Rais wa Tanzania John Magufuli amesema kuwa kwa mara ya kwanza mwaka 2019, Sekta ya Madini iliongoza kwa kuchangia Fedha za Kigeni kwenye pato la Taifa kiasi cha Dola za Marekani Bilioni 2.7.
Rais Magufuli ameyasema hayo wakati akifungua bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzanua ambapo alisema analipongeza Bunge la 11 kwa kufanikisha kupatikana kwa mafanikio hayo ikiwa ni pamoja na kutunga Sheria.
Aidha alisema kumekuwa na mafanikio makubwa katika Sekta ya Madini kwa kuongeza mapato kutoka Shilingi Bilioni 168 Mwaka 2014/2015 hadi shilingi bilioni 527 Mwaka 2019/2020.
"Mchango wa Sekta ya Madini kwenye pato la Taifa ulikuwa kutoka Asilimia 3.4 Mwaka 2015 hadi kufikia 5.2 Mwaka 2019. Katika kipindi cha miaka 5 ijayo tutaendelea kuimarisha usimamizi wa rasilimali madini kama tulivyofanya Mirerani kwa kujenga ukuta kuzunguka machimbo ya madini," alisema
Alisema nchi imebarikiwa kuwa na madini mbalimbali ikiwemo bati, gesi pamoja na Helium ambayo ipo Mkoani Rukwa.
"Rukwa kuna kiasi kikubwa cha Helium ambayo inatosha kusambaza dunia nzima kwa Miaka 20. Ndiyo maana nasema sisi ni matajiri," alisema
Vilevile Rais Magufuli alisema wanakusudia kufanya majadiliano na wawekezaji wakubwa kama walivyofanya kwa Kampuni ya Barrick.
"Katika kipindi cha Miaka 5 ijayo tutaendelea kuimarisha Shirika letu la Madini Stamico ili lishiriki katika shughuli za madini kikamilifu ikiwemo kuwasaidia wachimbaji wadogo.
"Tutafuta leseni zote za madini kwa wasiozifanyia kazi na maeneo hayo tutawapa wachimbaji wadogo. Tutaendelea kuimarisha masoko ya madini, kusimamia viwanda vya uyeyushaji, usafirishaji, tunataka kila bidhaa za madini zitengenezwe hapa nchini. Tunataka kutengeneza uchumi wa kutosha na ajira," alisema
No comments:
Post a Comment