HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 11, 2021

Benki ya Stanbic yashirikiana na Vijana Think Tank kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Mabinti kwenye Sayansi


Mkuu wa Huduma za Benki Binafsi na Kibiashara, Omari Mtiga (kushoto), akimkabidhi mfano wa hundi mwakilishi wa Vijana Think Tank, William Mshery.

 

Dar es Salaam, Tanzania

 

Benki ya Stanbic Tanzania imechangia shilingi milioni 10 kwa ajili ya kuunga mkono maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanawake na mabinti kwenye sayansi katika hafla iliyoratibiwa na shirika la Vijana Think Tank.

Mchango huo umelenga kutambua shughuli kubwa inayofanywa na wanawake na mabinti kwenye sayansi na teknolojia, pamoja na kuhimiza jinsia ya kike kuzidi kushiriki na kuzipenda kozi za sayansi, teknolojia, uhandisi na hesabu (STEM), ambazo zina mchango kubwa katika kufikia ajenda ya maendeleo ya viwanda pamoja na kupunguza mwanya uliopo wa kijinsia.

Tanzania pamoja na mataifa mengine yanayoendelea yanatambua kuwa sayansi, teknolojia na uvumbuzi ni maeneo yenye mchango mkubwa katika kuleta maendeleo ulimwenguni pamoja na maendeleo ya Viwanda. Benki ya Stanbic Tanzania kupitia ushiriki wake imeweza kubaini kuwa bado kuna idadi ndogo ya mabinti ambao wameandikishwa kwenye kozi za STEM katika vyuo mbalimbali.

Kwa mujibu wa data za Shirika la Umoja wa Mataifa linalojihusisha na Elimu, Sayansi na Tamaduni (UNESCO), asilimia 24 kati ya 40 ya wanawake ndio wamebainika kujiandikisha kwenye kozi za sayansi, uhandisi na teknolojia vyuoni. Mwanya ambao umeendelea kuwazibia nafasi wanawake kuweza kunufaika na fursa za ajira zilizopo sasa na baadae, wakati dunia ikiendelea kujikita kwenye mifumo kamili ya kidigitali na uvumbuzi wa teknolojia. 

Akizungumzia mchango wa Benki ya Stanbic, Mkuu wa Huduma za Benki Binafsi na Kibiashara, Omari Mtiga, amesema kuwa, “Ili taifa liendelee na liweze kufikia ajenda ya viwanda, ni lazima idadi ya wanawake wanaoandikishwa kwenye masomo ya sayansi, teknolojia na uvumbuzi iongezeke. Hii ni pamoja na kuboresha mbinu za kuwavuta wanawake kujiandikisha kwenye taaluma hizi. Ushirikiano huu ni moja ya kampeni za kijamii ambazo benki inaendelea kushiriki ili kuwahakikishia vijana kuwa, kupitia bidii, malengo na kujiendeleza wanaweza kufikia ndoto zao.”

Mtiga aliongeza kuwa, ukuaji wa kiuchumi unategemea sana matumizi mazuri ya mtaji wa watu waliopo. “Ili Kufanikiwa kuwa na usawa wa kijinsia katika eneo hili, sekta zote zinapaswa kuunda ushirikiano wenye kuwapa nguvu wanawake, mabinti na vijana wote ili kuwahamasisha waweze kushiriki na kuipenda sayansi.”

Kwa upande wake, William Mshery wa Vijana Think Tank alisema kuwa, “Tunaamini kupitia ubia huu na benki ya Stanbic Tanzania tutaweza kufungua uwezo wa kisayansi, teknolojia na uvumbuzi ambao ni nyenzo kuu ya ukuaji na maendeleo ya Tanzania. Tunashukuru kwa mchango uliotolewa na benki hii na tunaipongeza kwa kuendelea na jitihada za kuwainua vijana wakike na wakiume nchini Tanzania.”

No comments:

Post a Comment

Pages