Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe kuzindua jengo la Mpanda
Plaza ambalo ni kitegauchumi cha Shirika la Taifa la Nyumba (NHC), mjini
Mpanda, Julai 4, 2020. Wa pili kulia ni Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano
na Uchukuzi, Mhandisi Isack Kamwelwe, kulia ni Naibu Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula, kushoto ni Mkuu wa Mkoa
wa Katavi Juma Homela na wapili kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Dkt.
Maulid Banyani. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
engo la Mpanda Palaza ambalo ni kitegauchumi cha Shirika la Taifa la
Nyumba (NHC) limezinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mjini Mpanda,
Julai 4, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka Watazania waendelee
kufanya kazi kwa bidii ili nchi iendelee kukua kiuchumi na kufikia uchumi wa
juu kwa kuwa tayari imekuwa ya uchumi wa kati.
“Kama ni mkulima lima kwa bidii, mtumishi wa umma fanya
kazi kwa bidii, mlio viwandani fanyeni kazi na mamalishe nanyi pikeni sana ili
mzunguko wa fedha uweze kuendelea kuwa mkubwa nchini.”
Alitoa kauli hiyo jana (Jumamosi, Julai 04,
2020) alipozindua jengo la ofisi na biashara la Mpanda Plaza
lililojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Mpanda kwa gharama ya sh
bilioni 2.8.
Waziri Mkuu alisema Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani
pato la mwananchi kwa mwaka lilikuwa dogo na baada ya miaka mitano limeongezeka
na kufikia sh, milioni mbili.
Alisema ongezeko hilo la pato la mwananchi kwa mwaka limeliwezesha
Taifa kuingia katika uchumi wa kati kabla ya matarajio yaliyopendekezwa katika
Dira ya Taifa ya Maendeleo.
Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Tanzania ililenga kuifikisha Tanzania
kuwa nchi ya uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda ifikapo mwaka 2025 lakini
nchi imewezeka kufikia uchumi wa kati 2020.
Baada ya kuzindua jengo hilo, Waziri Mkuu alitembelea kijiji cha
Kasekese kilichoko wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi ambapo alizindua msimu wa
ununuzi wa zao la pamba kwa mwaka huu.
Waziri Mkuu alisema lengo la Serikali ni kurudisha ushirika ili uweze kuwa na tija kwa wakulima,
aliwataka viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) wawasaidie
wanachama wao.
Vilevile, Waziri Mkuu aliwaagiza Maafisa Kilimo nchini wawaelimishe
viongozi wa vyama vya ushirika namna bora ya uendeshaji wa vyama hivyo ili
waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Aliwahakikishia wananchi hao kwamba Serikali itaendelea kuwasaidia kwa
kuhakikisha Maafisa Ugani wanawafikia katika maeneo yao na kuwapa elimu itakayowawezesha
kujiongezea tija.
No comments:
Post a Comment