Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Ruvuma Addo Mwisho anayezungumza akiwa na Kamati ya Siasa ya chama hicho mkoani Ruvuma katika Hifadhi za Jumuiya za Mbarang'andu na Kimbanda Wilayani Namtumbo.
NA SULEIMAN MSUYA, SONGEA
CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Ruvuma kimepongeza Program ya Mnyororo wa
Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC) kwa kununua mashine na Shirika la
Mpingo na Mandeleo (MCDI) kujengea wananchi uwezo wa kuongeza thamani
ya mazao ya misitu mkoani hapo.
Pongezi
hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Ruvuma Addo Mwisho wakati
akizungumza kwenye uzinduzi wa mashine ya kuchakata mazao ya misitu
iliyonunuliwa na MCDI kwa ufadhili wa FORVAC.
FORVAC ni program inayotekelezwa chini ya Idara ya Misitu na Nyuki na kufadhiliwa na Serikali ya Tanzania na Finland.
Mwisho
amesema shughuli zinazofadhiliwa na FORVAC zimekuwa na matokeo chanya
hali ambayo inarahisisha utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020 hadi 2025
Ibara ya 69 kigungu F.
Amesema
awali miradi hiyo ilipotambulishwa baadhi ya wananchi walikataa na
wengine walishangaa ila wachache walielewa na leo wanaona faida.
Mwenyekiti amesema walipita katika vijiji vya mradi na kufanikiwa kutoa elimu ambapo leo matokeo mazuri yameanza kuonekana.
"Mradi
huu umepokelewa kwa changamoto ila leo tunaona matunda ambapo tumepokea
mashine ya kuchakata mazao hivyo Ilani ya CCM inatekelezwa," amesema.
Mwisho
amesema CCM mkoa inaomba Serikali kuendelea kutoa elimu ili wanufaika
wawe wengi zaidi hali itakayosaidia kupunguza umaskini.
Mwenyekiti amesema neema ya ardhi yenye rutuba ambayo Ruvuma imepewa inapaswa kutumika vizuri kwa uendelevu.
Amesema
CCM itaendelea kuunga mkono juhudi wadau wote ambao wameamua kujitolea
kusaidia huduma za kijamii, mazingira na nyingine nyingi.
"Tunapenda
kuwakaribisha wadau wengine waje waungane na FORVAC na MCDI kuhakikisha
dhana ya mnyororo wa thamani inaonekana kwenye mazao ya misitu,"
amesema.
Mwenyekiti wa
CCM Wilaya ya Songea Hamisi Abdallah amesema chama kitaunga mkono jambo
lolote ambalo linachochea kubadilisha maisha ya wananchi.
"Miradi
hii inachangia kuongeza kipato cha wananchi, ajira na thamani ya mazao
ya misitu hivyo CCM itaendelea kuunga mkono kwani ndio lengo la Ilani
yetu," amesema.
Naye
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Songea, Benas Komba amesema ujio wa mashine
hiyo itachochea uzalishaji kwenye mazao ya misitu hivyo watahakikisha
ushiriki wa Serikali unakuwa wa kutosha.
Komba amesema mashine hiyo itachangia ongezeko la mapato, ajira na ukuaji wa uchumi wa wananchi, vijiji na halmashauri.
No comments:
Post a Comment