>Viongozi,
wanavijiji wasema ni sawa na kumpa mchawi akulelee mtoto
Ofisa Maliasili wa Wilaya ya Kilosa, John Mtimbanjayo akieleza kwa
waandishi wa habari pichani hawapo namna vijiji vya wilaya hiyo
vilivyonufaika na mfumo wa USMJ na FBE.
Darasa la Shule ya Msingi Ulaya Mbuyuni wilayani Kilosa mkoani Morogoro lililojengwa kwa fedha za USMJ na FBE.
Tanki la maji lililopo Shule ya Msingi Ulaya Mbuyuni wilayani Kilosa mkoani Morogoro lililojengwa kwa fedha za USMJ na FBE.
Na Suleiman Msuya
UPO msemo wa Kiswahili
unasema ‘Mchawi mpe mtoto akulelee’. Msemo huo una maana nyingi na kubwa katika
jamii hasa ukilenga iwapo kuna mtu ambaye una wasiwasi naye katika maisha
unapaswa kumpa jukumu ili kumpima.
Hali hiyo inatokea
kuanzia ngazi ya familia, jamii na nchi kwa ujumla ambapo unapotaka kubaini
jambo fulani unaambiwa unaweza kutumia njia hiyo.
Pamoja na dhana hiyo
lakini imekuwa ngumu kutekelezeka katika jamii kwani hasa pale inapobainika
kuwa kuna mazingira ya kishirikina kuwa anayehusishwa na jambo hilo apewe
aliyelogwa akae naye.
Hili limeweza kutokea
katika kutekeleza dhana ya Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ) na
Biashara ya Mazao ya Misitu (FBE) ambapo wadau mbalimbali kwa kushiriana na
Serikali wamefanikiwa kuwapa wanavijiji mamlaka ya kulea mtoto misitu kwa wao
kunufaika nao kijamii, kiuchumi na maendeleo.
Wilaya ya Kilosa,
mkoani Morogoro ni moja ya wilaya ambayo asilimia 80 ya eneo lake liligubikwa
na migogoro ya wakulima na wafugaji huku uharibifu wa misitu hasa ya vijiji na
ile ya Serikali ukiota mizizi.
Hali hiyo iliibua
masharika kama Shirika la Kuhifadhi Misitu Tanzania (TFCG), Mtandao wa Jamii wa
Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA), Shirika la Kuendeleza Nishati Tanzania
(TaTEDO) chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo Uswiss (SDC) na kuhakikisha
wanavijiji wanaomiliki misitu ya vijiji wanakuwa wanakuwa wachawi kwa
kuwakabidhi kuilinda, kuisimamia na kuitumia kwa njia endelevu.
Mchango wa mashirika hayo
pamoja na Serikali umeweza kubadilisha maisha ya wananchi wa vijiji takribani
20 ambavyo vinatekeleza Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania
(TTCS).
DAS
KILOSA
Katibu Tawala wa Wilaya
ya Kilosa (DAS), Yohana Kasitila anaelezea kwa kina namna wilaya na wananchi wa
vijiji vilivyopo kwenye mradi wameweza kunufaika na dhana ya USMJ na FBE hasa
ikizingatiwa na historia ya huko nyuma.
Kastila anasema awali
misitu yote ilikuwa inaharibiwa na wananchi wenyewe ila ujio wa TFCG na MJUMITA
kupitia TTCS kuna manufaa makubwa ya kimazingira, kiuchumi, huduma za kijamii
na maisha ya mwananchi mmoja mmoja.
“Katika vijiji vile
ambavyo mradi umepita kuna manufaa makubwa sana kwani miradi mingi ya
kiujasiriamali imebuniwa na inaendelea kubadilisha maisha ya wananchi wenyewe.
Kila mwananchi katika
kijiji chenye mradi amekuwa mhifadhi na mtoa taarifa pale ambapo anaona kuna
uharibifu jambo ambalo awali halikuwepo,” anasema.
DAS Kastila anasema kinachofanyika
Kilosa kinapaswa kusambazwa kila kona ya nchi hasa kwenye misitu ya vijiji na
kuachana na dhana ya kuhamisha mamlaka kwa Serikali Kuu ambapo usimamizi
unaweza kuyumba.
