HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 17, 2021

WATEMBEA UMBALI MREFU KUFUATA HUDUMA ZA AFYA

 Na Lydia Lugakila, Muleba

Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Katembe wilayani Muleba mkoani Kagera wameomba halmashauri ya wilaya hiyo kuwakamilishia ujenzi wa zahanati yao ambayo waliianzisha kwa nguvu zao kwa kushirikiana na shirika la Tanapa Rubondo tangu mwaka 2020.

Wakizungumza mbele ya kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya hiyo baada ya kutembelea jengo hilo  wananchi hao wamesema kuwa kwa sasa wanapata huduma za afya katika kijiji jirani cha Nyakabango na kata jirani ya Kimwani hivyo baadhi yao wanapata adha ya kutembea umbali mrefu.

Wananchi hao wamesema kuwa endapo ikikamilika zahanati hiyo itawaondolea adha hiyo huku wakiiomba halmashauri ya Wilaya hiyo kukamilisha ujenzi uliobaki kutokana kwani wameishatumia nguvu nyingi katika ujenzi huo.

Kwa upande wake mtendaji wa Kijiji hicho cha Katembe Bwana Ulimwengu Richard amesema ujenzi wa zahanati hiyo umekwisha ghalimu zaidi ya shilingi milioni 76  ambapo kwa sasa wapo katika ujenzi wa nyumba ya waganga na vyoo kwa thamani ya zaidi ya shilingi milioni 30 na tayari halmashauri hiyo imeishaweka zaidi ya shilingi milioni 18 ili kukamilisha ujenzi uliobaki .

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhandis Richard Ruyango amewashukuru wananchi hao pamoja na wadau mbalimbali wa Maendeleo kwa kushirikiana kuanzisha ujenzi huo ambapo amewataka Wananchi pamoja na wadau kuendelea kushirikiana kukamilisha ujenzi huo kwa kipindi hiki ili wananchi waweze kuondokana na adha hiyo.

No comments:

Post a Comment

Pages