Na James K. Mwanamyoto-Dodoma
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro, amewataka Watumishi wa Umma nchini kulinda afya zao ili waweze kuwahudumia vema wananchi wanaofuata huduma mbalimbali katika taasisi zao.
Dkt. Ndumbaro ametoa wito huo mapema leo wakati akizungumza na Watumishi wa ofisi yake ikiwa ni sehemu ya utaratibu wake wa kukutana na watumishi hao kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.
Dkt. Ndumbaro amesema, ili Watumishi wa Umma waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu, hawana budi kulinda afya zao ikizingatiwa kuwa wakati wa utoaji huduma wanakutana na watu ambao baadhi yao wanaweza kuwa na changamoto mbalimbali za kiafya.
Ili kuhakikisha taifa linakuwa na rasilimaliwatu yenye tija, Dkt. Ndumbaro amewataka Watumishi wa Umma kuwa na utaratibu wa kupima afya mara kwa mara na kupata tiba mapema iwezekanavyo pindi wanapohisi kukabiliwa na changamoto yoyote ya kiafya.
Sanjali na hilo, Dkt. Ndumbaro amewahimiza Watumishi wa Umma kuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi ili kuimarisha afya kwa lengo la kuendelea kutoa mchango katika ujenzi wa taifa.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro amekuwa na utaratibu wa kukutana na Watumishi wa Umma katika maeneo mbalimbali nchini kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
No comments:
Post a Comment