HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 16, 2020

Shaka amvaa Membe, adai amehamia upinzani kipindi cha ukame

KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro, Shaka Hamdu Shaka.
 

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro Shaka Hamdu Shaka, amesema aliyekuwa Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje Benard Camillius Membe, kuhamia Chama Cha ACT-Wazalendo akifikiri chama hicho kitashinda, ni ndoto.

Kauli hiyo ya Shaka imekuja baada ya Waziri huyo wa zamani kuhamia ACT Wazalendo baada ya kufukuzwa na CCM.

Shaka amesema Membe anapania urais huku akifikiria kismati cha mgombea urais wa chama cha Mct huko malawi Rais Dkt. Lazarus Chakwera huko ni kuota ndoto mchana.

Ameongeza kuwa, Membe ameshindwa kuzipima nguvu zake kisiasa na alizokuwa nazo Waziri mkuu Mstaafu Edward Lowassa aliyewania urais mwaka 2015 kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akashindwa.

"Membe ni mwanasiasa ambaye hana ubavu wa kusimama kwa miguu yake mwenyewe kwenye majukwaa ya kisiasa akashinda hata ubunge nje ya CCM bali siku zote amekuwa akisafiria nyota za waliokuwa karibu yake.

"Asikubali kuamini nadharia ya kila anayekaa karibu na waridi hunukia. Akifanya hivyo ni makosa. Kukaa karibu ya Askofu au Sheikh ikiwa huna elimu ya dini ni kukubalika ni
kujidanganya...Mwanasiasa hashindi urais kwa kuitegemea njozi za jinamizi afriti au za kufikirika," amesema Shaka.

Ameongeza kuwa Membe anataka kuwania urais kwasababu aonekane yupo mbele ya wananchi na kudai hilo ni kosa, kwani atajikuta akipigwa mwereka mkali utakaomfuta katika ramani ya kisiasa na kujikuta akidondoa kura haba na matokeo ya aibu.

"Kwa siasa zetu kama alishindwa Lowassa kuibwaga CCM mwaka 2015 hatatokea mwenye jeuri ya kuitikisa kitaharuki, Lowassa alipikwa kisiasa akapikika, aliandaliwa kiitikadi na kifalsafa, akakomaa lakini mbele ya JPM amekikwaa kisiki cha mpingo ameamaua kurudi nyumbani," amesema Shaka.

Katibu huyo wa Mkoa amesema ikiwa Membe anawania urais baada ya kuona mgombea urais wa Malawi Rais Dkt. Chakwera wa Mct akimshinda Rais wa zamani Profesa Peter Mutharika wa DPP naye akitarajia atashinda, asubiri kipigo cha mbwa mwizi ambacho alidai hatakisahau katika maisha yake.

"Yawezekana sana Malawi walichoshwa na utawala wa Prof. Mutharika na DPP kwa sababu ambazo sasa ukizitazama hazipo Tanzania hivyo anachokifikiria Membe akidhani kinaweza kutokea Tanzania huo ni mtazamo hasi na matarajio batili.

"Kwa bahati mbaya amejiunga upinzani wakati wa msimu wa ukame kisiasa. Amefanya uamuzi wakati serikali ya Dkt. Magufuli imeshatenda maajabu yanayojadiliwa dunia nzima. Iko wapi nafasi ya ushindi wa Membe wakati huu huku nchi ikishamiri maendeleo kila kona nchini," ameeleza shaka.

No comments:

Post a Comment

Pages