Na Mwandishi Wetu
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dk. Agnes Kijazi, ameongoza mkutano wa pili wa Jopo la Kamati Kuu ya WMO ya Kujenga Uwezo.
Akizungumza wakati akifungua rasmi mkutano huo, Dk. Kijazi aliwataka wajumbe wa mkutano huo, kuzingatia lengo lililokasimiwa kwa jopo la kushauri namna bora ya kujenga uwezo katika uboreshaji wa huduma za hali ya hewa duniani.
“Mkutano huu umelenga kujadili taarifa za utekelezaji wa majukumu ya vikosi kazi vinavyounda jopo hili na kuandaa mapendekezo ya kuwasilisha kwenye Kamati Kuu ya WMO na mapendekezo ya maeneo ya vipaumbele kwa ajili ya kuandaa Mpango Mkakati wa kujenga uwezo katika utoaji huduma kimataifa,” amesena Dk. Kijazi.
Katika hatua nyingine, Dk. Kijazi alimpongeza Katibu Mkuu wa WMO, Profesa Petteri Taalas, kwa kupewa tuzo na jarida la “Reader’s Digest Magazine” kama Mtu Mashuhuri wa Bara la Ulaya wa mwaka 2020 ikiwa ni kutambua mchango wake wa kuongoza jitihada za WMO kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.
Profesa Taalas alimshukuru Dk. Kijazi na kusema kuwa tuzo hiyo ni maalum kwa wadau wote wa WMO na huduma za hali ya hewa kwa ujumla na alimpongeza Dk. Kijazi kwa uongozi wake mahiri unaosaidia kufanikisha utekelezaji wa malengo ya WMO.
Mkutano huo ulifanyika kwa njia ya mtandao chini ya Mwenyekiti wa jopo hilo, Dk. Kijazi na Katibu Mkuu wa WMO, Profesa Taalas na watendaji wengine waandamizi wa WMO.
Mkutano ulijadili taarifa za Vikosi kazi vinavyounda jopo hilo na kuandaa mapendekezo mbalimbali ya kujenga uwezo katika huduma za hali ya hewa.
Miongoni mwa mapendekezo hayo ni pamoja na yatakayowasilishwa katika mkutano wa 73 wa Kamati Kuu ya WMO na mapendekezo ya maeneo ya vipaumbele vitakavyotumika kuandaa Mpango Mkakati wa WMO wa kujenga uwezo.
Mjadala ulijielekeza kutambua kwamba hali ya hewa haina mipaka hivyo katika kipindi hiki cha kuongezeka majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa jopo hilo lihakikishe vipaombele katika kujenga uwezo vinaelekezwa kuzisadia nchi zinazoendelea pamoja na za Bara la Afrika ili kuhakikisha maendeleo katika sekta ya hali ya hewa hayamuachi mtu yoyote nyuma.
No comments:
Post a Comment