Anasema sera za nchi
zinazungumzia ugatuzi wa madaraka hivyo kinachofanyika katika vijiji ni tafsiri
sahihi ya sera hiyo kwani Serikali Kuu haina rasilimali watu, vitendea kazi vya
kutosha vya kuisimamia.
Kastila anasema
kinachohitajika ni elimu zaidi itolewe kwa wananchi kujua umuhimu wa kushiriki
katika ulinzi na usimamizi wa rasimali misitu na sio kujilimbikizia majukumu
ambayo kuyasimamia sio rahisi.
Anasema pia mradi
umewezesha kuwepo kwa Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi kwenye vijiji hali
ambayo inaongeza thamani kwenye ardhi za vijiji na wananchi kukopesheka jambo
ambalo Serikali Kuu imeshindwa kuwafikia kwa haraka.
Aidha, akizungumzia bei
elekezi ambayo imependekezwa kwenye Tangazo la Serikali GN 417 ambayo inataka
ushuru wa mkaa kwa gunia iwe shilingi 125,000 anasema kinachohitajika ni
usimamizi kwa kila eneo ambalo linazalisha ili kuwe na usawa.
“Hilo sio tatizo iwapo
kutakuwa na udhibiti wa biashara holela ya mkaa kwani faida itapatikana kwa
kila pande, ila kinyume na hapo watakaoumia ni wale waliopo mbali na baraba,”
anasema.
DED
KILOSA
Mkurugenzi wa Wilaya ya
Kilosa (DED), Asajile Mwambambale anasema USMJ na FBE ni njia muafaka ya
utunzaji misitu na kuifanya iwe endelevu kwa vizazi vijavyo.
Anasema wanavijiji
ambao wana rasilimali misitu wamekuwa walinzi na mabalozi wa uhifadhi jambo
ambalo linapaswa kupewa nguvu ili liwe endelevu.
“Wapo wanaona kuwa
wanavijiji wananufaika na fedha sio kweli manufaa makubwa yapo msituni kwa kuwa
kila mwananchi analinda msitu akiamini tofauti na kukata mkaa kuna manufaa ya
hewa safi, mvua na mazingira kwa ujumla,” anasema.
Mwambambale anasema
USMJ na FBE imechangia mapato ya Halmashauri ya Kilosa kuongezeka ambapo hupata
asilimia 10 ya makusanyo ya mazao yanayotokana na misitu jambo ambalo
halikuwepo awali.
Anasema mradi wa TTCS
umekuwa shamba darasa kwa vijiji vingine hivyo wao wanajipanga kusambaza kwa
vijiji vingine ambavyo vina misitu ya vijiji na kwamba haoni sababu ya
kubadilisha mamlaka ya usimamizi kama GN 417 inavyotaka.
Mkurugenzi anasema
kinachohitajika ni changamoto ambazo zipo zinapatiwaufumbuzi na sio kukimbilia
kubadilisha mamlaka ya usimamizi kwani inaweza kuwa sababu ya uharibufu
kuongezeka zaidi.
Anasema kuhusu bei
elekezi kinachohitajika ni usimamizi ambao utahakikisha kila anayejihusisha na
biashara ya mazao ya misitu anafuata taratibu zote.
DED huyo anasema
Serikali Kuu inapaswa kuhamasisha wawekezaji katika sekta ya uhifadhi na namna
ya kuitumia rasilimali misitu kwa njia endelevu kama yanavyofanya mashirika ya
TFCG na MJUMITA kupitia TTCS.
“Nisisitize ili misitu
iwe salama ni lazima vijiji viweze
kunufaika moja kwa moja ila ikiwa ni kusubiri muda mrefu ni dhahiri watashindwa
kuilinda,” anasema.
DNRO
KILOSA
“Mimi kwa muda ambao
nimekuwa hapa Kilosa ninadiriki kusema ‘USMJ ni sawa na kumpa mchawi akulelelew
mtoto hawezi kumloga’ ni maneno ya John Mtimbanjayo Ofisa Maliasili (DNFO).
Anasema miaka saba ya
utekelezaji mradi wa TTCS umeweza kuchochea maendeleo makubwa katika vijiji
huku uhifadhi ukiwa umechukua nafasi kubwa.
“Zaidi ya shilingi
bilioni 1 zimeweza kukusanywa na kutekeleza miradi ya maji, elimu, afya,
utaewala na mingine mingi hali ambayo inawapa nguvu wanavijiji kulinda misitu
yao hivyo iwapo kinachohitajika kwenye GN 417 kitapewa nafasi kuna uwezekano wa
hali kuwa mbaya kimapato na uhifadhi,” anasema.
