HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 19, 2020

NMB YATOA GAWIO KWA SERIKALI SH BILION 15.2

Waziri wa  Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, akipokea mfano wa hundi  ya Sh. Bilioni 15.2 kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya NMB, Dk. Edwin Mhede (wa pili kushoto), ikiwa ni gawio kwa Serikali wakati wa hafla iliyofanyika leo Agosti 19 Wizara ya Fedha jijini Dodoma. Kushoto ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna na wa pili kulia  ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Mary Maganga. Wa kwanza kulia ni Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka.

Waziri wa  Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, akimkabidhi mfano wa hundi  ya Sh. Bilioni 16, Ofisa wa Ubalozi wa Uholanzi nchini, Mathis van Eeuwen (kushoto), iliyotolewa na Benki ya NMB kwa Rabo Bank Group. Wengine  katika picha kutoka kushoni ni Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya NMB, Dk. Edwin Mhede na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo, Ruth Zaipuna.


DODOMA, TANZANIA 

 
BENKI ya NMB imetoa shilingi
bilioni 15. 2 kama gawio kwa Serikali ya Tanzania ambayo inamiliki asilimia 31.8 ya hisa zote ndani ya benki hiyo. 

 

Kiasi hicho ni ongezeko la asilimia 45 ya gawio lililotolewa mwaka uliopita ambazo Serikali ilipata Sh. bilioni 10.48 zilizotokana na faida ya mwaka 2018.
 

Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, alisema kuwa fedha zilizokabidhiwa ni sehemu ya faida iliyopatikana katika mwaka wa fedha 2019 baada ya kuondoa gharama na kodi ambayo ilikuwa shilingi bilioni 45.

Zaipuna amesema mbia mwingine ni Benki ya Rabo ya nchini Uholanzi imepata gawio la shilingi bilioni 16. 8, huku shilingi bilioni 16 zikienda kwa wawekezaji wengine ikiwemo taasisi za Serikali. 

 

Alisema kwa mwaka 2019 licha ya benki kuwa chini ya uongozi wa mpito, lakini iliendelea kufanya vizuri na hata kipindi cha corona bado waliendelea kufanya vizuri kwani katika nusu ya mwaka wa fedha 2020 NMB wameshasajili faida ya shilingi bilioni 93.

Kwa mujibu wa mtendaji huyo, wameshaanza mkakati wa kuinua kilimo nchini na tayari wamekopesha wakulima shilingi bilioni 800 huku wafanyabiashara wakikopa shilingi
trilioni 2.2. 

 

Nyingine ni ununuzi wa madawati 40,000 na kompyuta 1,000 zilizotolewa kwa ajili ya kusaidia shule mbalimbali na kuwa wameendelea kuwa benki bora kwenye tuzo za jarida la kimataifa la Euro Money kwa miaka 8 mfululizo.

Akipokea mfano wa hundi hiyo, Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango, alisema kiwango kilichotolewa ni kizuri na kuna matumaini makubwa ya gawio kupanda kwa mwaka huu. Dk. Mpango aliitaja Benki ya NMB kuwa miongoni mwa taasisi zinazofanya vizuri zaidi.

Awali Mwenyekiti wa Bodi ya NMB, Dk. Edwin Mhede, aliahidi benki hiyo itafanya vizuri zaidi mwaka ujao baada ya kupata Ofisa Mtendaji Mkuu, kwani alipokuwa akikaimu hakuwa na nguvu zaidi katika maamuzi, hivyo, wanaamini benki hiyo itaendelea kuwa imara zaidi na kuwa mfano kwa mabenki mengine nchini.

No comments:

Post a Comment

Pages