HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 18, 2020

WAZIRI MKUU: WATANZANIA TUBADILIKE, TUJIVUNIE VYETU

*Akagua mradi wa kiwanda cha sukari na shamba la miwa Bagamoyo

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wabadilike na wajifunze kujivunia kilicho chao. "Lazima tubadilike Watanzania, tuwe wazalendo, tukisemee kitu chetu, tujivunie kitu chetu na tujivunie ujuzi tulionao," amesema.

 

Ametoa wito huo leo (Jumanne Agosti 18, 2020) wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wa mkoa na wafanyakazi wa kiwanda cha sukari cha Bagamoyo (BSL), katika kata ya Makurunge, wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani.

 

Waziri Mkuu ambaye alifika kiwandani hapo na kukagua ujenzi wa kiwanda unaoendelea, pia alikagua miundombinu ya mradi wa shamba la miwa ikiwemo vitalu vya mbegu, miche, maabara ya kupima maji na udongo na miundombinu ya umwagiliaji.

 

"Ninasema tubadilike sababu nimeenda kwenye maabara yao na kukuta wataalamu wetu wako vizuri, wanafanya utafiti wa udongo, maji na mbegu. Wameelezea vizuri utafiti wao na matokeo tumeyaona ni mazuri.”

 

“Rais wetu alisema Watanzania tunaweza, na leo nimethibitisha kwamba Watanzania tunao uwezo wa kazi lakini tatizo letu hatuwezi kujisemea wenyewe. Lazima tujisifu, tujisemee kuhusu umahiri tulionao. Ni kwa nini tujidharau?", alihoji.

 

"Nataka tubadilike sababu Watanzania tunaweza. Baadhi yao wanatoka hapa hapa Bagamoyo. Nimemuuliza ulisoma wapi, akajibu Chuo cha Kilimo Kaole, na hiki kiko Bagamoyo. Wengine wanatoka SUA (Chuo cha Kilimo cha Sokoine). Lazima turingie nchi yetu, lazima tuitangaze nchi yetu na ni lazima tuisemee nchi yetu," amesisitiza.

 

Waziri Mkuu amesema uamuzi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kutoa eneo hilo lenye hekta 10,000 ili lilimwe miwa na kujenga kiwanda cha sukari, ulilenga kuongeza uzalishaji wa sukari nchini. "Tunahitaji kupata mashamba mengi ya miwa ili tuongeze uzalishaji wa sukari nchini".

 

“Hivi sasa mahitaji ya suakri nchini yamefikia tani 450,000 kwa sukari ya mezani. Ile sukari ya viwandani ambayo inatumika kutengeneza soda, biskuti na pipi mahitaji yake ni tani 165,000 ambayo hapa nchini hatuizalishi, kwa hiyo inabidi tuiagize kutoka nje ya nchi.”

 

Amesema uzalishaji wa sukari ya mezani kwa sasa unafikia tani 380,000 kwa viwanda vyote vilivyopo na kwamba bado kuna bakaa ya tani 70,000. Amesema mbali ya viwanda vilivyopo vya TPC, Kagera, Mtibwa, Kilombero, Manyara na Bagamoyo bado kuna maeneo ya kulima miwa huko Tarime na Kigoma. “Tunawaalika wawekezaji walime miwa na kuzalisha sukari zaidi.”

 

Akielezea kuhusu ujenzi wa kiwanda hicho, Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na kazi inayofanyika na kwamba kukamilika kwa mradi huo kutahakikisha sukari inapatikana kulekule na pia itatoa fursa ya kilimo cha miwa kwa wakazi wa maeneo jirani.

 

Amewataka maafisa kilimo waende wakatoe elimu kwa wananchi kuhusu kilimo cha miwa. “Wapeni uhakika wa soko ili wasisite kushiriki kwenye hiki kilimo. Wananchi watavutiwa wakijua kuna faida kwenye kilimo hicho lakini pia kiwanda kitapata tani za ziada na kuongeza uzalishaji wake,” amesisitiza.

 

Mapema, Mkurugenzi wa Makampuni ya Bakhresa, Bw. Abubakar Bakhresa alimshukuru Rais Magufuli kwa kuwapatia shamba hilo na kuahidi kuendana na dhamira ya Serikali ya kupunguza tatizo la upatikanaji wa sukari nchini.

 

Akielezea hatua zilizofikiwa kwenye mradi huo, Mkurugenzi wa Mahusiano wa Makampuni ya Bakhresa, Bw. Hussein Sufian alisema gharama ya mradi huo ni dola za Marekani milioni 100 na kwamba hadi sasa wameshapata asilimia 70 ya mtaji.

 

“Benki ya Kilimo (TADB) imetukopesha dola za Marekani milioni 6.5, Benki ya CRDB wametukopesha dola za Marekani milioni 25, makampuni ya Bakhresa tumetoa dola za Marekani milioni 30 na benki ya Standard Chartered imetukopesha dola za Marekani milioni 10. Tunayashukuru mabenki za ndani kwa kukubali kutuunga mkono,” alisema.

 

Alisema kampuni yao mpaka sasa imetoa ajira kwa watu 600 ambapo 500 kati yao wanatoka kwenye vijiji jirani vinavyozunguka eneo la mradi na kwamba mara baada ya awamu ya kwanza kukamilika, uzalishaji utakapoanza wataweza kuajiri watu 1,500. “Awamu ya pili inatarajiwa kuwahusisha wakulima wa nje (outgrowers scheme) kwani mradi utawapa fursa ya kushiriki kilimo cha miwa na kupata soko la uhakika kutoka kiwandani,” alisema.

 

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justin alisema mbali ya kiwanda hicho cha sukari, wamelenga pia kuwanufaisha wakulima wadogo wa miwa. “Kwa kawaida wenye mabenki wanaamini ili aweze kumkopesha mkulima ni lazima aone eneo lake analomiliki.”

 

“Sisi tumeona fursa, na tumeamua wakulima watakaopata mikataba baina yao na kiwanda cha sukari Bagamoyo, tutachukua mikataba hiyo iwe dhamana ya kupata mikopo ya kuendeleza mashamba yao. Hii ni kwa sababu kuna vijiji vitano tayari vimefanyiwa upimaji na kuna uwezekano wa hekta 3,600 zitakazotumika kulima miwa.”

 

Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, alisema anamshukuru Rais Magufuli kwa uamuzi wake wa kutoa eneo hilo ili BSL ianzishe kilimo cha miwa. “Tunamshukuru kwa sababu ametuongezea zao jingine la biashara.”


“Kabla ya hapo, tulikuwa na zao la korosho ambalo mwaka jana limewaingizia wakulima shilingi bilioni 60. Pia zao la ufuta liliwaingizia shilingi bilioni 19. Mwaka huu umetuita Tanga na kutuelekeza tuanzishe zao la mkonge, kwa hiyo kilimo cha miwa kimekuwa zao la nne mkoani kwetu na hivi sasa kuna kata tano ambazo ziko tayari kulima miwa.”

 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua shamba la miwa la  Bagamoyo Sugar Limited linalomilikiwa na Makampuni ya Bakhresa wakati alipotembelea mradi  wa ujenzi wa kiwanda cha kusindika sukari na shamba la miwa la Kampuni hiyo wilayani Bagamoyo, Agosti 18, 2020. Wa pili kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Makampuni ya Bakhresa, Abubakar Bakhresa,  wa tano kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarest Ndikilo, Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Kawawa na wa nne kushoto ni  Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Makampuni ya Bakhresa , Hussein Sufian. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

No comments:

Post a Comment

Pages