Afisa Mwandamizi wa Tekinolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Afande Boniphase Maliki, akieleza kuwa Shirika lilikua na Akaunti 100 na baada ya kujiunga na Mfumo wa Makusanyo ya malipo ya Serikali (GePG), imebaki na akaunti 8, wakati Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini walipotembelea Shirika hilo, jijini Arusha.
Afande Juma Kuji, (wa pili kulia) akiwa na maafande wengine wakisikiliza kwa makini maswali ya Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini kuhusu Mfumo wa GePG ulivyosaidia katika makusanyo.
Ramadhani Kissimba na Peter Haule, WFM, Arusha
Serikali
kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imefanikiwa kuongeza mapato maradufu
baada ya kuanzisha matumizi ya mfumo wa kukusanya mapato ya Serikali
(GePG), ambapo mpaka sasa taasisi zaidi ya 670 zimekwishajiunga katika
mfumo huo.
Hayo
yamebainishwa leo baada ya ziara iliyofanywa na wahariri wa vyombo
mbalimbali vya habari hapa nchini walipotembelea Shirika la Hifadhi za
Taifa Tanzania (TANAPA), Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) na Mamalaka ya
Maji Safi na Maji Taka mkoa wa Arusha, (AUWASA).
Akizungumza
wakati wa ziara hiyo Afande Juma Mussa Nasoro Kuji Kutoka Shirika la
Hifadhi za Taifa, (TANAPA) amesema tangu kuanzishwa kwa mfumo wa
makusanyo wa pesa za serikali, shirika hilo limeokoa kiasi kikubwa cha
fedha ambazo zilikuwa zikitumika kuwalipa watoa huduma kutoka benki
mbalimbali. Afande Kuji alisema TANAPA ilikuwa ikilipa asilimia moja ya
mapato yote wanayokusanya kwa mabenki hayo, ambazo ni kati ya shilingi
bilioni moja hadi bilioni tatu kwa mwaka. Na sasa hakuna malipo yoyote
yanayofanyika kwa benki hizo kutokana na matumizi ya mfumo wa GePG.
Akizungumzia
mafanikio ya TANAPA baada ya kuunganishwa na mfumo wa GePG, Mkuu wa
Kitengo cha Tehama Afande Boniphase Mariki alisema kuwa kabla shirika
hilo halijaanza kutumia mfumo huo kila geti la hifadhi lilikuwa na
akaunti yake hivyo kusababisha shirika hilo kuwa na akaunti
zinazokaribia mia moja (100), jambo ambalo lilikuwa linachelewesha
kupata taarifa za makusanyo na ufanyaji wa usuluhishi wa kifedha (Bank
reconciliation).
Afande
Maliki aliongeza kuwa baada ya kujiunga na GePG kwa sasa shirika lina
akaunti nane (8) tu ambazo akaunti nne (4) ni za sarafu ya Shilingi na
akaunti nne (4) ni za sarafu ya Dola, jambo linalowezesha shirika
kutatua changamoto nyingi za makusanyo kwa kuwa makusanyo yote
yanasimamiwa na mfumo wa GePG.
Aidha
akiwakaribisha wahariri na watumishi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango,
Afande Kuji alisema TANAPA walianza na hifadhi moja ya Serengeti mwaka
1959 na mpaka sasa wana hifadhi 22 nchini kote.
Katika
ziara hiyo wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini pia
walipata fursa ya kutembelea katika chuo cha Ufundi Arusha na Mamlaka ya
Maji Safi na Maji taka Mkoani Arusha ambapo walipata taarifa jinsi
mfumo wa GePG ulivyosaidia kurahisisha makusanyo kwa Taasisi hizo na
kupunguza usumbufu kwa wateja.
Akizungumzia
mafanikio hayo Mkuu wa Kitengo cha Tehama wa Mamlaka ya Maji Safi na
Maji taka Mkoani Arusha, Bw. Ndaki Titto alieleza kuwa baada ya kujiunga
na mfumo huo katika mwaka wa fedha 2017/18 shirika hilo limefanikiwa
kuongeza mapato yake kutoka shilingi bilioni 1.2 hadi bilioni 1.6 kwa
mwezi.
Bw. Titto amesema
kuwa mbali na shirika kuongeza mapato yake, pia wateja wamefaidika kwa
kiasi kikubwa kwa sababu mfumo wa GePG umeruhusu kufanya malipo kupitia
njia mbalimbali zikiwemo mitandao ya simu hivyo kupunguza usumbufu kwa
wateja wake. Bw. Ndaki amesema kuwa pamoja na mafanikio hayo kuna
changamoto wanazokumbana nazo kupitia mfumo huo wa GePG ikiwemo
changamoto ya mtandao.
‘’Changamoto
ninayoiona kwa upande wa GePG ni utegemezi zaidi kwa upande wa mtandao,
maana bila ya mtandao huwezi kuona mapato na changamoto nyingine ni
elimu kwa wananchi, ambapo wananchi wengi hawana uelewa kuhusu matumizi
ya namba ya malipo (control number) kuwa unaweza kulipia katika benki
yoyote’’ aliongeza Bw. Titto.
Akiongea
kwa niaba ya Mkuu wa chuo cha Ufundi Arusha, Mkuu wa Usajili wa
wanafunzi Dk. Baraka Kichonge amesema kuwa mfumo wa ukusanyaji mapato ya
serikali (GePG) umekuwa mkombozi wa matumizi ya fedha za umma kwa kuwa
mfumo huo umeweka uwazi katika makusanyo na hivyo kuongeza uadilifu
katika matumizi ya fedha za Umma.
Aidha
Dk. Kichonge amewaomba wahariri hao kufanya ziara ya mkakati katika
chuo hicho ili kujionea teknolojia kubwa inayotumika katika ufundishaji
chuoni hapo na kuzifikisha taarifa hizo kwa wananchi ili waweze kuwekeza
katika teknolojia kupitia vijana wao watakaowapeleka kupata mafunzo
katika chuo hicho.
Kwa
Upande wa Wizara, Afisa Tehama Mwandamizi anayesimamia Mfumo wa GePG Bw.
Basil S. Baligumya alisema katika semina ya siku mbili kwa wahariri
Wizara imepata zaidi ya kujifunza kuhusu ufanyaji kazi wa mfumo wa GePG.
Bw. Basil aliongeza kuwa Serikali itaendelea kutoa sapoti kwa taasisi
zake kuhakikisha kwamba changamoto zozote za mifumo zinatatuliwa kwa
wakati.
‘’Sisi kama
Wizara tupo tayari kuendelea kuwapa sapoti na tunashukuru kwa
ushirikiano wenu pia na tunaendelea kuwatia moyo ile mifumo yenu
inayochakata bili muendelee kuiboresha ili tuendelee kutoa huduma kwa
namna ambayo ni rahisi kwa watu wanaolipia huduma zetu” alisema Bw.
Basili.
No comments:
Post a Comment