HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 23, 2021

MOTO WA SIMBA WAWAUNGUZA WAARABU AL AHLY DAR, KONDE BOY SHUJAA

  

Mfungaji wa bao la Simba, Luis Miquissone 'Konde Boy' akiichachafya ngome ya timu ya Al Ahly ya Misri. (Picha kwa hisani ya Simba SC).


Mfungaji wa bao la Simba, Luis Miquissone 'Konde Boy' akiwaongoza wachezaji wenzake kushangilia bao alilofunga.

Wachezaji wa Simba wakishangilia bao pekee la timu yao katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League), dhidi ya Al Ahly ya Misri uliopigwa kwenye dimba la Benjamini Mpaka jijini Dar es Salaam leo Februari 23, 2021.


DAR ES SALAAM, TANZANIA

MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL), Simba SC, wamedumisha ushindi wa asilimia 100 wa mechi za hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League), baada ya kuwazabua mabingwa watetezi Al Ahly ya Misri kwa bao 1-0.

Pambano hilo la pili kwa kila timu katika Kundi A, limeunguruma ndani ya dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Wekundu wa Msimbazi waking'arishwa na bao la dakika ya 31 lililowekwa kambani na nyota wa kimataifa wa Msumbiji, Luis Miquissone 'Konde Boy' kwa mkwaju wa mbali kutokea nje ya boksi.

Kwa ushindi huo, Simba iliyoshuka dimbani ikichagizwa na kaulimbiu ya: 'TOTAL WAR - Point of no Return,' inaongoza msimamo wa Kundi A, kwa kufikisha alama sita, baada ya awali kujikusanyia pointi tatu za ushindi wa ugenini walipowafuata AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

AS Vita wao wamepanda kwenye msimamo na kushika nafasi ya pili nyuma ya Simba, baada ya leo kuzinduka na kuwachapa El Merreikh ya Sudan kwa mabao 4-1. Al Ahly inashika nafasi ya tatu kwa uwiano wa mabao ikiwa na pointi tatu, huku Merreikh wakiburuza mkia bila pointi.

Kipigo hicho ni cha pili kwa Al Ahly chini ya kocha Pitso Mosimane, ambaye tangu apewe timu ameshinda meshi 20, sare nne na kufungwa mbili, katika mechi 26 alizoisimamia timu hiyo. Ukiondoa Simba, timu nyingine iliyoichapa Ahly chini ya Mosimane ni Bayern Munich ya Ujerumani katika nusu fainali ya Klabu Bingwa ya Dunia (FIFA Club World Cup 2021).

No comments:

Post a Comment

Pages