HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 09, 2021

MWENYEKITI WA ZAMANI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA MKURANGA APINGWA MIAKA MINNE JELA KWA KOSA LA RUSHWA

 NA MWANDISHI WETU, MKURANGA 

  

HATIMAYE aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, Juma Abeid, aliyekuwa kiongozi katika kipindi kilichopita amehukumuiwa kwenda Jela kwa makosa ya  kupokea rushwa kitu ambacho ni kinyume na sheria na taratibu za nchi zilizowekwa.

Kwa mujibu wa taarifa ambayo imetolewa na Taasisi  ya  Kuzuia na Kupambana na Rushwa wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani  imeeleza kuwa  mnamo mwezi Novemba mwaka  2019 ilifungua mashitaka ya kuomba na kupokea rushwa dhidi ya mshitakiwa huyo Juma Abeid ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Mkuranga  kabla ya  kufanyika kwa uchaguzi Mkuu wa Viongozi wa mwaka 2020.

 Kesi hiyo  ambayo iliendeshwa  katika mahakama ya hakimu mkazi  Wilaya ya Mkuranga  mkoa wa Pwani mbele ya hakimu mkazi  Erieth Mwailolo .

Awali  ilidaiwa  kwamba Mshitakiwa alitenda kosa la kupokea hongo ili kumsaidia mwananchi (jina limehifadhiwa) ambaye alikuwa anahitaji uhamisho wa mke wake anayefanya kazi ya Ualimu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Babati mkoani Manyara kwenda Halmashauri ya wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.

Pia ilidaiwa  mshitakiwa aliomba na kupokea  kiasi cha Shilingi Laki mbili na elfu ishirini (Sh. 220,000/=)  ili kuwezesha  kufanyika kwa  uhamisho huo kwenda Halmashauri ya wilaya ya Mkuranga ambayo yeye alikuwa anaiongoza kwa nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo. Kitendo hiki ni kosa chini ya kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na 11 ya Mwaka 2007.

Hukumu ya kesi hiyo ilisomwa na hakimu mkazi Mheshimiwa Erieth Mwailolo mnamo tarehe 08 Februari, 2021 ambapo Mwenyekiti huyo wa Zamani Juma Abeid alihukumiwa kwenda jela miaka minne (4) au kulipa faini ya Shilingi laki saba (Sh.700,000/=) kwa kila kosa.

 Mshitakiwa alikubali kulipa faini ya  shilingi Milioni Moja na laki Nne (Sh. 1,400,000/=) na kuachiwa huru.

 Awali, Mwendesha mashitaka wa TAKUKURU Bw. NAFTAL MNZAVA alimwomba mheshimiwa hakimu kutoa adhabu kali dhidi ya mshitakiwa ili iwe fundisho kwa viongozi wengine wanaojihusisha na rushwa. 

Wakati huo huo jana tarehe 08 Februari, 2021 Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Pwani ilimfikisha mahakamani  Bw. GIDMAN BISHINWA ATHANAS mtumishi wa Mamlaka ya Maji safi na Maji taka (DAWASA) Mkoa wa Pwani kwa makosa ya kuomba na kupokea Rushwa kinyume na Kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na:11 ya mwaka 2007.

Mtuhumiwa huyo aliomba rushwa ya Shilingi laki mbili na elfu hamsini (Sh. 250,000/=) kutoka kwa mwananchi mkazi wa Kibaha (jina limehifadhiwa) ili mshitakiwa asiingize deni la matumizi ya maji analodaiwa kiasi cha Shilingi laki tano (Sh. 500,000/=) kwenye mfumo wa malipo ya maji wa DAWASA.

Hata hivyo baada ya kusomewa mashitaka mtuhumiwa huyo alikiri kutenda kosa mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama ya wilaya Kibaha Mhe. KIBONA na kuhukumiwa kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini kiasi cha Shilingi laki tano (Sh. 500,000/=) ambapo mtuhumiwa alilipa faini na kuachiwa huru.

 

Aidha Mkuu  wa Takukuru Mkoa wa Pwani Suzana Raymond  wamewaasa watumishi wa mkoa huo  wenye dhamana ya kutoa huduma kwa jamii kuzingatia misingi ya uadilifu katika utendaji wao wa kazi  kwani vitendo vya Rushwa katika kazi vinasababisha huduma kutolewa chini ya viwango na kwa upendeleo kinyume na malengo ya serikali.

 

No comments:

Post a Comment

Pages