Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions ya Dar, Alex Msama, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Agosti 21, 2020 kuhusu maandalizi ya tamasha la kuombea Uchaguzi Mkuu wa Tanzania litakalofanyika Agosti 23 kwenye Uwanja wa Uhuru.
DAR ES SALAAM, TANZANIA
MAANDALIZI ya Tamasha la kuombea Uchaguzi Mkuu wa Tanzania utakaofanyika Oktoba 28, 2020, litakalofanyika Jumapili hii ya Agosti 23, yanaendelea vizuri, huku waratibu wakisisitiza usalama tamashani sambamba na kuongeza idadi ya waimbaji.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions ya Dar, Alex Msama, amewahakikishia wahudhuriaji usalama wao na mali zao, huku akiongeza waimbaji na kualika watu wa dini nyingine.
“Maandalizi yanaendelea vizuri na waimbaji watakaotumbuiza wanaendelea kujifua ili kukata kiu ya watakaohudhuria, nasi kama waratibu wa tamasha, tumeongeza idadi ya wasanii watakaotumbuiza siku hiyo ya kuombea Uchaguzi Mkuu,” amesema.
Ukiachana na Bonny Mwaitege, Christopher Mhangira, Christina Shusho na Rose Mhando aliowataja siku ya utambulisho wa tamasha hilo lisilo la kiingilio, Msama amewaongeza Martha Mwaipaja, Upendo Nkone, Faustine Munishi na Mercy Changula.
“Huyu Faustine Munishi anayetambulika na wengi kwa wimbo wa Malebo, atakuja tamashani na Malebo mwenyewe ili watu wamuone huyo aliyemuimba katika wimbo wake huo,” alisisitiza Msama huku akisema usalama utakuwa mkubwa.
Kuhusu usalama wa watu watakaohudhuria, mali zao na familia zao kwa ujumla, Msama alisema: “Kutakuwa na usalama wa hali ya juu kutoka kwa askari wa Jeshi la Polisi na askari wa kampuni binafsi ili kuhakikisha kila anayeingia anakuwa salama.”
“Tunawaalika watu wa madhehebu na dini nyingine waje, hili ni tamasha la Watanzania. Waje ili kwa pamoja tuliombee taifa letu, tuuombee Uchaguzi Mkuu uende kwa salama na amani,” alisema Msama anayeratibu pia Matamasha ya Pasaka na Krismasi.
Akimuelezea Rose Mhando, Msama alifichua kuwa nyota huyo amejipanga kwa maandalizi makali, kutumbuiza nyimbo za Injili za zamani na mpya na kwamba kama ratiba zitaruhusu, basi atalitumia tamasha hilo kuzindua albamu yake mpya.
No comments:
Post a Comment