alisema Chuo cha Ufundi Stadi Mkowe kinatekeleza mradi wa kuongeza uzalishaji na masoko kwa wakulima wadogo wa mbogamboga na matunda katika bonde la Mnindu kwa ufadhili wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kupitia mfuko wa kuongeza na kuboresha elimu (SDF).

“Mradi huu umelenga kuwezesha kuwepo kwa soko la uhakika, ongezeko la ajira na uzalishaji, ongezeko la kipato kwa jamii, upatikanaji wa uhakika wa chakula lishe na uboreshiji wa miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji kwa mazao ya bustani,” alisema Bw. Mrope.

Alisema hadi sasa wamekamilisha kazi ya kuandaa mitala na miongozo ya kufundishia wakulima wote wa bustani kwa gharama ya sh. milioni nne na kwamba wanaendelea na ukarabati wa darasa moja litakalotumika kutoa elimu kwa wakulima wote wa bustani ambalo gharama yake ni sh. milioni 4.2.

No comments:

Post a Comment

Pages