Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega, akifungua semina ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Arusha kuhusu Mfumo wa Ukusanyaji Mapato Serikalini (GePG).
NA BETTY KANGONGA
MFUMO
wa kieletroniki wa Serikali wa ukusanyaji wa fedha za umma umesaidia
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuokoa zaidi ya Sh. Bilioni 38
iliyokuwa ikilipa kwa mwaka kwa mawakala wa kuuza umeme nchini.
Akifungua
semina ya wahariri wa vyombo vya habari nchini iliyofanyika jijini
Arusha, Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Richard Kwitega alisema, Wizara ya
Fedha na Mipango imebuni na kuunda Mfumo wa Kielektoniki unaotumika
kukusanya Fedha zote za Umma unaojulikana kama “Government e-Payment
Gateway” au kwa kifupi “GePG.
Alisema kuwa, mfumo huo umewezesha kupanda kwa mapato ya serikali baada ya kuboreshwa kwa mfumo huo.
Kwitega alisema, kutokana na kuanza kutumika kwa mfumo huo taasisi
zimepunguza gharama walizokuwa wanalipia ada za miamala ya
kielektroniki inayohusu makusanyo ya fedha za umma akitolea mfano
TANESCO iliyokuwa ikilipa zaidi ya Sh. Bilioni 38 kwa Mwaka kwa mawakala
wa kuuza umeme ambapo baada ya kufunga mfumo wa GePG kwa sasa shirika
halilipi chochote.
Alitaja
taasisi nyingine zilizopandisha makusanyo yake ni Wakala wa Huduma za
Misitu Tanzania (TFS) ambayo yameongezeka kutoka Sh. Bilioni 95 kabla ya
kuanza kwa mfumo hadi kufikia Sh.Bilioni 115 baada ya kuanza kutumia
mfumo wa kielektroniki.
Wengine
ni Wakala wa Vipimo (WMA) mapato yao yameongezeka kutoka kiasi cha Sh.
Bilioni 1kwa mwezi kabla ya Mfumo wa GePG mpaka kufikia Sh. Bilioni 2.5
kwa mwezi baada ya kujiunga na GePG.
Alisema
kuwa, Mfumo huu umebuniwa na kutengenezwa na wataalamu wa ndani wa
Serikali ambapo upo kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Umma (PFA) ya mwaka
2001 kupitia marekebisho ya mwaka 2017 (Sura 348), na Waraka wa HAZINA
Namba 3 wa mwaka 2017.
"Sheria
ya Fedha za Umma inawataka Maofisa Masuuli wote kukusanya fedha za Umma
kupitia Mfumo wa GePG. Mfumo huu ulianza kutumika rasmi Julai mosi,
mwaka 2017 ambapo ulianza na taasisi saba (7) lakini kwa sasa Mfumo huu
unatumiwa na taasisi za Umma zaidi ya 600. Mfumo huu ndiyo unatoa kumbu
kumbu namba (“Control number”) ya kulipia huduma na tozo mbalimbali za
Serikali," alisema.
Kwitega
alisema, kuwa Mfumo huu wa GePG ulianzishwa ili kukabiliana na
changamoto mbalimbali zilizokuweko serikalini katika zoezi zima la
ukusanyaji wa fedha za Umma.
Alitaja
changamoto hizo ni pamoja na; Gharama kubwa za miamala inayohusu
makusanyo ya fedha za umma; Utaratibu usio rafiki kwa mlipaji wa huduma
za Umma unaoanzia namna anavyopatiwa ankara, anavyolipia ankara yake,
anavyothibitisha malipo, anavyopatiwa stakabadhi hadi anavyopatiwa
huduma;
Pia
alitaja changamoto nyingine ni kulikuwa na machaguo (options) machache
ya njia za kulipia (Mabenki, Mitandao ya simu za mkononi au Mawakala)
kwa sababu kuongeza machaguo kulikuwa kunaongeza gharama za ukusanyaji
kwa taasisi;
"Ilipohitajika
kufungamanisha Mfumo wa Ankara wa taasisi na Mifumo ya Ulipaji (kama
vile mabenki, Mitandao ya simu za mkononi na Mawakala wakubwa
(Aggregators) gharama ilikuwa kubwa kwa sababu kila Mfumo
ulifungamanishwa peke yake; Ilikuwa ni vigumu sana kupata taarifa ya
makusanyo yanayofanyika kwa wakati huo huo (“Real time collection
reports”). Alisema.
Kwitega
alisema, Wizara ya Fedha na Mipango inatambua kuwa Mafanikio ya mfumo
huu wa GePG yanategemea sana ushiriki wa wananchi wote katika kuutumia.
Hivyo, kila mwananchi anayelipia huduma yoyote ya Umma ni lazima
ahakikishe kuwa amepewa “Control number” na taasisi inayotoa huduma
hiyo, na akiwa analipa ahakikishe amelipa kwa kutumia “Control number”
hiyo.
No comments:
Post a Comment