Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja, akieleza kuwa lengo la mafunzo ya Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo ya Fedha, ni pamoja na kupata uelewa ili kutoa huduma kwa mujibu wa Sera, Sheria na Kanuni za huduma hiyo, wakati wa mafunzo hayo, jijini Dodoma.
NA HAMIDA RAMADHANI, DODOMA
OFISI ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imefanikisha uteuzi wa waratibu 212, (Focal Person) katika ngazi ya Wilaya, Mkoa na Halmashauri kwa ajili ya uratibu na Uhamasishaji wa Biashara ya Huduma Ndogo ya Fedha nchini.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Adolf Ndunguru, amebainisha hayo leo jijini Dodoma wakati alipokua akifungua mafunzo ya Waratibu wa Biashara ya Huduma ndogo za Fedha.
Amesema kuwa, majukumu ya Waratibu hao yatakuwa ni kuratibu, kuhamasisha na kutathmini biashara ya huduma ndogo za fedha katika ngazi ya Wizara, Mkoa na Halmashauri ikiwa ni pamoja na kusajili wahamasishaji wa biashara ya huduma ndogo za fedha (Microfinance Business Promoters) na kuandaa taarifa za Sekta Ndogo ya Fedha kwa vipindi tofauti tofauti.
Kadhalika amesema kuwa, Sekta Ndogo ya Fedha ni miongoni mwa sekta muhimu katika uchumi wa nchi.
“Sekta hii inatoa huduma za fedha kwa wananchi wa kipato cha chini kwa lengo la kuongeza kipato na kuchangia katika kukuza uchumi”amebainisha Ndunguru
Amesema, kwa mujibu wa utafiti wa Finscope wa mwaka 2017, asilimia 55.3 ya nguvukazi ya Taifa wanapata huduma za fedha kutoka taasisi za huduma ndogo za fedha.
Pia, amesema kuwa kutokana na umuhimu wa Sekta hii, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango ilifanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2000.
Ambapo ilitunga Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2017 pamoja na Mkakati wa utekelezaji wake kwa kipindi cha miaka kumi kuanzia 2017/18 mpaka 2027/28.
Pia, amesema Sera hiyo pamoja na mambo mengine ilielekeza kutungwa kwa Sheria mahsusi ya kusimamia na kuendeleza Sekta ya Ndogo ya Fedha ili kuondoa changamoto za kisheria zilizokuwepo ambazo ziliathiri usimamizi, udhibiti na ustawi wa sekta hiyo.
“Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na Taasisi za huduma ndogo za fedha kutoa mikopo kwa wananchi kwa vigezo na masharti magumu na hivyo kusababisha madhara kwa wananchi ikiwa ni pamoja na viwango vikubwa vya riba na tozo, kukosekana kwa uwazi wa masharti ya mikataba ya mikopo, utoaji holela wa mikopo ambao unasababisha limbikizo la madeni kwa wateja”ameeleza Ndunguru
Vile vile, amesema sababu nyingine ni utaratibu usiofaa wa ukusanyaji wa madeni ambao unasababisha wananchi kupoteza mali zao pia kuwepo kwa baadhi ya taasisi za huduma ndogo za fedha zisizotoa gawio au faida kwa wanachama au wateja wanaoweka fedha kati ya asilimia 25 hadi 30 kama dhamana ya mikopo.
“Changamoto nyingine ni ukosefu wa takwimu/taarifa sahihi za uendeshaji wa taasisi za watoa huduma ndogo za fedha na hivyo serikali kutojua mchango wa sekta ndogo ya fedha katika uchumi wa Taifa, ukosefu wa utaratibu wa kuwalinda watumiaji wa huduma ndogo za fedha na kuwepo kwa mianya ya utakasishaji wa fedha haramu kutokana na taasisi za huduma ndogo za fedha kutokuwa na utaratibu wa kisheria unaozitaka kutekeleza matakwa ya Sheria ya Udhibiti wa Utakasishaji wa fedha haramu”ameeleza Ndunguru
Aidha, amesema kuwa ili kutatua changamoto zinazoikabili Sekta Ndogo ya Fedha serikali ilitunga Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 (The Microfinance Act, 2018) ili pamoja na mambo mengine ni kuzitambua taasisi za huduma ndogo za fedha katika madaraja manne.
“Daraja la kwanza ni taasisi za huduma ndogo za fedha zinazopokea amana (deposit taking microfinance providers), Daraja la Pili, taasisi za huduma ndogo za fedha zisizopokea amana (non-deposit taking microfinance service providers) wakiwemo wakopeshaji binafsi, watoa huduma kwa njia ya kielektroniki, Daraja la Tatu, Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) na Daraja la Nne ni vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha kama vile VICOBA, VSLA.”amefafanua Ndunguru
Kamishna wa uendelezaji wa sekta ndogo ya fedha Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Charles Mwamwaja alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kujenga uelewa kwa waratibu wa biashara ya huduma ndogo za fedha katika ngazi ya Wizara, Mkoa na Halmashauri.
“Mafunzo haya yatawawezesha pia kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sera, Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha pamoja na majukumu mengine kama yalivyoainishwa katika Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha za mwaka 2019”amesema Dkt. Mwamwaja
No comments:
Post a Comment