Mtimbanjayo anasema
vijiji vya Ulaya Mbuyuni, Ulaya Kibaoni, Msumba, Uhombwe, Kisanga, Kigunga,
Nyali, Kitundueta, Mhenda, Mvumi, Zombo, Chabima,, Gongwe, Rudewa Gongani na
vingine vimeweza kufanya mapinduzi ya kiuhifadhi.
DNFO Mtimbanjayo
anasema kuhusu bei elekezi ya GN 417 kunahitaji tafakuri ya kina ili isije kuwa
sababu ya kuchochea uvunaji ambao haufati taratibu zilizopo.
“Bei elekezi hadi sasa
imeshaleta athari kwa wavunaji wa mkaa kwani wapo ambao wanavuna kiholela hali
ambayo inaweza kuzalisha wavunaji haramu katika misitu ya vijiji yenye USMJ na
FBE,” anasema.
DIWANI
VITI MAALUM
Diwani wa Viti Maalum
Halmashauri ya Kilosa, Amina Laizer anasema USMJ na FBE ni mfumo ambao unapaswa
kusambaa nchini kote kwa kuwa unatatua changamoto za jamii na kuchochea
uhufadhi wa misitu.
Anasema vijiji ambavyo
vinatekeleza mfumo huo vimekuwa na mabadiliko makubwa ya kiuchumi, kijamii na
maendeleo jambo ambalo linasababisha halmashauri kuhangaika na vijiji vingine
ambavyo havina miradi ya maendeleo.
“Mimi nimekuwepo kwenye
Baraza la Madiwani kwa misimu miwili ninajua karibu vijiji vyote vya Kilosa
kusema kweli vijiji vyenye kutekeleza USMJ na FBE vimekuwa kwenye utulivu
mkubwa tofauti na ambavyo havina kwani vina uhakika wa kupata fedha na
kutekeleza miradi yake,” anasema.
MTENDAJI
WA KIJIJI ULAYA MBUYUNI
Mtendaji wa Kijiji cha
Ulaya Mbuyuni wilayani Kilosa, Piolon Lyatuu anasema USMJ, umefanya mapinduzi
makubwa katika kijiji hicho kwa kufanikiwa kutatua migogoro ya wakulima na
wafugaji baada ya kuweka mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Pia anasema manufaa
mengine ni ujenzi wa madarasa mawili na ofisi ya mwalimu kwa shilingi milioni
37, wamechimba kisima cha maji chenye urefu wa mita 60 kwa shilingi milioni 20,
ofisi ya kijiji imejengwa kwa shilingi milioni 50, afya wameweza kukatia CHF
kwa kaya zaidi ya 200.
“Tumeboresha uwanja wa
michezo kwa kutumia shilingi milioni moja ambazo zinatoka katika msitu na pia
tunaendelea kuboresha soko ili liwe la kisasa,” anasema.
Anasema kutokana na
manufaa hayo hawaoni sababu ya Serikali Kuu kujihusisha na USMJ moja kwa moja
kwani inaweza kukwamisha hayo ambayo yamepatikana kufanikiwa.
Lyatuu anasema USMJ
ambayo imesambazwa na TTCS imeweza kuwajengea uwezo wavunaji kujua ni aina gani
ya miti ya kuvuna ambayo inaweza kuwa endelevu.
MWENYEKITI
WA KIJIJI ULAYA MBUYUNI
Akizungumzia faida za
USMJ na FBE, Mwenyekiti wa Kijiji Selemani Hashimu anasema anaongoza kwa amani
kwa kuwa wanakijiji hawasumbuliwi na michango kwani msitu wao unatatua
changamoto zote.
Anasema kupitia msitu
wapo kwenye mchakato wa kujenga zahanati ya kijiji kwa shilingi milioni 84 hli
ambayo itaweza kusogeza huduma za jamii karibu na wananchi.
“USMJ na FBE imewezesha
kijiji kuingiza zaidi ya shilingi milioni 100 hali ambayo awali haikuwepo,
kinachotutesa kwa sasa ni kuwepo wavamizi kama saba ambao wanapewa kiburi na
aliyekuwa diwani,” anasema.
