Mkurugenzi Msaidizi wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania(TFCG)Emmanuel Lyimo akizungumza alipokuwa akifungua rasmi semina ya mafunzo ya masuala ya jinsia ambayo yameandaliwa na shirika hilo kwa ajili ya kuwajengea uwezo na uelewa waandishi wa habari kutambua mambo yanayohusu jinsia na jinsi katika shughuli mbalimbali zikiwemo za ushiriki wa wanawake na wanaume katika usimamizi wa misitu ya asili nchini.
Ofisa Uhusiano na Mawasiliano kwa umma kutoka TFCG, Bettie Luwuge (wa kwanza kushoto), akiwa na washiriki wengine wa semina ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuhusu masuala ya jinsi na jinsia ambayo inafanyika mkoani Morogoro.
Meneja Mradi wa Kuhifadhi Misitu kwa Kuwezesha Biashara Endelevu ya Mazao ya Misitu (CoFoREST) kutoka TFCG Charles Leonard akielezea mikakati ya shirika hilo katika kutekeleza miradi mbalimbali inayohusu usimamizi wa misitu ya asili nchini na namna ambavyo wamejipanga katika kuendeleza miradi iliyoanzishwa katika maeneo ya miradi kwa kushirikiana na wananchi wa maeneo husika pamoja na Serikali.
NA SULEIMAN MSUYA, MOROGORO
WAANDISHI
wa habari nchini wameshauriwa kuandika habari za Usimamizi Shirikishi
wa Misitu ya Jamii (USMJ) kwa kuzingatia usawa wa kijinsia ili kuchochea
maendeleo kwa jamii husika.
Ushauri
huo umetolewa na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine
(SUA), Profesa John Jeckoniah wakati akitoa mafunzo kwa waandishi wa
habari kutoka kwa vyombo vya habari mbalimbali nchini.
Alisema
mafunzo hayo jinsia ambayo yameamdaliwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu
ya Asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa Usimamizi wa Misitu ya Jamii
Tanzania ((MJUMITA) yataweza kubadilisha uelewa wa waandishi wa habari
nchini kwa kuandika habari zenye usawa na uwiano.
Prof.Jeckoniah
iwapo waandishi wa habari wakijengewa uwezo katika eneo hilo wataweza
kutoa habari zenye tija na kuchochea mabadiliko kwa jamii kwa ujumla.
Alisema
uwiano wa masuala ya kijinsia nchini bado upo chini hivyo njia sahihi
ya kufanikiwa katika eneo hilo ni kuwajengea uwezo waandishi ili wawe na
uwanja mpana katika kuripoti hasa kwenye USMJ.
"Katika
hali ya maendeleo nchini uwiano wa kijinsia bado haupo vizuri pamoja na
ukweli kuwa wanawake wanaweza kufikia rasilimali ila uamuzi wa mwisho
kuhusu matumizi ya rasilimali inabakia kwa wanaume jambo ambalo
linapaswa kupingwa na wadau wote," alisema.
Alisema juhudi za kubadilisha jamii zinafanyika kwa kuwajengea uwezo wahusika wote ili kwenda kwa pamoja.
"Serikali
imekuwa ikifanya jitihada kwa kuandaa sera, sheria na miongozo ila
tatizo kubwa lipo ngazi ya chini za utekelezaji hivyo wanawake kuwa
waathirika wakubwa na njia ya kutoka hapo ni waandishi kutumia nafasi
zao kubadilisha," alisema.
Mhadhiri
huyo alitoa rai kwa wawakilishi wa wananchi kuzingatia masuala ya
kijinsia katika mipango ya maendeleo ili kuchochea maendeleo.
"Viongozi
wapya ambao wamepewa nafasi na wananchi wanapaswa kujikita katika
kuelewa kwa kina namna ya dhana ya jinsia inavyoweza kuchochea maendeleo
kwa jamii ikiwemo inayojihusisha na USM," alisema.
Mkurugenzi
Msaidizi wa TFCG, Emmanuel Lyimo alisema mafunzo hayo kwa waandishi wa
habari kuhusu jinsia ni moja ya mkakati wao kwenye Mradi wa Kuleta
Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS) ambao umechochea mabadiliko
makubwa kwenye USM.
Alisema
mikakati mingine ni kuchochea shughuli za maendeleo, kulinda mazingira,
mawasiliano na uraghibishi, ushirikiano na wadau mbalimbali na kujenga
taasisi imara yenye nguvu.
"Imani
yetu ni kwamba kupitia mafunzo haya waandishi mtakuwa na uelewa mpana
wa kuandika habari za jinsia hasa kwenye eneo la USMJ," alisema.
Meneja
Mradi wa TTCS, Charles Leonard alisema mradi huo ulijikita kuwainua
wananchi kwa kuzingatia usawa wa kijinsia jambo ambalo limesaidia uwe
unapokelewa vizuri katika maeneo mengi.
Leonard alisema awamu ya kwanza na ya pili wamefanikiwa kuwepo kwa matumizi bora ya ardhi kwenye hekta 130,000.
"Pia
mradi umechochea uhifadhi wa misitu kwenye vijiji, kukuza uchumi wa
wanavijiji na kijiji kwa ujumla na kukabiliana na mabadiliko ya tabia
nchi," alisema.
Alisema
kwa sasa wanatekeleza awamu ya tatu ya mradi ambao unajulikana kama
Mradi wa Kuhifadhi Misitu kwa Kuwezesha Biashara Endelevu ya Misitu
(CoFoREST).
Meneja huyo
alisema mradi wa CoFoREST utahusisha wilaya nyingi zaidi huku mkazo
ukijikita kwenye kuwajengea uwezo watumishi na wataalam kutoka
Serikalini ili watekeleze mradi wenyewe.
No comments:
Post a Comment