HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 05, 2020

WANANCHI WILAYA YA KILOLO WAIPONGEZA SERIKALI

Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Asia Abdalah, akikata utepe kuzindua kikundi cha mradi wa vijana alichoanzisha kwa ajili ya wananchi wa kijiji cha Wotalisoli.


Na Denis Mlowe, Kilolo

WANANCHI wa Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa wameipongeza serikali ya Awamu ya Tano mara baada ya kushuhudia ujenzi wa miradi  mbali mbali ya maendeleo ikiwemo  vituo vya afya, zahanati, na  kujengwa  hospitali kubwa ya wilaya kuanza kufanya  kazi na kuwapunguzia adha walizokuwa kipata kupata huduma za afya.

Wakizungumza wakati wa ziara ya Mkuu wa wilaya ya Kilolo, Asia Abdallah yenye lengo la kukagua miradi ya maendeleo na kuzindua vikundi vya vijana alivyovianzisha katika kata zote wananchi hao walisema kuwa kufunguliwa kwa Hospitali ya Wilaya ya Kilolo, kumepunguza adha kwa akina mama wajawazito ya kusafiri umbali mrefu kufuata Huduma ya Afya, kwenye Hospitali ya Rufaa Mkoani Iringa.

Baadhi ya wananchi hao Damian Mwenda na Lufumiko Leonard walisema kuwa katika awamu ya tano wameshuhudia ujenzi wa vituo vya afya na zahanati mbalimbali zikijengwa na hospitali kubwa ya wilaya ikikamilika kwenye awamu hii ya tano chini ya Rais John Magufuli hali ambayo imeleta maendeleo makubwa kwa nchi.

Damian Mwenda alisema kuwa Rais Magufuli amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kufanya yale aliyoahidi hali ambayo wananchi wengi wamekuwa wakimpenda na kumwaahidi kumwongezea miaka mitano katika uongozi wake kwani maendeleo yanaonekana.

“ Chini ya Magufuli maisha yamekuwa safi kabisa kwani katika wilaya ya Kilolo kwa sasa kama unavyoona miradi mbalimbali imejengwa hasa vituo vya afya kw a kila kata hali ambayo tunampongeza sana rais na chini mkuu wa wilaya Asia Abdalah tunaona mabadiliko makubwa sana” alisema

Alisema kuwa awali walikuwa wakitumia gharama kubwa sana kuwasafirisha ndugu jamaa na marafiki pindi wakiumbwa na kina mama wajawazito kwenda hospitali ya rufaa lakini tangu kuingia kwa Magufuli hali imekuwa tofauti sana kwa wananchi wa Kilolo.

Naye Lufumiko Leonard alisema kuwa kwa sasa wilaya ya Kilolo chini ya Asia Abdalah imekuwa mfano bora kwa kuwa na huduma muhimu za afya, maji ambayo yalikuwa tabu ila kwa sasa hali safi na kutolea mfano wa ujenzi wa tenki kubwa la maji lililopo Ilula ambalo limekamilika kwa asilimia 90 kitu ambacho awali maji ilikuwa shida sana.

Alisema kuwa licha ya huduma ya maji kulikuwa na changamoto ya huduma za afya lakini ujenzi wa hospitali ya wilaya na kuboreshwa kwa vituo vya afya na zahanati katika kata mbalimbali kumesaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa adha walizokuwa wakizipata awamu zilizopita.

Akizungumza kuhusu utolewaji wa Huduma kwenye Hospitali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Asia Abdala amesema, Hospitali hiyo ina wataalamu wa kutosha pamoja na vifaa tiba, na tayari umeanza kuwahudumia wagonjwa.

Alisema kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya jemedari rais John Magufuli imefanikiwa kujipambanua katika kuwaletea maendeleo wananchi hasa katika huduma zote muhimu zikiwemo za afya, shule, maji na ujenzi wa miundo mbinu ambayo awali ilikuwa katika hali mbaya na kwasasa serikali imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutekeleza ahadi zake kwa wananchi.

Asia Abdallaha alisema kuwa kufunguliwa kwa Hospitali ya Wilaya ya Kilolo, kumepunguza adha kwa akina mama wajawazito ya kusafiri umbali mrefu kufuata Huduma ya Afya, kwenye Hospitali ya Rufaa Mkoani Iringa na huduma katika hospitali ya wilaya, zahanati na vituo vya afya zimeboreshwa na Rais John Pombe Magufuli kwani madawa yanapatikana na watoa huduma wapo hivyo kumshukuru Rais John Magufuli kwa kuwapati miradi hiyo.

Akiwa katika ziara hiyo Asia alikutana na wafanyakazi na madaktari wa vituo vya afya na zahanati ambapo  Daktari mfawidhi Dkt.  Selemani Jumbe  alizungumza juu ya kuwa na vifaa vya kufanyia kazi kama vile Full Blood Picture Machine, Ultra Sound, Na X-ray ambavyo anasema kwa wilaya nzima hakuna huduma ya X-ray hivyo inawawia vigumu kukamilisha tiba kwa wagonjwa wenye kuhitaji huduma hiyo.

DC Asia pia alikutana na wazee wa mji wa Kilolo ambao  wameiomba serikali kuwapatia watalaamu pamoja na vifaa vya upasuaji kwa kuwa tayari walishapata jengo la upasuaji kutoka kwa mdau wa maendeleo ila  wanakwama kuanza kutumia huduma hiyo ya upasuaje kufuatia ukosefu huo wa wataalamu na Vifaa.

Akiwajibu wazee hao Mkuu wa Wilaya huyo aliwaahidi kufuatilia na kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo, huku akitoa wito kwa wananchi kuendelea kutunza miundombinu iliyopo wilayani humo kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Akizungumza kuhusu mafanikio ya miaka mitano ya serikali ya Rais John Magufuli kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Mkuu wa Wilaya hiyo kwenye sekta ya elimu, Asia Abdala alisema elimu bure, imesaidia kuongezeka kwa uandikishaji wa wanafunzi kuanzia ngazi ya msingi mpaka sekondari, kwa halmashauri ya Wilaya ya Kilolo ambapo kwa shule ya msingi wanafunzi 8949 wamesajiliwa mwaka 2019 ukilinganisha na wanafunzi 7295 mwaka 2015.

Alisema kuwa kutokana na ongezeko hilo la wanafunzi wamefanikiwa kujenga vyumba vya madarasa 247 ili kukidhi uhitaji wa madarasa kwenye shule tofauti.

Kuhusu ufaulu wa wanafunzi kwenye masomo yao Asia amesema, ufaulu umeongezeka kwa asilimia 81.12 kwa mwaka 2019 ukilinganisha na asilimia 51 kwa mwaka 2015, huku, shule za sekondari zikiongeza ufaulu kwa asilimia 90.5 ukilinganisha na asilimia 71.14 kwa mwaka 2015.

Mmoja ya wazazi Mussa Hussein mkazi Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, alisema kuwa elimu bure imeleta unafuu wa Maisha kwa kuwa wameweza kuwasomesha watoto wao mpaka kidato nne kwa kutumia gharama ndogo ya kununua sare za shule na vifaa vya kutumia darasani.

No comments:

Post a Comment

Pages