Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema utakapokamilika mradi wa ujenzi wa Bandari ya Shumba Mjini utafungua fursa za kiuchumi kwa Wananchi wa Micheweni na Kisiwa cha Pemba kwa Ujumla.
Ameyasema hayo katika ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo inayojengwa katika Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Amesema kukamilika kwa bandari ya Shumba Mjini itakifungua Kisiwa cha Pemba kiuchumi kwa kuzalisha ajira na kukuza biashara jambo ambalo litaimarisha Pato la mtu mmoja mmoja na Taifa sambamba na kujenga ustawi bora wa maisha ya wananchi.
Makamu wa Pili wa Rais amewatoa hofu wananchi wa Shumba Mjini waliopisha ujenzi wa bandari hio kuwa kipindi kifupi kijacho Serikali itawalipa fidia zao kulingana na tathmini za maeneo na vipando vyao.
Aidha Mhe. Hemed ameuagiza uongozi wa Shirika la Bandari Zanzibar ( ZPC ) kuhakikisha malipo yote bandarini hapo yanalipwa kwa njia ya mifumo ili kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali pamojana na kuwataka ajira ambazo hazihitaji utaalamu na hazikinzani na kanuni na Miongozo ya ZPC wapatiwe wananchi wa Fumba Mjini ili waweze kufaidika na uwepo wa bandari hio.
Hata hivyo amewataka wannachi wa Shumba Mjini kushajihishana kuilinda amani ilipo nchini na kuwasisitiza kuacha tofauti zao za kisiasa na badala yake washirikiane katika harakati za kimaendeleo.
Nae Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar Mhe. Badria Atai Massoud amesema Bandari ya Shumba Mjini itaiwezesha Zanzibar kuwa kitovu cha Biashara kwa Ukanda wa Afrika Mashariki, kuimarika kwa Utalii na kukuza uhusiano mwena na Mataifa jirani.
Mhe. Badria amewashukuru wananchi wa shumba mjini kwa kukubali kupisha ujenzi wa bandari hio lakini pia kwa ushirikiano wao mkubwa wanaoendelea kuutowa katika kipindi chote cha ujenzi wa bandari hio na miradi mengine ya Maendeleo inayojengwa kijijini hapo.
Kwa upande wake mshauri elekezi kutoka kampuni ya Anova Consulting LTD Mhandisi Serafina Michael amesema bandari ya Shumba Mjini inatarajiwa kutoa huduma ya usafirishaji wa abiria na mizigo na kukadiriwa kuhudumia takriban abiria 1500 kwa wakati mmoja.
Mhandisi Michael amefahamisha kuwa kwa awamu ya kwanza ujenzi wa bandari hio utajumuisha Jengo la Abiria, Gati, Diko kwa ajili ya wavuvi, eneo la kufanyia Ibada na hadi kukamilika kwakwe itagharimu Shilingi za Kitanzania Bilioni 11.6.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa shumba Mjini Hussein Rashid Hussein amesema changamoto kubwa inayowakabili ni kuchelewa kulipwa fidia zao ambazo zingewawezesha kutafuta maeneo mengine ya makaazi pamoja na kufanya biashara zao hivyo ameiomba Serikali kuipatia ufumbuzi changamoto yao hio.
Hata hivyo Bwana Rashid ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendelea kujenga miradi mbali mbali ya maendeleo katika kijiji cha Shumba Mjini ambayo inakwenda kustawisha maisha ya wananchi na kuwakwamua na umasikini.
Awali Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikagua ujenzi wa Mahkama ya Wilaya inayojengwa Konde, Wilaya ya Micheweni na kumuagiza Mkadarasi ya ujenzi huo kampuni ya Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar (JKU ) kuhakikisha ifikapo tarehe 30 Ogosti ujenzi huo uwe umakamilika kwa viwango vilivyokusudiwa kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba.
Mhe.Hemed ametoa onyo kali kwa wakandarasi wasioheshimu mikataba ya ujenzi na kuwata kuacha tabia ya kuomba muda wa ziada ambao haupo katika makubaliano ( extension )kufanya hivyo ni kukwamisha mipango ya Serikali ya kuwaletea wananchi wake maendeleo.
Akikagua ujenzi wa Dakhali ya wanafunzi inayojengwa katika skuli ya Sekondari Micheweni pamoja na ujenzi wa skuli ya Msingi Micheweni, Makamu wa Pili wa Rais ameiagiza Wizara ya elimu na mafunzo ya Amali Zanzibar kuhakikisha dakhalia zote zinazojengwa Unguja na Pemba haziekwi Soketi za umeme katika vyumba vya kulalia wanafunzi ili kuepusha majanga ya mara kwa mara ya kuungua moto sambamba na kudhibiti usalama wa wanafunzi wanapokuwa kambini.
Ameahidi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa kila aina ya ushirikiano kwa wakandarasi wanaojenga miradi mbali mbali ya maendeleo Unguja na Pemba ili kuona miradi hio inajengwa kwa viwango bora na kukamilika kwa wakati uliokusudiwa.
Katika ziara hio makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amekagua miradi inayojengwa katika wilaya Micheweni kama vile UJENZI WA BANDARI YA SHUMBA MJINI, UJENZI WA MAHAKAMA YA WILAYA YA MICHEWENI, BARABARA YA KONDE MAKANGALE, UJENZI WA DAKHALIA MAZIWA NG’OMBE PAMOJA NA UJENZI WA SKULI YA GHOROFA MICHEWENI MSINGI.


.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)


No comments:
Post a Comment