Hashimu anasema
Serikali ikiamua kuchukua usimamizi wa misitu inaweza kuchangia uharibufu kuongezeka
kwani ulinzi utapungua na vijiji vitashindwa kujiendesha kama ilivyo sasa
ambapo wananchi wanapanga mambo yao,” anasema.
Anasema kinachohitajika
ni Serikali kuja na mpango ambao utaweza kuendeleza haya yaliyopatikana ili
misitu iweze kuwa endelevu.
KAMATI
YA MALIASILI ULAYA MBUYUNI
Katibu wa Kamati ya
Maliasili Kijiji cha Ulaya Mbuyuni, Victoria Ndekelo anasema pamoja na manufaa
ya USMJ na FBE pia wameweza kujifunza mbinu nyingine za ujasiriamali kama
mpango hisa, kilimo hifadhi hali ambayo inasaidia kujiingizai kipato.
Ndegelo anasema
uhifadhi umeboreka zaidi, ila anaomba Serikali iangalie uwezekano wa kiusimamia
kwa nguvu zote bei elekezi ambayo ipo kwenye GN mpya kwa kuwa vijiji vya ndani
na vinavyofuata utaratibu vitaumia zaidi.
Aidha, anasema yeye
binafsi amenufaika na USMJ na FBE ambapo ameweza kufuga kuku, amejenga nyumba
na uhakika wa milo mitatu hali ambayo awali haikuwepo.
Mohammed Titima
Mwenyekiti wa Kamati ya Maliasili kijijini hapo anasema USMJ kwakwe ni mkombozi
wa maisha kwani amefanikiwa kuanzisha mradi wa ufugaji kuku zaidi ya 300,
kilimo hifadhi na kushiriki mpango hisa kwa uhakika.
Anasema bei elekezi
itakuwa na faida iwapo kila muuza mkaa kijijini ataifuata kinyume na hapo ni
wazi kuwa uharibifu wa misitu utaongezeka zaidi na zaidi.
TFS
WILAYA
Meneja Misitu wa Wakala
wa Huduma za Misitu Wilaya ya Kilosa Samuel Nyabange anasema USMJ pekee haiwezi
kufanikisha uhifadhi hivyo jambo la msingi ni elimu zaidi kutolewa kuhusu
hasara na manufaa ya kutumia rasilimali misitu kinyume na utaratibu.
“Hakuna shaka kuwa USMJ
ni njia sahihi ya kukabiliana na uharibifu wa misitu na mazingira lakini jambo
la muhimu ni kujikita katika kutoa elimu zaidi kwani kokote ambapo kuna
uharibifu lazima wanavijiji wanashiriki,” anasema.
KAMISHNA
MHIFADHI TFS
Akijibu baadhi ya
maswali ya waandishi Kamishna Mhifadhi TFS, Profesa Dos Santos Silayo anasema ushiriki
wa wananchi kupitia kamati za maliasili
za vijiji ni muhimu katika kulinda
misitu ikiwa zitaelimishwa na kuratibiwa vizuri.
“Kamati hizi zinaweza
kwa kiasi kikubwa kulinda misitu iliyoko karibu na vijiji vyao. Suala muhimu ni
elimu na uwazi kwa kuwashirikisha ipasavyo katika maamuzi na hasa kuhusu
faida zitokazo na misitu wanyopaswa kuilinda. Kwa misitu inayoruhusu
uvunaji wananchi wanaweza kupata faida za moja kwa moja kutokana na mazao
yanayovunwa,” anasema.
Anasema tatizo kubwa ni
ushirikishwaji katika misitu isiyoruhusu uvunaji misitu ambayo
ni kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira. “Katika misitu hii ushirikishwaji
umeimarishwa kwa kusaidia wananchi kuanzisha miradi mbadala ya
kiuchumi kama ufugaji wa nyuki juhudi
ambazo zimeonyesha mafanikio katika
kuhifadhi misitu hiyo.
Kuhusu bei elekezi
anasema kwa kiwango kikubwa mkaa hutumika zaidi kwa wakazi
wa mijini maeneo ambayo pia upatikanaji wa nishati mbadala ikiwepo gesi
vinapatikana.
