HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 11, 2021

WAZAZI LUDEWA WAOMBA SOMO LA HISABATI KUINGIZWA KWENYE MRADI WA JIFUNZE

Mzazi Alpha Samuel Melele mkazi wa Kijiji cha Shaurimoyo akizungumza na mwandishi wa habarihizi hivi karibuni wilayani Ludewa.


Baadhi ya Wazazi ambao watoto wao wamenufaika na programu ya Jifunze wakiwa na mmoja wa walimu wa darasa la Jifunze Shule ya Msingi Shaurimoyo, Castory Muagama (wa kwanza kulia) mara baada ya mahojiano kuzungumzia programu ya jifunze.

Na Joachim Mushi, Ludewa

BAADHI ya wazazi ambao awali watoto wao walikuwa na changamoto ya kujua kusoma na kuandika na hatimaye kuingizwa kwenye mradi wa jifunze kutatua changamoto hiyo, wameiomba taasisi ya Twaweza kuingiza somo la hisabati katika mradi huo ili kutatua changamoto ya ujifunzaji wa somo hilo kwa baadhi ya watoto.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni, Wilayani Ludewa katika mahojiano na baadhi ya wazazi hao kwa nyakati tofauti kuzungumzia changamoto za watoto wao katika ujifunzaji na mafanikio na mradi wa Darasa la Jifunze uliokuwa ukitekelezwa baadhi ya shule kusaidia watoto wasiojua kusoma kuanzia darasa la tatu hadi la sita. 

Mzazi Alpha Samuel Melele mkazi wa Kijiji cha Shaurimoyo akizungumza aliiomba taasisi ya uwezo kwa kushirikiana na wadau wa elimu kukubaliana kuliingiza somo la hisabati katika mradi wao wa darasa la Jifunze ili kusaidia kutatua changamoto inayowakabili baadhi ya watoto kwenye somo hilo.

"...Mwanangu yupo darasa la tatu Shule ya Msingi Shaurimoyo ni miongoni mwa wanafunzi walionufaika na darasa la Jifunze, awali alikua hajui kusoma na kuandika lakini baada ya kuhudhuria darasa hilo amebadilika hadi nashangaa...anajua kusoma na kuandika tena kwa kujiamini tofauti na mwanzo. Hata hivyo kwenye hesabu bado hayupo vizuri sana ndio maana naomba somo hili pia liingizwe katika darasa la Jifunze," alisema Bw. Samuel Melele.

Naye mzazi Fausta Mtitu amepongeza ujio wa programu ya darasa la Jifunze kwenye Kata ya Lugarawa kwani imesaidia watoto waliokuwa na changamoto ya kusoma eneo hilo na kuomba somo la hisabati kujumuishwa katika programu hiyo ili kuwasaidia watoto wao. 

"Somo la hesabu bado ni tatizo sana kwa watoto wetu, mimi mwanangu licha ya sasa kumudu kusoma na kuandika lakini bado hesabu zinamtatiza ndio maana tunahoji kwanini mradi huu pia usijumuishe hili somo kuwasaidia watoto wetu," alihojia Bi. Fausta Mtitu katika mahojiano na mwandishi wa habari hizi.

Aidha aliongeza kuwa wamejaribu kuhoji kwa walimu wanaofundisha mradi wa Jifunze kwanini wasiingize somo hilo lakini wamejibiwa halimo katika programu hiyo, hivyo kuamua kuomba kwa asasi husika ili iangalie namna ya kujumuisha somo hilo la hesabu kwani bado linawatatiza wanafunzi hata wale ambao tayari wamenufaika na mpango wa Jifunze.


Baadhi ya wanafunzi wa darasa la jifunze waliofanya vizuri kwenye kipindi wakiwa wamevishwa kofia kupongezwa na walimu wao, ikiwa ni moja ya mbinu zinazotumika kuwavutia wengine kufanya vizuri darasani.

Kwa upande wake, Bi. Agnes Daniel Mtweve mwalimu wa darasa la Jifunze ameunga mkono maombi ya baadhi ya wazazi hao na kuongeza kuwa wapo tayari kuwasaidia wanafunzi hao hata kwenye somo la hisabati kama wataongezewa ujuzi na watekelezaji wa programu hiyo kama walivyoomba wazazi hao. 

"Ukiangalia kuna mafanikio makubwa katika muda mfupi wa kutekeleza mradi huu, watoto wengi wameweza kusoma vizuri na kuandika hivyo naamini hata kwenye somo la hisabati likiingizwa kutakuwa na mafanikio hivyo kujikuta tunawasaidia pia watoto hawa," alisema mwalimu huyo akizungumza na mwandishi wa habari hizi.

Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa Mkoa wa Njombe kwa kushirikiana na taasisi ya Uwezo Tanzania ni miongoni mwa wilaya zinazotekeleza mradi wa Darasa Jifunze kimajaribio kwa baadhi ya kata kusaidia wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika kwa darasa la tatu hadi la Sita, ikiwa ni kutatua changamoto ya ujifunzaji kwa wanafunzi walio na changamoto hiyo. Imekuwa ikiwatumia walimu waliopata mafunzo kufundisha kwa muda wa ziada kuwasaidia wanafunzi wenye changamoto hiyo, ukitekelezwa kwa siku 30, kabla ya kufanya tathmini kila baada ya siku 10.


No comments:

Post a Comment

Pages