“Kwa maoni yangu mimi
bei elekezi haina tatizo kwani mazao yote ya misitu yana bei elekezi hata magogo ya mbao yamewekewa bei na
serikali. Kuhusu uvunaji holela ambao
umekuwa ukilalamikiwa, uvunaji huu hufanyika kwa wingi kwenye maeneo ya ardhi
huria ambapo hata bila ya kuwepo kwa bei elekezi uvunaji huu utafanyika.
Ufumbuzi wa tatizo hili
sio bei elekezi bali ni usimamiaji wa sheriaa ili kuhakiksha uvunaji unafanyika
katika maeneo yanayoruhusiwa na kwa kuzingatia sharia. Bei elekezi ilipangwa kwa makusudi ya kupunguza matumizi
ya mkaa kwa kuufanya mkaa usiwe rahisi kiasi cha kuwafanya watu wasione umuhimu
wa kutumia gesi na nishati zingine mbadala,” anasema.
Prof. Silayo anasema
kwa mawazo yake anadhani tunapaswa kuongeza bei ya mkaa unaotokana na miti ya
asili zaidi ili kushawishi watu watumie nishati mbadala au kuzalisha mkaa
kutoka katika miti ya kupandwa inayokua haraka ili kuepusha nchi yetu kugeuka
jangwa.
Aidha, kuhusu Kanuni kudaiwa
kwenda kinyume na Sheria ya Vijiji vya mwaka 2002 ambayo katika 1(b) inasema
kwamba lengo la sheria hiyo ni pamoja na kuhamasisha katika kupanga, kusimamia,
kutumia na kuhifadhi rasilimali za misitu kiendelevu kupitia haki ya maendeleo
kwa mtu mmoja mmoja na jamii kama ilivyoelekezwa kwenye sheria ya kimila au
sheria ya misitu ya mwaka 2002 katika kutumia na kusimamia rasilimali za
misitu. Kwa nini wananchi wasiendelee
kujipangia bei zao na ushuru.
Profesa anasema wanapozungumzia
suala la biashara ya mkaa tusilichukulie
kiurahisu tu kuwa mkaa ni bidhaa ya kuuzwa sokoni, ni vyema tukaangalia
biashara ya mkaa kama biashara ambayo inapaswa kufanywa kwa umakini sana
kutoana na madhara ya biashara hiyo kimazingira.
“Badala ya kuhamasisha biashara
ya mkaa tunapaswa kufanya udhibiti kwani kushamiri kwa biashara holela ya mkaa ni kuchocheo kikubwa cha uharibifu wa
mazingira. Biashara hii ni lazima iwekewe utaratibu na serikali ikiwepo
kuwekewa masharti na bei elekezi ya
bidhaa hiyo ili kutunza mazingira.
Kuruhusu kila Kijiji
kijipangie bei kitakayo kutavutia watu wengi kukimbili vijiji ambavyo vimejipangia
bei ndogo na kuacha kazi rafiki wa
mazingira na kuanza kufanya kazi ya kuchoma mkaa jambo amblo linaweza kuathiri hali ya
hewa na kuchochea mabadiliko ya tabia ya nchi,” anasisitiza.
Kamishna Silayo anasema
kwa mujibu wa sheria ya misitu Mkurugenzi wa misitu amepewa malaka kusimamia
msitu yote hapa nchini. Tangazo la Serikali Na 417 kama mwenyewe
ulivyosema linalenga kuboresha usimamizi
na uendeleza wa misitu kwa kusisitiza umuhimu wa kuwa wa mipango ya usimamizi misitu na kuzuia
uvunaji holela wa misitu.
Kwa mamlaka aliyopewa
kwa mujibu wa sheria mkurugenzi wa
misitu anapaswa kuidhinisha mipango ya uvunaji ambao utakuwa umeandaliwa na
wamiliki wa msitu sharia kanuni na miongozo kwa kuhakikisha kuwa mipango hiyo
inafuata mwongozo kuapelekea kuwepo kwa uvunaji wa mazao ya misitu.
Anasema wananchi na wamiliki
hawapaswi kuwa na woga kwani mkurugenzi anaizinisha mipango ya usimamizi wa misitu kuhakikisha
inakidhi matakwa ya kisheria unazingaztia muongozo kabla ya kuruhusu uvunaji. Wajibu huu hauwapokonyi
wananchi mamlaka ya matumizi ya msitu wao bali unawataka watimize wajibu wao wa
kuhakikisha kuwa uvunaji unakuwa endelevu.
No comments:
Post a Comment